Tuesday, March 31, 2020

3️⃣ MAMBO MUHIMU UNAYOTAKIWA UYAFANYE ILI UPATE WOKOVU KATIKA ENEO LA MATATIZO YALETWAYO NA TAUNI

Na: MWL STEVEN & BETH MWAKATWILA.

FUATANA NASI:- KWENYE APP,  FACEBOOK, INSTAGRAM, ONLINE RADIO 📻, WEBSITE, WHATSAPP GROUPS & YOUTUBE; Kwa links zilizoko hapa kwenye link hii:

🖊️  31 /03/ 2020.

Bwana Yesu Kristo asifiwe sana. Nichukue nafasi hii kukukaribisha tena darasani. Kumbuka tuna somo maalumu ambalo linahusu sana kipindi hiki tunachopitia kwa sasa. 
Tukimaliza tu, tunarudi katika mfululizo wa somo la “JIFUNZE KUJUA MISINGI AU VYANZO VYA MAGUMU AU MATATIZO UNAYOKUTANA NAYO KABLA HAUJAAMUA KUYASHUGHULIKIA.”

Leo tusogee tena mbele kidogo.

HIKI NI KIPINDI CHA TATU

katika kipindi kilichopita nilikuonyesha jambo la tatu muhimu ambalo unatakiwa ulifanye katika kutafuta wokovu katika kipindi ambacho tauni inakuwa imeikumba ulimwengu.
Kumbuka hapa tunaiangalia tauni katika eneo la ulimwengu wa roho. Sina shida na mikakati yoote itakayoamuliwa na viongozi wa kitaifa, mimi najaribu kukuonyesha au kukuongezea maarifa mengine katika ulimwengu wa roho unatakiwa ufanyeje.

Fahamu kila jambo unaloliona humu duniani limeanzia katika ulimwengu wa roho. Ndiyo maana unasikia vita vyetu si vya ulimwengu wa mwili, au wa nyama bali vinapiganwa katika ulimwengu wa roho. Ili uokolewe katika vipindi hivi ni vizuri zaidi usikilize ujue au upate maarifa kutoka katika ulimwengu wa roho ndipo utavuka kirahisi sana katika ulimwengu huu wa mwili.

Katika kipindi kilichopita tulijifunza jambo la tatu nalo ni hili. LAZIMA UOMBE KWA MFUMO WA MAOMBI YA KUUTAFUTA USO WA MUNGU.

Nataka tuendelee kidogo kwenye eneo hilo hilo.

 Angalia tena mistari hii: “BWANA akamtokea Sulemani usiku, akamwambia, Nimesikia uliyoyaomba, na mahali hapa nimejichagulia kuwa nyumba ya dhabihu. Nikizifunga mbingu isiwe mvua, tena nikiamuru nzige kula nchi, au nikiwapelekea watu wangu tauni; ikiwa watu wangu, walioitwa kwa jina langu, watajinyenyekesha, na kuomba, na kunitafuta uso, na kuziacha njia zao mbaya; basi, nitasikia toka mbinguni, na kuwasamehe dhambi yao, na kuiponya nchi yao. Sasa macho yangu yatafumbuka, na masikio yangu yatasikiliza maombi ya watu waombao mahali hapa.” (2 Mambo ya Nyakati 7: 12-15)

Ukiipitia hiyo mistari utaona Mungu anasema “....Watajinyenyekesha, na kuomba na kunitafuta uso .....” Ukisikia neno tafuta maana yake hakipo, kimepotea, au hakionekani au ni kazi kubwa kukiona, n.k. 

Kwa nini Mungu katika kipindi hicho ambacho anasema akipeleka tauni inatakiwa watu walioitwa kwa jina lake  waombe na wamtafute uso wake? 

Uso wake unakuwa umekwenda wapi? Na kwanini kipindi hicho watu wake walioitwa kwa jina lake waingie gharama ya kuutafuta uso wake? Kwa nini ajifiche? Mungu hawezi kusema mnitafute kama hajajitenga na hao watu.

Sikiliza, sababu inayomfanya Mungu aufiche uso wake katika kipindi hicho inakuwa ni hasira. 

Sikiliza, Mungu huwa anakasirika sana tu, na huwa anafurahi sana tu n.k. Anapoona dhambi za wanadamu zimezidi kiwango hukasirika sana. Na akikasirika ana tabia ya kuachilia adhabu na anapoachilia adhabu huwa ana tabia kuuficha uso wake kwa sababu nyingi.

Sababu anaweza kuuficha uso wake ILI ASISIKIE KILIO CHA HAO WATU!!!! Kwa maana nzuri ndani yake huwa ana hasira kali. 


Mungu anapofurahia watu wake huzungumza nao uso kwa uso na haufichi uso wake. Angalia mistari hii: “Naye BWANA akasema na Musa uso kwa uso, kama vile mtu asemavyo na rafiki yake. Kisha akageuka akarejea hata maragoni; bali mtumishi wake Yoshua, mwana wa Nuni, naye ni kijana, hakutoka mle hemani.” (Kutoka 33:11)
Mungu alizungumza hapo na Musa uso kwa uso kabisaa kama rafiki yake. Angalia mistari hii mingine utaona kitu cha kujifunza katika eneo ambalo anasema wakiutafuta uso wake: “BWANA akanena na Musa, Haya, ondokeni, katokeni hapo, wewe na hao watu uliowaleta wakwee kutoka nchi ya Misri, waende nchi hiyo niliyomwapia Ibrahimu, na Isaka, na Yakobo, niliposema, Nitakipa kizazi chako nchi hii; nami nitamtuma malaika aende mbele yako; nami nitawafukuza Mkanaani, na Mwamori, na Mhiti, na Mperizi, na Mhivi, na Myebusi; waifikilie nchi imiminikayo maziwa na asali; kwa maana mimi sitakwenda kati yenu; kwa sababu ninyi ni watu wenye shingo ngumu; nisiwaangamize ninyi katika njia. Watu waliposikia habari hizo mbaya wakaomboleza wala hapana mtu aliyevaa vyombo vyake vya uzuri. BWANA akamwambia Musa, Waambie wana wa Israeli, Ninyi ni watu wenye shingo ngumu; kama mimi nikiingia kati yenu dakika moja, nitawaangamiza; basi sasa vueni vyombo vyenu vya uzuri ili nipate kujua nitakalowatenda. .......Basi, sasa nakuomba, ikiwa nimepata neema mbele zako, unionyeshe njia zako, nipate kukujua, ili nipate neema mbele zako; ukakumbuke ya kuwa taifa hilo ndilo watu wako. Akasema, Uso wangu utakwenda pamoja nawe, nami nitakupa raha. Naye akamwambia, Uso wako usipokwenda pamoja nami, usituchukue kutoka hapa. Kwa maana itajulikanaje kuwa nimepata neema mbele zako, mimi na watu wako? Siyo kwa sababu unakwenda pamoja nasi, hata mimi na watu wako tutengwe na watu wote walio juu ya uso wa nchi? BWANA akamwambia Musa, Nitafanya na neno hili ulilolinena, kwa maana umepata neema mbele zangu, nami nakujua jina lako.” (Kutoka 33:1-5 na 13-17)

Ukiipitia hiyo mistsri utaona Mungu alipowakasirikia wana wa Israeli aliuficha uso wake.  Alisema akiingia kati yao au akiuleta uso wake kwa sababu ya dhambi zao atawaangamiza dakika moja.

Sikiliza, Mungu anapokasirika na kuachia adhabu fahamu anakuwa ameuficha uso wake. Kipindi hicho usifikiri utakutana naye kama ulivyokuwa unakutana naye zamani.

Ngoja nikupe mfano. Mungu alipowakasirikia wana wa Israeli baada ya kuabudu sanamu, Musa alikaa mlimani akiutafuta uso wa Mungu kwa muda wa siku arobaini.

Fikiria siku ya arobaini ndipo akauonyesha uso wake na kumwambia Musa amekubali. Kwa lugha nzuri siku zooote hizo thelathini na tisa Mungu aliuficha uso wake.
Ngoja nikupe mfano mwingine. Unakumbuka Bwana wetu Yesu Kristo alipoichukua tu dhambi ya ulimwengu Mungu aliyekuwa pamoja naye siku zoote aliuficha uso wake? 
Bwana Yesu Kristo alijua ndiyo maana alilia “Baba mbona umeniacha?” Uso wake Mungu ulifichwa, dunia yoote ikawa giza, muda wa masaa matatu hivi. Alipourudisha uso wake nchi ikapata nuru tena.

Mungu anapouficha uso wake fahamu giza hutawala, hapo ndipo wanadamu hukutana na magumu kutoka ulimwengu wa giza kwa kiwango cha juu mno. 

