2⃣5⃣ MAMBO MUHIMU UNAYOTAKIWA UYAFANYE ILI UPATE KUISHINDA DHAMBI YA UZINZI
Na: MWL STEVEN & BETH MWAKATWILA
KUPATA APP YETU “HUSONEMU (MWAKATWILA) APP” BONYEZA LINK HII HAPA:
FUATANA NASI:- KWENYE APP, FACEBOOK, INSTAGRAM, ONLINE RADIO 📻, WHATSAPP, WEBSITE & YOUTUBE, Kwa links zilizoko kwenye HII LINK hapa:
🗓 01 Aprili, 2019
Bwana Yesu Kristo asifiwe sana. Ninamshukuru Mungu sana kwa mambo mema mno anayotutendea. Nimekuletea somo. Somo hili litakuwa linatufikisha mwisho wa mfululizo mzima wa somo hili.
Naamini kuna kitu kwa sehemu umejifunza, nakushauri yaweke kwenye matendo yale uliyojifunza. Yatakusaidia kuishinda dhambi ya uzinzi. Usisite kuniuliza swali mahali haujaelewa au unapohitaji msaada wa kishauri au hata maombi.
Hebu sasa tuendelee mbele. Nilianza kukuonyesha milango ambayo inayoweza kuwa chanzo cha pepo kumrudia mtu. Baada ya kukuonyesha mfumo wa dhambi unavyoweza kumpatia adui uhalali nataka nikuonyeshe kwa upana zaidi eneo hili la dhambi.
Bwana Yesu Kristo anatufundisha kuwa pepo mchafu amtokapo mtu ana tabia ya kufanya majaribio ya kumrudia tena huyo mtu. Maandiko yanatufundisha hivi.
“Pepo mchafu amtokapo mtu, hupitia mahali pasipo maji, akitafuta mahali pa kupumzika; asipoona, husema, Nitairudia nyumba yangu niliyotoka. Hata afikapo, akaiona imefagiwa na kupambwa, ndipo huenda akachukua pepo wengine saba, walio waovu kuliko yeye mwenyewe, wakaingia na kukaa humo; na mtu yule hali yake ya mwisho huwa mbaya kuliko ya kwanza.” (Luka11:24-26).
Ukiipitia hiyo mistari utagundua kuwa pepo lolote lile linapotolewa ndani ya mtu hapo Bwana ameita nyumba linakuwa na tabia ya kutafuta mpenyo wa kuirudia hiyo nyumba au kumrudia huyo mtu.
Kinachosababisha hamu au shauku ya kurudi ni mazingira ya hiyo nyuma au huyo mtu. Kuna vitu ataviona kwa huyo mtu navyo ni mfumo wa kumvutia. Mapepo yanavutiwa na dhambi zisizofubiwa. Hapo namaanisha hivi, unaweza kutenda dhambi lakini unaificha badala ya kuiungama na kuiacha.
Watu wengi waliotolewa mapepo hawajui kuwa wanapohifadhi dhambi au kuitenda hiyo dhambi mara kwa mara wanajiletea hatari ya kurudiwa na mapepo tena yanarudi mengi kuliko yale ya kwanza.
Nakumbuka niliwahi kukutana na binti mmoja ambaye alikuwa anafuatiliwa na shetani. Alinisimulia habari ndefu sana, alikuwa na mikataba na shetani na akamtumikia sana tu.
Baadaye akakutana na Bwana Yesu Kristo mapepo yaliyokuwa ndani yake yakatolewa akawa huru. Baada ya muda akashangaa anamwona shetani akimfuata na kudai anataka wafunge tena agano ili aendelee kumtumikia, wakati ananisimulia habari hiyo.
Niligundua moyoni mwangu kuwa lazima kutakuwa na mlango ambao shetani anautumia ili kumrudia huyo binti ingawa huyo binti hataki. Nilijua kuwa kuna kitu kibaya tu afanyacho huyo binti kinachomba shetani mvuto tena wa kumfuatilia huyo binti.
