Thursday, March 28, 2019

2⃣4⃣ MAMBO MUHIMU UNAYOTAKIWA UYAFANYE ILI UPATE KUISHINDA DHAMBI YA UZINZI

Na: MWL STEVEN & BETH MWAKATWILA

FUATANA NASI:- KWENYE APP, FACEBOOK, INSTAGRAM, ONLINE RADIO 📻, WHATSAPP, WEBSITE & YOUTUBE, Kwa links zilizoko kwenye HII LINK hapa:

KUPATA APP YETU “HUSONEMU (MWAKATWILA) APP” BONYEZA LINK HII HAPA:

🗓 28 Machi, 2019

Bwana Yesu Kristo asifiwe sana. Naamini unaendelea vizuri. Nimekuletea mfululizo wa somo nililokuahidi kukufundisha. Kumbuka katika kipindi kilichopita  nilikuonyesha eneo lile la namna ya kufanya ikiwa utaona dalili za kuwa kuna pepo la uzinzi  ndani ya mwili wako.

Nilikufundisha kuwa jambo la kufanya ni kulitoa tu hulo pepo.

Ngoja tuendelee mbele kidogo pepo hatakiwi atulizwe, anatakiwa atolewe ndani ya mtu. Na pia asipewe nafasi ya kumrudia huyo mtu tena.

Bwana Yesu Kristo siku moja alikutana na mtu mwenye pepo angalia alipokuwa analitoa alilipa amri ya kutokumrudia huyo mtu tena. “Naye Yesu akiona ya kuwa mkutano unakusanyika mbio, akamkemea yule pepo mchafu, akamwambia, Ewe pepo bubu na kiziwi, mimi nakuamuru, mtoke huyu, wala usimwingie tena. Akalia, akamtia kifafa sana, akamtoka; naye akawa kama amekufa; hata wengi wakasema, Amekufa. Lakini Yesu akamshika mkono akamwinua naye akasimama.” (Marko 9:25-27).

Ukiipitia hiyo mistari utaona wazi kuwa Bwana Yesu Kristo alitoa amri ya huyo pepo asimrudie huyo mtu tena. Unapoisoma hiyo mistari unaona umuhimu wa sisi leo tunapoyatoa hayo mapepo yaliyo ndani ya watu tujifunze kutoa amri kwa hayo mapepo kutowarudia hao watu tena.

Kumbuka huduma hii inabebwa na mamlaka ya ufalme wa Mungu. Kwa hiyo kinachoamrishwa kitatii kile kilichosemwa na mtoa amri kwa sababu amebeba mamlaka.

Mara nyingi tunajisahau sana tunapoyatoa hayo mapepo ndani ya watu kuyawekea amri hii ya kutokuwarudia hao watu tena. Unajua ulimwengu wa roho unaheshimu mno kile kilichosemwa kimamlaka. Pepo hatoki kwa kupenda anaamriwa na pia lazima aamriwe asirudi hapo alipotolewa.

Unaposoma maandiko unaona sababu nyingi tu zinazopelekea mtu kurudiwa na pepo.
Sababu nyingine ambayo inaweza kumfanya pepo wa uzinzi arudi kwa mtu aliyetolewa pepo ni HOFU KWA HUYO MTU ALIYETOLEWA PEPO.

Watu wengi waliotolewa pepo huwa wamebeba hofu ya kuona watarudiwa na hali hiyo tena. Maandiko yanasema kile unachokihofu ni rahisi sana kukupata. “Aogopacho mtu asiye haki ndicho kitakachomjilia; Na wenye haki watapewa matakwa yao.” (Mithali 10:24).

Unapotolewa pepo hilo jenga ndani yako imani isiyo na hofu kuwa litakurudia hata ukiona dalili za kuwaka tamaa ya uzinzi. Kumbuka mwili unaweza kuwasha tamaa ya kufanya tendo la ndoa.

Sasa wengi wanapokutana na hali hii ya mwili kuwaka tamaa badala ya kuushughulikia mwili huanza kufikiria ile hali yao ya kwanza ya pepo la uzinzi imewarudia.
Hubeba hofu na hofu hiyo huwaharibu katika imani na mwisho kweli huyo pepo huwarudia. Ukifanyiwa huduma ya namna hii jenga imani usiwe na mashaka kuwa halijatoka, au litarudi hata uonapo dalili yoyote.

Shetani ni mjaribu na mwongo, atakujaribu tu na kukudanganya kwa kukutisha kwa kukuonyesha kuwa hajatoka. Akiona imani uliyonayo kuwa huna pepo hilo tena atakuacha.

Unajua mtu mwenye hofu au mashaka maana yake hajaamini. Nenda kaombewe ukiambiwa na waombaji hao kuwa pepo ametoka amini. Ukiambiwa bado hajatoka usisite kuendelea kuombewa mpaka upate uhakika kuwa ametoka.

Ukiambiwa ametoka jenga imani hapo usihofu kuwa hajatoka hata kama alisumbua sana kutoka.

Sababu nyingine ni DHAMBI.
Nataka nikutazamishe hapo dhambi kwa aina mbili, kuna dhambi ikiyotangulia kufanywa na dhambi aifanyayo mtu huyo baada ya kutolewa pepo.
Nianze kwa dhambi iliyotangulia kufanywa. Kuna watu ambao wamejikuta wakiwa na mapepo kwa sababu ya kuyafungulia mlango wao wenyewe  kwa viapo au maangano fulani.

Wanaweza wakawa ni wao wenyewe au waliowatangulia, watu wa namna hiyo hujikuta wamefungiwa au kubanwa na hayo mapepo kihalali.

Biblia inasema hivi “Je! Aliye hodari aweza kunyang’anywa mateka yake, au jeshi lao waliofungwa halali wataokoka?” (Isaya 49:24).

