SALAMU ZA PASAKA 2020
Na MWL STEVEN & BETH MWAKATWILA
Ninawasalimu katika jina la Bwana Yesu Kristo. Mimi na familia yangu tunamshukuru sana Mungu kwa wema wake kwetu hata kutupatia siku hii maalumu ambayo tunaadhimisha kufufuka kwa Bwana wetu Yesu Kristo.
Hili ni tukio muhimu sana sana kwa wanadamu wote.
SIKUKUU YA PASAKA YA MWAKA HUU NI TOFAUTI SANA NA SIKUKUU ZA PASAKA ZINGINE
Sikiliza, sikukuu ya pasaka ya mwaka huu imekuja katika mfumo ambao ulimwengu unapitia katika kipindi kigumu mnoo cha kukutana na maradhi ya Corona (COVID-19).
Watu wengi mnoo katika mataifa mbalimbali wameingia katika siku hii ya pasaka wakiwa wameamliwa kutokutoka nje ya nyumba zao.
Hata wengi wanashindwa kwenda kwenye makusanyiko matakatifu ili kumfanyia Mungu ibada, wapo ndani hawajui nini kinaendelea huko nje.
Naona sasa umenielewa ninapokuambia sikukuu hii ni tofauti na sikukuu nyingine za pasaka.
Lengo langu mpaka kukuonyesha haya nina nia ya kutaka kukutia moyo. Maandiko yanatufundisha tuonapo mambo kama haya yakitukia tufanye nini.
JAMBO LA KWANZA: NI WAKATI WA KUCHANGAMKA
Angalia mistari hii: “Tena, kutakuwa na ishara katika jua, na mwezi, na nyota; na katika nchi dhiki ya mataifa wakishangaa kwa uvumi wa bahari na msukosuko wake; watu wakivunjika mioyo kwa hofu, na kwa kutazamia mambo yatakayoupata ulimwengu. Kwa kuwa nguvu za mbinguni zitatikisika. Hapo ndipo watakapomwona Mwana wa Adamu akija katika wingu pamoja na nguvu na utukufu mwingi. Basi mambo hayo yaanzapo kutokea, changamkeni, mkaviinue vichwa vyenu, kwa kuwa ukombozi wenu umekaribia.” (Luka 21:25-28)
Unapoipitia hiyo mistari utajifunza hiki ninachokuambia yaani changamka. Sikukuu ya Pasaka hii ndani yake imebeba fundisho hili kuwa Bwana Yesu Kristo yu karibu mlangoni.
Kwa lugha nzuri zaidi ni wakati wa kuinuka na kutokujiruhusu ukate tamaa au uchoke. Ni wakati wa kujiweka sawasawa katika mfumo wa Imani yako.
Mataifa yoote yanaishuhudia dhiki hii ya Corona, hofu imeikumba Dunia ghafla, watu wengi wamevunjika moyo, wengi hawana tumaini tena, uchumi wa mataifa umeanguka ghafla, uchumi wa mtu mmoja mmoja umeanguka ghafra.
Dunia imepoteza watu wengi mnoo tena muhimu mnoo kwa kipindi kifupi mnoo na hakuna ajuaye hii janga litaisha lini. Sikia maandiko yanasema mwonapo mambo kama hayo yakitokea ulimwenguni Basi changamkeni.
Changamkia maombi mpendwa, ondoa uvivu, changamkia Neno la Mungu, soma na sikiliza. Changamka katika utumishi uliopewa. Panga namna utakavyomtumikia Mungu katika kipindi hiki hiki.
Unajua ni rahisi ukafa moyo kisa mikutano ya injili imezuiliwa, semina zimezuiliwa, makusanyiko ya maombi yamezuiliwa, nk. Changamka mpendwa panga ratiba zako, tafuta mwongozo wa Roho Mtakatifu wa namna utavyowafikia watu katika kipindi hiki.
Si kipindi cha kulala kiutumishi. Unajua Mungu ana njia nyingi mnoo za kuwafikia watu? Bahati mbaya watu wengi hawakuwa na maandalizi kama siku wakikutana na hali kama hii inakuwaje?
Soma Biblia uone kama Bwana Yesu Kristo alikuwa na mfumo mmoja tu wa kuhubiri na kufundisha. Fikiria mchungaji unategemea kondoo waje katika jengo tu siku ya Jumapili na ghafla unakutana na hali kama hii?
Sijui wachungaji wangapi Watanzania wamejipanga namna ya kuchunga watu kwa mtindo wa namna hii?
Kanisa halikuwa na maono ya namna hii, wainjilisti hatukuwa na maono ya namna hii, ndiyo maana utaona baada ya mambo haya kutokea watumishi wengi wamevunjika mioyo.
