Salamu – Agosti, 2020
Bwana Yesu Kristo asifiwe sana. Pole na hongera kwa kila jambo ulilokutana nalo mwezi uliopita. Tunamshukuru Mungu aliyetupatia nafasi hii ya kuuona mwezi huu mpya. Naamini katika mwezi huu kuna baraka ambazo Mungu ameziweka au kuzifunga ndani ya mwezi huu. Muombe Mungu akujarie kukutana nazo.
Nimekuletea salamu za mwezi. Naamini umekua ukibarikiwa na salamu za miezi iliyopita. Kumbuka tuna salamu zenye kichwa
MAMBO MUHIMU UNAYOTAKIWA UYAFANYE ILI UPATE WOKOVU (ENEO LA KUOKOLEWA KATIKA KIPINDI CHA MAJANGA ULIMWENGUNI)
JAMBO LA SABA JIFUNZE KUTOKUISHI KWA HOFU ISIYOFAA
Sikiliza ili leo hii upate kuokolewa na Mungu katika majanga ambayo chanzo chake ni tauni iliyoachiliwa na Mungu, ikiwa wewe ni kuhani na umewajibika kwa sehemu yako unatakiwa uhakikishe unaondoa hofu moyoni mwako ya kukutana na mauti hiyo iliyobebwa na tauni iliyoachiliwa na Mungu
KUNA HOFU AU WOGA WA AINA MBILI
Unaposoma maandiko matakatifu utaona ndani ya Biblia tunafundishwa kuwa kuna hofu za aina mbili;
HOFU INAYOTOKA KWA MUNGU
Angalia mistari hii: _“Basi tukiijua hofu ya Bwana, twawavuta wanadamu; lakini tumedhihirishwa mbele za Mungu. Nami natumaini ya kuwa tumedhihirishwa katika dhamiri zenu pia.” *(2 Wakorintho 5:11)
Angalia na mistari hii: “Tazama, nitatia roho ya hofu ndani yake, naye atasikia kivumi, na kuirudia nchi yake mwenyewe; nami nitamwangusha kwa upanga katika nchi yake mwenyewe.” *(2 Wafalme 19-7)
Hofu ni roho. Ukiipitia hiyo mistari hiyo utaona kuwa kuna hofu ya Bwana,ambayo hutoka kwa Mungu kabisa. Hofu hii Mungu huitumia kwa kazi nyingi tu.
Moja ya kazi ya hofu hii ni kuwafanya wanadamu wamwogope Mungu na kuacha matendo yao mabaya.
Angalia mfano huu angalia na mistari hii: “Hasira ya Mungu ikapanda juu yao, Akawaua waliokuwa wanono; Akawaangusha chini vijana wa Israeli. Pamoja na hayo wakazidi kutenda dhambi, Wala hawakuyaamini matendo yake ya ajabu. Kwa hiyo akazikomesha siku zao kama pumzi, Na miaka yao kwa hofu ya kuwasitusha. Alipowaua ndipo walipokuwa wakimtafuta; Wakarudi wakamtaka Mungu kwa bidii. Wakakumbuka kuwa Mungu ni mwamba wao, Na Mungu Aliye juu ni mkombozi wao (Zaburi 78:31-35)
Ukiipitia hiyo mistari utagundua kuwa Mungu anapoona wanadamu wamezidisha uovu juu ya nchi huchukua hatua ya kuwatiisha hao watu kwa jambo fulani ambalo ndani yake huibeba roho hiyo ya hofu na hofu hiyo maandiko husema huwashitua watu na watu hao ndipo huona umuhimu wa kumtafuta Mungu na kuacha njia zao mbaya.
TAUNI HUBEBA HOFU YA MUNGU NDANI YAKE
Mungu ana akili nyingi mnoo ya kutuvuta kwake ukiona majanga kama ya ya tauni fahamu ndani yake majanga haya hubeba hofu ya Mungu ndani yake.
Watu wanapokufa kwa tauni unajua ndipo wanadamu wengi huanza kumkumbuka Mungu na kumwogopa?