Umeona hapo? Kuna wafungwa waliofungwa kihalali kabisaa, kwenye ulimwengu wa roho kuna watu wamefungwa na vifungo mbalimbali kihalali. Maana yake kuna makosa yalifanyika au maagano fulani yalifanyika na hayo ndiyo yanayotumika kumpa shetani na mapepo uhalali wa kuwabana au kuwafungia watu hata tabia mbaya zilizobebwa na mapepo.

Sasa unaweza kuombewa pepo akatoka lakini akarudi haraka kwa sababu bado ana uhalali wa kumtesa huyo mtu kwa sababu ya kutokutubiwa au kuondolewa kitu kile  kinachompa uhalali huyo pepo wa kumfuatilia huyo mtu.

Ngoja nikupe mfano huu. Kuna ndugu alikuwa amewekewa ndani ya tumbo lake hirizi. Aliwekewa na mganga kwa kutumia maji aliyoyaoga tu. Mganga huyo akamwambia nimekuwekea zindiko tumboni.

Sasa siku mimi nakutana naye anaumwa ili nimwombee pepo akalipuka. Ilinichukua zaidi ya masaa nane kumwombea ili hilo pepo limwachie mpaka alipokunya hiyo hirizi.
Alipoitoa hiyo hili kwa kupitia njia ya haja kubwa tu akafunguka. Uhalali wa hilo pepo kumbana na kumfuatilia huyo mtu ulikuwa katika ile hirizi aliyokuwa nanyo ndani ya tumbo lake.

Unajua siku ile nilijifunza kitu kikubwa sana. Kuna watu walipewa vitu na wachawi au waganga wa kienyeji vinaonekana vya kawaida tu kumbe ndani yake vimebeba mapepo mengi tu. Sasa unaweza kukemea hilo pepo litoke, pepo litatoka lakini kama kile alichopewa huyo mtu hakijashughulikiwa fahamu pepo anapata uhalali wa kurudi hapo kwa sababu kibebeo chake kikichombeba huyo pepo na kumwingia huyo mtu bado kipo

Cha msingi hapo wewe mwenye hiyo shida yaani hilo pepo usisite kumweleza ukweli huyo mtumishi chanzo cha wewe kuingiliwa na hiyo roho. Watu wengi hujitahidi sana kuficha mambo yao mabaya. Hilo linawagharimu sana.

Unakuta mtu anakueleza leo kimoja ndani ya vitu kumi ambavyo ilitakiwa akueleze. Watumishi wengi wakikuona siyo mkweli au haupo wazi kwao wanakuacha. Wakifikiri wewe hupendi kufunguliwa.

Eleza ukweli, mwingine anasema kwani Mungu hawezi kumuambia huyo mtumishi? Si kila mtumishi ni nabii. Nabii anaona anasikia kwa uwazi mno mambo ya ulimwengu wa roho. Na si kila kitu nabii pia huonyeshwa. Huyo nabii pia ni mtu anaweza ona na kusikia asielewe kabisaa.

Sasa fikiria wewe unayejua ukweli hauusemi unaficha. Unapokuwa mkweli fahamu ndipo unapowekwa huru mapema mnoo. Unapomueleza mtumishi dhambi yako au yenu iliyofungulia mlango wa pepo kuwafuatilia ni rahisi kufanya toba iliyonyooka.

Mnapofanya toba na kuachilia damu ya Yesu Kristo mahali palipokosewa ili iondoe hiyo dhambi ndipo uhalali wa hayo mapepo kukumiliki unapokosa nguvu  na yanapotolewa ni ngumu kuludi kwasababu hayana haki tena ya kukumiliki.

Ndiyo maana mkianza kufanya maombi ya toba tu utaona  mapepo yanaanza kupata shida mno mahali hapo. Nimeona mara nyingi tu. Mnapokuwa katika kusanyiko lenye watu wengi, mnapoanza kufanya maombi ya namna hiyo tu, usishangae kuona mapepo yanaanza kuangaika.

Mengine yatapiga kelele mengine kuanguka chini  yatafanya kila aina ya fujo. Toba ya kweli inamwondolea shetani uhalali wa kuwamiliki watu. Dhambi ndiyo chanzo kikubwa cha kumpa adui uhalali wa kummiliki mtu na kumtesa.

Naamini umenielewa. Angalia je! Kuna uhalali wowote umpao shetani kukumiliki? Tubia hapo. Mweleze huyo mtu anayekuombea nini unaona kinampa adui nafasi ya kukumiliki. Ndiyo itakuwa rahisi pepo kutoka au kutokukurudia.

Mungu akubariki sana

Wako

Mwl Steven & Beth Mwakatwila


  • 28-03-2019

Saturday, March 23, 2019

2⃣3⃣ MAMBO MUHIMU UNAYOTAKIWA UYAFANYE ILI UPATE KUISHINDA DHAMBI YA UZINZI

2⃣3⃣ MAMBO MUHIMU UNAYOTAKIWA UYAFANYE ILI UPATE KUISHINDA DHAMBI YA UZINZI

Na: MWL STEVEN & BETH MWAKATWILA

FUATANA NASI FACEBOOK

FUATANA NASI INSTAGRAM

KUPATA APP YETU “HUSONEMU (MWAKATWILA) APP”, BONYEZA LINK HAPA:

FUATANA NASI WHATSAPP

FUATANA NASI YOUTUBE
&
FUATANA NASI ONLINE RADIO

🗓 23 Machi, 2019

Bwana Yesu Kristo asifiwe. Nianze kwa kukuomba msamaha kwa sababu ni muda mrefu kidogo sikukuletea mfululizo wa somo hili.

Nimekuwa na mambo mengi kweli kweli sasa kuupata muda wa kukuandikia somo ndiyo inakuwa taabu kidogo. Nimeupata huu muda nimeona niiutumie kukuandikia na  kukuletea somo hili.