Nikamwuliza je! Ana mahusiano yoyote na kijana wa kiume? Akasema ndiyo. Nikamkazia macho niambie mahusiano yenu yakoje? Unajua niligundua katika mahusiano yao na huyo kijana wamevuka mpaka mnoo. Wanaweza kukumbatiana kutomasana mpaka kupigana busu ya kikubwa!!!! wengine wanaita busu la ulimi. Nikamwambia dhambi hiyo ndiyo mlango wa shetani anautumia ili kukurudia.
Akaniambia itakuwa ni kweli kwani tokea ameanza mahusiano na huyo kijana tu ndipo anamuona shetani akianza kumfuatilia. Yeye alikuwa anayaona mapepo macho kwa macho kwani alikuwa na mambo ya ajabu kweli huyo binti. Kufunguliwa kwake tu ilikuwa si mchezo.
Nikamwamuru aachane na huyo kijana haraka sana kwa usalama wake. Alinikubalia. Sasa sikia, unapotolewa mapepo fahamu tena kuwa adui atataka kurudi na atatumia mfumo wa tabia zako mbaya ili kuwa mlango wa kuingilia tena ndani ya mwili wako.
Ikimbie zinaa ya namna yoyote ile. Usimruhusu kijana wa kiume au wa kike akuzoee na kuvuka mipaka. Angalia unaongea naye nini huyo kijana. Unapotolewa pepo la uzinzi na halafu wewe mwenyewe ukaenda kuzini tena kwa kuzifuata tamaa za mwili wako fahamu anaweza kuutumia mlango wa dhambi hiyo hiyo kukurudia.
Usifanye punyeto au kujisaga, ukifanya hivyo baada ya kutolewa pepo la uzinzi fahamu huo unaweza kuwa mlango wa roho ya uzinzi kurudia tena.
ACHA UONGO, Biblia inasema shetani ni baba wa uongo. “Ninyi ni wa baba yenu, Ibilisi, na tamaa za baba yenu ndizo mpendazo kuzitenda. Yeye alikuwa mwuaji tangu mwanzo; wala hakusimama katika kweli, kwa kuwa hamna hiyo kweli ndani yake. Asemapo uongo, husema yaliyo yake mwenyewe; kwa sababu yeye ni mwongo, na baba wa huo.” (Yohana 8:44).
Ukiipitia hiyo mistari utagundua dhambi ya uongo chanzo chake ni ibilisi mwenyewe, na mtu asemapo uongo huungana kabisa na mwanzilishi wa hiyo tabia. Yaani baba wa uongo ni shetani sasa angalia kitu hiki unaposema uongo unaungana kabisa na taasisi ya mwanzilishi wa uongo.
Ngoja nikuonyeshe kitu. Mungu aliumba miili yetu hii akaweka tendo la ndoa. Akaliweka litumike kihalali kwa wanandoa. Fahamu ni tendo lililoumbwa na Mungu shetani yeye anapowashawishi watu walifanye tendo lile lile kwa waisooana tunaita uzinzi.
Sasa kwenye uongo fahamu Mungu hajawahi kuumba hilo jambo. Linapofanywa na mtu fahamu halijachakachuliwa kama vile uzinzi. Yaani tendo la ndoa tuliumbiwa lakini kwa utaratibu uliowekwa. Adui anachofanya ni kukutoa tu kwenye utaratibu.
Uongo haukutoi kwenye utaratibu, unaungana na alichokizalisha yeye mwenyewe. Umenielewa lakini hapo? Unapojifunza somo la dhambi usifikiri dhambi zinafanana. Kuna zingine nguvu yake ni tofauti na nyingine.
Bahati mbaya sana watu wengi wanapoutazama uongo wanautazama kama ni dhambi ndogo sana. Aisee uongo ni dhambi mbaya sana sana. Mimi zamani zile kabla ya kuokoka nilikuwa mwongo sana, yaani nilizoelea na niliona uongo ni kitu cha kawaida tu. Niliupenda na niliusema kweli.
