1⃣7⃣ MAMBO MUHIMU UNAYOTAKIWA UYAFANYE ILI UPATE KUISHINDA DHAMBI YA UZINZI
Na: MWL STEVEN & BETH MWAKATWILA
FUATANA NASI:- APP, FACEBOOK, INSTAGRAM, ONLINE RADIO 📻, WHATSAPP, WEBSITE & YOUTUBE, Kwa links zilizoko kwenye HII LINK hapa:
KUPATA APP YETU “HUSONEMU (MWAKATWILA) APP” BONYEZA LINK HII HAPA:
🗓 20 Februari, 2019
Bwana Yesu Kristo asifiwe sana. Nina imani kuwa umzima na una shauku kubwa ya kupokea mwendelezo wa somo nililokuahidi kukufundisha ili upate kuwa mshindi dhidi ya dhambi ya uzinzi.
Katika somo lililopita nilianza kukuonyesha sababu ambazo zinaweza kupelekea mtu akawa na mapepo.
Nilikuonyesha sababu ya kwanza ni Kuabudu miungu. Nataka nikuonyeshe sababu nyingine
SABABU YA PILI NI; KUHIFADHI UCHUNGU AU KUWA NA HASIRA MUDA MREFU
Moja ya mlango ambao shetani au mapepo wanaweza kuutumia kumwingia mtu na kummiliki ni hii ya kuwa na uchungu uliohifadhiwa muda mrefu au kuwa na hasira inayokaa muda mrefu.
Unapowaangalia watu wengi ambao wamejikuta wakiwa na mapepo utagundua wengi sana ni watu ambao wamekuwa na tabia ya ukali mnoo au hasira mnoo au watu waliojirundikia uchungu kwa wingi na kwa muda mrefu mnoo. Au ni watu wenye moyo wa majuto mnoo, au ni watu wenye kujihurumia mnoo au kujilaumu sanaa.
Sikiliza mtu ambaye moyoni mwake hana msamaha au si mtu mwenye kuachilia waliomkosea akawa ni mtu mwenye kuwashikilia sana hao watu waliomkosea ni rahisi sana watu wa namna hiyo kujikuta wakivamiwa na mapepo.
Watu wengi ambao wameishi maisha ya muda mrefu ya kujeruhiwa na bahati mbaya wakakosa elimu kama hii wakajikuta kuwa ni watu wanaoona kujisikitikia ni sehemu ya maisha yao watu wa namna hiyo ni rahisi mno kuvamiwa na mapepo ya aina mbalimbali na yakawatawala kabisa.
Unapokutana na mtu mwenye mapepo na mkayakemea na mkayatoa bahati mbaya mtu huyo asifundishwe habari za kusamehe na kutokuhifadhi huzuni na uchungu unajua ni rahisi sana mtu huyo kujikuta akirudiwa tena na mapepo hayo.
Mnaweza mkahangaika na mtu muda mrefu mnoo hafunguliwi kisa nihiki hiki ninachokufundisha.
Hasira na uchungu ni miongoni mwa milango ambayo adui anatumia kuwaingia watu na kuwatengenezea tabia mbaya mnoo.
Angalia mistari hii uone. “Mwe na hasira, ila msitende dhambi; jua lisichwe na uchungu wenu bado haujawatoka;wala msimpe Ibilisi nafasi.” (Waefeso 4:26-27).
Ukiipitia hiyo mistari utagundua kuwa kila mtu ameruhusiwa kuwa na hasira na uchungu kabisaa, lakini tumeagizwa tuhakikishe hasira zetu zisitufikishe kwenye kona ya kufanya dhambi.
Na moja ya dhambi itokanayo na hasira ni hii ya kuhifadhi uchungu muda mrefu. Angalia unaambiwa uwe na hasira ila usitende dhambi jua lisichwe na uchungu wako bado haujakutoka wala msimpe ibilisi nafasi.