Katika kipindi kilichopita nilikuwa nakuonyesha  mlango wa pili wa tabia ya uzinzi nayo ilikuwa ni pepo au roho ya uzinzi.

Hebu tusogee mbele kidogo nataka kukuonyesha namna ya kufanya ili utoke kwenye tabia ya uzinzi iliyotokana na pepo.

NJIA YA KWANZA NI; KUTUMIA MAMLAKA MAALUMU YA KULITOA HILO PEPO MWILINI MWAKO.

Ikiwa unaona dalili zote za kuwa una roho au pepo la uzinzi mwilini mwako na unataka uondokane na hiyo tabia ya uzinzi njia ya kutoka hapo ni kulitoa hilo pepo mwilini mwako.

Fahamu pepo hilo ndilo linalozalisha hiyo tabia na ili hiyo tabia iondoke ni lazima ulitoe hilo pepo ndipo hiyo tabia utaicha.

Unaweza ukawa umeokoka kabisa lakini hiyo roho ukawa nayo kabisa. Wengi huhisi kama hawajaokoka vizuri. Sikiliza kuokoka ndiyo hatua ya kwanza ya kukamilishwa.
Unapookoka ndipo unaanza kutengenezwa mpaka kufikia utimilifu. Kwa maana hiyo unaweza kuokoka au kuupokea wokovu lakini ukawa bado na pepo tu.  

Mpaka utakapoanza kufundishwa na kukutana na watu waliotangulia katika huo wokovu waitwao watumishi  ambao watatumia mamlaka waliyopewa na Mungu ya kuwakamilisha hao waliookoka.

Na moja ya ukamilishaji wao ni huu wa kuyatoa hayo mapepo yaliyo ndani ya hao waaminio. Biblia inatufundisha hivi “Naye alitoa wengine kuwa mitume, na wengine kuwa manabii; na wengine kuwa wainjilisti na wengine kuwa wachungaji na waalimu; kwa kusudi la kuwakamilisha watakatifu, hata kazi ya huduma itendeke, hata mwili wa Kristo ujengwe;” (Waefeso 4:11-12)

Mungu anajua kuwa watakatifu au watu waliotengwa kwa ajili yake au waliochaguliwa si wakamilifu na wanahitaji kukamilishwa. Sasa angalia watu wengi wanaingia ndani ya wokovu wakiwa na tabia mbaya tu zingine zimebebwa kwenye mwili zingine zimewabana kwa kutumia roho au mapepo.

Kuongozwa sala ya toba au kubatizwa usifikirie kunaweza kuondoa pepo. Hili ni jambo muhimu sana ambalo unahitaji ulijue. Unaweza batizwa na pia kuongozwa sala ya toba lakini bado ukawa na pepo la uzinzi tu.

Pepo litamuachia mtu atakayefanyiwa huduma maalumu ya kulitoa hilo pepo kwa njia ya kuliamuru limtoke huyo mtu kwa kutumia jina la Bwana Yesu Kristo.

Bwana Yesu Kristo anatufundisha hivi. “Na ishara hizi zitafuatana na hao waaminio; kwa jina langu watatoa pepo; watasema kwa lugha mpya;” (Marko 16:17).’

Pepo anatolewa. Kama hakujafanyika kazi hiyo ya kumtoa hapo alipo fahamu atakuwepo tu, mpaka watu wajue kuwa kuna pepo au wafanye huduma maalumu ya kuyaamuru mapepo yaliyo ndani ya watu yawatoke ndipo unaweza ukashangaa hata watu ambao hukuwahi fikiria wana mapepo siku hiyo ukagundua kuwa walikuwa na mapepo.

Nakumbuka mwaka fulani nilisukumwa kufanya huduma maalumu ya namna hii kwa ajili ya wanakamati unajua kilichotokea? Mapepo yalilipuka kwa watu ambao hata sikuwafikiria.

Siyo kuwa hawajaokoka na hawampendi Bwana Yesu Kristo, mapepo yanaweza kabisa yakaja hata mahali watoto wa Mungu wamekusanyika. Unaweza kuniuliza kivipi.

Angalia mistari hii uone. “Ilikuwa, siku moja ambayo hao wana wa Mungu walikwenda kujihudhurisha mbele za BWANA, Shetani naye akaenda kati yao.BWANA akamwuliza Shetani, Umetoka wapi wewe? Ndipo Shetani akamjibu BWANA, na kusema, Natoka katika kuzunguka-zunguka duniani, na katika kutembea huku na huku humo. Kisha BWANA akamwuliza Shetani, Je! Umemwangalia huyo mtumishi wangu Ayubu? Kwa kuwa hapana mmoja aliye kama yeye duniani, mtu mkamilifu na mwelekevu, mwenye kumcha Mungu na kuepukana na uovu.Ndipo Shetani akamjibu BWANA, na kusema, Je! Huyo Ayubu yuamcha BWANA bure?” (Ayubu 1:6-9)

Ukiipitia hiyo mistari ndipo utanielewa vizuri au utaelewa kwa nini neno la Mungu linasema mpingeni shetani. Angalia hii mistari. “Basi mtiini Mungu. Mpingeni Shetani, naye atawakimbia. Mkaribieni Mungu, naye atawakaribia ninyi. Itakaseni mikono yenu, enyi wenye dhambi, na kuisafisha mioyo yenu, enyi wenye nia mbili.” (Yakobo 4:7-8)

Maandiko yanatufundisha kuwa watoto wa Mungu walipojihudhurisha mbele za Mungu shetani na yeye akaenda kati yao. Maana yake miongoni mwao kuna mtu ndani yake alimbeba  shetani kabisa. Unanielewa lakini?

Ngoja nijaribu tena kukuonyesha hili jambo. Maandiko yanasema mpingeni shetani naye atawakimbia mkaribieni Mungu naye atawakaribia. Fikiria kidogo hao wanaoambiwa wampinge ni watoto wa Mungu kabisa, kabla hawajamkaribia Mungu wanatakiwa wampinge kwanza shetani inamaana wale wana katika kipindi kile cha Ayubu hawakushughulikia jambo hilo walipomkaribia Mungu adui akawa kati yao.