Yaani kusema uongo niliona ni kama umjini hivi. Nilipookoka Mungu akaanza taratibu kunifundisha tabia hii inavyomwudhi na asili yake ni wapi na waongo na shetani wakoje. Niliogopa sana. Kitendo cha kuiogopa hiyo dhambi ndiko kulifanya nianze kuichukia hii hiyo tabia.
Nilipoichukia tu nikashangaa ninaanza kuishinda taratibu mpaka leo hii mimi eti nawashangaa waongo na kujiuliza kwa nini huyu anasema uongo?
Uongo ni dhambi ambayo wapendwa wengi hasa Watanzania wanaipenda sana. Watu wengi hawapendi mtu anayewaambia ukweli. Wanapenda kuambiwa uongo mnaita “udaku”.
Yaani mtu analeta habari ina kaukweli asilimia tano lakini asilimia tisini na tano ni uongo mtupu. Hooo! huyo atauza sana habari yake. Watu si ndiyo wanapenda?
Hata kiongozi akiwa mkweli watu hawampendi, ngoja nikuchekeshe. Siku moja zamani zile nimetoka kuokoka alikuja mwalimu mmoja nampenda sana, alituuliza swali hivi leo mmeoga? Mmeogea sabuni gani? Akasema hivi kweli mtu umeokoka unaogea sabuni ya kufulia nguo?
Humo ndani asilimia tisini hivi tulikuwa tunaogea sabuni za kufulia. Yaani kipindi hicho mpendwa ni mtu aliyejizira hivi, mtu mchafu mchafu hivi eti ndiyo wa kiroho. Nakumbuka kipindi kile kulikuwa na vitambaa fulani vina urembo wa shangashanga yaani vilichomwa moto.
Mwalimu alipofundisha tena alichomekea kidogo tu habari za kuogea sabuni ya kufulia. Watu wengi walimchukia. Naamini wengi hata somo lile lote zuri alilolifundisha mwalimu yule hawakulishika. Unajua mimi nilitulia. Nikampenda yule mwalimu niliona yule katuambia ukweli kabisaaa.
Nikishangaa akija mtu akisema uongo hooo Mungu anataka tuogee foma. Foma ilikuwa sabuni ya kufulia ilikuwa ya unga sina uhakika kama miaka hii ipo. Watu ndiyo wanafurahi. Ohoo Mungu kasema watu waache kazi, tudumu kuhubiri na kuomba tuu!!! Watu ndiyo wanafurahia, mwalimu aliyesema kweli kuwa Mungu kasema asiyefanya kazi asile, watu wanamchukia.
Nilikaa chini nikagundua mkweli hapendwi tena haeleweki haraka. Nikaanza kuyachukia mafundisho ya uongo uongo yanayokuja kama yana ukweli hivi. Na nikagundua shetani ndiye chanzo cha hayo mafundisho ya uongo.
Sasa sirahisi kukubali ukweli, kwa sababu kuna vita kali mnooo kati ya ukweli na uongo. Bahati mbaya watu wengi mno wanapenda sana uongo kwa sababu hawajui madhara yake.
Wewe angalia watu kwenye vikundi vya maombi, kwaya nk. Utagundua dhambi hii imewabana wengi mnoo na inawaharibia kweli ila hawajui. Fikiria wewe ni mtumishi halafu unawaambia watu uongo, Ohooo! Mungu kanibariki sana mimi nina hiki na hiki. Hao watu siku wakigundua huna hivyo ulivyowaambia unavyo watakudharau sana.
Kwa nini usiseme ukweli tu? Fikiria unawaomba watu fedha au wakutunze kwa kusema uongo!!! Hooo! Mungu kaniambia fulani na fulani watoe kiasi fulani na tukanunue mabati. Kumbe Mungu hajakuambia ni uongo tu umeutunga.
Hivi ukisema ukweli tu kuwa ndugu zangu NAOMBA FEDHA NIKANUNUE MABATI BADALA YA KUMSINGIZIA MUNGU KUWA KASEMA?