Hapana tunahitaji kuchangamka. Mwombe Mungu akupe maarifa ya namna ya kuwafikia watu na kuwachunga. Ni kipindi kingine Mungu anatupa shule kubwa hapo.
Soma uone wenzetu walitumikaje walipozuiliwa kwenda kwenye mikusanyiko, angalia nchi za wenzetu ambao mpaka leo hii walikatazwa katika nchi zao kuhubiri au kujenga majengo ya kuwakusanyia Wakristo na kuwachungia humo ndani.
Soma mchungaji uone ni mbinu gani wanatumia kuwachunga waaminio bila serikali zao kujua.
Kipindi hiki ndiyo cha kuchangamka sana. Ni kipindi cha kuhakikisha kanisa linabadili mfumo wa kuwaandaa waaminio bila kumtegemea mchungaji au mtumishi yeyote.
Fikiria mchungaji hukuwaandaa waumini wako, kusoma Biblia, kuomba na kujisimamia, na inatokea mwezi mmoja tu hakuna kukutana na hao waumini unafikiri siku ya kukutana nao kuna Ukristo hapo?
Yes!!!! Naona moyoni mwangu kuchangamka kweli kweli katika kipindi hiki, kwa sababu naona kanisa kuanza kujenga imani kwa Bwana Yesu Kristo mfufuka kuliko kujenga imani kwa mtu, watu, dini, n.k.
Kuna nchi nimesikia waaminio ambao zamani waliambiwa ni marufuku wao kuomba toba mpaka mtumishi awaombee, sasa imani imekuja ghafla kwa watumishi kuwaambia waaminio kuwa hata wao wanaweza kuomba toba huko huko nyumbani walikofungiwa.
Shida yangu ipo hapa je! Waumini hao waliandaliwa vema? Usifikiri ni rahisi mtu kuomba ikiwa hakuandaliwa kuomba, usifikiri ni rahisi mtu kumwamini Mungu kuwa amemsamehe kama hakuandaliwa mapema.
JAMBO LA PILI: INUA MACHO YAKO JUU AU IMARISHA IMANI YAKO KWA BWANA YESU KRISTO
Kama mpendwa ulikuwa hauko vizuri katika mfumo wa imani yako chukua hatua mpendwa ya kuimarisha imani yako vizuri kwa Bwana Yesu Kristo. Maandiko yanasema “Basi mambo hayo yaanzapo kutokea, changamkeni, mkaviinue vichwa vyenu, kwa kuwa ukombozi wenu umekaribia.”
Sikiliza pasaka hii unatakiwa ujitathmini wewe mwenyewe moyoni mwako kiwango cha imani yako au unavyomtazama mwokozi wako unamtazama kwa kiwango kipi?
Fahamu Bwana Yesu Kristo anasema hivi: “walakini, atakapokuja Mwana wa Adamu, je! Ataiona imani duniani?” (Luka 18:8B)
Bwana Yesu Kristo anapokuja je! Ataiona imani yako kwake? Umejenga imani yako wapi? Unajua ni rahisi kujenga imani yako kwa mapokeo, au dini, au watumishi, mume, mke, baba, huduma, n.k, na usiijenge hiyo imani yako kwa Bwana Yesu mfufuka.
Anza kujenga imani yako kwa Bwana Yesu Kristo si kwa kitu kingine mpendwa.
JAMBO LA TATU: BADILISHA MFUMO WA MAISHA YAKO; ONDOA TABIA MBAYA.
Ni kipindi ambacho kuanzia dakika hii uhakikishe unaishi maisha ya utakaso: “Mwenye kudhulumu na azidi kudhulumu; na mwenye uchafu na azidi kuwa mchafu; na mwenye haki na azidi kufanya haki; na mtakatifu na azidi kutakaswa. Tazama, naja upesi, na ujira wangu u pamoja nami, kumlipa kila mtu kama kazi yake ilivyo.” (Ufunuo 22:11-12)
Uyaonapo hayo, jifunze kuzidi kujitakasa. Kuna njia mbili kuu za kujitakasa, njia ya kwanza ni kwa Damu ya Bwana Yesu Kristo. Na njia ya pili wewe kutogusa vichafu, yaani dhambi.
Kiwango chako cha kuishi maisha safi kinatakiwa mpendwa ukiongezee yaani uzidi. Acha dhambi, ndiyo umeokoka na umeitwa hata umtumikie Bwana Yesu Kristo, lakini kumbuka Bwana yupo karibu mlangoni.
Anataka akuone ukiwa mtakatifu, ondoa mwenendo wowote wa uovu. Ishi maisha ya kumpendeza.
Nikutakie Sikukuu njema. Barikiwa.
Wako
Steven & Beth Mwakatwila
11/04/2020.
No comments:
Post a Comment