Ibilisi anapata nafasi ya kukuvamia na kukutengenezea tabia iwe ya magonjwa au dhambi kwa sababu hii tu ya hasira iliyobeba uchungu kwa muda mrefu. Wewe wafuatilie watu wenye kusumbuliwa na roho mbaya au mapepo utagundua wengi ni watu wenye uchungu ulioambatana na huzuni sana.
Na hii inatokana na namna watu wanavyojihurumia mnoo na kujihesabia haki sanaa na wengine ni kutokana na wivu au husuda. Mtu mwenye wivu mkali lazima atakuwa ni mtu mwenye uchungu na kuhuzunika kila siku.
Huzuni na uchungu haina cha umri, anaweza akawa mtoto au mtu wa kati au mtu mzima kabisaa akawa ni mtu mwenye tabia ya hasira, wivu, husuda, huzuni, uchungu, nk.
Kuna tabia mtu anaanza nazo tokea akiwa mtoto, na wazazi wasipochukua tahadhari ya kuzirekebisha mapema kwa fimbo nk mtoto huyo anakua na hizo tabia na mwisho wake hujikuta yupo kwenye hatari kubwa ya kuvamiwa na mapepo.
Mfano mzuri tu watu wengi wenye hasira na wivu na uchungu mkali hujikuta wakivamiwa na roho ya uchawi. Wacha ile tabia ya uchawi wa kuzaliwa nao, nazungumzia hapa tabia ya KUVAMIWA NA MAPEPO. Kuna watu hawavamiwi ila wanaushirika na hayo mapepo tokea tumboni mwa mama zao.
Nimekuonyesha kuhusu watu waabuduo miungu, wao hujenga ushirika na hayo mapepo wengine tokea tumboni mwa mama zao.
Fikiria kuzaliwa kwa huyo mtoto chanzo chake ni mapepo unafikiri kavamiwa huyo?
Nimewahi kukutana na mtu yeye alifanya maamuzi yeye mwenyewe aoe pepo au jini. Alienda mwenyewe hakuvamiwa, wapo wengine wanaenda wenyewe huko ili waolewe na mapepo wanataka wao wenyewe.
Ninaposema kuvamiwa maana yake huyo aliyevamiwa si kuwa anayahitaji hayo mapepo lakini kutokana na tabia yake fulani yeye anakuwa anayafungulia mlango au kuyapatia kibali hayo mapepo kumvamia.
Angalia kama wewe una wivu hutaki kuona fulani anaendekea nk, nakuambia ukweli usishangae utavamiwa ndani yako na mapepo na yatakutengenezea tabia hata ya uuaji kabisa.
Ibilisi alipata nafasi ya kuwavamia wale makuhani na waandishi na Mafarisayo kwa kupitia tabia yao ya wivu tu mpaka wakafikiria kumwua Bwana Yesu Kristo.
Walitoa mashitaka ya uongo wakatafuta mashahidi wa uongo ili tu kutimiza shauri lililotokana na wivu wao tu.
Bwana Yesu Kristo alijua kuwa kiini cha hayo yoote anayotendewa ni ufalme wa giza umewabana hao watu na kuwatumikisha ili wayatende hayo.
Maandiko yanasema hivi “Yesu akawaambia wakuu wa makuhani, na maakida wa hekalu, na wazee, waliokuja juu yake, Je! Mmekuja wenye panga na marungu kama kukamata mnyang’anyi? Kila siku nilipokuwa pamoja nanyi hekaluni hamkuninyoshea mikono, lakini hii ndiyo saa yenu, na mamlaka ya giza.” (Luka 22:52-53)
Umegundua kitu hapo? Mamlaka iliyokuwa ikiwaendesha hao ndugu ilikuwa ni mamlaka ya giza. Ukijiuza maswali hiyo mamlaka ilipata mlango gani hata kuwamiliki hao watumishi mpaka wakaingia kwenye dhambi ya kuua mtu asiye na hatia?