Si useme tu MWENZENU SINA CHAKULA NAOMBA MSAADA!!! Nenda kwenye timu za maombi fuatilia maono yao usishangae kuona mtu anatengeneza ono kiuongo-uongo kabisaa kisa akubalike aonekane kuwa na yeye Mungu anamuonyesha.
Sikiliza mpendwa dhambi hii ni mbaya mnooo tusiiendekeze kabisa tuikatae. Fikiria mtu anamsemea maneno ya uongo kwa watu, mke wake au mume wake huku akishinda kanisani hashituki hata kushituka?
Umewahi fikiria makuhani na waandishi walimshitaki Bwana Yesu Kristo kwa uongo tu? Yohana aliwaambia hawa watu maneno haya. “Askari nao wakamwuliza, wakisema, Sisi nasi tufanye nini? Akawaambia, Msidhulumu mtu, wala msishitaki kwa uongo; tena mtoshewe na mshahara wenu.” (Luka 3:14)
Umewahi fikiria leo hii watoto wa Mungu wanavyoshitakiana tena mashitaka ya uongo? Ukiingia ndani ya uongo utagundua humo ndani kufungwa, wivu, husuda, mashindano, kiburi, uuaji, majivuno, hasira, ukatili, chuki, nk.
Huwezi kumsemea mtu umpendaye uongo, huwezi kumsemea uongo mtu usiyeshindana naye nk. Uongo ni dhambi mbaya mnoo kuliko unavyofikiria.
Tena ni dhambi inayowaambukiza na kuwaangamiza wengine. Ngoja nikupe mfano. Nikikuambia uongo na ukaniamini na wewe utaenda kumwambia mwingine uongo na yeye akikuamini maana yake woooote mliouamini uongo mnangia kwenye kapu moja la WAONGO.
Umewahi kufikiria hili? Ukidanganya na watu wakadanganyika fahamu wote wanaingia kwenye kundi la wadanganyifu. Sasa angalia ulivyomtumikia shetani kwa neno la uongo tu? Ukawaingiza wooote kwenye dhambi hiyo.
Dhambi hii ina sehemu kubwa sana ya kuyafanya mapepo yawarudie watu walioondolewa mapepo ambao hawajauacha uongo.
Unajua dhambi ya uongo na uzinzi vipo jirani mno ni kama pua na mdomo hivi. Wewe wafuatilie waongo wengi, utagundua wengi ni wazinzi. Fuatilia mwanamke mzinzi hawagi mkweli. Mfuatilie mwanaume mzinzi utagundua ni mwongo kweli kadanganya wasichana wengi mnoo, mwanamke mzinzi ni vivyo hivyo anawadanya wanaume wengi kweli mnoo.
Kwa hiyo jihadhari mno na dhambi hii kama umeombewa na mapepo yakatoka ili yasikurudie acha uongo. Umenielewa? Acha hiyo tabia ni dhambi mbaya. Sema ukweli upende ukweli uwe vile ulivyo usimdanganye mtu kwa kuishi kwa kuigiza.
Jambo lingine ni hili JIFUNZE KUZIHIFADHI NGUVU ZA MUNGU KWA WINGI NDANI YAKO.
Msikilize Bwana Yesu Kristo asemavyo.
“Lakini, ikiwa mimi natoa pepo kwa kidole cha Mungu, basi ufalme wa Mungu umekwisha kuwajilia.Mtu mwenye nguvu aliyejifunga silaha zake, alindapo nyumba yake, vitu vyake vi salama;lakini mtu mwenye nguvu kuliko yeye atakapomwendea na kumshinda, amnyang’anya silaha zake zote alizokuwa akizitegemea, na kuyagawanya mateka yake. Mtu ambaye si pamoja nami yu kinyume changu; na mtu asiyekusanya pamoja nami hutawanya. Pepo mchafu amtokapo mtu, hupitia mahali pasipo maji, akitafuta mahali pa kupumzika; asipoona, husema, Nitairudia nyumba yangu niliyotoka. Hata afikapo, akaiona imefagiwa na kupambwa, ndipo huenda akachukua pepo wengine saba, walio waovu kuliko yeye mwenyewe, wakaingia na kukaa humo; na mtu yule hali yake ya mwisho huwa mbaya kuliko ya kwanza.” (Luka 11:20:26)
Ukiipitia hiyo mistari utagundua pia ili mtu asiingiliwe na adui ni lazima awe na nguvu na silaha.