Wanadamu wengi huingia katika mashaka makubwa na mifadhaiko mingi mioyo yao hubeba huzuni n.k. Biblia inasema huzuni hubeba hofu na pia zipo huzuni za aina mbili pia
Angalia mistari hii: “Kwa sababu, ijapokuwa naliwahuzunisha kwa waraka ule, sijuti; hata ikiwa nalijuta, naona ya kwamba waraka ule uliwahuzunisha, ingawa ni kwa kitambo tu.Sasa nafurahi, si kwa sababu ya ninyi kuhuzunishwa, bali kwa sababu mlihuzunishwa, hata mkatubu. Maana mlihuzunishwa kwa jinsi ya Mungu, ili msipate hasara kwa tendo letu katika neno lo lote. Maana huzuni iliyo kwa jinsi ya Mungu hufanya toba liletalo wokovu lisilo na majuto; bali huzuni ya dunia hufanya mauti. Maana, angalieni, kuhuzunishwa kuko huko kwa jinsi ya Mungu kulitenda bidii kama nini ndani yenu; naam, na kujitetea, naam, na kukasirika, naam, na hofu, naam, na shauku, naam, na kujitahidi, naam, na kisasi! Kwa kila njia mmejionyesha wenyewe kuwa safi katika jambo hilo.” (2 Wakorintho 2: 7-11)
Ukiipitia hiyo mistari utaona kuwa huzuni pia hubeba hofu. Hofu itokayo kwa Mungu huibeba huzuni pia itokayo kwa Mungu. Mungu anapotuhuzunisha wanadamu kwa kutuletea hofu fahamu anachokitafuta ni kuona hao wanadamu wanatubia matendo yao.
Biblia inasema haya majanga yanapotokea huleta faida, angalia anasema “Maana mlihuzunishwa kwa jinsi ya Mungu, ili msipate hasara kwa tendo letu katika neno lo lote. Maana huzuni iliyo kwa jinsi ya Mungu hufanya toba liletalo wokovu lisilo na majuto;”
Mtu yeyote yule mwenye akili timamu hawezi kuendelea kufanya jambo ambalo anajua kabisa mwenzie kaadhibiwa tena kwa kuuawa. Mwenye akili ataliacha hilo jambo haraka sana. Na ataogopa kuendelea kulifanya.
Leo hii hofu hii ya Corona imewavuta watu wengi waanze kumkumbuka Muumba wao. Hata wale wanaomkumbuka wanajipanga vizuri kweli kweli. Ehehee!!
Ngoja nikukumbushe kitu. Kumbuka zamani ulipokuwa shule ya msingi siku ya mkaguo na iwe zamu ya yule mwalimu ambaye anafahamika kwa ukali mpaka shule ya tatu ambayo hajawahi hata kufundisha?
Wanafunzi woote siku hiyo huingiwa na hofu na kila mmoja utaona muda wa dakika chache tu alivyojifanyia usafi; iwe kwa mate, kwa kula kucha, kama nywele hakuchana na kichanio hakipo unajua hutafuta chelewa zinapangwa na kuwa kichanio siku hiyo mpaka nywele zionekane sawa.
Mungu anapowajilia wanadamu kwa mtindo huo wa kuwatia adhabu fahamu ndani yake hutaka kuona watu wakiwa na hofu ya kumwogopa.
Biblia inasema hivi: “Mwe na hofu wala msitende dhambi, Tafakarini vitandani mwenu na kutulia.” (Zaburi 4:4)
Hii ni hofu ya Mungu inayotufanya sisi tusifanye dhambi. Ukimhofu Mungu au kumcha fahamu huwezi kutenda dhambi. Na hofu hii inaweza kubebwa na taarifa uliyoipata kuwa Mungu amewafanyia jambo fulani watu waliotenda dhambi, huwezi wewe ukatenda dhambi wakati wenzio wamepigwa.
Biblia inatufundisha kuwa tunatakiwa tuwakemee watu wadumuo kutenda dhambi mbele za watu ili watu wengine waogope. Angalia mistari hii: “Wale wadumuo kutenda dhambi uwakemee mbele ya wote, ili na wengine waogope.” *(1 Timotheo 5:20)
Kama Mungu anampa mwanadamu maarifa haya unafikiri yeye hawezi kuwaogopesha watu kwa kuyafanya mambo kama yayo hayo? Mungu huleta tauni ili tu kutujengea sisi wanadamu hofu ya kutokudumu katika kutenda maovu.
HOFU ILETAYO MAUTI AU MABAYA
Pia Biblia inatufundisha kuwa kuna hofu ambayo chanzo chake si Mungu. Na hofu hiyo inaweza kumsababishia huyo mwenye hofu kukipata kitu hicho kibaya anachokiogopa.
Angalia mistari hii: “Aogopacho mtu asiye haki ndicho kitakachomjilia; Na wenye haki watapewa matakwa yao.” (Mithali 10:24)
Ukiipitia hiyo mistari utagundua kuwa. Haikupasi ndugu kuwa na hofu ya kupatwa na tauni. Kwa mujibu wa mistari hiyo tunafundishwa kuwa ili tusipatwe na tauni au jambo baya tunatakiwa tuhakikishe hatukiogopi hicho kitu.
Sikiliza mwogope Mungu, usiogope kitu kingine. Angalia hii mifano: “Ulalapo hutaona hofu; Naam, utalala na usingizi wako utakuwa mtamu. Usiogope hofu ya ghafula, Wala uharibifu wa waovu utakapofika.” (Mithali 3:24-25)
Unapoona kuna mambo kama hayo wewe mpendwa unatakiwa usiingize hofu yoyote.
