2⃣1⃣ MAMBO MUHIMU UNAYOTAKIWA UYAFANYE ILI UPATE KUISHINDA DHAMBI YA UZINZI
Na: MWL STEVEN & BETH MWAKATWILA
FUATANA NASI:- KWENYE APP, FACEBOOK, INSTAGRAM, ONLINE RADIO 📻, WHATSAPP, WEBSITE & YOUTUBE, Kwa links zilizoko kwenye HII LINK hapa:
KUPATA APP YETU “HUSONEMU (MWAKATWILA) APP” BONYEZA LINK HII HAPA:
🗓 10 Machi, 2019
Bwana Yesu Kristo asifiwe sana. Nimeupata huu muda nimeona niutumie kukuletea somo. Katika kipindi kilichopita nilikuonyesha njia ya sita ambayo inaweza kuwa chanzo cha mtu kuvamiwa na mapepo.
Nacho kilikuwa ni kuwepo mahali penye uwepo mbaya usio na hofu ya Mungu. Nataka ni kuonyeshe chanzo kingine
NJIA YA SABA; NI KUINGILIWA NA ROHO MBAYA KWA KUTUMIA NDOTO.
Sina nia ya kukufundisha somo linalohusu ndoto. Ni somo lingine kabisa tena refu kweli kweli. Ninachotaka kukuonyesha ni namna mtu anavyoweza kujikuta ameingiliwa na mapepo.
Moja ya mlango ambao adui anaweza kuutumia na kumwingia mtu kabisa ni kwa kutumia mlango huu wa ndoto. Ndoto ni mlango mkubwa wa mawasiliano halisi kati ya mwanadamu na ulimwengu wa roho.
Mungu aliamua kuutengeneza mlango huo ili awe na mawasiliano kati ya ufalme wake na mtu aliyeko duniani.
Kumbuka sisi tumeumbwa na Mungu tuishi katika maeneo mawili yaani katika ulimwengu huu wa mwili na pia katika ulimwengu wa roho. Ili mtu yaani roho aingie katika ulimwengu wa roho na aishi huko lazima atoke katika ulimwengu wa mwili.
Sasa hapo kuna mambo mawili moja afe au alale (nusu kifo) ngoja nikuchekeshe unapolala fahamu hapo unafanya zoezi la kufa. Unapokuwa umelala roho yako nikuambie hailali ila mwili ndiyo unaolala, roho yako inakuwa MACHO TU.
Roho yako inakuwa katika ulimwengu wa roho. Sasa huko ndiko unakoweza kukutana na roho zingine nyingi tu. Ziwe za Malaika, mapepo na hata Mungu unaweza kukutana naye kabisa.
Tatizo kubwa tulilonalo ni mfumo wa ulalaji wetu tu. Watu wengi hulala ili kupumzisha mwili, sikiliza nikuambie watu wengine hawalali ili wapumzishe mwili tu.
Hulala wakijua wanaenda katika ulimwengu wa roho kabisa na huenda wakawa na kazi maalumu huko na wakaitekeleza kabisa na kupokea taarifa na kurudi tena katika ulimwengu huu wa mwili.
Umewahi kufikiria namna wachawi na wakuu wa giza wanavyoutumia usingizi? Wanapolala wengine ndipo wanapoingia kwenye ulimwengu wa roho na kwenda kuziharibu roho za watu wengine mpaka miili yao na hata vitu vyao.
Ngoja nikuambie kitu, kuna watu au mtu akilala huwezi kumwamsha mpaka aamke mwenyewe. Watu wa namna hiyo mara nyingi roho zao huwa mahali zikitumika kabisaa nakuambia.
Kama si mchawi basi hutumikishwa mahali na hao wachawi. Sikuambii utani, kuna mtu akilala hata mmwagie maji haamki, mmchape haamki, yaani unagundua kabisa kuwa huyu hayupo hapa kuna mahali yupo. Akiamka mwulize vipi, hana jibu la kukujibu..
