Saturday, March 23, 2019

2⃣3⃣ MAMBO MUHIMU UNAYOTAKIWA UYAFANYE ILI UPATE KUISHINDA DHAMBI YA UZINZI

2⃣3⃣ MAMBO MUHIMU UNAYOTAKIWA UYAFANYE ILI UPATE KUISHINDA DHAMBI YA UZINZI

Na: MWL STEVEN & BETH MWAKATWILA

FUATANA NASI FACEBOOK

FUATANA NASI INSTAGRAM

KUPATA APP YETU “HUSONEMU (MWAKATWILA) APP”, BONYEZA LINK HAPA:

FUATANA NASI WHATSAPP

FUATANA NASI YOUTUBE
&
FUATANA NASI ONLINE RADIO

🗓 23 Machi, 2019

Bwana Yesu Kristo asifiwe. Nianze kwa kukuomba msamaha kwa sababu ni muda mrefu kidogo sikukuletea mfululizo wa somo hili.

Nimekuwa na mambo mengi kweli kweli sasa kuupata muda wa kukuandikia somo ndiyo inakuwa taabu kidogo. Nimeupata huu muda nimeona niiutumie kukuandikia na  kukuletea somo hili.

Katika kipindi kilichopita nilikuwa nakuonyesha  mlango wa pili wa tabia ya uzinzi nayo ilikuwa ni pepo au roho ya uzinzi.

Hebu tusogee mbele kidogo nataka kukuonyesha namna ya kufanya ili utoke kwenye tabia ya uzinzi iliyotokana na pepo.

NJIA YA KWANZA NI; KUTUMIA MAMLAKA MAALUMU YA KULITOA HILO PEPO MWILINI MWAKO.

Ikiwa unaona dalili zote za kuwa una roho au pepo la uzinzi mwilini mwako na unataka uondokane na hiyo tabia ya uzinzi njia ya kutoka hapo ni kulitoa hilo pepo mwilini mwako.

Fahamu pepo hilo ndilo linalozalisha hiyo tabia na ili hiyo tabia iondoke ni lazima ulitoe hilo pepo ndipo hiyo tabia utaicha.

Unaweza ukawa umeokoka kabisa lakini hiyo roho ukawa nayo kabisa. Wengi huhisi kama hawajaokoka vizuri. Sikiliza kuokoka ndiyo hatua ya kwanza ya kukamilishwa.
Unapookoka ndipo unaanza kutengenezwa mpaka kufikia utimilifu. Kwa maana hiyo unaweza kuokoka au kuupokea wokovu lakini ukawa bado na pepo tu.  

Mpaka utakapoanza kufundishwa na kukutana na watu waliotangulia katika huo wokovu waitwao watumishi  ambao watatumia mamlaka waliyopewa na Mungu ya kuwakamilisha hao waliookoka.

Na moja ya ukamilishaji wao ni huu wa kuyatoa hayo mapepo yaliyo ndani ya hao waaminio. Biblia inatufundisha hivi “Naye alitoa wengine kuwa mitume, na wengine kuwa manabii; na wengine kuwa wainjilisti na wengine kuwa wachungaji na waalimu; kwa kusudi la kuwakamilisha watakatifu, hata kazi ya huduma itendeke, hata mwili wa Kristo ujengwe;” (Waefeso 4:11-12)

Mungu anajua kuwa watakatifu au watu waliotengwa kwa ajili yake au waliochaguliwa si wakamilifu na wanahitaji kukamilishwa. Sasa angalia watu wengi wanaingia ndani ya wokovu wakiwa na tabia mbaya tu zingine zimebebwa kwenye mwili zingine zimewabana kwa kutumia roho au mapepo.

Kuongozwa sala ya toba au kubatizwa usifikirie kunaweza kuondoa pepo. Hili ni jambo muhimu sana ambalo unahitaji ulijue. Unaweza batizwa na pia kuongozwa sala ya toba lakini bado ukawa na pepo la uzinzi tu.

Pepo litamuachia mtu atakayefanyiwa huduma maalumu ya kulitoa hilo pepo kwa njia ya kuliamuru limtoke huyo mtu kwa kutumia jina la Bwana Yesu Kristo.

