Friday, February 1, 2019

1⃣3⃣ MAMBO MUHIMU UNAYOTAKIWA UYAFANYE ILI UPATE KUISHINDA DHAMBI YA UZINZI

Na: MWL STEVEN & BETH MWAKATWILA

FUATANA NASI INSTAGRAM

KUPATA APP YETU “HUSONEMU (MWAKATWILA) APP”, BONYEZA LINK HAPA:

FUATANA NASI WHATSAPP

FUATANA NASI FACEBOOK

FUATANA NASI YOUTUBE
&
FUATANA NASI ONLINE RADIO

🗓 01 Februari, 2019

Bwana Yesu Kristo asifiwe sana.  Naamini unaendelea vizuri. Pia nashukuru kwa ushuhuda ulionipa wa namna unavyopokea somo hili.

Tunakuombea ili Mungu  Roho Mtakatifu akusaidie katika kuyatendea kazi hayo yote.
Baada ya kukuonyesha kwa upana kidogo kwenye eneo la akili, hili eneo ni muhimu sana katika kuushinda mwili wako huo  wenye kuchagua dhambi.

Nakushauri kila mara ombea huo mfumo wa akili. Nataka nikufundishe jambo lingine muhimu sana ili uwe mshindi dhidi ya dhambi ya uzinzi.

UKIWA UMEOLEWA AU KUOA JIFUNZE KULITUMIA TENDO LA NDOA KAMA SILAHA YA KUUSHINDA MWILI DHIDI YA DHAMBI YA UZINZI.

Ngoja kidogo niseme neno hili kabla sijaendelea mbele. Nafahamu haujaingia bado kwenye ndoa, naamini siku moja Mungu atakupa mumeo au atakupa ndoa.
Sikiliza utakapopewa mume au mke  fahamu ya kuwa moja ya sababu ya wewe kupata mke au mume ni kukulinda wewe na dhambi ya uzinzi.

Kumbuka tunaangalia tabia ya uzinzi inayotokana na mwili. Mwili wako umeumbiwa kulifanya hilo tendo, Mungu ameweka utaratibu wa kila mtu mwenye uhalali wa kulifanya hilo tendo ahakikishe anaoa au anaolewa.

Nje ya utaratibu huo ukilifanya tendo hilo unahesabika mdhambi na hukumu yake ni jehanamu.

Maandiko matakatifu yanatufundisha kuwa  ili usiingie kwenye dhambi hii basi uoe au uolewe, angalia mistari hii. “Basi kwa habari ya mambo yale mliyoandika, ni heri mwanamume asimguse mwanamke. Lakini kwa sababu ya zinaa kila mwanamume na awe na mke wake mwenyewe, na kila mwanamke na awe na mume wake mwenyewe. Mume na ampe mkewe haki yake, na vivyo hivyo mke na ampe mumewe haki yake.” (1 Wakorintho 7:1-3).

Ukiipitia hiyo mistari utaona kuwa moja ya jambo unalotakiwa ulifanye ili upate kuwa mshindi dhidi ya dhambi ya uzinzi ni hili, unaambiwa uoe au uolewe.

Angalia na mistari hii, “Lakini nawaambia wale wasiooa bado, na wajane, Ni heri wakae kama mimi nilivyo. Lakini ikiwa hawawezi kujizuia, na waoe; maana ni afadhali kuoa kuliko kuwaka tamaa. Lakini wale waliokwisha kuoana nawaagiza; wala hapo si mimi, ila Bwana; mke asiachane na mumewe;” (1 Wakorintho 7:8-10)

Maandiko hapo yanatufundisha kuwa wajane na watu wasiooa au kuolewa ili wasiingie kwenye tatizo la kuwaka tamaa au mwili usiwasumbue kwenye eneo la kulihitaji tendo la ndoa basi wameagizwa waoe au waolewe.

Ohoo!! Hapo napata akili kuwa Neno la Mungu linatupa ufahamu kuwa kama wewe unaona mwili unalihitaji tendo hilo na huna uwezo wa kujizuia yaani usiingie kwenye uzinzi basi jitafutie wa kwako kihalali kabisa, mwende kwa wazazi wenu wawahalalishie kwa mwanaume kulipa mahari na mwende madhabahuni ili watumishi walibariki hilo jambo kabisa ili usiitwe mzinzi, nk.