Sikiliza nikuambie. Uso wa Mungu unapotutazama humu ulimwenguni ulinzi wa ulimwengu na kila kitu huwa mkubwa. Mimi nakuambia Mungu akificha uso wake ambao ni nuru kwa ulimwengu watu waishio humo ulimwenguni hujikuta kwenye misiba ya kila aina.

Uso wake unapokwenda nasi fahamu anatuona na anatuhurumia mnooo na kutuokoa na maradhi nk. Sasa Anapokasirika na kuachilia tauni ulimwenguni au nzige nk. Ana tabia ya kuuficha uso wake ili asiwaone wanadamu wanavyoteseka. Ili akawaokoe. SI ANA HURUMA SANA!!!

Mungu ana akili nyingi mnoo anajua akituangalia tu atatuonea huruma kwa hiyo hukimbilia kuuficha uso wake ili asiangalie. 

Umewahi kufikiri siku ile ya Sodoma na Gomora kwa nini hakwenda kule? Unaweza kuniuliza kivipi. Sikiliza maneno haya: “BWANA akasema, Kwa kuwa kilio cha Sodoma na Gomora kimezidi, na dhambi zao zimeongezeka sana, basi, nitashuka sasa nione kama wanayotenda ni kiasi cha kilio kilichonijia; na kama sivyo, nitajua. Basi wale watu wakatoka huko wakaelekea Sodoma; lakini Ibrahimu alikuwa akali akisimama mbele za BWANA. Ibrahimu akakaribia, akasema, Je! Utaharibu mwenye haki pamoja na mwovu? .....Akasema, Bwana asiwe na hasira, nami nitasema mara hii tu, Huenda wakaonekana huko kumi? Akasema, Sitaharibu kwa ajili ya hao kumi. Basi BWANA alipokwisha kuzungumza na Ibrahimu, akaenda zake; Ibrahimu naye akarudi mahali pake....” (Mwanzo 18:20-23 na 32)

Angalia hii mistari uone ninachokuambia. “Basi, wale malaika wawili wakaja Sodoma jioni; na Lutu alikuwa amekaa mlangoni pa Sodoma. Lutu akawaona akaondoka akaenda kuwalaki, akainama kifudifudi.” (Kutoka 19:1)

Ukiipitia hiyo mistari utaona Mungu alipomfuata Ibrahimu hakuwa peke yake, alikuwa na malaika wawili. Mungu alibaki na Ibrahimu akiongea naye kwa ajili ya Sodoma na Gomora, wale malaika wawili wakawaacha wanaongea. 

Mungu alipomaliza mazungumzo na Ibrahimu aliondoka. Biblia haisemi alienda Sodoma na Gomora. Walioingia Sodoma na Gomora ni malaika wawili. Jiulize Mungu alienda wapi?

Mimi naamini alirudi mbinguni na alienda kuuficha uso wake. Kwani alichokitarajia kukipata kutoka kwa Ibrahimu alikikosa, nacho kilikuwa ni utetezi. Ibrahimu hakufanya toba iliyoshiba kwa ajili ya watu wa Sodoma na Gomora kama Musa alivyofanya kwa ajili ya wana wa Israeli.

Malaika walichoma Sodoma na Gomora kilio chao hakikusikika kwa sababu Mungu aliuficha uso wake asione. 

Mungu hapendi kututesa au kutuua: “Kwa kuwa Bwana hatamtupa mtu Hata milele. Maana ajapomhuzunisha atamrehemu, Kwa kadiri ya wingi wa huruma zake. Maana moyo wake hapendi kuwatesa wanadamu. Wala kuwahuzunisha.” (Maombolezo ya Yeremia 3:31-33)

Mungu ukiona ameamua kuachia tauni fahamu hata uso wake huuficha kwa sababu hapendi kuona wanadamu wakiteseka. 

Mungu ni Baba yetu, ndiye aliyetuumba, kama mzazi yoyote yule mwenye uungwana anatabia ya kuwachapa au kuwapiga watoto wake ili wawe na adabu.

Unajua watu wengi hawajui kuwa Mungu anapiga. Angalia mistari hii: “Basi hivi karibu nitamwaga ghadhabu yangu juu yako, nitazitimiza hasira zangu juu yako, nami nitakuhukumu sawasawa na njia zako; nami nitakupatiliza machukizo yako yote. Jicho langu halitaachilia, wala sitaona huruma; nitakupatiliza njia zako na machukizo yako yote yatakuwa katikati yako; nanyi mtajua ya kuwa mimi, BWANA, napiga.” (Ezekieli  7:8-9)
Umesikia maneno hayo mpendwa? Anasema “nanyi mtajua ya kuwa mimi, BWANA, napiga.” Mungu akikasirika anapiga tena anapiga kweli. Unaweza kusema haiwezekani bwana!!

Umewahi kufikiria hivi. Kama Mungu huyu alimuua mtoto wake wa kwanza ampendaye sana yaani Bwana Yesu Kristo ili amuokoe mwanadamu? Na Kama aliweza kuua mtoto wake mpendwa asiye na dhambi kwa ajili ya wenye dhambi unafikiri itakuwa shida kuwaua hao wanadamu halafu wenye dhambi na jeuri na ukorofi?

Mimi nawaambia ukweli Mungu anaweza kabisa kuruhusu tauni na akauficha uso wake kabisaa ili dawa au adhabu iwaingie vizuri wanadamu!!!! 

Angalia mistari hii tena katika agano jipya: “tena mmeyasahau yale maonyo, yasemayo nanyi kama kusema na wana, Mwanangu, usiyadharau marudia ya Bwana, Wala usizimie moyo ukikemewa naye; Maana yeye ambaye Bwana ampenda, humrudi, Naye humpiga kila mwana amkubaliye. Ni kwa ajili ya kurudiwa mwastahimili; Mungu awatendea kama wana; maana ni mwana yupi asiyerudiwa na babaye? Basi kama mkiwa hamna kurudiwa, ambako ni fungu la wote, ndipo mmekuwa wana wa haramu ninyi, wala si wana wa halali. Na pamoja na hayo tulikuwa na baba zetu wa mwili walioturudi, nasi tukawastahi; basi si afadhali sana kujitia chini ya Baba wa roho zetu na kuishi? Maana ni hakika, hao kwa siku chache waliturudi kama walivyoona vema wenyewe; bali yeye kwa faida yetu, ili tuushiriki utakatifu wake. Kila adhabu wakati wake haionekani kuwa kitu cha furaha, bali cha huzuni; lakini baadaye huwaletea wao waliozoezwa nayo matunda ya haki yenye amani.” (Waebrania 12:5-11)

Mungu anaweza kabisa kuturudi sisi watoto wake. Fikiria wasio watoto wake itakuwaje? Kumbuka watoto wake tu huturudi ili tuwe na adabu fikiria watu wake waliomo ulimwenguni je!

Kama anaweza kupiga kuanzia madhabahuni huko nje itakuwaje? 
JIFUNZE KUUTAFUTA USO WAKE KWA TOBA NENDA KWA KUTUMIA NAFASI YA UKUHANI TU.

Sikiliza Mungu anapokuwa katika hali ya namna hii lazima wamwombao wabadili mfumo wa maombi waombe maombi ya toba tu, na ili Mungu asikie huko aliko atawasikia makuhani tu.

Kuhani ni mpatanishi, au kwa lugha nzuri ni mwombezi. Kuhani si mchungaji, au nabii, au mwalimu, au mtume. Mungu akikasirika na kuuficha uso wake ni kuhani peke yake anaweza kumsikiliza.

Kipindi hicho hasikilizagi nabii, mwalimu, mchungaji au mtume. Ngoja nikupe mfano uone: “Musa akamwambia Haruni, Haya, shika chetezo chako, ukatie moto ndani yake, moto wa madhabahuni, kisha utie na uvumba juu ya moto, ukakichukue haraka, wende nacho katika huo mkutano, ukawafanyie upatanisho; kwa kuwa ghadhabu zimetoka kwa BWANA; hiyo tauni imeanza. Basi Haruni akakishika chetezo kama Musa alivyonena, akapiga mbio akaenda katikati ya mkutano; na tazama, tauni ilikuwa imeanza kati ya watu; akatia uvumba juu ya moto na kufanya upatanisho kwa ajili ya hao watu. Akasimama kati ya hao waliokufa na hao waliokuwa wakali hai; tauni ikazuiwa. Basi waliokufa kwa tauni walikuwa kumi na nne elfu na mia saba, zaidi ya hao waliokufa katika jambo la Kora. Haruni akamrudia Musa pale mlangoni pa hema ya kukutania; hiyo tauni ikazuiwa.” (Hesabu 16:46-50)

Ukiipitia hiyo mistari utaona hiki ninachokuambia. Musa ni nabii hakugusa chetezo wala hakuingia katika huduma ya kufanya upatanisho. 