Bwana Yesu Kristo anatufundisha hivi. “Na ishara hizi zitafuatana na hao waaminio; kwa jina langu watatoa pepo; watasema kwa lugha mpya;” (Marko 16:17).’

Pepo anatolewa. Kama hakujafanyika kazi hiyo ya kumtoa hapo alipo fahamu atakuwepo tu, mpaka watu wajue kuwa kuna pepo au wafanye huduma maalumu ya kuyaamuru mapepo yaliyo ndani ya watu yawatoke ndipo unaweza ukashangaa hata watu ambao hukuwahi fikiria wana mapepo siku hiyo ukagundua kuwa walikuwa na mapepo.

Nakumbuka mwaka fulani nilisukumwa kufanya huduma maalumu ya namna hii kwa ajili ya wanakamati unajua kilichotokea? Mapepo yalilipuka kwa watu ambao hata sikuwafikiria.

Siyo kuwa hawajaokoka na hawampendi Bwana Yesu Kristo, mapepo yanaweza kabisa yakaja hata mahali watoto wa Mungu wamekusanyika. Unaweza kuniuliza kivipi.

Angalia mistari hii uone. “Ilikuwa, siku moja ambayo hao wana wa Mungu walikwenda kujihudhurisha mbele za BWANA, Shetani naye akaenda kati yao.BWANA akamwuliza Shetani, Umetoka wapi wewe? Ndipo Shetani akamjibu BWANA, na kusema, Natoka katika kuzunguka-zunguka duniani, na katika kutembea huku na huku humo. Kisha BWANA akamwuliza Shetani, Je! Umemwangalia huyo mtumishi wangu Ayubu? Kwa kuwa hapana mmoja aliye kama yeye duniani, mtu mkamilifu na mwelekevu, mwenye kumcha Mungu na kuepukana na uovu.Ndipo Shetani akamjibu BWANA, na kusema, Je! Huyo Ayubu yuamcha BWANA bure?” (Ayubu 1:6-9)

Ukiipitia hiyo mistari ndipo utanielewa vizuri au utaelewa kwa nini neno la Mungu linasema mpingeni shetani. Angalia hii mistari. “Basi mtiini Mungu. Mpingeni Shetani, naye atawakimbia. Mkaribieni Mungu, naye atawakaribia ninyi. Itakaseni mikono yenu, enyi wenye dhambi, na kuisafisha mioyo yenu, enyi wenye nia mbili.” (Yakobo 4:7-8)

Maandiko yanatufundisha kuwa watoto wa Mungu walipojihudhurisha mbele za Mungu shetani na yeye akaenda kati yao. Maana yake miongoni mwao kuna mtu ndani yake alimbeba  shetani kabisa. Unanielewa lakini?

Ngoja nijaribu tena kukuonyesha hili jambo. Maandiko yanasema mpingeni shetani naye atawakimbia mkaribieni Mungu naye atawakaribia. Fikiria kidogo hao wanaoambiwa wampinge ni watoto wa Mungu kabisa, kabla hawajamkaribia Mungu wanatakiwa wampinge kwanza shetani inamaana wale wana katika kipindi kile cha Ayubu hawakushughulikia jambo hilo walipomkaribia Mungu adui akawa kati yao.

Unajua hata kipindi kile cha Bwana Yesu yupo na timu yake ile shetani alijihudhurisha katikati yao kabisaa. Alikuwa ndani ya Yuda. Maandiko yanasema hivi. “Yesu akawajibu, Je! Mimi sikuwachagua ninyi Thenashara, na mmoja wenu ni shetani? Alimnena Yuda, mwana wa Simoni Iskariote; maana huyo ndiye atakayemsaliti; naye ni mmojawapo wa wale Thenashara.” (Yohana 6:70-71).

Bwana Yesu Kristo alilijua jambo hili kabisa kuwa katika ile timu yake shetani yupo lakini hakumpinga au kumtoa. Na kweli alikuja kumsaliti. Angalia kitu hiki labda utaelewa kuwa mapepo yanaweza kumwingia mtu aliyeokoka kabisaa angalia mfano huu.