Mungu anapotupa ndoa fahamu moja ya jambo lililokusudiwa ndani ya kitu ndoa ni kumlinda mtu na uzinzi. Yaani mwili ukihitaji hilo tendo tu usiwe na shida unamwendea WA KWAKO MNALIMALIZA KIHALALI KABISA NA HAPO MNAKUWA MMEUKOMESHA AU KUUSHINDA HUO MWILI.

Unapooa au kuolewa na tunakukuta umewaparamia wanawake wengine au wanaume wengine huko nje kwa kweli tutakuingiza kwenye kundi lileeee la WASIO NA AKILI.

Kumbuka akili ni ufahamu ni kujua ni kuelewa, sasa kama hujaelewa kuwa umepewa mke kwa sababu gani basi hutafahamu kuwa huyo mke au huyo mume umepewa ndiye atumikaye kukulinda au wewe kumlinda na zinaa.

Unajua watoto wa Mungu wengi hasa wanawake (SI WOTE) kwenye eneo hili kwa kweli wengi ni wazembe mnoo. Wanawake wengi ndiyo wana kesi nyingi za kuwalalamikia waume zao kuwa wazinzi.

Siku moja Mungu alinionyesha jambo la ajabu mno, alinionyesha namna wanawake wengi wanavyosababisha waume zao wawe wazinzi na wengi hawajui ila wanajihesababia sana haki.

Utamsikia analia anakuambia “mtumishi, mimi ninejitunza sana sana nafuatwa na wanaume wengi mnoo nakataa lakini huyu mume wangu yeye ananiumiza anazini huko nje sana tuu!!!”

Ngoja leo nikuambie ukweli, sikia mwanamke kufuatwa na wanaume hilo siyo jambo hata la kuwasimulia watu. Mwanamke yeyote mzuri atafuatwa tuuuu!!! Kama Sara na hata Rebeka tu wanaume waliwamezea mate unafikiri wewe hautafutwa?

Tena nakuhakikishia watakufuata hata wanaokufahamu kabisaa kuwa umeolewa na fulani na una watoto wangapi na umeokoka na ni mtumishi au mke wa mtumishi watakufuata tu hata kama wewe ni mke wa mwanajeshi watakufuata tuu, uwe tajiri au maskini watakufuata tu. Wanaume wewe wasikiage tu.

Mwanamke mwenye akili analijua hili na anajipanga tokea akiwa mtoto yaani binti mdogo.

Ehehee!!! hivi ulipokuwa mdogo tu si ulikuwa unasikia unaonywa kuwa “mwanangu waogope hawa waitwao wanaume?” Eee ulikuwa unajulishwa kuwa watakufuata tuu mpaka siku unaondoka duniani.

Mimi siogopi mwanamke kufuatwa na mwanamume kwa sababu nawafahamu wanaume, woga wangu upo hapa wakifuatwa wanajipangaje?

Nimejaribu kukufundisha hivyo ili usijihesabie sana haki kwa sababu wewe unawakataa wanaume. Ni halali yako kabisaa uwakatae na uliumbwa hivyo ili uwe na mume wako tu.
Ukikaa na huyo mwanamke katika mazungumzo utagundua kuwa yeye mwenyewe ndiye ufunguo unaotumika mume wake afanye uzinzi.

Wanawake wengi hasa walokole hawajui kuwa Mungu anawataka wao wahakikishe wanawalinda waume zao ili wasizini kwa kulitumia tendo la ndoa tu.

Wengi ni mabingwa wa kuwaombea hao wanaume wasizini lakini hawajui kuwa wakiomba lazima wajitoe mhanga kwa kuwapa waume zao tendo la ndoa tena kwa uzuri, yaani ufund, ubunifu nk. HAPO NAZUNGUMZIA KWA AKILI!!!

Mimi nakuambia ukweli wanawake wengi ndio wenye kesi hizi za wanaume wazinzi mimi kama mwalimu Mungu alinifundisha kuwa ndoa nyingi zenye kesi za namna hii moja ya sababu kuu ni hii ya kunyimana tu.

Angalia mistari hii. “Basi kwa habari ya mambo yale mliyoandika, ni heri mwanamume asimguse mwanamke. Lakini kwa sababu ya zinaa kila mwanamume na awe na mke wake mwenyewe, na kila mwanamke na awe na mume wake mwenyewe. Mume na ampe mkewe haki yake, na vivyo hivyo mke na ampe mumewe haki yake. Mke hana amri juu ya mwili wake, bali mumewe; vivyo hivyo mume hana amri juu ya mwili wake, bali mkewe. Msinyimane isipokuwa mmepatana kwa muda, ili mpate faragha kwa kusali; mkajiane tena, Shetani asije akawajaribu kwa kutokuwa na kiasi kwenu.” (1 Wakorintho 7:1-5).