Utagundua ilipitia kwenye tabia ya wivu na husuda iliyowajaa hao ndugu. Angalia kitu hiki, wivu na husuda huzaa hasira, uchungu, huzuni, kisasi, nk. unamkuta mwanamke anaomba kwa kulia weeee akiwa amejaa huzuni wee.
Wewe mwulize nini kinachokuliza hivyo, ngoja akupe maelezo utagundua ni wivu tu umemjaa na ndiyo unampelekea hasira, kilio, uchungu na huzuni tele.
Anapowatazama watu fulani hasa wanawake wenzake wanavyoendelea wanavyostawi anaumia weee!! Kesho usishangae akavamiwa na pepo la uongo akaanza kuwasemea hao wanawake wengine uongo ambao chanzo chake ni pepo.
Fikiria mtu anapanda mabasi mawili na bodaboda moja kwenda kusema uongo mahali fulani. Unafikiri uongo huo chanzo chake ni mwili? Ehehee, sikiliza kitendo cha kupanda basi moja tu mpaka anashuka kama ni uongo uliozaliwa na tabia ya mwilini utachoka.
Aingie kwenye basi la pili, atafute na bodaboda kwenda tu kusema uongo nakuambia kama ni tabia ya mwili lazima atashituka tu. Atasema ngoja nirudi. Kwanza napoteza muda na fedha zangu na akijua huyo mtu kuwa mimi nimetoka huku mbali kwenda kusema uongo? Mmhh siendi ngoja ninunue vitunguu hapa hapa nirudi navyo nyumbani badala ya kutumia hizi fedha kwa kwenda kumsemea fulani uongo.
Unaweza usinielewe. Sikiliza uongo unaotokana na pepo haumwachii mtu mpaka auseme hata iwe kwa kupanda ndege. Labda akutane na Roho Mtakatifu aliyeamua kulikomesha hilo pepo.
Ngoja nikupe mfano huu angalia siku ile Bwana Yesu Kristo anakamatwa pale bustanini. “Yesu akamwambia, Yuda, wamsaliti Mwana wa Adamu kwa kumbusu? Na wale waliokuwa karibu naye walipoona yatakayotukia, walisema, Bwana, tuwapige kwa upanga? Mmoja wao akampiga mtumwa wa Kuhani Mkuu, akamkata sikio la kuume. Yesu akajibu akasema, Mwe radhi kwa hili. Akamgusa sikio, akamponya. Yesu akawaambia wakuu wa makuhani, na maakida wa hekalu, na wazee, waliokuja juu yake, Je! Mmekuja wenye panga na marungu kama kukamata mnyang’anyi? Kila siku nilipokuwa pamoja nanyi hekaluni hamkuninyoshea mikono, lakini hii ndiyo saa yenu, na mamlaka ya giza.” (Luka 22:48-53).
Ukiipitia hiyo mistari utagundua kile Bwana Yesu Kristo alikigundua kuwa mamlaka ya giza ndiyo imewabana hao ndugu na wanayafanya hayo kwa kutumwana na kusimamiwa na kuamrishwa na kuendeshwa na mamlaka hiyo ya giza.
Fikiria mmeenda kumkamata mtu na miongoni mwa ndugu zake akainua panga na kumkata mmoja wenu sikio, na sikio likadondoka chini mnaona kabisaa, huyo mnaeenda kumkamata anawaomba radhi kabisaa na analipachika hilo sikio na linashika kama alivyozaliwa damu inaacha kutoka, hivi mtakuwa na ujasiri wa kumshika huyo mtu kama kweli mna akili sawasawa?
Mapepo hapo yameitwa mamlaka ya giza yaliwabana hao ndugu ndiyo maana hata hilo tu hawakuliona wakamkamata.
Nataka nikuonyeshe namna hasira na wivu na uchungu na huzuni vinavyoweza kutumiwa na mamlaka ya giza.
Siku moja nilikuwa nimesimama mbele ya watu wengi sana nafundisha semina, ghafla nilisikia moyoni mwangu huzuni kali sana. Sikujui ni nini. Nikafikiri nimekosea kitu Roho Mtakatifu anahuzunika ndani yangu.