Huduma hiyo ya upatanisho aliifanya kuhani tu. Mungu anapoleta tauni na tauni ikaanza kuua watu fahamu uso wake anakuwa ameuficha. Wanaoweza kumbembeleza na uso wake ukaonekana ni makuhani peke yao.

Hapo hakuna wafalme, wakuu, manabii au walimu, au waimbaji, au wainjilisti au mitumie. Atawasikiliza makuhani peke yao.

Sikiliza makuhani leo hii ni kanisa, unaweza kuwa mchungaji au askofu au mwalimu au padri au mwinjilisti au mtume au nabii lakini usiwe kuhani. 

Katika agano jipya kuhani ni mtu yeyote aliyenunuliwa kwa damu ya Bwana Yesu Kristo:
“Tena zitokazo kwa Yesu Kristo, shahidi aliye mwaminifu, mzaliwa wa kwanza wa waliokufa, na mkuu wa wafalme wa dunia. Yeye atupendaye na kutuosha dhambi zetu katika damu yake, na kutufanya kuwa ufalme, na makuhani kwa Mungu, naye ni Baba yake; utukufu na ukuu una Yeye hata milele na milele. Amina.” (Ufunuo 1:5-6)

Angalia na mistari. “Nao waimba wimbo mpya wakisema, Wastahili wewe kukitwaa hicho kitabu na kuzifungua muhuri zake; kwa kuwa ulichinjwa, ukamnunulia Mungu kwa damu yako watu wa kila kabila na lugha na jamaa na taifa, ukawafanya kuwa ufalme na makuhani kwa Mungu wetu; nao wanamiliki juu ya nchi.” (Ufunuo 5:9-10)

Kila aliyenunuliwa kwa hiyo damu ni kuhani. Sikiliza makuhani, wewe ndiwe pekee umewekewa kazi hii ya kufanya maombezi yaliyobeba toba iletayo upatanisho ili Mungu aturehemu na tauni izuiliwe.

Kanisa tusipojitambua katika kipindi na sisi tukakaa kama watu wengine nawaambia ukweli uso wa Mungu utakuwa mbali; ataendelea kuuficha tu na tauni haitazuiliwa ulimwenguni.

Angalia mistari hii uone hiki ninachokuambia: “Pigeni tarumbeta katika Sayuni, Takaseni saumu, kusanyeni kusanyiko kuu; Kusanyeni watu, litakaseni kusanyiko, Kusanyeni wazee, kusanyeni watoto, Na hao wanyonyao maziwa; Bwana arusi na atoke chumbani mwake, Na bibi arusi katika hema yake. Hao makuhani, wahudumu wa BWANA, na walie Kati ya patakatifu na madhabahu, Na waseme, Uwaachilie watu wako, Ee BWANA, Wala usiutoe urithi wako upate aibu, Hata mataifa watawale juu yao; Kwani waseme kati ya watu, Yuko wapi Mungu wao? Hapo ndipo BWANA alipoona wivu kwa ajili ya nchi yake, akawahurumia watu wake. BWANA akajibu, akawaambia watu wake; Tazameni, nitawaletea nafaka, na divai, na mafuta, nanyi mtashiba kwa vitu hivyo; wala sitawafanya tena kuwa aibu kati ya mataifa; lakini jeshi lililotoka kaskazini nitaliondolea mbali nanyi, nami nitalifukuza mpaka nchi ya ukame na ukiwa; sehemu yake iliyo mbele itaingia katika bahari ya mashariki, na sehemu yake iliyo nyuma itaingia katika bahari ya magharibi; na uvundo wake utapanda juu, na harufu yake mbaya itapanda juu, kwa sababu ametenda mambo makubwa.” (Yoeli 2:17-20)

Ukiipitia hiyo mistari utaona Mungu aliuficha uso wake ili awaadhibu wanadamu. Alichokifanya ili aone yaani uso wake urudi kuwatazama hao watu, aliagiza makuhani walie au wakamtafute.

Hakusema manabii, n.k. Alisema makuhani. Sikilizeni kanisa: MUNGU ANAWASUBIRI NINYI MLIE. Bahati mbaya kipindi hiki akili ya kanisa ipo kwa viongozi wa nchi, ipo kwa maaskofu ipo kwa manabii, n.k.

Sikiliza wewe kuhani yaani wewe uliyenunuliwa kwa damu ya Bwana Yesu Kristo unaweza ukawa askofu, kiongozi fulani au mchungaji, mwinjilisti na inawezekana kabisa  usiwe kiongozi au nabii au mwinjilisti, n.k. ANZA KUUTAFUTA USO WA MUNGU KWA TOBA. Tafuta ingia gharama, kwa ajili ya watu wako, nchi yako, taifa lako, ulimwengu woote.

Tubia maovu hayo TULIE SI KUKEMEA TUUUU WAPENDWA; KUHANI LIA MBELE ZAKE MUNGU NDIPO USO WAKE UTAONEKANA NA TAUNI YAANI CORONA ITAZUIWA KWA MAARIFA ATAKAYOYAACHILIA.

Nataka kukutia moyo usijidharau wewe kuhani ndiwe pekee mwenye kuurejesha uso wa Mungu ili uende na watu walioko duniani.

Unaweza kumshirikisha mpendwa mwingine ujumbe huu.

Tuonane katika kipindi kijacho

Tunapoachana nataka nikupe taarifa hii kuwa ukihitaji masomo yetu unaweza kuyapata kwa njia hizi zifuatazo:-

1. App yetu ya huduma yenye jina  “MWAKATWILA” utaipata Play Store kwenye link pale juu, ambapo kuna masomo mengi sana hapo.

2. Tovuti yetu ya www.mwakatwila.org

3. YouTube - Mwakatwila au HUDUMA YA SOMA NENO LA MUNGU (HUSONEMU).

4. Facebook ingia katika hiyo tovuti au website yetu utaona alama ya Facebook (f) "like" na utapata maelezo ya kujiunga au ingia Facebook halafu andika “SOMA NENO LA MUNGU”

5. Instagram ingia Instagram app halafu andika “steven-mwakatwila

6. DVDs 📀 au CDs 💿

7. VITABU.

NB: Wasiliana na mhudumu ofisini kwa namba +255 763 109 733, ili kupata VITABU, DVD & CD.

8. Kwa njia ya REDIO:- Utapata mafundisho yetu kwa redio zifuatazo:-
➖Rungwe FM 102.5 Kila siku ya Jumapili  saa tatu mpaka saa nne usiku.
➖Baraka FM 107.7 Kila siku ya Jumanne saa kumi na mbili jioni mpaka saa moja usiku.
➖Bomba FM 104.1 Kila siku ya Ijumaa saa tatu usiku mpaka saa nne usiku.

9. Unaweza kutupata kwenye ONLINE RADIO yetu:-  radio.mwakatwila.org

Kwa Mawasiliano zaidi Utatupata kwa namba hizi:-
+255 754 849 924 Au
+255 756 715 222

Wako
Mwl Mr & Mrs Steven Mwakatwila.

🖊️ 31/03/2020.


2️⃣ MAMBO MUHIMU UNAYOTAKIWA UYAFANYE ILI UPATE WOKOVU KATIKA ENEO LA MATATIZO YALETWAYO NA TAUNI

Na: MWL STEVEN & BETH MWAKATWILA.

FUATANA NASI:- KWENYE APP,  FACEBOOK, INSTAGRAM, ONLINE RADIO 📻, WEBSITE, WHATSAPP & YOUTUBE Kwa links zilizoko hapa kwenye link hii:

KUPATA APP YETU “HUSONEMU (MWAKATWILA) APP”: (humo utapata masomo haya yote ninayokuletea darasani na mengine mengi) bonyeza link hapa.

🖊️  30 /03/ 2020.

Bwana Yesu Kristo asifiwe sana. Ni imani yangu kuwa Mungu amekupa uzima na kukulinda.  Nimeupata muda huu na nimeona niutumie kukuletea somo ambalo nilikuahidi kuwa nitakuletea. 

Kumbuka somo hilo lina kichwa. MAMBO MUHIMU UNAYOTAKIWA UYAFANYE ILI UPATE WOKOVU KATIKA ENEO LA MATATIZO YALETWAYO NA TAUNI

HIKI NI KIPINDI CHA PILI

Katika kipindi cha kwanza nilikuonyesha  mambo mawili ambayo unatakiwa uyafanye ili upate kuokolewa na tauni iliyoachiliwa kutoka kwa Mungu.

