1⃣9⃣ MAMBO MUHIMU UNAYOTAKIWA UYAFANYE ILI UPATE KUISHINDA DHAMBI YA UZINZI
Na: MWL STEVEN & BETH MWAKATWILA
FUATANA NASI INSTAGRAM
KUPATA APP YETU “HUSONEMU (MWAKATWILA) APP”, BONYEZA LINK HAPA:
FUATANA NASI WHATSAPP
FUATANA NASI FACEBOOK
FUATANA NASI YOUTUBE
&
FUATANA NASI ONLINE RADIO
🗓 01 Machi, 2019
Bwana Yesu Kristo asifiwe. Nianze kwa kukuomba msamaha kwa kutokukuletea mapema somo nililokuahidi kukufundisha ili ujifunze namna ya kuishinda dhambi ya uzinzi.
Nimekuwa na mambo mengi kidogo sasa najikuta wakati fulani nimebanwa kwa kweli. Leo hii tuna semina Bethel KKKT na ni semina ya tatu mfululizo naona umeona namna nilivyobanwa kidogo.
Nikukaribishe karibu sana au unaweza kutupata katika radio.mwakatwila.org kuanzia saa kumi na nusu tupo live.
Hebu tujifunze sasa. Kumbuka katika somo lililopita nilikufundisha ile sababu ya tatu inayoweza kuwa chanzo cha mapepo au roho mbaya kumwingia mtu.
Baada ya kuiangalia hiyo sababu ya tatu nataka nikuonyeshe sababu ya nne.
SABABU YA NNE NI HII; UNAPOACHANA AU KUACHWA NA MUNGU.
Unaposoma maandiko unaona kuwa Mungu anapofanya maamuzi ya kumwacha mtu au mtu anapofanya maamuzi ya kumwacha Mungu ndipo mapepo au roho mbaya hupata nafasi ya kumwingia huyo mtu na kumsumbua sana.
Unaweza kujiuliza hivi Mungu anaweza kumwacha mtu? Jibu ni ndiyo, angalia mifano hii michache. “Akasema, Umefanya nini? Sauti ya damu ya ndugu yako inanililia kutoka katika ardhi. Basi sasa, umelaaniwa wewe katika ardhi, iliyofumbua kinywa chake ipokee damu ya ndugu yako kwa mkono wako; utakapoilima ardhi haitakupa mazao yake; utakuwa mtoro na mtu asiye na kikao duniani. Kaini akamwambia BWANA, Adhabu yangu imenikulia kubwa, haichukuliki. Tazama, umenifukuza leo katika uso wa ardhi, nitasitirika mbali na uso wako, nami nitakuwa mtoro na mtu asiye na kikao duniani; hata itakuwa kila anionaye ataniua.” (Mwanzo 4:1-14).
Ukiipitia hiyo mistari utaona vitu vya ajabu mno hapo. Kaini alipoua au kumwaga damu alijikuta ameachana na uso wa Mungu, msikilize asemavyo yeye mwenyewe anasema “Tazama, umenifukuza leo katika uso wa ardhi, nitasitirika mbali na uso wako, nami nitakuwa mtoro na mtu asiye na kikao duniani;”
Ukiisoma hiyo mistari kwa kutulia utagundua Mungu alimwacha Kaini, tena utashangaa Kaini alifukuzwa usoni pa ardhi na alikuwa mtoro na asiye na kikao duniani.
Fikiria kidogo Kaini katika ulimwengu huu wa mwili alikuwa duniani juu ya ardhi, lakini katika ulimwengu wa roho Kaini alishafukuzwa usoni pa ardhi na uso wa Mungu ulikuwa mbali naye kabisa maandiko yanasema alisitirika mbali na uso wa Mungu. Na alitoroka duniani.
Hivi mtu wa namna hiyo unafikiri atakutana na nini au na roho ipi? Kumbuka duniani humu mapepo au malaika waasi waliotupwa kutoka mbinguni ni wengi mno.
Fikiria Mungu kaamua kukufanyia kama alivyomfanyia Kaini unafikiri utamilikiwa au utakutana na roho zipi? Mimi nakuambia wazi kuwa unauhitaji uso wa Mungu kwa ukubwa zaidi kuliko uwazavyo ili akuokoe na hizo roho mbaya zinazozunguka huku na huku zikitafuta mtu wa kumwingia sehemu nyingine maandiko yanasema ili awameze.