Ngoja nikuchekeshe haujawahi kusikia kuwa watu wa namna hiyo eti nasema eti kwa sababu sina uhakika kuwa ni kweli. Ukimgeuza au kumtoa mahali alipokuwa amelala ndiyo haamki tena. Yaani anakufa huku jasho linamtoka.
Ukikutana na mtu wa namna hiyo usije ukafanya majaribio usishangae ni kweli akapitiliza Eheheee!! Fikiria ni kweli akafa unajua nafsi yako itapata shida miaka yako yote utakayoishi.
Sikiliza ulimwengu wa roho ni halisi kabisa huko kuna roho za aina mbalimbali, sasa unapolala unaingia huko, unayoyaona huko na kuyatenda huko na kuyasikia huko yanaitwa ndoto. Usishangae mengi unayoyaota ni mambo ya kweli kabisaaa mpendwa.
Sasa sikia. Shetani anaiga kila kitu kutoka kwa Mungu, na yeye anaweza kuutumia mlango huo huo wa ndoto yaani akakutegea ndotoni kabisa na kukujilia au kukuingia ukiwa ndotoni.
Ngoja nikupe mifano hii naamini utapata ufahamu namaanisha nini. Angalia mistari hii. “Lakini Mungu akamjia Abimeleki katika ndoto ya usiku, akamwambia, Umekuwa mfu wewe kwa sababu ya mwanamke huyu uliyemtwaa, maana ni mkewe mtu” (Mwanzo 20:3).
Angalia hapo kwa kutulia. Maandiko yanasema Lakini Mungu AKAMJILIA ABIMELEKI KATIKA NDOTO. Maandiko yanatufundisha kuwa Mungu alimjilia Abimeleki katika ndoto. Ninapokuambia kuwa unapolala ndipo unaingia katika ulimwengu wa roho na huko unajiliwa na Mungu kabisa sikosei.
Si kujiliwa tu na Mungu pia unaweza kuzungumza naye kabisa mkabishana kabisa. Angalia mistari hii uone. “Lakini Mungu akamjia Abimeleki katika ndoto ya usiku, akamwambia, Umekuwa mfu wewe kwa sababu ya mwanamke huyu uliyemtwaa, maana ni mkewe mtu. Basi Abimeleki alikuwa hakumkaribia, akasema, Ee Bwana, Je! Utaua hata taifa lenye haki? Je! Hakuniambia mwenyewe, Huyu ni ndugu yangu? Na mwanamke mwenyewe naye alisema, Huyu ni ndugu yangu. Kwa ukamilifu wa moyo wangu, na kwa kuwa safi mikono yangu, nimefanya hivi. Mungu akamwambia katika ndoto, Nami nimejua ya kwamba kwa ukamilifu wa moyo wako umefanya hivi, ndipo nami nikakuzuia usinitendee dhambi, kwa hiyo sikukuacha umguse. Basi sasa umrudishe mwanamke kwa mtu huyo, maana yeye ni nabii, naye atakuombea, upate kuishi. Bali usipomrudisha, fahamu ya kwamba kwa hakika utakufa wewe na watu wote ulio nao.” (Mwanzo 20:3-7).
Unapoisoma hiyo mistari utagundua ndoto si kitu cha mchezo. Abimeleki alijiliwa na Mungu kabisa wakazungumza kabisa akauliza maswali akajibiwa akapewa angalizo na maelekezo ya kufanya kabisaa. Jiulize swali, walikutania wapi? Jibu ni rahisi tu katika ulimwengu wa roho.
Mungu ni Roho anaishi katika ulimwengu wa roho ili akutane na roho ya mtu lazima hiyo roho iingie kwenye ulimwengu wa roho na ndipo wakutane huko na Mungu aliye Roho.