Mambo hayo ni;

A. JAMBO LA KWANZA NI: LAZIMA UWE MTU ULIYEITWA KWA JINA LAKE.

B. JAMBO LA PILI NI HILI: JIFUNZE KUWA MNYENYEKEVU.

Hebu tusogee mbele tuliangalie jambo la tatu.

JAMBO LA TATU.
C. LAZIMA UOMBE KWA MFUMO WA MAOMBI YA KUUTAFUTA USO WA MUNGU

Angalia hii mistari tena: “BWANA akamtokea Sulemani usiku, akamwambia, Nimesikia uliyoyaomba, na mahali hapa nimejichagulia kuwa nyumba ya dhabihu. Nikizifunga mbingu isiwe mvua, tena nikiamuru nzige kula nchi, au nikiwapelekea watu wangu tauni; ikiwa watu wangu, walioitwa kwa jina langu, watajinyenyekesha, na kuomba, na kunitafuta uso, na kuziacha njia zao mbaya; basi, nitasikia toka mbinguni, na kuwasamehe dhambi yao, na kuiponya nchi yao. Sasa macho yangu yatafumbuka, na masikio yangu yatasikiliza maombi ya watu waombao mahali hapa.” (Mambo ya Nyakati 7: 12-15)

Ninachotaka tukione katika hili jambo la tatu ni hiki Mungu asemacho kuwa. “Tena nikiamuru nzige kula nchi, au nikiwapelekea watu wangu tauni; ikiwa watu wangu, walioitwa kwa jina langu, watajinyenyekesha, na kuomba, na kunitafuta uso…”


Mungu anaporuhusu tauni kama Corona (COVID-19), ili iwapige watu na kuua miili yao ili awaokoe hao watu na hiyo tauni au awalinde hao watu na hiyo tauni anasema ni lazima hao watu waingie katika maombi ya kuutafuta uso wake.

Hao watu wanaoambiwa wafanye hivyo kumbuka  ni wale walioitwa kwa jina lake na walio wanyenyekevu. Ili leo hii mpendwa Mungu akulinde na kukuokoa na tauni inatakiwa ujifunze kuomba ili Mungu akuokoe wewe, nduguzo, taifa lako, n.k.

Unajua unaweza ukasema si nimeokoka mimi na nina matendo mema mimi bado tauni haitanipata kwa sababu nimeahidiwa na Mungu kulindwa. Sikia ndugu, Mungu huyo aliyetuahidi kutulinda ndiye anatupa maarifa hapo ya nini tufanye ili tauni isitupige.
Anasema watu walioitwa kwa jina lake walio wanyenyekevu lazima waombe tena maombi ya kuutafuta uso wake.


Kipindi hiki ni kipindi ambacho kwa kweli wewe uliyeokoka unatakiwa uombe kuliko kipindi chochote. Usijidanganye kuwa utapona kisa umeokoka. Msikilize Mungu anasema wakijinyenyekesha na kuomba na kuutafuta uso wangu....!!!!

Watoto wa Mungu wengi sana hawajui pona yao itategemea kiwango cha wao kuomba. 

Ngoja nikupe mfano huu. Msikilize Bwana Yesu Kristo asemavyo: “Alipofika mahali pale aliwaambia, Ombeni kwamba msiingie majaribuni. Mwenyewe akajitenga nao kama kiasi cha kutupa jiwe, akapiga magoti akaomba, akisema, Ee Baba, ikiwa ni mapenzi yako, uniondolee kikombe hiki; walakini si mapenzi yangu, bali yako yatendeke. [Malaika kutoka mbinguni akamtokea akamtia nguvu.Naye kwa vile alivyokuwa katika dhiki, akazidi sana kuomba; hari yake ikawa kama matone ya damu yakidondoka nchini.] Alipoondoka katika kuomba kwake, akawajia wanafunzi wake, akawakuta wamelala usingizi kwa huzuni. Akawaambia, Mbona mmelala usingizi? Ondokeni, mkaombe, msije mkaingia majaribuni.” (Luka 22:40-46)

Ukiipitia hiyo mistari utaona hiki ninachokuambia. Bwana Yesu Kristo aliwapa hao ndugu maarifa ya nini wafanye ili wasiingie kwenye magumu. Kumbuka magumu hayo Mungu ndiye aliyeyaruhusu.

Sikiliza, Bwana Yesu aliwaambia hao ndugu shetani anawataka ili awapepete kama ngano. Umewahi jiuliza aliwataka kwa nani? Alitafuta kibali kwa Mungu. Bwana Yesu alilijua hili, akawahi haraka kuwapa taarifa hao walioitwa kwa jina lake kuwa na wao waende kwa Mungu wakaombe Mungu awapitishe mbali na tatizo hilo.

Wao walizembea walilala. Unaweza kujiuliza kwa nini Mungu asiwaokoe tu na hilo jaribu au teso au gumu? Mungu ameweka utaratibu huo tokea zamani sana. 

Usipoomba yeye haangalii tu kuwa wewe ni nani kwake. Ngoja nikupe mfano huu labda utaelewa.

Wana wa Israeli waliambiwa na Mungu kuwa, Mungu amepania kuleta tauni Misri. Tauni iliyowalenga watu wa sifa ya wazaliwa wa kwanza, wawe wanyama n.k.

Ili tauni hiyo isiwapige wazaliwa wa kwanza wa Waisraeli ambao ni watu wa Mungu walioitwa kwa jina lake Mungu aliwaambie kila mmoja akaweke alama katika milango ya nyumba zao.

Ili tauni ikianza isiwapige hao wazaliwa wa kwanza waliomo ndani ya nyumba zao. Fikiria kwa nini asiwaokoe tu? Kwani alikuwa hawajui? 

Mungu aliwafahamu wazaliwa wa kwanza wooote wawe wa Wamisri au wa Wana wa Israeli. Lakini alitafuta kuona unyenyekevu na uhitaji wa kuokolewa wa hao wana wa Israeli.

Fahamuni wapendwa kuwa Mungu anatafuta kuona mtu akiomba kuokolewa, asipoomba usifikiri ataokoa. Ngoja nikupe mfano mwingine. Angalia mistari hii: “Hata baada ya siku zile nyingi mfalme wa Misri akafa; wana wa Israeli wakaugua kwa sababu ya ule utumwa, wakalia; kilio chao kikafika juu kwa Mungu kwa sababu ya ule utumwa. Mungu akasikia kuugua kwao, Mungu akakumbuka agano lake alilolifanya na Ibrahimu na Isaka na Yakobo. Mungu akawaona wana wa Israeli, na Mungu akawaangalia.” (Kutoka 2:23-25)


Ukiipitia hiyo mistari utaona kitu hiki ninachokufundisha. Hao ndugu, Mungu aliwaona na kuwaangalia na kulikumbuka agano hilo kipindi hao watu walipotafuta msaada kutoka kwake tena walipolia na kuugua kwa sababu ya ule utumwa.
Fahamu, walipokuwa hawalii, haugui, kwa sababu ya utumwa wao Mungu hakuwaangalia wala hakuwaona.

Kumbuka sana hao ndugu ni watu wa Mungu walioitwa kwa jina lake kabisaa. Alisubiri waombe kwa maombi ya mfumo huo ndipo akawaokoa.

JIFUNZE KUJIWEKEA ALAMA ILI TAUNI ISIKUPATE

Unapoingia kuomba kwa ajili ya tauni ili isikupate ndipo unapojiwekea alama maalumu ili tauni inapoijilia nchi yako au mji wako ikiona alama hiyo inakupita. 

Usipojiwekea hiyo alama fahamu itakupiga tu haitajalisha wewe ni askofu, daktari, mchungaji, n.k. 

Ngoja nikupe mfano huu ili uone tauni inaletwaje katika ulimwengu wa roho na watu watakaopona wanakuwa na sifa zipi hasa.