JENGA IMANI YA KUOKOLEWA KATIKA JANGA HILI
Kumbuka unapopata hofu ni rahisi kujikuta unakutana na hicho, unachokiogopa.
Mfano, angalia umesikia habari za tauni yoyote au nzige au vita yaani upanga moyoni mwako unalitazamaje hili jambo?
Wewe ni kuhani, mwombezi unatakiwa uhakikishe unajenga imani moyoni mwako ya kuokolewa na Mungu katika janga hili.
Usiogope na kujaa mashaka na kukosa amani kisa eti umesikia tauni ya aina yoyote ile inaua wazee, vijana, nk.
Ili uokolewe unatakiwa ujifunze kutokuwa na mashaka. (SINA MAANA USICHUKUE HATUA YOYOTE UTAKAYO AMBIWA NA SAREKALI) Ninachotaka kukujengea ni hiki usiogope amini kuokolewa hata kama ukikutana nao.
Kwa nini uwaze kufa wakati kuna watu wameugua tauni hiyo na umewaona wamepona? Kwa nini ufikiri utaambukizwa wakati kuna watu wengi tu wapo katika nchi iliyojaa tauni hiyo na hawajaambukizwa?
KAA MBALI NA MTU AKULETEAYE MANENO YA HOFU
Biblia inasema hivi: “Tena maakida na waseme zaidi na watu, wawaambie, Ni mtu gani aliye hapa tena mwenye hofu na moyo mnyonge? Aende akarudi nyumbani kwake, isije mioyo ya nduguze ikayeyuka mfano wa moyo wake.” (Kumbukumbu la Torati 20:8)
Ukiipitia hiyo mistari utaona hiki ninachokuambia. Mtu ambaye ana moyo wa hofu haifai kukaa naye karibu. Atakuambukiza hiyo roho ya kuogopa.
HOFU AU MASHAKA NI SUMU YA IMANI
Unapomwomba Mungu akuokoe na tauni unatakiwa ujenge imani ya kuokolewa wewe na nyumba yako na taifa lako. Imani ni kuwa na hakika ya mambo yatarajiwayo.
Jenga uhakika moyoni mwako ya kuwa Mungu ameokoa. SIYO ATAKUOKOA NASEMA AMEKUOKOA.
Ukijenga imani hiyo fahamu hautazama ndani ya tauni. Angalia mifano hii: _“Mara akawalazimisha wanafunzi wake wapande chomboni na kutangulia mbele yake kwenda ng’ambo, wakati yeye alipokuwa akiwaaga mkutano. Naye alipokwisha kuwaaga makutano, alipanda mlimani faraghani, kwenda kuomba. Na kulipokuwa jioni, alikuwako huko peke yake. Na kile chombo kimekwisha kufika katikati ya bahari, kinataabika sana na mawimbi; maana upepo ulikuwa wa mbisho. Hata wakati wa zamu ya nne ya usiku Yesu akawaendea, akienda kwa miguu juu ya bahari. Wanafunzi walipomwona akienda juu ya bahari, wakafadhaika, wakisema, Ni kivuli; wakapiga yowe kwa hofu. Mara Yesu alinena, akawaambia, Jipeni moyo ni mimi; msiogope. Petro akamjibu, akasema, Bwana, ikiwa ni wewe, niamuru nije kwako juu ya maji. Akasema, Njoo. Petro akashuka chomboni, akaenda kwa miguu juu ya maji, ili kumwendea Yesu. Lakini alipouona upepo, akaogopa; akaanza kuzama, akapiga yowe, akisema, Bwana, niokoe. Mara Yesu akanyosha mkono wake, akamshika, akamwambia, Ewe mwenye imani haba, mbona uliona shaka?” (Mathayo 14:22-31)
Ukiipitia hiyo mistari utakigundua hiki ninachokuambia. Kilichomfanya Petro azame ni hofu ya maji. Fikiria alianza kutembea juu ya maji. Fikiria mwokozi yupo na ndiye amemwambia njoo yeye aliona shaka!!
Shaka ndiyo sumu ya imani. Na sisi tunaokokewa kwa imani. Hata hili janga tunaokolewa kwa imani.
Ondoa woga amini umeokolewa mpendwa!!! Usiangalie unasikia nini wangapi wamekufa wangapi wameambukizwa n.k.
Katika kipindi watoto wa Mungu wengi hujikuta wakiacha hata kufanya kazi ya kuwaingizia kipato kisa eti hofu ya tauni.. Usihofu ondoa masikio yako kusikia habari za kukutisha tamaa.
Fanya kazi zako kama kawaida, panga mipango yako kama kawaida. Mwenye kwenda shamba nenda shamba. Ngoja nikuchekeshe, katika kipindi cha corona 19, tauni hiyo ilikua ikileta mafua yaani tatizo la upuaji.