Ukiipitia hiyo mistari utagundua kiini cha mtu kuachana au kuachwa na Mungu ni dhambi. Kaini alipofanya dhambi ya kuua tu, alichwa na uso wa Mungu yakamkuta yote yale yaliyomkuta. Akajikuta mtoro usoni pa dunia, akajikuta hakubaliki katika ardhi nk.
Sikiliza nikuambie, unapoua mtu au kumwaga damu fahamu hata wewe yanakukuta hayo hayo. Wewe soma maandiko utagundua kila mtu aliyeua watu alijikuta anakuwa na sifa kama zile za Kaini tu.
Watu wengi wanaua watu hujikuta katika hatari ya kuvamiwa na mapepo kisa wanakuwa mbali na Mungu. Sisi humu duniani tunawaona ohooo ni watu tuko nao na wako juu ya ardhi kumbe aisee Mungu aliishawaacha na ardhi imewaacha duniani watoro. Kwa lugha nzuri MUNGU HAWAONI KABISAA.
Watu wanaoua watu iwe kwa kuloga au kuwauwa kwa sumu au kwa kutoa mimba au risasi, nk wewe wafuatilie utagundua wengi hawako sawa kabisaa. Mpaka waingie kuitubia hiyo dhambi na kumwamini Bwana Yesu Kristo na kuamua kutembea au kujenga ushirika upya na Mungu kwa kupitia Bwana Yesu Kristo.
Na wengi unapowaombea usishangae mapepo yanalipuka ndani yao, na baada ya hapo unauona utulivu katika maisha yao kwa sababu pia hupatana na ardhi iliyowakataa.
Angalia mfano huu mwingine utagundua Mungu anaweza kumwacha mtu na akimwacha tu mapepo humvamia mtu huyo.
“Basi, roho ya BWANA ilikuwa imemwacha Sauli, na roho mbaya kutoka kwa BWANA ikamsumbua. Nao watumishi wa Sauli wakamwambia, Angalia, sasa roho mbaya kutoka kwa Mungu inakusumbua. Basi bwana wetu na atuamuru sisi watumishi wake waliopo hapa mbele yako watafute mtu aliye stadi wa kupiga kinubi; basi itakuwa, roho ile mbaya kutoka kwa Mungu itakapokujilia, yeye atapiga kinubi kwa mkono wake, nawe utapona.” (1 Samweli 16:14-16).
Angalia hii mistari. “Sauli akamwonea Daudi wivu tangu siku ile.Ikawa siku ya pili yake, roho mbaya kutoka kwa Mungu ikamjilia Sauli kwa nguvu, naye akatabiri ndani ya nyumba. Basi Daudi alikuwa akipiga kinubi kwa mkono wake kama siku zote; naye Sauli alikuwa na mkuki mkononi mwake. Mara Sauli akautupa ule mkuki; maana alisema, Nitampiga Daudi hata ukutani.” (1 Samweli 18:9-11).
Ukiisoma hiyo mistari utagundua kuwa baada tu ya Roho ya Bwana au Mungu kumwacha Sauli kilichotokea ni roho mbaya kumwingia Sauli. Hapo unajifunza kuwa Roho Ya Bwana Mungu inaweza kumwacha mtu.
Na utaona inapomwacha huyo mtu, huyo mtu anakuwa katika hatari ya kuvamiwa na roho mbaya au mapepo. Ngoja nikufundishe leo unapomwacha Bwana Yesu Kristo tu nakuambia unakuwa katika hatari kubwa mno ya kuingiliwa na mapepo.
Sasa yanapokuingia usifikirie yatakutesa kwa magonjwa tu hapana yaweza kukutengenezea tabia. Moja ya tabia ni wivu, kuna wivu ambao chanzo chake ni pepo, linaweza kukutengenezea tabia ya uzinzi.
Mimi naamini mtu yeyote yule ambaye hana ushirika na Bwana Yesu Kristo ana hatari muda wowote kuvamiwa na mapepo. Sitanii ni ukweli kabisaa. Mungu alipomwacha Sauli tu, Sauli akajikuta akivamiwa na mapepo yakambana kweli. Fikiria mfalme kavamiwa na mapepo? Maamuzi yake yatakuaje?
Ngoja nikupe mfano huu mwingine uone, angalia mistari hii. “Na wakuu wa makuhani na waandishi walikuwa wakitafuta njia ya kumwua; maana walikuwa wakiwaogopa watu.Shetani akamwingia Yuda, aitwaye Iskariote, naye ni mmoja wa wale Thenashara. Akaondoka, akaenda akasema na wakuu wa makuhani na majemadari, jinsi atakavyoweza kumtia mikononi mwao. Wakafurahi, wakapatana naye kumpa fedha. Akakubali, akatafuta nafasi ya kumsaliti kwao pasipokuwapo mkutano.” (Luka 22:2-5).