Ngoja nikuonyeshe na mstari huu uone “Mungu akamjia Labani, Mshami, katika ndoto ya usiku, akamwambia, Ujihadhari, usimwambie Yakobo neno la heri wala la shari.” (Mwanzo 31:24)
Umeona hicho kitu? Mungu alimjia Labani kwa kupitia mlango huu uitwao ndoto. Alimjia akamwonya kabisa na Labani alijua kabisa na alielewa kabisa kuwa kajiliwa na Mungu.
Angalia na huu mstari huu,
“Na malaika wa Mungu akaniambia katika ndoto, Yakobo! Nikasema, Mimi hapa.” (Mwanzo 31:11). Ukiisoma hiyo mistari utanielewa ninapokuambia unapolala unaingia katika ulimwengu wa roho ambako huko unaweza kukutana na roho za aina mbalimbali.
Yakobo hapo anatuambia alipolala ndotoni akakutana na malaika wa Mungu na malaika huyo alimwambia mambo fulani Yakobo. Angalia maandiko hayasemi kuwa Yakobo alijiliwa na Mungu yanasema alikutana na malaika wa Mungu.
Kuna utofauti na hiyo mistari miwili niliyokuonyesha mwanzo ya Abimeleki na Labani hao walijiliwa na Mungu. Yakobo alijiliwa na malaika wa Mungu kumbuka malaika ni roho na Mungu ni Roho na hao watu wana roho na mwili ili wapate mawasiliano katika ulimwengu wa roho iliwalazimu walale na waote ndoto. Sasa naona umeanza kunielewa.
Angalia tena hii mistari. “Basi, nililetewa neno kwa siri, Sikio langu likasikia manong’ono yake. Katika mawazo yaliyotoka katika maono ya usiku, Hapo usingizi mzito uwaangukiapo wanadamu. Hofu iliniangukia na kutetema, Iliyoitetemesha mifupa yangu yote. Ndipo pepo ilipita mbele ya uso wangu; Na nywele za mwili wangu zilisimama. Hiyo pepo ilisimama kimya, nisiweze kutambua sura zake, Mfano ulikuwa mbele ya macho yangu; Kulikuwa kimya, nami nilisikia sauti, ikinena, Je! Binadamu atakuwa na haki kuliko Mungu? Je! Mtu atakuwa safi kuliko Muumba wake? Tazama, yeye hawategemei watumishi wake; Na malaika zake huwahesabia upuzi; Je! Si zaidi sana hao wakaao katika nyumba za udongo, Ambazo misingi yao i katika mchanga, Hao waliosetwa mbele ya nondo! Kati ya asubuhi na jioni huvunjwa-vunjwa; Waangamia milele wala hapana atiaye moyoni. Je! Kamba ya hema yao haikung’olewa ndani yao? Wafa, kisha hali hawana akili.” (Ayubu 4:12-21).
Ukiipitia hiyo mistari utagundua kuwa Ayubu alilala usingizi akaona na kusikia pepo likizungumza na aliliona kabisa ingawa sura ya hilo pepo hakuitambua ila aliona.
Pepo hilo lilimjilia Ayubu kwa kupitia usingizi, alilala akaona.
Maandiko yanasema hivi. “Basi, nililetewa neno kwa siri, Sikio langu likasikia manong’ono yake. Katika mawazo yaliyotoka katika maono ya usiku, Hapo usingizi mzito uwaangukiapo wanadamu. Hofu iliniangukia na kutetema, Iliyoitetemesha mifupa yangu yote. Ndipo pepo ilipita mbele ya uso wangu;”
Pepo huyo alimjilia Ayubu akiwa usingizini, kwa mujibu wa hiyo mistari unaanza kuona kuwa kuna watu kabisa wamevamiwa na mapepo ya aina mbalimbali hata hili la uzinzi kwa kupitia usingizi tu.
Kumbuka usingizi au unapolala wewe mwenyewe unaingia kwenye ulimwengu wa roho huko unaweza kukutana na roho za namna hii kabisa na zikakuingia kabisaa.
