1️⃣ MAMBO MUHIMU UNAYOTAKIWA UYAFANYE ILI UPATE WOKOVU KATIKA ENEO LA MATATIZO YALETWAYO NA TAUNI
Na: MWL STEVEN & BETH MWAKATWILA.
FUATANA NASI:- KWENYE APP, YOUTUBE, FACEBOOK, INSTAGRAM, ONLINE RADIO 📻, WHATSAPP & WEBSITE, Kwa links zilizoko hapa kwenye link hii:
🖊️ 29 /03/ 2020.
Bwana Yesu Kristo asifiwe sana. Nichukue nafasi hii kukukaribisha ndugu yangu mpendwa ili kwa pamoja tupate kujifunza somo hili muhimu sana ambalo Roho Mtakatifu aliliweka ndani ya moyo wangu.
Na ndani yangu nimepata kibali cha kukushirikisha hata wewe kitu hiki ambacho nimejifunza.
Naamini hata wewe kuna kitu utajifunza na ninaamini kitakusaidia sana. Na ukiona umepokea kitu chema usisite kumpatia somo hili na mtu mwingine.
Hebu tuanze kujifunza.
HIKI NI KIPINDI CHA KWANZA
Ninaamini kabisa kuwa unajua kuwa Bwana Yesu Kristo ndiye mwokozi. Na sijui kama unajua huyu Bwana Yesu Kristo ndiye mwenye uwezo wa kutuokoa katika mambo mengi sana.
Angalia mfano huu: “Kwa maana jinsi hii Mungu aliupenda ulimwengu, hata akamtoa Mwanawe pekee, ili kila mtu amwaminiye asipotee, bali awe na uzima wa milele. Maana Mungu hakumtuma Mwana ulimwenguni ili auhukumu ulimwengu, bali ulimwengu uokolewe katika yeye.” (Yohana 3:16-17).
Ukiipitia hiyo mistari kwa kutulia utaona uwezo alionao Bwana Yesu Kristo katika eneo la kuokoa ni mkubwa kuliko watu wengi tunavyowaza na kufikiri. Watu wengi wanapolitazama suala la wokovu wanalitazama kwa kiwango kidogo sana.
Bwana Yesu Kristo yeye ndiye pekee mwenye uwezo wa kuuokoa ulimwengu. Kuna utofauti mkubwa wa maneno haya mawili. Ulimwengu na neno Dunia. Neno ulimwengu kwa maana nzuri ni mkusanyiko wa vitu vyote vilivyoumbwa na Mungu ikiwemo hiyo Dunia.
Mwanadamu anaishi Duniani, na Dunia imo ndani ya ulimwengu. Mungu ameumba vitu vingi mno, vinavyoonekana na visivyoonekana, vitu hivyo vyoote vimo ulimwenguni.
Mwenye uwezo wa kuviokoa vitu hivyo ni Bwana Yesu Kristo peke yake. Sikia kama anaweza kuviokoa maana yake yeye pakee ndiye mwenye kuvifahamu vema, na mwenye mamlaka na huo ulimwengu.
Huwezi kuviokoa vitu ambavyo huna uwezo navyo, na pia unaposikia neno kuokoa maana yake ulimwengu ulikuwa hatarini. Bwana Yesu Kristo yeye pekee ndiye mwenye uwezo au nguvu au mamlaka ya kumudu huyo aliyeuweka huo ulimwengu katika hatari au aliyeuteka huo ulimwengu.
Kwa nini nasema hivyo ni kwa sababu yeye ndiye mwokozi wa ulimwengu. Kama yeye ndiye mwokozi wa ulimwengu maana yake huyo aliyeutia ulimwengu hatarini hawezi kumzuia Bwana Yesu Kristo kuuondoa ulimwengu katika hatari yoyote ile ambayo ulimwengu ulitiwa ndani yake.