Unajua hata kipindi kile cha Bwana Yesu yupo na timu yake ile shetani alijihudhurisha katikati yao kabisaa. Alikuwa ndani ya Yuda. Maandiko yanasema hivi. “Yesu akawajibu, Je! Mimi sikuwachagua ninyi Thenashara, na mmoja wenu ni shetani? Alimnena Yuda, mwana wa Simoni Iskariote; maana huyo ndiye atakayemsaliti; naye ni mmojawapo wa wale Thenashara.” (Yohana 6:70-71).

Bwana Yesu Kristo alilijua jambo hili kabisa kuwa katika ile timu yake shetani yupo lakini hakumpinga au kumtoa. Na kweli alikuja kumsaliti. Angalia kitu hiki labda utaelewa kuwa mapepo yanaweza kumwingia mtu aliyeokoka kabisaa angalia mfano huu.

“Yesu akajibu, akamwambia, Heri wewe Simoni Bar-yona; kwa kuwa mwili na damu havikukufunulia hili, bali Baba yangu aliye mbinguni. Nami nakuambia, Wewe ndiwe Petro, na juu ya mwamba huu nitalijenga kanisa langu; wala milango ya kuzimu haitalishinda. Nami nitakupa wewe funguo za ufalme wa mbinguni; na lo lote utakalolifunga duniani, litakuwa limefungwa mbinguni; na lo lote utakalolifungua duniani, litakuwa limefunguliwa mbinguni. Ndipo alipowakataza sana wanafunzi wake wasimwambie mtu ye yote ya kwamba yeye ndiye Kristo Tangu wakati huo Yesu alianza kuwaonya wanafunzi wake ya kwamba imempasa kwenda Yerusalemu, na kupata mateso mengi kwa wazee na wakuu wa makuhani, na waandishi, na kuuawa, na siku ya tatu kufufuka. Petro akamchukua, akaanza kumkemea, akisema, Hasha, Bwana, hayo hayatakupata. Akageuka, akamwambia Petro, Nenda nyuma yangu, Shetani; u kikwazo kwangu; maana huyawazi yaliyo ya Mungu, bali ya wanadamu.” (Mathayo 16:17-23).

Ukiipitia hiyo mistari utagundua Bwana Yesu Kristo alilitoa pepo au shetani aliyekuwa ndani ya Petro. Petro alishakuwa amepewa taarifa kuwa atapewa ufunguo au mamlaka kubwa sana katika ufalme wa Mungu. Petro huyo huyo shetani alimwingia.

Hebu jiulize swali Bwana Yesu alikuwepo shetani akamwingia Petro je! Asingefanya huduma ya kumtoa huyo shetani Je? Petro angeondolewa huyo shetani kisa eti ni mtumishi au ameokoka? Bwana Yesu Kristo hakumkemea  shetani au pepo aliyekuwa ndani ya Yuda kwa sababu alikuwa anataka kutimiza maandiko katika habari za kusalitiwa kwake.

Naamini kama isingekuwa hivyo angemkemea au kumtoa shetani ndani ya Yuda. Naamini umenielewa sasa ninavyokuambia kuwa tatizo kubwa ambalo watu wengi wanalo ni hili la kutokufanyiwa maombi mara kwa mara ya kuondolewa mapepo yaliyo ndani yao.
Biblia inatufundisha kuwa moja ya kazi ambayo Bwana Yesu Kristo alikuwa akiifanya ni kuyatoa mapepo yaliyo ndani ya watu.

Angalia mistari hii. “Hata kulipokuwa jioni, wakamletea wengi wenye pepo; akawatoa pepo kwa neno lake, akawaponya wote waliokuwa hawawezi, ili litimie lile neno lililonenwa na nabii Isaya, akisema, Mwenyewe aliutwaa udhaifu wetu, Na kuyachukua magonjwa yetu.” (Mathayo 8:16-17)

Angalia na mistari hii  “na wanawake kadha wa kadha ambao walikuwa na pepo wabaya na magonjwa wakaponywa; nao ni Mariamu aitwaye Magdalene aliyetokwa na pepo saba,” (Luka 8:2)

Ukiipitia hiyo mistari utagundua kuwa moja ya kazi aliyokuwa anaifanya Bwana Yesu Kristo ni hii ya kukemea au kuyaondoa mapepo yaliyo ndani ya miili ya watu.  Kazi hii hata leo hii Bwana Yesu Kristo anataka kuona ikiendelea kufanywa. Ndiyo maana anasema hivi. “Akawaita wanafunzi wake kumi na wawili, akawapa amri juu ya pepo wachafu, wawatoe, na kupoza magonjwa yote na udhaifu wa kila aina.” (Mathayo 10:1)

Maandiko yanasema waliopewa wajibu wa kuyatoa hayo mapepo ni wanafunzi. Unaposoma neno wanafunzi lina utofauti sana na ukisoma neno mitume. Unaweza ukawa mwanafunzi lakini usiwe mtume. Watu wengi hawajui kuwa unapofanyika kuwa mwanafunzi tu wa Bwana Yesu Kristo kwa kumpokea na kumwamini kama Bwana kwako unapewa hii nafasi ya kuyatoa mapepo yaliyo ndani ya watu.

Tatizo tulilonalo ni mfumo uliopo ndani ya kanisa. Wanafunzi wa Bwana Yesu hawaandaliwi hawakufundishwa mambo kama haya. Biblia inasema “Basi, enendeni, mkawafanye mataifa yote kuwa wanafunzi, mkiwabatiza kwa jina la Baba, na Mwana, na Roho Mtakatifu; na kuwafundisha kuyashika yote niliyowaamuru ninyi; na tazama, mimi nipo pamoja nanyi siku zote, hata ukamilifu wa dahari.” (Mathayo 28:19-20).