Ngoja nikupe mfano. Kuna watu huwa wanaota ndoto wanazini na wanawake au wanaume ambao hawawajui kabisa. Na baada ya kuzini tu na hao watu ndotoni wengine ndipo hujikuta wakiwa na tabia ya uzinzi kabisaaa.
Wanajikuta wanaanza kuwaka tamaa na kujikuta ni wazinzi mnoo. Wanaokoka kabisa lakini tabia hiyo ya uzinzi haiwaachii, wengi huhama madhehebu ili waondokane na tabia hiyo ya uzinzi lakini bado hiyo tabia haiwaachilii mpaka wajue chanzo cha hiyo tabia ni nini na wakishughulikie.
Wengine bebo hilo huwamiliki wao na kuwazuia wasioe au kuolewa na hujikuta wazini ndotoni na hilo pepo mara kwa mara. Sasa watu wengi hufikiri ni ndoto tu. Sikiliza wakati mwingine si ndoto tu ni jambo halisia kabisaa.
Kuna watu unamsikia anasema alikuwa anaota ndoto anafukuzwa na mbwa na mara alipowakemea hao mbwa wakageuka watu na wakamuachia au mara kwa mara unaota mbwa anakufukuza au nyoka au mwanaume au mwanamke anakufuatilia weee kwa sura tofauti tofauti.
Fahamu kwenye ulimwengu wa roho ni kweli kuna roho inakufuatilia. Kuna mwinge anaota watu wanafanya uzinzi na wanamwita na yeye aungane nao unasikia nilipokuwa naenda tu nikaamka. Ehehee wakati mwingine ni taarifa unapewa au ni kitu halisi kabisa kuwa pepo la uzinzi linakutafuta au kama ulienda kufanya maana yake unaambiwa una roho hiyo na ulikutana nayo ndotoni.
Unapofanya maamuzi ya kulala usingizi jifunze kuiombea roho yako ulinzi mkubwa kutoka kwa Mungu ili adui asiutumie huo mlango wa usingizi wako kukujilia na kukupata.
Hebu anza kujikagua ndoto zako zikoje? Huoti mara kwa mara unazini na watu wanyama au nyoka, nk? Hebu jiangalie unapolala mara nyingi unaota nini? Shughulikia hizo ndoto, tubu, kemea, vunja mahusiano na hizo roho nk.
Mungu akubariki sana
Ukihitaji masomo yetu unaweza kuyapata kwa njia hizi zifuatazo:-
1. Tovuti yetu ya www.mwakatwila.org
2. YouTube - Mwakatwila au HUDUMA YA SOMA NENO LA MUNGU (HUSONEMU).
3. Facebook ingia katika hiyo tovuti au website yetu utaona alama ya facebook(f) like na utapata maelezo ya kujiunga au ingia Facebook halafu andika “SOMA NENO LA MUNGU”
4. Instagram ingia Instagram app halafu andika “Steven Mwakatwila”
5. DVDs 📀 au CDs 💿
6. VITABU.
NB: Wasiliana na mhudumu ofisini kwa namba +255 763 109 733, kupata VITABU, DVD & CD.
7. Kwa njia ya REDIO:- Utapata mafundisho yetu kwa redio zifuatazo:-
➖Rungwe FM 102.5 Kila siku ya Jumapili saa tatu mpaka saa nne usiku.
➖Baraka FM 107.7 Kila siku ya Jumanne saa kumi na mbili jioni mpaka saa moja usiku.
➖Bomba FM 104.1 Kila siku ya Ijumaa saa tatu usiku mpaka saa nne usiku.
Kwa Mawasiliano zaidi Utatupata kwa namba hizi:-
+255 754 849 924 Au +255 756 715 222
Wako
Mwl Steven & Beth Mwakatwila.
10/03/2019
No comments:
Post a Comment