Watu wengi sana hufikiri Bwana Yesu Kristo hufanya kazi ya kuwaokoa wao tu. Sikiliza huyu Bwana Yesu Kristo tuliye naye yeye ana uwezo wa kukuokoa wewe mwanadamu na vitu vyoooote vinavyoonekana na visivyoonekana!!!
BWANA YESU KRISTO ANAWEZA KUIKOA ROHO YAKO MWILI WAKO NA NAFSI YAKO
Sikiliza, kuna maeneo mengi tu huyu Bwana anaweza kabisa kuyatoa kwenye maangamizo. Nataka nikuonyeshe machache ndipo utanielewa zaidi ninapokuambia nini unafanye ili uokolewe kwenye tauni.
Bwana Yesu anaweza kuuokoa mwili. Angalia mistari hii: “Msiwaogope wauuao mwili, wasiweze kuiua na roho; afadhali mwogopeni yule awezaye kuangamiza mwili na roho pia katika jehanum.” ( Mathayo 10: 28).
Ukiipitia hiyo mistari utagundua kuwa mwili wako unaweza kabisa ukajikuta kwenye hatari ya kuuawa. Angalia anayeuua si MUNGU, Yeye anasema wauuao mwili. Mwili wako huo usiku na mchana nakuambia hao wauuao mwili wanautafutia kifo huo mwili wako.
Biblia haiwezi kusema kuwa hao wauuao mwili kama hawapo. Wapo, na wanautafuta huo mwili wako ili wauue. Mwenye uwezo wa kuuokoa nakuambia ni mmoja tu NI BWANA YESU KRISTO.
Eneo la pili ni hatari ya kuuawa roho yako. Neno la Mungu linasema wapo watu wanaotafuta kuziua roho za watu. Ngoja nikupe mfano huu uone: “Na wewe, mwanadamu, kaza uso wako juu ya binti za watu wako, watabirio kwa akili zao wenyewe; ukatabiri juu yao, useme, Bwana MUNGU asema hivi; Ole wao wanawake wale, washonao hirizi katika viungo vyote vya mikono, wawekao leso juu ya vichwa vya kila kimo, ili wawinde roho za watu; je! Mtaziwinda roho za watu wangu, na kuzihifadhi hai roho zenu wenyewe? Nanyi mmeninajisi kati ya watu wangu, kwa ajili ya makonzi ya shayiri na vipande vya mkate, ili kuziua roho za watu ambao haiwapasi kufa, na kuzihifadhi hai roho za watu ambao haikuwapasa kuwa hai, kwa kuwaambia uongo watu wangu wasikilizao uongo. Basi Bwana MUNGU asema hivi; Tazama, mimi ni kinyume cha hirizi zenu, ambazo kwa hizo mnaziwinda roho za watu kama ndege, nami nitazitoa katika mikono yenu kwa nguvu; nami nitaziachilia roho zile mnazoziwinda kama ndege. Na leso zenu nazo nitazirarua, na kuwaokoa watu wangu katika mikono yenu, wala hawatakuwa katika mikono yenu tena kuwindwa; nanyi mtajua ya kuwa mimi ndimi BWANA.” (Ezekieli 13:18:-21)
Unapoisoma hiyo mistari naamini utaona roho za watu namna zilivyo kwenye hatari ya kuuawa. Biblia ipo wazi inasema kuna watu wanawinda roho za watu ili waziue kabisa. Maana yake hizi roho zipo hatarini mno.
Natamani leo hii uanze kumtazama Bwana Yesu Kama mwokozi wako kwa kiwango kingine kabisaa. Watu wengi humtazama kama mwokozi wao katika eneo la kuwatoa kwenye jehanum tu na kutupa uzima wa milele.
Sikiliza huyu Bwana ndiye mwokozi wa mwili wako ili USIUAWE. Sikiliza sizungumzii hapo wokovu wa mwili katika eneo la kupata uzima wa milele. Kwenye eneo hilo mwili hauokoki wenyewe umechagua mauti.
Nazungumzia kwenye eneo la mwili kutafutiwa kifo na watu. Huyu Bwana Yesu ndiye mwokozi wa nafsi zetu pia.