Moja ya jambo Bwana Yesu Kristo katuamuru tulifanye ni hili la kuyatoa mapepo. Sasa angalia kama wanafunzi leo hii wamefundishwa jambo hili. Ndiyo maana utaona wanafunzi wengi wa Bwana Yesu Kristo na watu wengine wasio wanafunzi wamebanwa na mapepo ya uzinzi.

Sikiliza mwanafunzi wa Bwana Yesu Kristo anapoona mwanafunzi mwenzake ana dalili za roho au pepo ndani yake ilitakiwa yeye ndiye alishughulikie hilo pepo. Sasa siku hizi mpaka akatafutwe mtume au nabii.

Amri ya kutoa pepo walipewa hata wanafunzi, siyo manabii au waalimu au wachungaji au wainjilisti au mitume tu. Wakifundishwa hao wanafunzi wakaamini kuwa wanayo hayo mamlaka nakuambia ukweli watayatoa mapepo mengi tu yaliyo ndani ya watu.

Ili kukabiliana na tabia ya uzinzi iliyoletwa na pepo lazima pepo hilo au mapepo hayo yatolewe ndani ya mtu huyo, kinyume cha hapo atakuwa mzinzi tu hata awe mwimbaji au mwombaji nk.

Ikiwa unaona dalili kama hizi tafuta wanafunzi wenzio wa Bwana Yesu Kristo au watumishi wenye ufahamu walitoe hilo pepo likitoka tu fahamu tabia ya uzinzi iliyoletwa na pepo itakuacha.

Mungu akusaidie na kukuongoza vema katika hatua hii. Katika somo lijalo nitakuonyesha sababu ya watu wengine kurudiwa na mapepo baada ya kutolewa ndani yao.

Ukihitaji masomo yetu unaweza kuyapata kwa njia hizi zifuatazo:-

1. Tovuti yetu ya www.mwakatwila.org

2. YouTube - Mwakatwila au HUDUMA YA SOMA NENO LA MUNGU (HUSONEMU).

3. Facebook ingia katika hiyo tovuti au website yetu utaona alama ya facebook(f) like na utapata maelezo ya kujiunga au ingia Facebook halafu andika  “SOMA NENO LA MUNGU”

4. Instagram ingia Instagram app halafu andika “Steven Mwakatwila”

5. DVDs 📀 au CDs 💿

6. VITABU.
NB: Wasiliana na Mhudumu ofisini kwa namba +255 (0) 763 109 733, kupata VITABU, DVD & CD.

7. Kwa njia ya REDIO:- Utapata mafundisho yetu kwa redio zifuatazo:-
➖Rungwe FM 102.5 Kila siku ya Jumapili  saa tatu mpaka saa nne usiku.
➖Baraka FM 107.7 Kila siku ya Jumanne saa kumi na mbili jioni mpaka saa moja usiku.
➖Bomba FM 104.1 Kila siku ya Ijumaa saa tatu usiku mpaka saa nne usiku.

8. Unaweza kutupata kwenye ONLINE RADIO yetu:-  radio.mwakatwila.org

Kwa Mawasiliano zaidi Utatupata kwa namba hizi:-
+255 (0) 754 849 924 Au +255 (0) 756 715 222

Wako
Mwl Steven & Beth Mwakatwila.
23/03/2019

Wednesday, March 13, 2019

2⃣2⃣ MAMBO MUHIMU UNAYOTAKIWA UYAFANYE ILI UPATE KUISHINDA DHAMBI YA UZINZI

2⃣2⃣ MAMBO MUHIMU UNAYOTAKIWA UYAFANYE ILI UPATE KUISHINDA DHAMBI YA UZINZI

Na: MWL STEVEN & BETH MWAKATWILA

KUPATA APP YETU “HUSONEMU (MWAKATWILA) APP” BONYEZA LINK HII HAPA:

FUATANA NASI:- KWENYE APP, FACEBOOK, INSTAGRAM, ONLINE RADIO 📻, WHATSAPP, WEBSITE & YOUTUBE, Kwa links zilizoko kwenye HII LINK hapa:

🗓 13 Machi, 2019

Bwana Yesu Kristo asifiwe sana. Naamini unaendelea vizuri mimi na familia yangu hatujambo tunamshukuru Mungu atutunzaye na kutupigania.

Nakuletea mwendelezo wa hili somo nililokuahidi kukufundisha ili upate ufahamu wa namna unavyoweza kuishinda dhambi ya uzinzi.

Katika somo lililopita nilikuonyesha  mlango au chanzo cha saba ambacho kinaweza kuwa mlango wa pepo kumwingia mtu.

Hebu tusogee mbele nikuonyeshe chanzo kingine kinachoweza kufungulia mlango wa mtu kuingiliwa na pepo hasa la uzinzi nacho ni

CHANZO CHA NANE NI; TABIA MBAYA YA KUFANYA UZINZI AU UASHERATI

Sikiliza ikiwa wewe ni mtu mwenye tabia ya uzinzi fahamu ni rahisi sana kuvamiwa na pepo la uzinzi.

Fahamu linaitwa pepo la uzinzi, sasa kama mwili wako huo wewe mwenyewe umeshindwa kuudhibiti katika eneo la kuzipinga tamaa zake na moja ya tamaa ya mwili ni uzinzi, fahamu kwa kupitia hiyo tabia ya uzinzi iliyobebwa mwilini mwako  pepo la uzinzi linaweza itumia hiyo tabia kukuingia ili kukufanya uwe mzinzi kweli kweli.