Nikawa natubu kimoyomoyo huku nafundisha, unajua nikasikia Roho Mtakatifu akinifundisha huko moyoni kwangu kuwa niwaite watu wenye huzuni kali na uchungu.
Nikawaita walikuja wengi sana, nikafundishwa nitubu kwanza kwa ajili ya hao watu. Dhambi yao ilikuwa ni kukalisha uchungu na huzuni moyoni mwao. Na nikitubu nikemee pepo waliowaingia kutokana na uchungu huo. Unajua ile tunatubu kuhusu uchungu na hasira na huzuni zilizowakalia tu nilianza kuona mapepo yanavyoanza kuhangaika, wengine wakadondoka chini puuu, wengine wakaanza kupiga wahudumu ngumi hata mimi mwenyewe na mke wangu tulianza kupigwa ngumi..
Tukayakemea yawatoke hao watu. Unajua niligundua siku hiyo kuwa chanzo cha mapepo hayo kupata uhalali wa kukaa ndani yao kilitokana na hasira uchungu na huzuni iliyowakalia hao watu na wengine wakawa wanafikiria bora wafe na walifanya hata majaribio ya kujiua.
Hasira isiyo na kiasi ni hatari sana, na ili uitawale isivuke mpaka kwa kukujengea uchungu na huzuni ni lazima ujifunze kuwa mtu mwenye kusamehe na uwe mtu mwenye moyo wa rehema.
Mungu ametuagiza tujivike moyo wa rehema na mambo mengi tu tunatakiwa tuyaweke moyoni angalia mistari hii.
“Basi, kwa kuwa mmekuwa wateule wa Mungu, watakatifu wapendwao, jivikeni moyo wa rehema, utu wema, unyenyekevu, upole, uvumilivu,mkichukuliana, na kusameheana, mtu akiwa na sababu ya kumlaumu mwenzake; kama Bwana alivyowasamehe ninyi, vivyo na ninyi.Zaidi ya hayo yote jivikeni upendo, ndio kifungo cha ukamilifu.” (Wakolosai 3:12-14).
Ukiipitia hiyo mistari utagundua kuwa ikiwa mtu atajivika moyo wa namna hiyo hawezi kamwe kujikuta na uchungu au huzuni. Moyo wa namna hiyo atakayeukalia ni Roho Mtakatifu.
Kama unataka kuona kila siku unaishi maisha ya amani moyoni basi hakikisha unajivika moyo wa namna hiyo.
Naamini umenielewa Mungu akubariki sana.
Ukihitaji masomo yetu unaweza kuyapata kwa njia hizi zifuatazo:-
1. Tovuti yetu ya www.mwakatwila.org
2. YouTube - Mwakatwila au HUDUMA YA SOMA NENO LA MUNGU (HUSONEMU).
3. Facebook ingia katika hiyo tovuti au website yetu utaona alama ya facebook(f) like na utapata maelezo ya kujiunga au ingia Facebook halafu andika “SOMA NENO LA MUNGU”
4. Instagram ingia Instagram app halafu andika “Steven Mwakatwila”
5. DVDs 📀 au CDs 💿
6. VITABU.
NB: Wasiliana na Brigitha kwa namba +255 (0) 763 109 733, kupata VITABU, DVD & CD.
7. Kwa njia ya REDIO:- Utapata mafundisho yetu kwa redio zifuatazo:-
➖Rungwe FM 102.5 Kila siku ya Jumapili saa tatu mpaka saa nne usiku.
➖Baraka FM 107.7 Kila siku ya Jumanne saa kumi na mbili jioni mpaka saa moja usiku.
➖Bomba FM 104.1 Kila siku ya Ijumaa saa tatu usiku mpaka saa nne usiku.
Kwa Mawasiliano zaidi Utatupata kwa namba hizi:-
+255 (0) 754 849 924 Au +255 (0) 756 715 222
Wako
Mwl Steven & Beth Mwakatwila.
20/02/2019