Ngoja nijaribu kukuonyesha kwa ufupi. Ili leo ndani yako uwe na nguvu za Mungu, ni lazima umruhusu huyo Mungu mwenye hizo nguvu akae ndani yako. Huwezi kumtofautisha Mungu na Bwana Yesu Kristo na Roho Mtakatifu. Kwa hiyo ili nyumba yako au mwili wako uweze kupewa nguvu za Mungu ni lazima uhakikishe unampokea Bwana Yesu Kristo moyoni au ndani yako.
Ni hatari sana ukalitoa pepo ndani ya mtu na mtu huyo ndani yake asiwe na mtoaji pepo yaani Roho Mtakatifu. Maandiko yanasema hivi. “Lakini mimi nikitoa pepo kwa Roho wa Mungu, basi ufalme wa Mungu umekwisha kuwajilia.” (Mathayo 12:28)
Umeona pepo anatolewa kwa Roho Mtakatifu. Kwa lugha nzuri mapepo kiboko yao ni huyu Roho Mtakatifu. Sasa unapomhifadhi huyu Roho Mtakatifu ndani yako ni ngumu mno kwa pepo kukufuatilia.
Fanya hivi. Hakikisha kila siku unasoma neno la Mungu. Kumbuka neno la Mungu ni moto au ni nguvu au upanga wa Roho wa Mungu. Soma neno liweke moyoni mwako lifanyie kazi. Jifunze kusikiliza mafundisho au mahubiri ya neno la Mungu.
Hakikisha kila siku uwe na muda kuomba wewe binafsi. Omba Ulinzi wa Mungu kwako, ombea na watu wengine. Omba ujazo wa Roho Mtakatifu na nguvu zake zijae ndani yako.
Usiache kwenda kanisani au kwenye vikundi mbalimbali vya maombi au mahali neno la kweli linasema hapo. Ni rahisi kuwa na nguvu za Mungu ukifanya hayo niliyokuambia.
Naamini umenielewa katika hili somo lote nililokuahidi kukufundisha.
Mungu akubariki sana.
Ukihitaji masomo yetu unaweza kuyapata kwa njia hizi zifuatazo:-
3. YouTube - Mwakatwila au HUDUMA YA SOMA NENO LA MUNGU (HUSONEMU).
4. Facebook ingia katika hiyo tovuti au website yetu utaona alama ya Facebook(f) like na utapata maelezo ya kujiunga au ingia Facebook halafu andika “SOMA NENO LA MUNGU”
5. Instagram ingia Instagram app halafu andika “Steven Mwakatwila”
6. DVDs 📀 au CDs 💿
7. VITABU.
NB: Wasiliana na mhudumu ofisini kwa namba +255 763 109 733, kupata VITABU, DVD & CD.
8. Kwa njia ya REDIO:- Utapata mafundisho yetu kwa redio zifuatazo:-
➖Rungwe FM 102.5 Kila siku ya Jumapili saa tatu mpaka saa nne usiku.
➖Baraka FM 107.7 Kila siku ya Jumanne saa kumi na mbili jioni mpaka saa moja usiku.
➖Bomba FM 104.1 Kila siku ya Ijumaa saa tatu usiku mpaka saa nne usiku.
Kwa Mawasiliano zaidi Utatupata kwa namba hizi:-
+255 754 849 924 Au +255 756 715 222
Wako
Mwl Steven & Beth Mwakatwila.
01/04/2019