Unajua unapofanya uzinzi au unapojamiiana na mtu awe wa kike au kiume  usifikiri ni mwili wako tu unaolifanya hilo tendo, fahamu hata roho inashiriki. Maandiko yanasema hivi “Watu wangu hutaka shauri kwa gongo lao, na fimbo yao huwahubiri mambo; maana roho ya uzinzi imewakosesha, nao wamekwenda kuzini mbali na Mungu wao.” (Hosea 4:12).

Angalia maandiko yanasema roho ya uzinzi imewakosesha. Hiyo roho si mwili, kwa mujibu wa hiyo mistari tunapata ufahamu kuwa kuna ushirika kabisa wa roho ya mtu au mapepo katika suala zima la mtu kufanya ngono.

Ukilijua hili ni rahisi sana kuelewa pia mistari hii isemayo “Je! Hamjui ya kuwa miili yenu ni viungo vya Kristo? Basi nivitwae viungo vya Kristo na kuvifanya viungo vya kahaba? Hasha! Au hamjui ya kuwa yeye aliyeungwa na kahaba ni mwili mmoja naye? Maana asema, Wale wawili watakuwa mwili mmoja. Lakini yeye aliyeungwa na Bwana ni roho moja naye. Ikimbieni zinaa. Kila dhambi aitendayo mwanadamu ni nje ya mwili wake; ila yeye afanyaye zinaa hutenda dhambi juu ya mwili wake mwenyewe. Au hamjui ya kuwa mwili wenu ni hekalu la Roho Mtakatifu aliye ndani yenu, mliyepewa na Mungu? Wala ninyi si mali yenu wenyewe;” (1 Wakorintho 6:15-19)

Ukisoma hiyo mistari utagundua kuna mahusiano makubwa kati ya mwili na roho katika eneo hili la tendo la ndoa. Mwili huu unamilikiwa na roho yako na Roho Mtakatifu angalia sasa ikiwa wewe unafanya zinaa fahamu ni rahisi zaidi roho au pepo la uzinzi likaumiliki mwili wako kwa sababu unapofanya hilo tendo hata roho yako ina sehemu ya ushiriki wa tendo hilo.

Roho Mtakatifu anapoumiliki mwili wa mtu fahamu hatapenda kuona mtu huyo anafanya uzinzi, kwa sababu Roho Mtakatifu ametupa utaratibu wa kuoa na kila mtu alieoa kwa kufuata utaratibu anapolifanya hilo tendo mwili wake hauwi najisi kwa sababu kalifanya kihalali.

Mtu anapolifanya hilo tendo nje ya utaratibu fahamu anaungana na mwili wake na huyo anayefanya naye hicho kitendo, sasa hebu fikiri huyo unayeungana naye anapepo la ngono au uzinzi?

Sikiliza watu wengine hujikuta wakiungana na roho mbaya au pepo la uzinzi kwa kupitia kujamiana au kuzini tu. Si mnakuwa hapo mnaachana na Roho Mtakatifu aumilikie mwili wako?

Unakuwa unakaribisha mmiliki mwingine wa mwili naye ni shetani. Shetani hawezi kujigawa na kuwa ndani ya kila mtu anachofanya ni kuyatuma mapepo ili yawaingie watu hao waliofanya maamuzi ya kuzini na kumwondolea Roho Mtakatifu uhalali wa kuimiliki miili yao wanakuwa wanaungana na hao wazinio na ni rahisi sana hapo kujikuta unaungana au kupokea roho au pepo la uzinzi.

Sikiliza watu wengi wanaofanya tendo la ndoa kinyume cha maumbile au wale wanaosagana au kufanya punyeto unajua wanakuwa katika hatari kubwa sana tena mnooo kuvamiwa na pepo hili la uzinzi.

Watu wengi walio na mapepo mbalimbali unapowauliza mfumo wa maisha yao hasa eneo hili la uzinzi utashangaa wengi waliingiliwa walipoanza kuzini na kuzini kwa mitindo hiyo ya kunyume cha maumbile au kusagana au  ushoga au kufanya punyeto.
Sikikiza nikuambia ibada za kishetani au ibada za kipagani unajua ndani ya hizo ibada wanaruhusu watu kuyafanya hayo.

Unajua ni kwanini wanafanya zinaa? Sikiliza wanafanya hivyo ili kuyafungulia mlango mapepo  au mashetani kuwaingia.

Kama unafikiri nakutania wewe fuatilia mahali popote ambapo kunafanyika mambo mabaya angalia mazingira hayo utagundua ni mazingira yanayojengwa ili kuchochea mno uzinzi.

Wewe nenda kwenye mikusanyiko yoote ya ibada za kishetani utaona huko watu wanakaa uchi au nusu uchi ili tu kuwatengenezea hao walioko hapo tamaa ya uzinzi tu.

Angalia wanavyocheza, angalia wanavyosema angalia wanavyotazamana, angalia wanavyokaa utaona ni kuchochea uzinzi tu angalia nyimbo zao wanazoimba ni mapenzi tuu na kuchochea uzinzi tuuu.

Unajua ni kwa nini uzinzi ndiyo unachukua nafasi ya kwanza hapo? Ni kwa sababu ndiyo mlango unaoyaruhusu mapepo kuwaingia hao watu na kuwatawala na kuwatengenezea tabia mbaya.

Mungu anapotuambia kuwa miili yenu ni hekalu la Roho Mtakatifu, ikimbieni zinaa anajua kabisa kuwa ukiendekeza zinaa tu mwili wako hauwi tena hekalu la Roho Mtakatifu unakua hekalu la mapepo.

Shetani akitaka kukuharibia masomo, biashara, kazi, heshima yako utumishi wako unajua atakachokifanya ni kukusukuma mnoo uingie kwenye tabia ya uzinzi tu, akikupata hapo amekupiga pakubwa mnoo.

Ndiyo njia anayoweza kukuingizia mapepo yatakayokuvurugia mnooo. Hata kama hajakuingia lakini yatakujeruhi tuuuu nakuambia.