Sikiliza, shetani anaweza kuifungia nafsi kifungo. Angalia kwenye nafsi au moyo kuna akili, hisia na utashi; huko kuna mawazo, fikra, n.k. Biblia inasema Tunatakiwa tuziteke nyara fikra za watu: “Maana ingawa tunaenenda katika mwili, hatufanyi vita kwa jinsi ya mwili; (maana silaha za vita vyetu si za mwili, bali zina uwezo katika Mungu hata kuangusha ngome;) tukiangusha mawazo na kila kitu kilichoinuka, kijiinuacho juu ya elimu ya Mungu; na tukiteka nyara kila fikira ipate kumtii Kristo;” (2 Wakorintho 10:3-5)
Biblia inasema wazi kuwa fikra zinahitajika kutekwa. Angalia zinatekwaje kama hazikutekwa? Fikra zinakaa moyoni au nafsini ni sehemu ya akili. Kwa mujibu wa hiyo mistari unaona wazi moyo au nafsi inaweza kutekwa.
Kama unafikiri nakutania wewe angalia mfumo wa wapendwa wengi kwenye eneo la akili, iwe kuwaza kwao, kufikiri kwao, kutafakari mambo, kuwekewa kujua, kukumbuka kupanga au kubuni, nk. Utagundua tu kuna shinda na wengi wanahitaji msaada.
Mwenye uwezo wa kuwaokoa kwenye eneo hili ni mmoja tu ni Bwana Yesu Kristo.
Naona sasa umenielewa ninavyokuambia Bwana Yesu Kristo ndiye mwokozi wa ulimwengu.
BWANA YESU KRISTO NDIYE MWOKOZI KATIKA MAJANGA YA TAUNI
Sikiliza, mwanadamu anayeishi duniani na dunia iliyo ndani ya ulimwengu anaweza kujikuta akikutana na hatari za namna tofauti tofauti. Na hatari hizo zina nia ya kutafuta uhai wa mwanadamu.
Na moja ya hatari anayoweza kukutana nayo ni hii ya kukutana na tauni. Tauni ni magonjwa ya mlipuko ya kuambukiza ambayo kwa kweli hayana tiba.
Magonjwa ya mtindo huo ndani yake yamebeba mauti ya mwili. Yaani kuua mwili.
Biblia inasema wazi juu ya tauni, leo hii ulimwengu unashuhudia tauni iitwayo Corona. Sikiliza ugonjwa huu ni tauni. Ni ugonjwa wa mlipuko unaoambukiza na kuua mwili. Na ni ugonjwa hatari sana.
Sikiliza kwa kizazi cha sasa jinsi kilivyojaliwa akili na maarifa lakini mpaka sasa ugonjwa huu umekua tishio mnoo. Fikiria kidogo, unawaua watu wa kila aina, wawe matajiri au maskini, viongozi na wanaoongozwa, watumishi wa Mungu na wasio watumishi, Wazungu kwa Wachina, Waarabu kwa Waafrika n.k.
Sikiliza, ili leo hii ndugu yangu upate kupona ni lazima ujue ni mambo gani unatakiwa uyajue kutoka kwa mwokozi wa ulimwengu anayosema kuhusu tauni inapotokea ulimwenguni.
Kuna mambo mengi unatakiwa uyafanye ili uupate wokovu huu katika kipindi kama hiki.
Angalia mistari hii uone mambo muhimu ya kufanya: “BWANA akamtokea Sulemani usiku, akamwambia, Nimesikia uliyoyaomba, na mahali hapa nimejichagulia kuwa nyumba ya dhabihu. Nikizifunga mbingu isiwe mvua, tena nikiamuru nzige kula nchi, au nikiwapelekea watu wangu tauni; ikiwa watu wangu, walioitwa kwa jina langu, watajinyenyekesha, na kuomba, na kunitafuta uso, na kuziacha njia zao mbaya; basi, nitasikia toka mbinguni, na kuwasamehe dhambi yao, na kuiponya nchi yao. Sasa macho yangu yatafumbuka, na masikio yangu yatasikiliza maombi ya watu waombao mahali hapa.” ( 2 Mambo ya Nyakati 7: 12-15).