“Yesu akajibu, akamwambia, Heri wewe Simoni Bar-yona; kwa kuwa mwili na damu havikukufunulia hili, bali Baba yangu aliye mbinguni. Nami nakuambia, Wewe ndiwe Petro, na juu ya mwamba huu nitalijenga kanisa langu; wala milango ya kuzimu haitalishinda. Nami nitakupa wewe funguo za ufalme wa mbinguni; na lo lote utakalolifunga duniani, litakuwa limefungwa mbinguni; na lo lote utakalolifungua duniani, litakuwa limefunguliwa mbinguni. Ndipo alipowakataza sana wanafunzi wake wasimwambie mtu ye yote ya kwamba yeye ndiye Kristo Tangu wakati huo Yesu alianza kuwaonya wanafunzi wake ya kwamba imempasa kwenda Yerusalemu, na kupata mateso mengi kwa wazee na wakuu wa makuhani, na waandishi, na kuuawa, na siku ya tatu kufufuka. Petro akamchukua, akaanza kumkemea, akisema, Hasha, Bwana, hayo hayatakupata. Akageuka, akamwambia Petro, Nenda nyuma yangu, Shetani; u kikwazo kwangu; maana huyawazi yaliyo ya Mungu, bali ya wanadamu.” (Mathayo 16:17-23).

Ukiipitia hiyo mistari utagundua Bwana Yesu Kristo alilitoa pepo au shetani aliyekuwa ndani ya Petro. Petro alishakuwa amepewa taarifa kuwa atapewa ufunguo au mamlaka kubwa sana katika ufalme wa Mungu. Petro huyo huyo shetani alimwingia.

Hebu jiulize swali Bwana Yesu alikuwepo shetani akamwingia Petro je! Asingefanya huduma ya kumtoa huyo shetani Je? Petro angeondolewa huyo shetani kisa eti ni mtumishi au ameokoka? Bwana Yesu Kristo hakumkemea  shetani au pepo aliyekuwa ndani ya Yuda kwa sababu alikuwa anataka kutimiza maandiko katika habari za kusalitiwa kwake.

Naamini kama isingekuwa hivyo angemkemea au kumtoa shetani ndani ya Yuda. Naamini umenielewa sasa ninavyokuambia kuwa tatizo kubwa ambalo watu wengi wanalo ni hili la kutokufanyiwa maombi mara kwa mara ya kuondolewa mapepo yaliyo ndani yao.
Biblia inatufundisha kuwa moja ya kazi ambayo Bwana Yesu Kristo alikuwa akiifanya ni kuyatoa mapepo yaliyo ndani ya watu.

Angalia mistari hii. “Hata kulipokuwa jioni, wakamletea wengi wenye pepo; akawatoa pepo kwa neno lake, akawaponya wote waliokuwa hawawezi, ili litimie lile neno lililonenwa na nabii Isaya, akisema, Mwenyewe aliutwaa udhaifu wetu, Na kuyachukua magonjwa yetu.” (Mathayo 8:16-17)

Angalia na mistari hii  “na wanawake kadha wa kadha ambao walikuwa na pepo wabaya na magonjwa wakaponywa; nao ni Mariamu aitwaye Magdalene aliyetokwa na pepo saba,” (Luka 8:2)

Ukiipitia hiyo mistari utagundua kuwa moja ya kazi aliyokuwa anaifanya Bwana Yesu Kristo ni hii ya kukemea au kuyaondoa mapepo yaliyo ndani ya miili ya watu.  Kazi hii hata leo hii Bwana Yesu Kristo anataka kuona ikiendelea kufanywa. Ndiyo maana anasema hivi. “Akawaita wanafunzi wake kumi na wawili, akawapa amri juu ya pepo wachafu, wawatoe, na kupoza magonjwa yote na udhaifu wa kila aina.” (Mathayo 10:1)

Maandiko yanasema waliopewa wajibu wa kuyatoa hayo mapepo ni wanafunzi. Unaposoma neno wanafunzi lina utofauti sana na ukisoma neno mitume. Unaweza ukawa mwanafunzi lakini usiwe mtume. Watu wengi hawajui kuwa unapofanyika kuwa mwanafunzi tu wa Bwana Yesu Kristo kwa kumpokea na kumwamini kama Bwana kwako unapewa hii nafasi ya kuyatoa mapepo yaliyo ndani ya watu.