Fikiria mtu anahofu, na akapita kwenye vumbi hivi au akapita kwenye eneo la watu wanaopaka ukuta rangi, ni rahisi kujikuta ana mafua, sasa hapooo!!
Nirahi mpendwa kuanza kuwasumbua watu tu na wauguzi. Kisa hofu ya tauni hiyo.
“Nirahisi kila waki kusema hivi Ohoooo! Nahisi ninao!!!” Sikiliza ukikutana na hali hiyo ondoa hofu mpendwa, yamkini ni mafua ya kawaida tu. Fikiria ndiyo umekutana na mtu ana mafua tu. Hapo sasa? Niliwaona watu wengi wakiwaogopa watu sana.
Usishangae kwa ajili ya hofu watu wengi walishuka kwenye magari au bajaji, kisa waliogopa tauni ya Corona, ukifikia hali hiyo mpendwa wewe sasa ni mtumwa na ni mtu asiye na imani kwa Mungu wake.
Hebu angalia ahadi ya Mungu katika maneno haya. “Mungu, unirehemu, maana yuko atakaye kunimeza, Mchana kutwa ananionea akileta vita. Adui zangu wanataka kunimeza mchana kutwa, Maana waletao vita juu yangu kwa kiburi ni wengi. Siku ya hofu yangu nitakutumaini Wewe; Kwa msaada wa MUNGU nitalisifu neno lake. Nimemtumaini Mungu, sitaogopa; Mwenye mwili atanitenda nini?” (Zaburi 56:1-4)
Angalia na mistari hii mingine.“Aketiye mahali pa siri pake Aliye juu Atakaa katika uvuli wake Mwenyezi.Nitasema, BWANA ndiye kimbilio langu na ngome yangu, Mungu wangu nitakayemtumaini. Maana Yeye atakuokoa na mtego wa mwindaji, Na katika tauni iharibuyo. Kwa manyoya yake atakufunika, Chini ya mbawa zake utapata kimbilio; Uaminifu wake ni ngao na kigao. Hutaogopa hofu ya usiku, Wala mshale urukao mchana, Wala tauni ipitayo gizani, Wala uele uharibuo adhuhuri, Ijapo watu elfu waanguka ubavuni pako. Naam, kumi elfu mkono wako wa kuume! Hata hivyo hautakukaribia wewe. Ila kwa macho yako utatazama, Na kuyaona malipo ya wasio haki. Kwa kuwa Wewe BWANA ndiwe kimbilio langu; Umemfanya Aliye juu kuwa makao yako.Mabaya hayatakupata wewe, Wala tauni haitaikaribia hema yako.Kwa kuwa atakuagizia malaika zake Wakulinde katika njia zako zote.” (Zaburi 91:1-11)
Sikiliza keti na Mungu kaa chini ya uvuli wake yaani jiachie kwake utaokolewa na tauni mpendwa. Usihofu sasa. Fanya unayoweza kufanya lakini jenga matumaini yako kwake. Matumai ya kuwa Bwana Yesu Kristo kukuokoa.
Mungu akubariki sana. Tuonane tena katika kona hii mwezi ujao.Naamini umenielewa sana.Ukihitaji masomo yetu unaweza kuyapata kwa njia hizi zifuatazo:-
App yetu ya huduma yenye jina “MWAKATWILA (HUSONEMU)” utaipata Play Store ambapo kuna masomo mengi sana hapo.
Tovuti yetu ya www.mwakatwila.org
YouTube – Mwakatwila au HUDUMA YA SOMA NENO LA MUNGU (HUSONEMU).
Facebook ingia katika hiyo tovuti (website) yetu utaona alama ya Facebook (f) “like” na utapata maelezo ya kujiunga au ingia Facebook halafu andika “SOMA NENO LA MUNGU”
Instagram ingia Instagram app halafu andika “Steven Mwakatwila”
DVDs au CDs
VITABU. Wasiliana na mhudumu ofisini kwa namba +255 763 109 733, ili kupata VITABU, DVD & CD.
Kwa njia ya REDIO:- Utapata mafundisho yetu kwa redio zifuatazo:-
Rungwe FM 102.5 Kila siku ya Jumapili saa tatu mpaka saa nne usiku.
Baraka FM 107.7 Kila siku ya Jumanne saa kumi na mbili jioni mpaka saa moja usiku.
Bomba FM 104.1 Kila siku ya Ijumaa saa tatu usiku mpaka saa nne usiku.
Unaweza kutupata kwenye ONLINE RADIO yetu:- radio.mwakatwila.org
Kwa Mawasiliano zaidi Utatupata kwa namba hizi:-
+255 754 849 924 au +255 756 715 222
Wako
Mwl Mr & Mrs Steven Mwakatwila.