Unapoisoma hiyo mistari utagundua vitu vingi mnoo. Angalia kuna vitu vipo hapo ambavyo vimewekwa ili kuua mwili, kitu cha kwanza ni njaa, Neno la Mungu linasema Mungu anaweza kuzifunga mbingu isiwepo mvua dunia.
Kama dunia itakosa chakula kinachotokea ni njaa, na njaa hiyo hubeba mauti kwa mwili wa mwanadamu.
Anasema anaweza kuleta nzige, nzige wakiingia mahali watasababisha njaa, na hiyo njaa ndani yake inakuwa imekusudiwa iuue mwili. Jambo lingine hapo utaona ni tauni.
Tauni nayo ndani yake inakuwa imebeba mauti ili kuua mwili au kuwaua walioko ulimwenguni.
Sikiliza, kwa mujibu wa hiyo mistari utaona tauni hiyo hutoka kwa Mungu, Nzige hao hutoka kwa Mungu, Njaa hiyo iletwayo na ukame pia hutoka kwa Mungu.
Unaweza kusema kivipi? Anasema, “Nikizifunga mbingu isiwe mvua, tena nikiamuru nzige kula nchi, au nikiwapelekea watu wangu tauni;”
Mungu anasema anaweza kuwapelekea watu wake mambo hayo. Watu wengi sana sana wanamtazama Mungu kama ni Baba mmoja hivi asiyechukia. Mungu anapoona watu wake wamemwacha na kuanza kufanya dhambi na kuabudu miungu mingine fahamu anaweza kuviachia hivyo vitu kabisa, iwe kwenye taifa, au miji au duniani.
Sasa sikia anapoviachia hivyo vitu ili watu wapate wokovu tena kutoka kwake Mungu kuna mambo hapo amesema watu hao wanatakiwa wavifanye.
JAMBO LA KWANZA:
A. LAZIMA UWE MTU ULIYEITWA KWA JINA LAKE
“BWANA akamtokea Sulemani usiku, akamwambia, Nimesikia uliyoyaomba, na mahali hapa nimejichagulia kuwa nyumba ya dhabihu. Nikizifunga mbingu isiwe mvua, tena nikiamuru nzige kula nchi, au nikiwapelekea watu wangu tauni; ikiwa watu wangu, walioitwa kwa jina langu, watajinyenyekesha, na kuomba, na kunitafuta uso, na kuziacha njia zao mbaya; basi, nitasikia toka mbinguni, na kuwasamehe dhambi yao, na kuiponya nchi yao. Sasa macho yangu yatafumbuka, na masikio yangu yatasikiliza maombi ya watu waombao mahali hapa.” (2 Mambo ya Nyakati 7: 12-15)
Angalia vizuri hiyo mistari. Kama unataka leo wokovu kutoka kwenye majanga ya tauni ni lazima uhakikishe wewe ni mtu wa Mungu tena uliyeitwa kwa jina lake.
Unaweza kujiuliza nifanyeje? Ni kazima uhakikishe unamwamini Bwana Yesu Kristo kuwa ndiye Bwana wako na mwokozi wako: “Kwa sababu, ukimkiri Yesu kwa kinywa chako ya kuwa ni Bwana, na kuamini moyoni mwako ya kuwa Mungu alimfufua katika wafu, utaokoka. Kwa maana kwa moyo mtu huamini hata kupata haki, na kwa kinywa hukiri hata kupata wokovu. Kwa maana andiko lanena, Kila amwaminiye hatatahayarika. Kwa maana hakuna tofauti ya Myahudi na Myunani; maana yeye yule ni Bwana wa wote, mwenye utajiri kwa wote wamwitao;kwa kuwa, Kila atakayeliitia Jina la Bwana ataokoka” (Warumi 10:9-13)
Ukiipitia hiyo mistari utaona wazi kabisa ili uokoke: iwe rohoni, mwilini, nafsini, n.k unatakiwa umwamini Bwana Yesu Kristo aliyekuja kwa jina la Mungu.