Pata picha hii ndiyo utanielewa sana ninapokuambia omba: “Kisha akalia kwa sauti kuu masikioni mwangu, akisema, Waamuru wale wanaousimamia mji wakaribie, kila mmoja na awe na kitu chake cha kuangamiza mkononi mwake. Na tazama, watu sita wakaja, wakitokea kwa njia ya lango la juu, lielekealo upande wa kaskazini, kila mmoja ana kitu chake cha kufisha mkononi mwake; na mtu mmoja kati yao amevaa bafta, naye ana kidau cha wino cha mwandishi kiunoni. Wakaingia, wakasimama karibu na madhabahu ya shaba. Na huo utukufu wa Bwana wa Israeli ulikuwa umepanda juu kutoka kwa kerubi, ambaye ulikuwa juu yake, mpaka kizingiti cha nyumba; akamwita mtu yule aliyekuwa amevaa bafta, mwenye kidau cha wino cha mwandishi kiunoni. BWANA akamwambia, Pita kati ya mji, kati ya Yerusalemu, ukatie alama katika vipaji vya nyuso vya watu wanaougua na kulia kwa sababu ya machukizo yote yanayofanyika kati yake. Na hao wengine aliwaambia, nami nalisikia, Piteni kati ya mji nyuma yake, mkapige; jicho lenu lisiachilie, wala msione huruma; Waueni kabisa, mzee, na kijana, na msichana, na watoto wachanga, na wanawake; lakini msimkaribie mtu ye yote mwenye hiyo alama; tena anzeni katika patakatifu pangu. Basi, wakaanza kwa wazee waliokuwa mbele ya nyumba. Akawaambia, itieni nyumba unajisi, mkazijaze nyua mizoga ya hao waliouawa; haya, enendeni. Wakaenenda, wakapiga-piga katika mji. Tena ikawa, walipokuwa wakipiga, nami nikiachwa, nalianguka kifudifudi, nikalia, nikasema, Ee Bwana MUNGU! Utaangamiza mabaki yote ya Israeli, wakati wa kumwaga ghadhabu yako juu ya Yerusalemu? Ndipo akaniambia, Uovu wa nyumba ya Israeli na Yuda ni mwingi sana, nayo nchi imejaa damu, nao mji umejaa kupotosha hukumu; maana husema, BWANA ameiacha nchi hii, naye BWANA haoni. Nami, jicho langu halitaachilia, wala sitaona huruma; lakini nitaleta njia yao juu ya vichwa vyao. Na tazama, mtu yule aliyevaa bafta, mwenye kidau cha wino kiunoni, akaleta habari, akisema, Nimefanya kama ulivyoniamuru.” (Ezekieli  9:1-11)

Hebu irudie hata mara tatu kuisoma hiyo mistari. Utaona kinachofanyika katika ulimwengu wa roho kinakuwaje.

Ni rahisi ninyi huku duniani kuona virusi. Lakini kwenye ulimwengu wa roho huwa ni viumbe kamili wanaoifanya hiyo kazi. 

Sikiliza jambo hilo Ezekieli aliliona likifanywa katika ulimwengu wa roho. Na likatokea kabisaa katika ulimwengu huu wa mwili.

Fahamu katika kila mji au taifa kuna malaika wamewekwa ili kuwa wasimamizi wa miji au taifa. Kazi yao ni kutoa taarifa kwa Mungu kwa ajili ya hiyo miji au hilo taifa. 

Sikiliza Mungu anapotaka kuachilia tauni ikaipige miji au mataifa hao unaowasikia hapo wapo hata hii leo ndiyo wanaohusika kuyafanya hayo. Wapo ambao kazi yao ni kutia alama watu ambao tauni inatakiwa isiwapate..

Kwa taarifa yako hakuna kinga zaidi ya hiyo alama. Kama unafikiri nakutania umewahi kufikiri Ulaya na Marekani walivyo wasafi? Huku sisi ndiyo tunafundishwa kunawa, wenzetu hunawa na hizo sabuni za kuua wadudu kila siku.

Lakini virusi hivyo haijajali wewe nani vimewavaa hata mawaziri wakuu, wafalme, n.k. Kama waziri mkuu anavyofahamu baraza looote la mawaziri hawako salama ila usishangae wengine hawapati. Ni sawa na UKIMWI nakuambia mgejua kinachotendeka kwenye ulimwengu wa roho mpaka mtu akapata UKIMWI nakuambia ukweli wengi wangeacha tu kuzini HAKUNA KINGA.

Ngoja nikuonyeshe labda utaniekewa. Angalia mistari hii: “Na kwa malaika wa kanisa lililoko Thiatira andika; Haya ndiyo anenayo Mwana wa Mungu, yeye aliye na macho yake kama mwali wa moto, na miguu yake mfano wa shaba iliyosuguliwa sana. Nayajua matendo yako na upendo na imani na huduma na subira yako; tena kwamba matendo yako ya mwisho yamezidi yale ya kwanza. Lakini nina neno juu yako, ya kwamba wamridhia yule mwanamke Yezebeli, yeye ajiitaye nabii na kuwafundisha watumishi wangu na kuwapoteza, ili wazini na kula vitu vilivyotolewa sadaka kwa sanamu. Nami nimempa muda ili atubu, wala hataki kuutubia uzinzi wake. Tazama, nitamtupa juu ya kitanda, na hao wazinio pamoja naye, wapate dhiki kubwa wasipotubia matendo yake; nami nitawaua watoto wake kwa mauti. Na makanisa yote watajua ya kuwa mimi ndiye achunguzaye viuno na mioyo. Nami nitampa kila mmoja wenu kwa kadiri ya matendo yake. Lakini nawaambia ninyi wengine mlioko Thiatira, wo wote wasio na mafundisho hayo, wasiozijua fumbo za Shetani, kama vile wasemavyo, Sitaweka juu yenu mzigo mwingine.” (Ufunuo 2:18-24)

Ukiipitia hiyo mistari utanielewa haraka ninapokupa picha hii ili uone ni nini huwa kinafanyika kwenye ulimwengu wa roho.  Haya mambo yanavyofanyika kwenye ulimwengu wa roho ni ngumu huku kwenye ulimwengu wa mwili kukinga.

Lazima utafute msaada kutoka kwenye ulimwengu wa roho ili Mungu aamue yeye kukuwekea alama. Tauni inapoachiliwa usifikiri kuna kinga, ni malaika hutumwa kufanya hivyo. Angalia Ezekieli aliona picha zima linavyokwenda. Aliyewekewa alama alipona; hakufa.

Ukiitazama ile mistari waliowekewa alama ni wale tu waliokuwa wanaomba au kulia kwa ajili ya maovu yaliyokuwa yakifanywa katika mji ule. Nitakuonyesha vizuri katika kipindi kijacho.

Fikiria kidogo, adhabu ile au tauni ile ilianzia madhabauni pa Mungu. Wale viumbe walimwacha Ezekieli kwa sababu tu alikuwa na alama, kumbuka huyo alikuwa mtu wa madhabahuni. Wenzie walikufa, kisa hawakua na alama.

Kwa lugha nzuri walikuwa hawaombi hao. Nikuulize swali umenielewa?

Usifikiri tauni hii inaweza kuishia huko huko Ulaya na Uchina. Wamarekani hawakufikiri kuwa tauni hiyo itawapiga, Waitalia vivyo hivyo. Walifikiri itawapiga Wachina tu, sikiliza ANZA LEO KUOMBA MPENDWA TAUNI HIYO ISIKUPIGE WEWE AU TAIFA, N.K.

Lazima Watanzania tuombe tena tuombe sana. Fikiria leo hii majirani zetu wameambiwa wasitoke nje siku 21 n.k. Ni nani leo nchini humu ataweza kuhifadhi chakula, maji n.k kwa siku hizo? 

Fikiria kidogo ni nani leo hii akakaa siku hizo na akarudi kwenye biashara yake salama. JIBU HAKUNA. Sasa kabla hayajatukuta, 

Tunahitaji kuomba hasa sisi watoto wa Mungu. Mungu aliyetuokoa na nzige, Mungu aliyetuokoa na vimbunga HUYU TUMLILIE TENA KILA FAMILIA ILIE KWELI TUTAVUKA SALAMA BILA MAAFA MENGI.

Tumepewa AGIZO HATA NA RAIS WA NCHI KUWA TUSIMSAHAU MUNGU. TUOMBE. HILI NENO NI ZITO KULIKO UNAVYOFIKIRI.

Ukiwa mchungaji au mtumishi unayesimamia watu, TAFUTA LUGHA NZURI YA HEKIMA ONGEA NA VIONGOZI WA SEREKALI ILI WAJUE KUWA KUNA MAOMBI KWA SABABU NENO LA RAIS NI SHERIA AMETUAGIZA TUOMBE; SIJUI HATA WALIO CHINI YAKE WAMELITAZAMAJE HILI? 

Sikilizeni viongozi wa serikali hii MUNGU ANALIPENDA SANA TAIFA HILI. Si kuwa sisi ni wema kuliko hayo mataifa mengine. Ni NEEMA. SASA HIMIZENI WATU WAOMBE SI TU KUNAWA, N.K. 

Itakuwa vema kila kiongozi eneo aliopohimiza watu wa eneo hilo pia waombe juu ya tauni hii. Pangeni hata siku maalumu na mfumo mzuri tu wa watu wakae mkao wa kuomba kama Taifa, Mkoa, Wilaya, Kitongoji, n.k. 

