Salamu – Juni, 2019
Bwana Yesu Kristo asifiwe sana. Tunamshukuru sana Mungu ambaye amekuwa pamoja nasi katika mwezi wa tano uliopita.
Tumekuwa na semina tatu kubwa ambazo tulifunga hema katika mikoa miwili. Tumekuwa na semina mkoa wa Songwe maeneo ya Vwawa na Tunduma. Pia tumekuwa na semina katika mkoa wa Rukwa pale Sumbawanga Mjini.
Zilikuwa ni semina nzuri mnoo.
Hebu tuendelee na salamu maalumu katika mwezi huu.
JIFUNZE KUTAKASA KILA TENDO LILILOANDIKWA KATIKA VITABU VYA MATENDO MBINGUNI NA DUNIANI
Hebu tuangalie eneo hili.
ONDOA KUMBUKUMBU HIZO ZILIZOKO KWENYE NAKALA HIZO ILI ZISIKULETEE MADHARA
Sikiliza, unaweza ukafanya dhambi fulani huko nyuma, mfano ulizini au uliua na ukaomba msamaha kabisa. Lakini lazima ujifunze kuifuta au kuiondoa hiyo dhambi kwenye kumbukumbu yoyote itakayokumbukwa hapa hapa duniani.
Kumbuka dhambi inapofanywa, kumbukumbu zake zinatunzwa hapa hapa duniani na huko mbinguni. Dhambi uliyoifanya inaweza kukufuata hapa duniani au wewe ukaifuata huko mbinguni kwa lugha nzuri utaikuta.
Ngoja nikupe mfano huu uone. Angalia mistari hii: “Kulikuwa na njaa siku za Daudi muda wa miaka mitatu, mwaka kwa mwaka; naye Daudi akautafuta uso wa BWANA. BWANA akasema, Ni kwa ajili ya Sauli, na kwa nyumba yake yenye damu, kwa kuwa aliwaua hao Wagibeoni. Ndipo mfalme akawaita Wagibeoni akawaambia; (basi Wagibeoni si wa wana wa Israeli, ila ni wa masalio ya Waamori; na wana wa Israeli walikuwa wamewaapia; lakini Sauli akatafuta kuwaua katika juhudi yake kwa ajili ya wana wa Israeli na Yuda;)” (2 Samweli 21:1-2)
Ukiisoma hiyo mistari utaelewa hiki ninachokufundisha. Angalia. Mfalme Sauli aliua hao watu, Sauli akafa na ikapita miaka mingi mnoo, siku moja njaa ikatokea katika taifa la Israeli.
Njaa hiyo ikadumu miaka mitatu. Angalia kitu cha ajabu ambacho ndicho nataka nikutazamishe. Njaa hiyo chanzo chake ilikuwa ni dhambi ya damu ambayo Sauli aliimwaga.
Kumbuka Sauli hakuwepo aliishakufa. Cha kujifunza hapo ni nini? Ni hiki, dhambi hutunzwa katika nakala kama kivuli duniani na nakala kama halisi huko juu mbinguni. Hii dhambi iliandikwa mahali na ndiyo maana ikaifuata hiyo taifa la Israeli lililo chini ya utawala wa mfalme mwingine kabisa yaani mfalme Daudi tena rafiki wa Mungu.
Maana yake nini? Daudi hakushughulikia hizo nakala zilizotunza hizo kumbukumbu za dhambi iliyofanywa na aliyemtangulia.
Naamini kumbukumbu hizo zilitunzwa sehemu zote mbili. Sauli siamini kama alifanikiwa kuzifuta hizo kumbukumbu za damu ambazo alizimwaga katika zile nakala za kutunzia matendo maovu zilizoko mbinguni.
Unaweza kuniuliza kwa nini unasema hivyo? Kwa mujibu wa Biblia agano la kale lilikuwa halina damu bora inayoweza kushughulikia hizo nakala za mbinguni.
Ukitulia tena unaona Sauli hakushughulikia nakala zinazotunza kumbukumbu za mambo duniani. Ndiyo maana dhambi iliyofanywa na mfalme ambaye alitumia nafasi ya ufalme wake kuua watu, dhambi hiyo ilikumbukwa katika ufalme wa Daudi na ikamfuata Daudi na ufalme wake yaani taifa zima la Israeli.
Dhambi ikitunzwa kwenye kumbukumbu za huku duniani fahamu zitawafuata watu walioko duniani na zitapitisha madhara makubwa sana.
Kumbukumbu za maovu yako zilizotunzwa mbinguni kama hazikushughulikiwa fahamu ndizo zitatumika kama ushahidi wa kukupeleka jehanum.