Yatajeruhi ndoa kama si kuiua, yatajeruhi akili kama si kuziua nk. Biblia inasema hivi “Je! Mtu aweza kuua moto kifuani pake, Na nguo zake zisiteketezwe?Je! Mtu aweza kukanyaga makaa ya moto, Na nyayo zake zisiungue? Ndivyo alivyo aingiaye kwa mke wa jirani yake; Kila mtu amgusaye huyo atakuwa na hatia. Watu hawamdharau mwivi, Akiiba ili kujishibisha, iwapo aona njaa;Lakini akipatikana, atalipa mara saba; Atatoa mali yote ya nyumba yake. Mtu aziniye na mwanamke hana akili kabisa; Afanya jambo litakalomwangamiza nafsi yake.Atapata jeraha na kuvunjiwa heshima; Wala fedheha yake haitafutika.” (Mithali 6:28:33)

Ukiipitia hiyo mistari utaona namna shetani anavyowajeruhi watu kwa kupitia uzinzi tu. Mapepo yanapomtafuta mtu ili yamjeruhi au kumtesa au kumharibia yanaweza mtegea kwenye kona hiyo ya uzinzi tu.

Ngoja nikuambie kitu unaweza usikaliwe na hilo pepo la uzinzi baada ya kuzini, lakini litaacha jeraha fulani tu. Lazima likutandike tu, dhambi ni dhambi iwe uongo nk. Lakini hazifanani kwenye eneo la madhara yake.

Uzinzi unamadhara makubwa mnoo nakuambia. Watu wengi wamejeruhiwa we acha tu. Siku moja Roho Mtakatifu   alinifundisha ni kwa nini au nini chanzo cha ndoa nyingi leo kuingia kwenye migogoro. Unajua chanzo kikubwa ni jeraha hili la uzinzi?

Wanandoa wengi mno chanzo kikubwa  cha ugomvi wao kimefungwa hapo tu. Utasikia ohooo mume wangu au mke wangu si mwaminifu. Maana yake anakuambia jeraha la ndoa yako ni zinaa aliyoifanya mke wangu au mume wangu.

Sikiliza wengi hapo huachana wengine hutengana. Pepo la uzinzi ni haribifu kweli kweli wa ndoa za watu. Ukigundua kuwa kuna jeraha yaani huwezi samehe una uchungu mnoo anza kuliona hilo pepo kwanza kabla ya kumwangalia mumeo au mkeo.
Usipokaa vizuri tu usishangae litakuvamia na wewe utaanza ghafla kufikiri kutoka kwenye ndoa yako ili ukazini nje ya ndoa. Unafikiri mawazo hayo chanzo chake ni nini? Ni hilo pepo tu linakutengenezea wewe tabia hiyo hiyo ya uzinzi.

Ndiyo hapo kesho unasikia mke wa fulani mzinzi, unamwuliza anasema ALIANZA YEYE KUTOKA NJE YA NDOA NA MIMI NIKAFUATA!!!! Au utaona pepo anakushauri achana na mumeo dai talaka au achana na mkeo dai talaka ili ukaolewe au kuoa mwingine. Aisee ee kumbe unasakiziwa hapo tabia ya uzinzi tu.

Usipolitazama pepo utamtazama mkeo au mumeo na mtaachana au kutengana tu. Ikimbie zinaa ili pepo la uzinzi au roho ya uzinzi usiipe nafasi ya kukuingia au kukujeruhi.
Angalia watu wengi leo hii wametoa mimba kisa uzinzi angalia alivyojeruhiwa, wengine hawana watoto na usishangae hawatapata kabisaa kisa pepo hili tu limewatengenezea jeraha baya kweli, liliwaingiza kwenye zinaa likawashauri watoe likawapigia hapohapo.
Fuatilia maisha ya watu walioua kwa kutoa mimba. Utashangaa ni watoro usoni pa ardhi, wanaishi maisha ya ajabu ajabu kama watu wasio na kikao duniani. Hawana amani kabisaa, waliotubu wamejikuta wamekaa na fadhaiko maisha yao yoote.

Unajua ukijeruhiwa ukipona jeraha unabaki na kovu kulingana na kiwango cha jeraha kilivyokuwa. Fikiria ulizini halafu ukapata mimba ukaitoa na unaishi bila mtoto au kuolewa au kuoa?

Ni sawa umetubu dhambi hiyo lakini kovu litakuwepo tu yaani kumbukumbu zitakuja tu, utafikiria aisee nisingezini yasingenikuta haya, aisee nisingetoa ileee mimba huenda ningekuwa na mtoto anayenifariji leo.

Hali hiyo ndiyo inayoitwa fedheha isiyofutika. Naona unanielewa sasa ninapokuambia kuhusu mlango huu wa zinaa unavyoweza kupitisha roho mbaya au mapepo ya uharibifu katika maisha ya mtu.

Siku moja nilikuwa nawaza namna ya watu wengi niliokuwa nao wakike na wakiume yaani niligundua wengi wamekufa hawapo. Na walikufa na umri mdogo sana. Kisa uzinzi tu.
Nilianza kuangalia fulani nini kilimuua niligundua ni UKIMWI tu, chanzo ni mlango huu huu tu. pepo la mauti lilipitia mlango huu kuwa walipolifungulia mlango wa kwa kuzini tu. Kila mtu atakufa, lakini wengine wanakufa kwa sababu mwili umechakaa tu.

Biblia inasema UMEISHA NGUVU ZAKE!!!! Na nguvu hizo huisha kutokana na UMRI WAPENDWA? Maandiko yanasema sabini kwa themanini.

Sasa angalia hao ninaowazungumza ni wengi mnoo, unaweza kusema unajuaje walikufa kwa UKIMWI? Sikiliza UKIMWI haunaga siri upo wazi hata watu waseme ni kisukari watu watajua si figo ni UKIMWI. Ninavyosema hivi usifikiri nafurahia.