NAWAAMBIENI UKWELI KWA KUFANYA HIVI TUTAVUKA. Angalia mfano wa mataifa mengine, walipowafungia watu tu ndani. Maambukizi yamezidi kuliko kwanza. Tunajifunza nini hapo. WATU WENGI HAWANA ALAMA. ILI WAELEWE ALAMA LAZIMA WAFUNDISHWE KUOMBA KILA FAMILIA.

Naamini kwa sehemu umenielewa FANYIA KAZI HAYO. 

Tuonane katika kipindi kijacho

Tunapoachana nataka nikupe taarifa hii kuwa ukihitaji masomo yetu unaweza kuyapata kwa njia hizi zifuatazo:-

1. App yetu ya huduma yenye jina  “MWAKATWILA” utaipata Play Store kwenye link pale juu, ambapo kuna masomo mengi sana hapo.

2. Tovuti yetu ya www.mwakatwila.org

3. YouTube - Mwakatwila au HUDUMA YA SOMA NENO LA MUNGU (HUSONEMU).

4. Facebook ingia katika hiyo tovuti au website yetu utaona alama ya Facebook (f) "like" na utapata maelezo ya kujiunga au ingia Facebook halafu andika “SOMA NENO LA MUNGU”

5. Instagram ingia Instagram app halafu andika “steven-mwakatwila

6. DVDs 📀 au CDs 💿

7. VITABU.

NB: Wasiliana na mhudumu ofisini kwa namba +255 763 109 733, ili kupata VITABU, DVD & CD.

8. Kwa njia ya REDIO:- Utapata mafundisho yetu kwa redio zifuatazo:-
➖Rungwe FM 102.5 Kila siku ya Jumapili  saa tatu mpaka saa nne usiku.
➖Baraka FM 107.7 Kila siku ya Jumanne saa kumi na mbili jioni mpaka saa moja usiku.
➖Bomba FM 104.1 Kila siku ya Ijumaa saa tatu usiku mpaka saa nne usiku.

9. Unaweza kutupata kwenye ONLINE RADIO yetu:-  radio.mwakatwila.org

Kwa Mawasiliano zaidi Utatupata kwa namba hizi:-
+255 754 849 924 Au
+255 756 715 222

Wako
Mwl Mr & Mrs Steven Mwakatwila.

🖊️ 30/03/2020.

Sunday, March 29, 2020

1️⃣ MAMBO MUHIMU UNAYOTAKIWA UYAFANYE ILI UPATE WOKOVU KATIKA ENEO LA MATATIZO YALETWAYO NA TAUNI

Na: MWL STEVEN & BETH MWAKATWILA.

FUATANA NASI:- KWENYE APP, YOUTUBE, FACEBOOK, INSTAGRAM, ONLINE RADIO 📻, WHATSAPP & WEBSITE, Kwa links zilizoko hapa kwenye link hii:

🖊️  29 /03/ 2020.

Bwana Yesu Kristo asifiwe sana. Nichukue nafasi hii kukukaribisha ndugu yangu mpendwa ili kwa pamoja tupate kujifunza somo hili muhimu sana ambalo Roho Mtakatifu aliliweka ndani ya moyo wangu.

Na ndani yangu nimepata kibali cha kukushirikisha hata wewe kitu hiki ambacho nimejifunza. 

Naamini hata wewe kuna kitu utajifunza na ninaamini kitakusaidia sana. Na ukiona umepokea kitu chema usisite kumpatia somo hili na mtu mwingine.

Hebu tuanze kujifunza.

HIKI NI KIPINDI CHA KWANZA

Ninaamini kabisa kuwa unajua kuwa Bwana Yesu Kristo ndiye mwokozi. Na sijui kama unajua huyu Bwana Yesu Kristo ndiye mwenye uwezo wa kutuokoa katika mambo mengi sana.

Angalia mfano huu: “Kwa maana jinsi hii Mungu aliupenda ulimwengu, hata akamtoa Mwanawe pekee, ili kila mtu amwaminiye asipotee, bali awe na uzima wa milele. Maana Mungu hakumtuma Mwana ulimwenguni ili auhukumu ulimwengu, bali ulimwengu uokolewe katika yeye.” (Yohana  3:16-17).

Ukiipitia hiyo mistari kwa kutulia utaona uwezo alionao Bwana Yesu Kristo katika eneo la kuokoa ni mkubwa kuliko watu wengi tunavyowaza na kufikiri. Watu wengi wanapolitazama suala la wokovu wanalitazama kwa kiwango kidogo sana.

Bwana Yesu Kristo yeye ndiye pekee mwenye uwezo wa kuuokoa ulimwengu. Kuna utofauti mkubwa wa maneno haya mawili. Ulimwengu na neno Dunia. Neno ulimwengu kwa maana nzuri ni mkusanyiko wa vitu vyote vilivyoumbwa na Mungu ikiwemo hiyo Dunia.

Mwanadamu anaishi Duniani, na Dunia imo ndani ya ulimwengu. Mungu ameumba vitu vingi mno, vinavyoonekana na visivyoonekana, vitu hivyo vyoote vimo ulimwenguni. 
Mwenye uwezo wa kuviokoa vitu hivyo ni Bwana Yesu Kristo peke yake. Sikia kama anaweza kuviokoa maana yake yeye pakee ndiye mwenye kuvifahamu vema, na mwenye mamlaka na huo ulimwengu. 

Huwezi kuviokoa vitu ambavyo huna uwezo navyo,  na pia unaposikia neno kuokoa maana yake ulimwengu ulikuwa hatarini. Bwana Yesu Kristo yeye pekee ndiye mwenye uwezo au nguvu au mamlaka ya kumudu huyo aliyeuweka huo ulimwengu katika hatari au aliyeuteka huo ulimwengu.

Kwa nini nasema hivyo ni kwa sababu yeye ndiye mwokozi wa ulimwengu. Kama yeye ndiye mwokozi wa ulimwengu maana yake huyo aliyeutia ulimwengu hatarini hawezi kumzuia Bwana Yesu Kristo kuuondoa ulimwengu katika hatari yoyote ile ambayo ulimwengu ulitiwa ndani yake.

Watu wengi sana hufikiri Bwana Yesu Kristo hufanya kazi ya kuwaokoa wao tu. Sikiliza huyu Bwana Yesu Kristo tuliye naye yeye ana uwezo wa kukuokoa wewe mwanadamu na vitu vyoooote vinavyoonekana na visivyoonekana!!! 

BWANA YESU KRISTO ANAWEZA KUIKOA ROHO YAKO MWILI WAKO NA NAFSI YAKO
Sikiliza, kuna maeneo mengi tu huyu Bwana anaweza kabisa kuyatoa kwenye maangamizo. Nataka nikuonyeshe machache ndipo utanielewa zaidi ninapokuambia nini unafanye ili uokolewe kwenye tauni.

Bwana Yesu anaweza kuuokoa mwili. Angalia mistari hii: “Msiwaogope wauuao mwili, wasiweze kuiua na roho; afadhali mwogopeni yule awezaye kuangamiza mwili na roho pia katika jehanum.” ( Mathayo 10: 28).

Ukiipitia hiyo mistari utagundua kuwa mwili wako unaweza kabisa ukajikuta kwenye hatari ya kuuawa. Angalia anayeuua si MUNGU, Yeye anasema wauuao mwili. Mwili wako huo usiku na mchana nakuambia hao wauuao mwili wanautafutia kifo huo mwili wako.
Biblia haiwezi kusema kuwa hao wauuao mwili kama hawapo. Wapo, na wanautafuta huo mwili wako ili wauue. Mwenye uwezo wa kuuokoa nakuambia ni mmoja tu NI BWANA YESU KRISTO. 