Unaposoma maandiko utagundua wazi kuwa tatizo lililokuwepo kwa Yuda ni hili la yeye kumwacha Mungu. Yuda kabla ya kuingiwa na shetani utagundua tokea mwanzo aliishafanya maamuzi ya kumwacha Mungu.
Angalia mistari hii utagundua Yuda alikuwa na matatizo siku nyingi. “Basi Yuda Iskariote, mmojawapo wa wanafunzi wake, ambaye ndiye atakaye kumsaliti, akasema, Mbona marhamu hii haikuuzwa kwa dinari mia tatu, wakapewa maskini? Naye aliyasema hayo, si kwa kuwahurumia maskini; bali kwa kuwa ni mwivi, naye ndiye aliyeshika mfuko, akavichukua vilivyotiwa humo. Basi Yesu alisema, Mwache aiweke kwa siku ya maziko yangu. Kwa maana maskini mnao sikuzote pamoja nanyi; bali mimi hamnami sikuzote” (Yohana 12:4-8).
Ukiisoma hiyo mistari unauona moyo wa Yuda ulivyokuwa. Yuda alikuwa na nia ya kumsaliti Bwana Yesu Kristo siku nyingi sana. Maandiko yanasema ATAKAYE KUMSALITI. Yuda aliachana na Bwana Yesu Kristo muda mrefu mno hao wanafunzi hawakumjua tu.
Unajua shetani aliupata ule mlango kwa urahisi sana kwa sababu alimwona Yuda alikuwa hakubaliani na Bwana Yesu Kristo ingawa alikuwa mwanafunzi wake na pia alipewa nafasi ya uhasibu kwani ndiye aliyekuwa mchukua mafungu ya fedha ya timu nzima ya Bwana Yesu Kristo.
Yuda maandiko yanasema alikuwa mwizi, fahamu yeye alishaachana na Mungu siku nyingi mno. Fikiria unaiba fedha ya Bwana Yesu Kristo tena akiwepo kabisa katika mwili huu unaoonekana?
Mtu wa sifa hii fahamu hakuwa mtu wa kawaida nakuambia. Hivi umewahi mfikiria Yuda kwa undani mpendwa? Yuda alipochaguliwa tu awe miongoni mwa wanafunzi Bwana Yesu Kristo alimshitukia, alimwona namna walivyo na utofauti kati yao.
Maandiko yanasema hivi. “Lakini kuna wengine miongoni mwenu wasioamini. Kwa maana Yesu alijua tangu mwanzo ni nani wasioamini, naye ni nani atakayemsaliti. Akasema, Kwa sababu hiyo nimewaambia ya kwamba hakuna mtu awezaye kuja kwangu isipokuwa amejaliwa na Baba yangu. Kwa ajili ya hayo wengi miongoni mwa wanafunzi wake wakarejea nyuma, wasiandamane naye tena. Basi Yesu akawaambia wale Thenashara, Je! Ninyi nanyi mwataka kuondoka? Basi Simoni Petro akamjibu, Bwana! Twende kwa nani? Wewe unayo maneno ya uzima wa milele.Nasi tumesadiki, tena tumejua, ya kuwa wewe ndiwe Mtakatifu wa Mungu. Yesu akawajibu, Je! Mimi sikuwachagua ninyi Thenashara, na mmoja wenu ni shetani? Alimnena Yuda, mwana wa Simoni Iskariote; maana huyo ndiye atakayemsaliti; naye ni mmojawapo wa wale Thenashara.” (Yohana 6:64-71)
Ukiyasoma maneno hayo utanielewa ninavyokuambia kuwa Yuda yeye alimwacha Bwana Yesu Kristo. Unajua unapoyasoma hayo maandiko unagundua kuwa Yuda hakuwa anamwamini Bwana Yesu Kristo ingawa alikuwa mwanafunzi wake.
Angalia hapo Bwana Yesu Kristo anasema hivi “Lakini kuna wengine miongoni mwenu wasioamini. Kwa maana Yesu alijua tangu mwanzo ni nani wasioamini, naye ni nani atakayemsaliti.,”
Yuda alikuwa hamwamini tokea alipomchagua, Yuda alikaa upande wa washika dini, yaani Mafarisayo na makuhani na waandishi. Yale aliyokuwa anayafanya na kuyasema Bwana Yesu Kristo, Yuda hakuyaamini kabisa, alikaa hapo kama mpelekezi hivi ambaye alikuwa akitoa taarifa kwa wanaompinga Bwana Yesu Kristo.