Msikilize Bwana Yesu asemavyo: “Wala mimi simo tena ulimwenguni, lakini hawa wamo ulimwenguni, nami naja kwako. Baba mtakatifu, kwa jina lako ulilonipa uwalinde hawa, ili wawe na umoja kama sisi tulivyo. Nilipokuwapo pamoja nao, mimi naliwalinda kwa jina lako ulilonipa, nikawatunza; wala hapana mmojawapo wao aliyepotea, ila yule mwana wa upotevu, ili andiko litimie” (Yohana 17:11-12)
Jina hilo alilonalo Bwana Yesu anatuambia wazi kuwa si jina lake, ni jina la Mungu. Sasa ili wewe uitwe kwa jina lake Mungu ni lazima umwamini Bwana Yesu Kristo ili uwe mtu uliyeitwa kwa jina la Mungu ambalo ni YESU.
Hapo ndipo utaanza kupata ulinzi mpendwa. Msikilize Vizuri Bwana Yesu anasema hivi: “Mimi nimewapa neno lako; na ulimwengu umewachukia; kwa kuwa wao si wa ulimwengu, kama mimi nisivyo wa ulimwengu. Mimi siombi kwamba uwatoe katika ulimwengu; bali uwalinde na yule mwovu. Wao si wa ulimwengu, kama mimi nisivyo wa ulimwengu.” (Yohana 17:14-16)
Umeyasikia maneno hayo? Huyo mwokozi wa ulimwengu anasema wazi kabisa kuwa anao uwezo wa kuwalinda waliomo ulimwenguni ambamo yumo hata mwovu yaani shetani.
Ili uupate ulinzi humu ulimwenguni lazima umwamini Bwana Yesu Kristo ndipo UNAPOPATA TIKETI YA KULINDWA HUMU ULIMWENGUNI. Nje ya hapo ni ngumu kupokea ulinzi kutoka kwa Bwana Yesu Kristo.
Sikiliza Mungu anasema “ikiwa watu wangu walioitwa kwa jina langu…” IKIWA UNATAKA KUOKOLEWA NA TAUNI lazima uhakikishe wewe umeitwa au umo ndani ya jina lake Mungu liitwalo YESU.
Kama haumo humo ndani tafuta haraka kuingia humo ndani kwa imani. Tafuta kila uwezalo kumruhusu Bwana Yesu Kristo awe ndani yako.
JAMBO LA PILI:
B. JIFUNZE KUWA MNYENYEKEVU
Sikiliza unaweza ukawa ndani ya Bwana Yesu Kristo lakini ukakosa sifa hii ya kuwa mnyenyekevu. Ndani ya unyenyekevu kuna utii. Nikuulize swali wewe ni mtii katika maagizo aliyokupa Bwana Yesu Kristo?
Watu wengi wameokoka na wanajifariji mnoo kuwa aiseee! Mungu atatulinda hawajui kuwa Mungu ameweka utaratibu huu wa watu wake walioitwa kwa jina lake wanatakiwa wawe wanyenyekevu kwa Mungu.