Najisikia huzuni sana moyoni mwangu. Naona namna ya watu wengi tunakosa siri hizi na adui anawaangamiza kirahisi sana kwa kupitia tendo la zinaa la dakika kumi tu.
Ikimbie zinaa mpendwa yaani usijiamini wala kuiendekeza tabia hii utapata jeraha au mapepo yatakuingia tu. Biblia inasema usiwaendee wenye pepo na kuzini nao. “Na mtu yule atakayewaendea wenye pepo, na wachawi, ili kuzini pamoja nao, nitakaza uso wangu juu ya mtu yule, nitamtenga na watu wake.Jitakaseni basi, iweni watakatifu, kwa kuwa mimi ndimi BWANA, Mungu wenu.” (Mambo ya Walawi 20:6-7).

Ukiipitia hiyo mistari utapata tafsiri nyingi tu, moja ya tafsiri ni kitendo cha kuyauliza mapepo au kuongozwa na mapepo mbele za Mungu ni sawa na uzinzi. Lakini tafsiri nyingine ni hii ninayokuambia kuwa unapozini unaungana na yule mtu.

Sasa sikia, unapozini na mtu mwenye pepo ni rahisi ukajikuta unajiunganisha na hayo mapepo aliyonayo. Fahamu si kila mtu aliyewahi kuzini basi kapokea mapepo hapana nasema ni rahisi kuyapokea.

Ila unapozini fahamu hayo mapepo yasipokuingia lazima tu yatakuwa yamekujeruhi mahali fulani. Kama siyo ugonjwa basi ni jeraha la ndoa kuvunjika, akili kupigwa au kutoaminika.

Wewe fanya uzinzi leo hii huku ukiwa umeokoka utashangaa utatubu, lakini jeraha lako fahamu hautaaminika. Ukihubiri watasema leo yule mwanamke amehubiri sana usishangae mmoja atauliza yupi? Watasema yule mzinzi.

Ukisikia hivyo jipe moyo tu ni sehemu ya kovu, wewe sogea mbele. Lakini kwa nini ujitengenezee haya yooote? IKIMBIE ZINAA nakuambia.

Unajua hata ndani ya ndoa. Ukizini ukatubu fahamu umejitengenezea jeraha au kovu la kutokuaminika nakuambia. Mungu atakuamini ila watu au huyo mumeo au mkeo usishangae hakuamini tena.

Ukichelewa tu atafikiri ulipitia koloni lako hilo. Ngoja nikupe mfano huu. Kuna wanandoa walipokuwa wanaingia kuoana walizini, na hawataki kutubu au kutengeneza, unajua kwa kutokutubu kwao tu, ndipo mapepo yanapopata mlango wa kuwabamizia hapo hapo.

Nakushauri usizini na huyo mchumba wako, pepo litawaletea madanganyo kuwa si mtaoana? Sawa mtaoana lakini fahamu tendo hilo lisipotengenezwa tu, adui atawapigia kwa kutumia mlango huo huo.

Anaweza huko mbele yenu akaivunja hiyo ndoa msishangae hamuelewani, mnagomba wee hamaminiani, sikiliza mwenzio atakuaminije wakati mnaficha siri ya uzinzi mlioufanya? Shetani atautumia mlango huo kuwanong’oneza moja moja kuwa huyu mzinzi anaficha kama mlivyoficha uzinzi mlioufanya nyuma si mwaminifu huyu.

Hapo hapo maelewano kwenu yanaanza kuvunjika. Akichelewa sokoni nafsi iliyojeruhika inakuambia si uliwahi zini naye? Kwanza ulimkuta bikira? Eheheee!! Akirudi tu mkeo ugomvi, wivu nk mwisho ndoa kuvunjika.

Ikimbie zinaa. Vunja mahusiano mabaya na mwanaume au mwanamke yeyote yule. Kama unataka kumuoa muoe kihalali, usikubali mwanaume anayekushawishi uzini naye, mwanaume wa namna hiyo ni hatari kwako hebu jipange vizuri. Msichana anayejileta kwako na unaona wazi anataka uzini naye nakushauri mkimbie ni hatari kwako.

Kama uliwahi zini na huyo mumeo au mkeo kabla hamjaoana mkiwa kwenye uchumba nawashauri mkaufunge mlango huo mapema kwa toba, ungameni hiyo dhambi yenu.
Naamini umenielewa.

Ukihitaji masomo yetu unaweza kuyapata kwa njia hizi zifuatazo:-

1. Tovuti yetu ya www.mwakatwila.org

2. YouTube - Mwakatwila au HUDUMA YA SOMA NENO LA MUNGU (HUSONEMU).

3. Facebook ingia katika hiyo tovuti au website yetu utaona alama ya facebook(f) like na utapata maelezo ya kujiunga au ingia Facebook halafu andika  “SOMA NENO LA MUNGU”

4. Instagram ingia Instagram app halafu andika “Steven Mwakatwila”

5. DVDs 📀 au CDs 💿

6. VITABU.
NB: Wasiliana na mhudumu ofisini kwa namba +255 763 109 733, kupata VITABU, DVD & CD.

7. Kwa njia ya REDIO:- Utapata mafundisho yetu kwa redio zifuatazo:-
➖Rungwe FM 102.5 Kila siku ya Jumapili  saa tatu mpaka saa nne usiku.
➖Baraka FM 107.7 Kila siku ya Jumanne saa kumi na mbili jioni mpaka saa moja usiku.
➖Bomba FM 104.1 Kila siku ya Ijumaa saa tatu usiku mpaka saa nne usiku.

8. Unaweza kutupata kwenye ONLINE RADIO yetu:-  radio.mwakatwila.org

Kwa Mawasiliano zaidi Utatupata kwa namba hizi:-
+255 754 849 924 Au +255 756 715 222

Wako
Mwl Steven & Beth Mwakatwila.
13/03/2019