Bwana Yesu Kristo aligundua kuwa Yuda hamwamini yaani Yuda kaamua kumwacha Bwana Yesu Kristo, kitendo hicho alichokifanya Yuda kilimleta kwenye hatari ya kuingiliwa na shetani au mapepo.
Naona umenielewa sasa ninavyokuambia sababu nyingine inayoweza kuwa chanzo cha mtu kuvamiwa na mapepo ni hiki cha kumwacha au kuachwa na Mungu.
Maandiko yanasema mtu aliyekuwa na ushirika na Bwana Yesu Kristo yaani aliyeonja kipawa cha wokovu na akaamua kumwacha Bwana Yesu Kristo kumrejesha mtu huyo ni ngumu.
Si kuwa haiwezekani; inawezekana kabisaa kumrudisha ila ni ngumu. Ugumu wake hutokana na namna alivyovamiwa na roho hizi mbaya kwa wingi. Warejeshaji wanahitaji nguvu mno na hekima kubwa mno.
Kinachowafanya watu kuachana na Mungu ni dhambi na hasa ile tabia ya kuficha dhambi badala ya kuitubu.
Adamu alipofanya dhambi aliificha hiyo hali yake, si unajua alimkimbia Mungu? Alienda kujificha yaani alipofanya dhambi Adamu yeye ndiye aliyefanya maamuzi ya kuachana na Mungu.
Alimkimbia Mungu akaenda kujificha, Adamu alimkataa Mungu, Mungu akamfuata Adamu bado hakuwa na moyo wa toba ila alijaa laumu kwa mkewe na alimlaumu hata Mungu mwenyewe. Unajua kilichotokea MUNGU AKAMFUKUZA ADAMU.
Mungu alimwacha Adamu, ukitaka kujua Adamu alipomwacha Mungu alikutana na roho gani wewe soma maisha yake yeye na watoto wake yalikuwaje. Utaona walianza kutawaliwa na roho mbaya; Kaini akamwua Habili, nk.
Mtu wa kwanza kufa katika ulimwengu huu unaoonekana ni Habili. Kaini kabla hakuua aliambiwa kuna dhambi inamwotea mlangoni kwa lugha nzuri kulikuwa na roho mbaya kama ileee iliyomjia Sauli ya kutaka kuua bila kosa kisa wivu tu.
Ukiachwa au kumwacha Mungu tu fahamu roho hizo mbaya hukuotea tena mlangoni ili kukuingia na kukutengenezea tabia. Mungu ukiwa naye fahamu pepo hakuingii mpaka wewe uamue umwache Mungu au Mungu aamue kukuacha kisa haumtii na umekuwa mdhambi.
Hebu angalia ushirika wako na Mungu ukoje? Mrudie Mungu wako katika Bwana Yesu Kristo. Tubu atakurudishia ushirika uliopotea kati yenu. Ukigundua kulikuwa na mapepo tafuta watu waliomwamini Bwana Yesu Kristo waambie wakuombee walikee hilo pepo litakuacha hata kama yalikuwa mengi yatatoka tu.
Naamini umenielewa
Mungu akubariki sana
Ukihitaji masomo yetu unaweza kuyapata kwa njia hizi zifuatazo:-
2. YouTube - Mwakatwila au HUDUMA YA SOMA NENO LA MUNGU (HUSONEMU).
3. Facebook ingia katika hiyo tovuti au website yetu utaona alama ya facebook(f) like na utapata maelezo ya kujiunga au ingia Facebook halafu andika “SOMA NENO LA MUNGU”
4. Instagram ingia Instagram app halafu andika “Steven Mwakatwila”
5. DVDs 📀 au CDs 💿
6. VITABU.
NB: Wasiliana na Mhudumu ofisini kwa namba +255 (0) 763 109 733, kupata VITABU, DVD & CD.
7. Kwa njia ya REDIO:- Utapata mafundisho yetu kwa redio zifuatazo:-
➖Rungwe FM 102.5 Kila siku ya Jumapili saa tatu mpaka saa nne usiku.
➖Baraka FM 107.7 Kila siku ya Jumanne saa kumi na mbili jioni mpaka saa moja usiku.
➖Bomba FM 104.1 Kila siku ya Ijumaa saa tatu usiku mpaka saa nne usiku.
Kwa Mawasiliano zaidi Utatupata kwa namba hizi:-
+255 (0) 754 849 924 Au +255 (0) 756 715 222
Wako
Mwl Steven & Beth Mwakatwila.
01/03/2019
No comments:
Post a Comment