Angalia wewe ni mnyenyekevu? Kweli unampenda Mungu? Angalia mistari hii: “Maana Yeye atakuokoa na mtego wa mwindaji, Na katika tauni iharibuyo. Kwa manyoya yake atakufunika, Chini ya mbawa zake utapata kimbilio; Uaminifu wake ni ngao na kigao. Hutaogopa hofu ya usiku, Wala mshale urukao mchana, Wala tauni ipitayo gizani, Wala uele uharibuo adhuhuri, Ijapo watu elfu waanguka ubavuni pako. Naam, kumi elfu mkono wako wa kuume! Hata hivyo hautakukaribia wewe. Ila kwa macho yako utatazama, Na kuyaona malipo ya wasio haki. Kwa kuwa Wewe BWANA ndiwe kimbilio langu; Umemfanya Aliye juu kuwa makao yako. Mabaya hayatakupata wewe, Wala tauni haitaikaribia hema yako. Kwa kuwa atakuagizia malaika zake Wakulinde katika njia zako zote. Mikononi mwao watakuchukua, Usije ukajikwaa mguu wako katika jiwe. Utawakanyaga simba na nyoka, Mwana-simba na joka utawaseta kwa miguu. Kwa kuwa amekaza kunipenda Nitamwokoa; na kumweka palipo juu, Kwa kuwa amenijua Jina langu. Ataniita nami nitamwitikia; Nitakuwa pamoja naye taabuni, Nitamwokoa na kumtukuza;” (Zaburi 91:3-15)
Angalia hapo anasema yupo tayari kutuokoa na tauni, lakini kuna neno hili anasema “KWA KUWA AMEKAZA KUNIPENDA NITAMWOKOA!!”
Hasemi nitamwokoa kwa sababu ananiamini tu, anasema kwa kuwa amekaza kunipenda. Angalia leo hii ukoje? Mungu akiangalia moyoni mwako anauona upendo ule wa kwanza?
Mbona umeacha kumtumikia, leo hii hata kusoma Biblia tu husomi, angalia mwenendo wako ulivyo wewe mwenyewe unaona wazi haujawa mnyenyekevu kwa Mungu. Haumtii, kuna dhambi amekutaza usifanye lakini unafanya kabisaa hata huna hofu ya Mungu.
Sikiliza yaani ili Mungu akuokoe ni lazima uhakikishe leo hii unaanza kumnyenyekea Mungu mtii. Mpende, fanyia kazi yale anayokuagiza uyafanye.
Acha njia zako mbaya mpendwa.
Sikiliza unaweza kuwa mtu aliyeitwa kwa jina la Mungu lakini ukawa ni mtu mwenye njia mbaya kabisa. Anasema acha njia mbaya.
FANYIA KAZI HAYO.
Tuonane katika kipindi kijacho
Tunapoachana nataka nikupe taarifa hii kuwa ukihitaji masomo yetu unaweza kuyapata kwa njia hizi zifuatazo:-
1. App yetu ya huduma yenye jina “MWAKATWILA” utaipata Play Store kwenye link pale juu, ambapo kuna masomo mengi sana hapo.
2. Tovuti yetu ya www.mwakatwila.org
3. YouTube - Mwakatwila au HUDUMA YA SOMA NENO LA MUNGU (HUSONEMU).
4. Facebook ingia katika hiyo tovuti au website yetu utaona alama ya Facebook (f) "like" na utapata maelezo ya kujiunga au ingia Facebook halafu andika “SOMA NENO LA MUNGU”
5. Instagram ingia Instagram app halafu andika “steven-mwakatwila”
6. DVDs 📀 au CDs 💿
7. VITABU.
NB: Wasiliana na mhudumu ofisini kwa namba +255 763 109 733, ili kupata VITABU, DVD & CD.
8. Kwa njia ya REDIO:- Utapata mafundisho yetu kwa redio zifuatazo:-
➖Rungwe FM 102.5 Kila siku ya Jumapili saa tatu mpaka saa nne usiku.
➖Baraka FM 107.7 Kila siku ya Jumanne saa kumi na mbili jioni mpaka saa moja usiku.
➖Bomba FM 104.1 Kila siku ya Ijumaa saa tatu usiku mpaka saa nne usiku.
9. Unaweza kutupata kwenye ONLINE RADIO yetu:- radio.mwakatwila.org
Kwa Mawasiliano zaidi Utatupata kwa namba hizi:-
+255 754 849 924 Au
+255 756 715 222
Wako
Mwl Mr & Mrs Steven Mwakatwila.
🖊️ 29/03/2020.
No comments:
Post a Comment