Tatizo tulilonalo ni mfumo uliopo ndani ya kanisa. Wanafunzi wa Bwana Yesu hawaandaliwi hawakufundishwa mambo kama haya. Biblia inasema “Basi, enendeni, mkawafanye mataifa yote kuwa wanafunzi, mkiwabatiza kwa jina la Baba, na Mwana, na Roho Mtakatifu; na kuwafundisha kuyashika yote niliyowaamuru ninyi; na tazama, mimi nipo pamoja nanyi siku zote, hata ukamilifu wa dahari.” (Mathayo 28:19-20).

Moja ya jambo Bwana Yesu Kristo katuamuru tulifanye ni hili la kuyatoa mapepo. Sasa angalia kama wanafunzi leo hii wamefundishwa jambo hili. Ndiyo maana utaona wanafunzi wengi wa Bwana Yesu Kristo na watu wengine wasio wanafunzi wamebanwa na mapepo ya uzinzi.

Sikiliza mwanafunzi wa Bwana Yesu Kristo anapoona mwanafunzi mwenzake ana dalili za roho au pepo ndani yake ilitakiwa yeye ndiye alishughulikie hilo pepo. Sasa siku hizi mpaka akatafutwe mtume au nabii.

Amri ya kutoa pepo walipewa hata wanafunzi, siyo manabii au waalimu au wachungaji au wainjilisti au mitume tu. Wakifundishwa hao wanafunzi wakaamini kuwa wanayo hayo mamlaka nakuambia ukweli watayatoa mapepo mengi tu yaliyo ndani ya watu.

Ili kukabiliana na tabia ya uzinzi iliyoletwa na pepo lazima pepo hilo au mapepo hayo yatolewe ndani ya mtu huyo, kinyume cha hapo atakuwa mzinzi tu hata awe mwimbaji au mwombaji nk.

Ikiwa unaona dalili kama hizi tafuta wanafunzi wenzio wa Bwana Yesu Kristo au watumishi wenye ufahamu walitoe hilo pepo likitoka tu fahamu tabia ya uzinzi iliyoletwa na pepo itakuacha.

Mungu akusaidie na kukuongoza vema katika hatua hii. Katika somo lijalo nitakuonyesha sababu ya watu wengine kurudiwa na mapepo baada ya kutolewa ndani yao.

Ukihitaji masomo yetu unaweza kuyapata kwa njia hizi zifuatazo:-

1. Tovuti yetu ya www.mwakatwila.org

2. YouTube - Mwakatwila au HUDUMA YA SOMA NENO LA MUNGU (HUSONEMU).

3. Facebook ingia katika hiyo tovuti au website yetu utaona alama ya facebook(f) like na utapata maelezo ya kujiunga au ingia Facebook halafu andika  “SOMA NENO LA MUNGU”

4. Instagram ingia Instagram app halafu andika “Steven Mwakatwila”

5. DVDs 📀 au CDs 💿

6. VITABU.
NB: Wasiliana na Mhudumu ofisini kwa namba +255 (0) 763 109 733, kupata VITABU, DVD & CD.

7. Kwa njia ya REDIO:- Utapata mafundisho yetu kwa redio zifuatazo:-
➖Rungwe FM 102.5 Kila siku ya Jumapili  saa tatu mpaka saa nne usiku.
➖Baraka FM 107.7 Kila siku ya Jumanne saa kumi na mbili jioni mpaka saa moja usiku.
➖Bomba FM 104.1 Kila siku ya Ijumaa saa tatu usiku mpaka saa nne usiku.

8. Unaweza kutupata kwenye ONLINE RADIO yetu:-  radio.mwakatwila.org

Kwa Mawasiliano zaidi Utatupata kwa namba hizi:-
+255 (0) 754 849 924 Au +255 (0) 756 715 222

Wako
Mwl Steven & Beth Mwakatwila.
23/03/2019

No comments:

Post a Comment