Eneo la pili ni hatari ya kuuawa roho yako. Neno la Mungu linasema wapo watu wanaotafuta kuziua roho za watu. Ngoja nikupe mfano huu uone: “Na wewe, mwanadamu, kaza uso wako juu ya binti za watu wako, watabirio kwa akili zao wenyewe; ukatabiri juu yao, useme, Bwana MUNGU asema hivi; Ole wao wanawake wale, washonao hirizi katika viungo vyote vya mikono, wawekao leso juu ya vichwa vya kila kimo, ili wawinde roho za watu; je! Mtaziwinda roho za watu wangu, na kuzihifadhi hai roho zenu wenyewe? Nanyi mmeninajisi kati ya watu wangu, kwa ajili ya makonzi ya shayiri na vipande vya mkate, ili kuziua roho za watu ambao haiwapasi kufa, na kuzihifadhi hai roho za watu ambao haikuwapasa kuwa hai, kwa kuwaambia uongo watu wangu wasikilizao uongo. Basi Bwana MUNGU asema hivi; Tazama, mimi ni kinyume cha hirizi zenu, ambazo kwa hizo mnaziwinda roho za watu kama ndege, nami nitazitoa katika mikono yenu kwa nguvu; nami nitaziachilia roho zile mnazoziwinda kama ndege. Na leso zenu nazo nitazirarua, na kuwaokoa watu wangu katika mikono yenu, wala hawatakuwa katika mikono yenu tena kuwindwa; nanyi mtajua ya kuwa mimi ndimi BWANA.” (Ezekieli 13:18:-21)

Unapoisoma hiyo mistari naamini utaona roho za watu namna zilivyo kwenye hatari ya kuuawa. Biblia ipo wazi inasema kuna watu wanawinda roho za watu ili waziue kabisa. Maana yake hizi roho zipo hatarini mno. 

Natamani leo hii uanze kumtazama Bwana Yesu Kama mwokozi wako kwa kiwango kingine kabisaa. Watu wengi humtazama kama mwokozi wao katika eneo la kuwatoa kwenye jehanum tu na kutupa uzima wa milele. 

Sikiliza huyu Bwana ndiye mwokozi wa mwili wako ili USIUAWE. Sikiliza sizungumzii hapo wokovu wa mwili katika eneo la kupata uzima wa milele. Kwenye eneo hilo mwili hauokoki wenyewe umechagua mauti.

Nazungumzia kwenye eneo la mwili kutafutiwa kifo na watu. Huyu Bwana Yesu ndiye mwokozi wa nafsi zetu pia.

Sikiliza, shetani anaweza kuifungia nafsi kifungo. Angalia kwenye nafsi au moyo kuna akili, hisia na utashi; huko kuna mawazo, fikra, n.k. Biblia inasema  Tunatakiwa tuziteke nyara fikra za watu: “Maana ingawa tunaenenda katika mwili, hatufanyi vita kwa jinsi ya mwili; (maana silaha za vita vyetu si za mwili, bali zina uwezo katika Mungu hata kuangusha ngome;) tukiangusha mawazo na kila kitu kilichoinuka, kijiinuacho juu ya elimu ya Mungu; na tukiteka nyara kila fikira ipate kumtii Kristo;” (2 Wakorintho 10:3-5)

Biblia inasema wazi kuwa fikra zinahitajika kutekwa. Angalia zinatekwaje kama hazikutekwa? Fikra zinakaa moyoni au nafsini ni sehemu ya akili. Kwa mujibu wa hiyo mistari unaona wazi moyo au nafsi inaweza kutekwa.

Kama unafikiri nakutania wewe angalia mfumo wa wapendwa wengi kwenye eneo la akili, iwe kuwaza kwao, kufikiri kwao, kutafakari mambo, kuwekewa kujua, kukumbuka kupanga au kubuni, nk. Utagundua tu kuna shinda na wengi wanahitaji msaada.

 Mwenye uwezo wa kuwaokoa kwenye eneo hili ni mmoja tu ni Bwana Yesu Kristo.
Naona sasa umenielewa ninavyokuambia Bwana Yesu Kristo ndiye mwokozi wa ulimwengu.

BWANA YESU KRISTO NDIYE MWOKOZI KATIKA MAJANGA YA TAUNI

Sikiliza, mwanadamu anayeishi duniani na dunia iliyo ndani ya ulimwengu anaweza kujikuta akikutana na hatari za namna tofauti tofauti. Na hatari hizo zina nia ya kutafuta uhai wa mwanadamu.

Na moja ya hatari anayoweza kukutana nayo ni hii ya kukutana na tauni. Tauni ni magonjwa ya mlipuko ya kuambukiza  ambayo kwa kweli hayana tiba.

Magonjwa ya mtindo huo ndani yake yamebeba mauti ya mwili. Yaani kuua mwili.
Biblia inasema wazi juu ya tauni, leo hii ulimwengu unashuhudia tauni iitwayo Corona. Sikiliza ugonjwa huu ni tauni. Ni ugonjwa wa mlipuko unaoambukiza na kuua mwili. Na ni ugonjwa hatari sana. 

Sikiliza kwa kizazi cha sasa jinsi kilivyojaliwa akili na maarifa lakini mpaka sasa ugonjwa huu umekua tishio mnoo. Fikiria kidogo, unawaua watu wa kila aina, wawe matajiri au maskini, viongozi na wanaoongozwa, watumishi wa Mungu na wasio watumishi, Wazungu kwa Wachina, Waarabu kwa Waafrika n.k.

Sikiliza, ili leo hii ndugu yangu upate kupona ni lazima ujue ni mambo gani unatakiwa uyajue kutoka kwa mwokozi wa ulimwengu anayosema kuhusu tauni inapotokea ulimwenguni.

Kuna mambo mengi unatakiwa uyafanye ili uupate wokovu huu katika kipindi kama hiki.
Angalia mistari hii uone mambo muhimu ya kufanya: “BWANA akamtokea Sulemani usiku, akamwambia, Nimesikia uliyoyaomba, na mahali hapa nimejichagulia kuwa nyumba ya dhabihu. Nikizifunga mbingu isiwe mvua, tena nikiamuru nzige kula nchi, au nikiwapelekea watu wangu tauni; ikiwa watu wangu, walioitwa kwa jina langu, watajinyenyekesha, na kuomba, na kunitafuta uso, na kuziacha njia zao mbaya; basi, nitasikia toka mbinguni, na kuwasamehe dhambi yao, na kuiponya nchi yao. Sasa macho yangu yatafumbuka, na masikio yangu yatasikiliza maombi ya watu waombao mahali hapa.” ( 2 Mambo ya Nyakati 7: 12-15).

Unapoisoma hiyo mistari utagundua vitu vingi mnoo. Angalia kuna vitu vipo hapo ambavyo vimewekwa ili kuua mwili, kitu cha kwanza ni njaa, Neno la Mungu linasema Mungu anaweza kuzifunga mbingu isiwepo mvua dunia.

Kama dunia itakosa chakula kinachotokea ni njaa, na njaa hiyo hubeba mauti kwa mwili wa mwanadamu.

Anasema anaweza kuleta nzige, nzige wakiingia mahali watasababisha njaa, na hiyo njaa ndani yake inakuwa imekusudiwa iuue mwili. Jambo lingine hapo utaona ni tauni.
Tauni nayo ndani yake inakuwa imebeba mauti ili kuua mwili au kuwaua walioko ulimwenguni.

Sikiliza, kwa mujibu wa hiyo mistari utaona tauni hiyo hutoka kwa Mungu, Nzige hao hutoka kwa Mungu, Njaa hiyo iletwayo na ukame pia hutoka kwa Mungu.
Unaweza kusema kivipi? Anasema, “Nikizifunga mbingu isiwe mvua, tena nikiamuru nzige kula nchi, au nikiwapelekea watu wangu tauni;”

Mungu anasema anaweza kuwapelekea watu wake mambo hayo. Watu wengi sana sana wanamtazama Mungu kama ni Baba mmoja hivi asiyechukia. Mungu anapoona watu wake wamemwacha na kuanza kufanya dhambi na kuabudu miungu mingine fahamu anaweza kuviachia hivyo vitu kabisa, iwe kwenye taifa, au miji au duniani.

Sasa sikia anapoviachia hivyo vitu ili watu wapate wokovu tena kutoka kwake Mungu kuna mambo hapo amesema watu hao wanatakiwa wavifanye.

JAMBO LA KWANZA:
A. LAZIMA UWE MTU ULIYEITWA KWA JINA LAKE

“BWANA akamtokea Sulemani usiku, akamwambia, Nimesikia uliyoyaomba, na mahali hapa nimejichagulia kuwa nyumba ya dhabihu. Nikizifunga mbingu isiwe mvua, tena nikiamuru nzige kula nchi, au nikiwapelekea watu wangu tauni; ikiwa watu wangu, walioitwa kwa jina langu, watajinyenyekesha, na kuomba, na kunitafuta uso, na kuziacha njia zao mbaya; basi, nitasikia toka mbinguni, na kuwasamehe dhambi yao, na kuiponya nchi yao. Sasa macho yangu yatafumbuka, na masikio yangu yatasikiliza maombi ya watu waombao mahali hapa.” (2 Mambo ya Nyakati 7: 12-15)

Angalia vizuri hiyo mistari. Kama unataka leo wokovu kutoka kwenye majanga ya tauni ni lazima uhakikishe wewe ni mtu wa Mungu tena uliyeitwa kwa jina lake. 