Kumbukumbu za dhambi zilizotunzwa kwenye nakala zilizopo duniani kama hazikushughulikiwa fahamu zitatumika kama ushahidi unaotafuta uhalali wa wewe kuadhibiwa ukiwa humu humu duniani.
Ngoja nikupe mfano mwingine labda utanielewa. Kuna mwaka ambao serikali ilifanya uamuzi wa kupitia vyeti vya wafanyakazi ambao wameajiriwa na serikali.
Unajua watu wengi sana walijikuta wamepoteza kazi na elimu zao kisa ni dhambi waliyoifanya zamani sana ilipokumbukwa katika nakala zilizotunza matendo ya uovu ambayo yaliwekwa dhahiri humu humu duniani.
Fikiria watu wengi walisahau kama waliifanya hiyo dhambi. Wengine waliokoka kabisa na kuwa watumishi wa Mungu. Bahati mbaya hawakujua namna ya kushughulikia kumbukumbu za dhambi yao hiyo walioifanya.
Fikiria cheti kilicholeta shida kilikuwa cha kidato cha nne. Mtu alisoma mpaka akachukua shahada mbili wengine wakawa madaktari n.k. Siku dhambi hiyo ilipowafuata tu wakajikuta wamekwama katika kila kona. Sikiliza jifunze katika kushughulikia mara kwa mara nakala zilizotunza hizo kumbukumbu zako.
Inawezekana kabisa ni dhambi ulizofanya wewe au walizofanya waliokutangulia. Yaani wazazi wako, viongozi waliokutangulia wewe ukachukua nafasi yao au ulizofanya wewe mwenyewe.
Unaweza kusema mbona kila mtu atahukumiwa kwa matendo yake? Ni sawa, lakini lazima ujue kuwa kuna dhambi akiifanya mtu mwingine kumbukumbu zikikumbukwa, wanaoweza kupata madhara ni watu ambao yamkini hata wao hawakushiriki hiyo dhambi kabisaa.
Mfano: Mfalme Daudi hakuwaua hao watu, lakini Israeli yoote ilitumikia adhabu hiyo siku dhambi hiyo ilipokumbukwa. Hata watoto saba wa Sauli, waliitumikia dhambi ilipowafuata. Soma hicho kitabu chote cha 2 Samweli 21, utaona hiki ninachokuambia.
“Na kwa sababu hiyo hekima ya Mungu ilisema, Tazama, nitatuma kwao manabii na mitume, nao watawaua baadhi yao na kuwafukuza, ili kwa kizazi hiki itakwe damu ya manabii wote, iliyomwagika tangu kupigwa msingi wa ulimwengu; tangu damu ya Habili hata damu ya Zakaria, aliyeuawa kati ya madhabahu na hekalu. Naam, nawaambieni ya kwamba itatakwa kwa kizazi hiki.
Ngoja nikupe mfano huu mwingie.” (Luka 11:49-51)
Fikiria kidogo kama damu za watu zikitakwa mikononi mwa hao ndugu maana yake kuna nakala zilizotunza kumbukumbu za maovu waliyoyafanya watu waliowatangulia hao watu.
Na dhambi hiyo iliwafuata hao watu ambao hawakuwepo kabisa Kaini alipokuwa amuua Habili na pia Zakaria alipouawa kati ya madhabahu na hekalu.
Naona sasa umenielewa ninapokuambia jifunze kushughulikia katika kuzitakasa hizo nakala zilizoko mbinguni na duniani zilizobeba kumbukumbu za uovu.
Mungu akubariki sana. Tuonane katika kona hii mwezi ujao.
Ukihitaji masomo yetu unaweza kuyapata kwa njia hizi zifuatazo;
1.Website yetu ya www.makatwila.org
2. Youtube- Mwakatwila au HUDUMA YA SOMA NENO LA MUNGU
3.Facebook ingia katika hiyo tovuti au website yetu utaona alama ya facebook(f) like na utapata maelezo ya kujiunga
4.Dvds au Cd
5.Vitabu
6.Kwa njia ya Redio mbalimbali Rungwe fm102.5 Kila siku Jumapili saa tatu mpaka saa nne usiku
na Baraka Fm107.5 kila siku ya jumanne saa kumi na mbili jioni mpaka saa moja usiku na Bomba fm 104.1 kila siku ya ijumaa saa tatu usiku mpaka saa nne usiku
7: Unaweza kutupata kwenye redio yetu online ya. radio.mwakatwila.org
Kwa mawasiliano zaidi Utatupata kwa namba hizi. 0754849924-0756715222
Wako
Mr &Mrs Steven Mwakatwila