Ukiipitia hiyo mistari utaona umuhimu wa tendo la ndoa imewekwa kwa wanandoa ili shetani asiwavuruge.

Fikiria unamkuta mmama sasa yeye ni mfungaji tuu, tena anafunga kula chakula mpaka tendo la ndoa kafunga sasa mama nanii bila kupatana na mumewe kuwa baba nanii mimi nina maombi nataka tupatane tusitishe.

Biblia inasema mpatane tena hilo patano lenu liwe na kiasi la sivyo shetani atawavuruga tu.

Sasa wanawake wengi wameokoka kuliko Biblia hawawashirikishi waume zao mfumo huo wa maombi wanajifungia na akija huyo mwanaume kakwepa mishale mingi huko sasa anakimbilia kwa mkewe ndiyo anamkuta amelala anaota ndoto za mfungo wake. Ehehee kama huyo mbaba ndiyo wale wale wasio na akili usishangae sana kesho binti wa kazi anakudharau si kaishampitia.

Mimi sijawakataza kufunga. Funga kwa akili mwanamke. Huyo Mungu unayemtumikia kwa kumwomba kwa kufunga ndiye huyo huyo anayekupa tahadhari kuwa usipokuwa makini kwenye funga yako hiyo adui unayempiga kwa kutumia maombi yeye atakupiga kwa kumtumia mumeo na mlango umeufungua wewe mwenyewe.

Ukitaka kujua kuwa hiki mwalimu anakifundisha kikoje wewe fanya utafiti, utagundua kuwa ndoa nyingi zimeanza kusumbua ni baada ya wanawake kuchukua mimba au wakaumwa, au wameenda kusoma mbali na waume zao na miaka ya sasa hivi shetani anazipiga ndoa nyingi mno kutokana na mifumo au taratibu za kazi zinazowekwa.
Moja ya jambo ambalo leo ukiwa kiongozi uwe wa serikali, shirika au taasisi fulani unatakiwa ulijue na uliogope ni hili la ndoa.

Biblia inaonya inasema hivi “(Ndoa na iheshimiwe na watu wote, na malazi yawe safi; kwa maana waasherati na wazinzi Mungu atawahukumia adhabu.” (Waebrania 13:4).
Kila mtu anatakiwa aiheshimu ndoa yake au ndoa ya mtu mwingine. Ni rahisi ukafanya jambo fulani ukiangalia kona moja tu ya utendaji wa kazi, kumbe ndani yake haujaiheshimu ndoa ya mtu.

Ukamhamishia huyo mtu mkewe ukampeleka huko mbali bila kujua kuwa unavyofanya hivyo unaupa nafasi mwili wa hao wanandoa kuingia kwenye vita ambayo mara nyingi wengi wanashindwa.

Mungu anajua kabisa kuwa ili huyu ashinde dhambi ya uzinzi ni lazima aoe au aolewe sasa fikiria umetenganisha na mmoja wao akazini? Mimi nakuambia ukweli lazima Mungu atakuadhibu siku moja. YAANI HILI NAJUA WATU WENGI HUPATWA NA MATATIZO NA HAWAJUI CHANZO KUMBE NI HILI TU LA KUTOKUHESHIMU NDOA ZA WATU.

Watu wengi sana ukiwafuatilia utagundua uzinzi waliufanya baada ya kutopeana tendo la ndoa kwa wakati. Mfano mzuri wewe mama ni mjamzito unafikiri wewe kuwa mjamzito ndiyo kunamfanya mumeo mwili wake utulie unakusubiri mpaka ujifungue?

Lazima hapo uwe na akili ya namna ya kufanya ili mumeo asishindwe na mwili. Najaribu sana kujizuia kuingia ndani sana kwa sababu ujumbe huu unasomwa na watu wengine ni watoto.

Hata kwa wanaume ni vivyo hivyo. Lazima ujue kuwa umepewa mke ili akulinde usiingie kwenye uzinzi.

Yaani unapowaka tamaa unatakiwa uishinde kwa kuoa na pia ili mkeo asiingie kwenye uzinzi wewe ndiyo umetakiwa uhakikishe unamlinda kwa kumpa haki yake ya tendo la ndoa.