 Unaweza kujiuliza nifanyeje? Ni kazima uhakikishe unamwamini Bwana Yesu Kristo kuwa ndiye Bwana wako na mwokozi wako: “Kwa sababu, ukimkiri Yesu kwa kinywa chako ya kuwa ni Bwana, na kuamini moyoni mwako ya kuwa Mungu alimfufua katika wafu, utaokoka. Kwa maana kwa moyo mtu huamini hata kupata haki, na kwa kinywa hukiri hata kupata wokovu. Kwa maana andiko lanena, Kila amwaminiye hatatahayarika. Kwa maana hakuna tofauti ya Myahudi na Myunani; maana yeye yule ni Bwana wa wote, mwenye utajiri kwa wote wamwitao;kwa kuwa, Kila atakayeliitia Jina la Bwana ataokoka(Warumi 10:9-13)

Ukiipitia hiyo mistari utaona wazi kabisa ili uokoke: iwe rohoni, mwilini, nafsini, n.k unatakiwa umwamini Bwana Yesu Kristo aliyekuja kwa jina la Mungu.

 Msikilize Bwana Yesu asemavyo: “Wala mimi simo tena ulimwenguni, lakini hawa wamo ulimwenguni, nami naja kwako. Baba mtakatifu, kwa jina lako ulilonipa uwalinde hawa, ili wawe na umoja kama sisi tulivyo. Nilipokuwapo pamoja nao, mimi naliwalinda kwa jina lako ulilonipa, nikawatunza; wala hapana mmojawapo wao aliyepotea, ila yule mwana wa upotevu, ili andiko litimie” (Yohana 17:11-12)

Jina hilo alilonalo Bwana Yesu anatuambia wazi kuwa si jina lake, ni jina la Mungu. Sasa ili wewe uitwe kwa jina lake Mungu ni lazima umwamini Bwana Yesu Kristo ili uwe mtu uliyeitwa kwa jina la Mungu ambalo ni YESU.

Hapo ndipo utaanza kupata ulinzi mpendwa. Msikilize Vizuri Bwana Yesu anasema hivi: “Mimi nimewapa neno lako; na ulimwengu umewachukia; kwa kuwa wao si wa ulimwengu, kama mimi nisivyo wa ulimwengu. Mimi siombi kwamba uwatoe katika ulimwengu; bali uwalinde na yule mwovu. Wao si wa ulimwengu, kama mimi nisivyo wa ulimwengu.” (Yohana 17:14-16)

Umeyasikia maneno hayo? Huyo mwokozi wa ulimwengu anasema wazi kabisa kuwa anao uwezo wa kuwalinda waliomo ulimwenguni ambamo yumo hata mwovu yaani shetani.

Ili uupate ulinzi humu ulimwenguni lazima umwamini Bwana Yesu Kristo ndipo UNAPOPATA TIKETI YA KULINDWA HUMU ULIMWENGUNI. Nje ya hapo ni ngumu kupokea ulinzi kutoka kwa Bwana Yesu Kristo.

Sikiliza Mungu anasema “ikiwa watu wangu walioitwa kwa jina langu…” IKIWA UNATAKA KUOKOLEWA NA TAUNI  lazima uhakikishe wewe umeitwa au umo ndani ya jina lake Mungu liitwalo YESU.

Kama haumo humo ndani tafuta haraka kuingia humo ndani kwa imani. Tafuta kila uwezalo kumruhusu Bwana Yesu Kristo awe ndani yako.

JAMBO LA PILI:
B. JIFUNZE KUWA MNYENYEKEVU

Sikiliza unaweza ukawa ndani ya Bwana Yesu Kristo lakini ukakosa sifa hii ya kuwa mnyenyekevu. Ndani ya unyenyekevu kuna utii. Nikuulize swali wewe ni mtii katika maagizo aliyokupa Bwana Yesu Kristo?

Watu wengi wameokoka na wanajifariji mnoo kuwa aiseee! Mungu atatulinda hawajui kuwa Mungu ameweka utaratibu huu wa watu wake walioitwa kwa jina lake wanatakiwa wawe wanyenyekevu kwa Mungu.

Angalia wewe ni mnyenyekevu? Kweli unampenda Mungu? Angalia mistari hii: “Maana Yeye atakuokoa na mtego wa mwindaji, Na katika tauni iharibuyo. Kwa manyoya yake atakufunika, Chini ya mbawa zake utapata kimbilio; Uaminifu wake ni ngao na kigao. Hutaogopa hofu ya usiku, Wala mshale urukao mchana, Wala tauni ipitayo gizani, Wala uele uharibuo adhuhuri, Ijapo watu elfu waanguka ubavuni pako. Naam, kumi elfu mkono wako wa kuume! Hata hivyo hautakukaribia wewe. Ila kwa macho yako utatazama, Na kuyaona malipo ya wasio haki. Kwa kuwa Wewe BWANA ndiwe kimbilio langu; Umemfanya Aliye juu kuwa makao yako. Mabaya hayatakupata wewe, Wala tauni haitaikaribia hema yako. Kwa kuwa atakuagizia malaika zake Wakulinde katika njia zako zote. Mikononi mwao watakuchukua, Usije ukajikwaa mguu wako katika jiwe. Utawakanyaga simba na nyoka, Mwana-simba na joka utawaseta kwa miguu. Kwa kuwa amekaza kunipenda Nitamwokoa; na kumweka palipo juu, Kwa kuwa amenijua Jina langu. Ataniita nami nitamwitikia; Nitakuwa pamoja naye taabuni, Nitamwokoa na kumtukuza;” (Zaburi 91:3-15)

Angalia hapo anasema yupo tayari kutuokoa na tauni, lakini kuna neno hili anasema “KWA KUWA AMEKAZA KUNIPENDA NITAMWOKOA!!”

Hasemi nitamwokoa kwa sababu ananiamini tu, anasema kwa kuwa amekaza kunipenda. Angalia leo hii ukoje? Mungu akiangalia moyoni mwako anauona upendo ule wa kwanza?
Mbona umeacha kumtumikia, leo hii hata kusoma Biblia tu husomi, angalia mwenendo wako ulivyo wewe mwenyewe unaona wazi haujawa mnyenyekevu kwa Mungu. Haumtii, kuna dhambi amekutaza usifanye lakini unafanya kabisaa hata huna hofu ya Mungu. 
Sikiliza yaani ili Mungu akuokoe ni lazima uhakikishe leo hii unaanza kumnyenyekea Mungu mtii. Mpende, fanyia kazi yale anayokuagiza uyafanye.

Acha njia zako mbaya mpendwa.

Sikiliza unaweza kuwa mtu aliyeitwa kwa jina la Mungu lakini ukawa ni mtu mwenye njia mbaya kabisa. Anasema acha njia mbaya.

FANYIA KAZI HAYO. 

Tuonane katika kipindi kijacho

Tunapoachana nataka nikupe taarifa hii kuwa ukihitaji masomo yetu unaweza kuyapata kwa njia hizi zifuatazo:-

1. App yetu ya huduma yenye jina  “MWAKATWILA” utaipata Play Store kwenye link pale juu, ambapo kuna masomo mengi sana hapo.

2. Tovuti yetu ya www.mwakatwila.org

3. YouTube - Mwakatwila au HUDUMA YA SOMA NENO LA MUNGU (HUSONEMU).

4. Facebook ingia katika hiyo tovuti au website yetu utaona alama ya Facebook (f) "like" na utapata maelezo ya kujiunga au ingia Facebook halafu andika “SOMA NENO LA MUNGU”

5. Instagram ingia Instagram app halafu andika “steven-mwakatwila

6. DVDs 📀 au CDs 💿

7. VITABU.

NB: Wasiliana na mhudumu ofisini kwa namba +255 763 109 733, ili kupata VITABU, DVD & CD.

8. Kwa njia ya REDIO:- Utapata mafundisho yetu kwa redio zifuatazo:-

➖Rungwe FM 102.5 Kila siku ya Jumapili  saa tatu mpaka saa nne usiku.
➖Baraka FM 107.7 Kila siku ya Jumanne saa kumi na mbili jioni mpaka saa moja usiku.
➖Bomba FM 104.1 Kila siku ya Ijumaa saa tatu usiku mpaka saa nne usiku.

9. Unaweza kutupata kwenye ONLINE RADIO yetu:-  radio.mwakatwila.org

Kwa Mawasiliano zaidi Utatupata kwa namba hizi:-
+255 754 849 924 Au
+255 756 715 222

Wako
Mwl Mr & Mrs Steven Mwakatwila.

🖊️ 29/03/2020.