Sasa angalia unavyojipanga kimapenzi. Wanaume wengi hasa walokole hapo ndipo imekuwa taabu kweli. Sikiliza unatakiwa ujifunze kumpa haki ya mapenzi mkeo ili asishindwe na mwili. Usiseme hooo huyu mwanamke kila wakati ananitaka sasa, JIPANGE MPENDWA.

Unamkuta mpendwa yeye akili zake ziko kwenye fedha tuu kazi tuu huko ndiko anakuwa mbunifu weee lakini kwenye eneo la mapenzi sifuli kabisaaa.

Hebu jifunze mwanaume angalia hata wanaume watakatifu walikuwa vizuri kona hii. “Kwa sababu Ibrahimu alisikia sauti yangu, akayahifadhi maagizo yangu, na amri zangu, na hukumu zangu, na sheria zangu. Isaka akakaa katika Gerari. Watu wa mahali hapo wakamwuliza habari za mkewe. Akasema, Ni ndugu yangu huyu maana aliogopa kusema, Ni mke wangu, watu wa nchi wasije wakamwua kwa ajili ya Rebeka; kwa maana alikuwa mzuri wa uso. Ikawa alipokuwa amekaa huko siku nyingi, Abimeleki, mfalme wa Wafilisti, akachungulia dirishani, akamwona Isaka anacheza-cheza na Rebeka mkewe. Abimeleki akamwita Isaka, akasema, Yakini huyu ni mkeo, mbona ulisema, Ni ndugu yangu huyu? Isaka akamwambia, Kwa sababu nalisema, Nisife kwa ajili yake. Abimeleki akasema, Ni nini hii uliyotutendea? Labda mtu mmojawapo angalilala na mkeo bila kufikiri, nawe ungalitutia hatiani. Basi Abimeleki akawaamuru watu wote, akisema, Amgusaye mtu huyu au mkewe lazima atauawa.” (Mwanzo 26:5-6)

Umemwona Isaka alivyokuwa? Unafikiri alichezacheza na mkewe mchezo wa namna gani mpaka mfalme akawashtukia kuwa hawa ni mume na mke?

Ngoja niishie hapo nisije kufunguka sanaaa!!! Najua ujumbe huu unapitiwa na wengi hawajaoa na kuolewa sasa nikiingia huko ndani hatutawatendea vema.

Somo hili au kipengele hiki tunaweza kujifunza kona ya mapenzi tu Kibiblia kwa siku, miezi mingi sana tu. Hebu angalia jambo hili ni muhimu unaweza kulitumia kuushinda mwili.

Kama unaona una wito wa kuoa au kuolewa na umri unaruhusu na mazingira yanaruhusu nakushauri oa au olewa kuliko kuzini. Hiyo dhambi itakupeleka jehanamu. Jehanamu ipo wapendwa nakusihi jihadhari usiende huko.

Mungu akubariki

Ukihitaji masomo yetu unaweza kuyapata kwa njia hizi zifuatazo:-

1. Tovuti yetu ya www.mwakatwila.org

2. YouTube - Mwakatwila au HUDUMA YA SOMA NENO LA MUNGU (HUSONEMU).

3. Facebook ingia katika hiyo tovuti au website yetu utaona alama ya facebook(f) like na utapata maelezo ya kujiunga au ingia Facebook halafu andika  “SOMA NENO LA MUNGU”

4. Instagram ingia Instagram app halafu andika “Steven Mwakatwila”

5. DVDs 📀 au CDs 💿

6. VITABU.
NB: Wasiliana na Brigitha kwa namba +255 (0) 763 109 733, kupata VITABU, DVD & CD.

7. Kwa njia ya REDIO:- Utapata mafundisho yetu kwa redio zifuatazo:-
➖Rungwe FM 102.5 Kila siku ya Jumapili  saa tatu mpaka saa nne usiku.
➖Baraka FM 107.7 Kila siku ya Jumanne saa kumi na mbili jioni mpaka saa moja usiku.
➖Bomba FM 104.1 Kila siku ya Ijumaa saa tatu usiku mpaka saa nne usiku.

8. Unaweza kutupata kwenye ONLINE RADIO yetu:-  radio.mwakatwila.org

Kwa Mawasiliano zaidi Utatupata kwa namba hizi:-
+255 (0) 754 849 924 Au +255 (0) 756 715 222

Wako
Mwl Steven & Beth Mwakatwila.
01/02/2019

No comments:

Post a Comment