2⃣0⃣ MAMBO MUHIMU UNAYOTAKIWA UYAFANYE ILI UPATE KUISHINDA DHAMBI YA UZINZI
Na: MWL STEVEN & BETH MWAKATWILA
FUATANA NASI:- APP, FACEBOOK, INSTAGRAM, ONLINE RADIO 📻, WHATSAPP, WEBSITE & YOUTUBE, Kwa links zilizoko kwenye HII LINK hapa:
KUPATA APP YETU “HUSONEMU (MWAKATWILA) APP” BONYEZA LINK HII HAPA:
🗓 06 Machi, 2019
Bwana Yesu Kristo asifiwe Sana. Ninaamini tunaenda sambamba katika somo hili na umeanza kuyafanyia kazi mambo unayofundishwa.
Kumbuka tunajifunza eneo lile la chanzo cha pili cha tabia ya uzinzi ambacho ni chanzo cha uzinzi uletwao na mapepo au pepo la uzinzi. Katika kipindi kilichopita tuliendelea kuangalia sababu zinazoweza kuwa chanzo cha mtu kuwa na mapepo.
Baada ya kujifunza ile sababu ya nne nataka nikuonyeshe sababu nyingine ya tano. nayo ni
SABABU YA TANO NI; KUONEWA NA IBILISI
Moja ya sababu ambayo inaweza kuwa chanzo cha mtu kuwa na roho au pepo la uzinzi ni hii ya kuonewa tu na shetani au na hizo roho mbaya.
Maandiko yanasema hivi. “Neno lile alilowapelekea wana wa Israeli akihubiri habari njema ya amani kwa Yesu Kristo (ndiye Bwana wa wote), jambo lile ninyi mmelijua, lililoenea katika Uyahudi wote likianzia Galilaya, baada ya ubatizo aliouhubiri Yohana; habari za Yesu wa Nazareti, jinsi Mungu alivyomtia mafuta kwa Roho Mtakatifu na nguvu naye akazunguka huko na huko, akitenda kazi njema na kuponya wote walioonewa na Ibilisi; kwa maana Mungu alikuwa pamoja naye” (Matendo ya Mitume 10:36-38)
Ukiipitia hiyo mistari utagundua kuwa kuna watu wanapitia taabu mbalimbali kisa ni hiki wameonewa tu na shetani. Bwana Yesu Kristo alishughulika na huduma mbalimbali zilizobeba uponyaji kwa watu.
Moja ya kazi aliyoifanya ilikuwa ni kutoa mapepo yaliyokuwa ndani ya miili ya watu. Kumbuka si kila pepo linatengeneza tabia ya ugonjwa tu. Yanaweza kumtengenezea mtu magonjwa ya aina mbalimbali au tabia mbalimbali kama tulivyojifunza huko nyuma.
Maandiko yanasema hivi “Naye alikuwa akizunguka katika Galilaya yote, akifundisha katika masinagogi yao, na kuihubiri Habari Njema ya ufalme, na kuponya ugonjwa na udhaifu wa kila namna katika watu. Na habari zake zikaenea katika Shamu yote; wakamletea wote waliokuwa hawawezi, walioshikwa na maradhi mbalimbali na mateso, wenye pepo, na wenye kifafa, na wenye kupooza; akawaponya.” (Mathayo 4:23-24).
Bwana Yesu Kristo alishughulikia mambo mengi sana sana, moja ya mambo aliyoyashughulikia ni hili la kuwatoa pepo wachafu waliokuwa ndani ya watu.
Sasa sikia watu wengine walijikuta wamebanwa na hayo mapepo ni kwa sababu ya kuonewa tu na ibilisi. Ninaposema kuonewa tu nina maana hawakufanya dhambi yoyote, ila walijikuta wakibanwa na ufalme wa giza na ukawatawala na wakajikuta wakiwa chini ya mamlaka ya adui akiwatumikisha kwa kutumia mapepo ili wawe wazinzi na wawaangushe wengi kwenye hii dhambi.
Nimewahi kukutana na mtu aliniambia kuwa yeye alikuwa anawabana mabinti shuleni na kuwaaingizia roho hizo mbaya. Alikuwa binti mdogo tu siku hiyo nilitembelea shuleni kwao na nikawaombea na nilipowauliza ni nani anakula nyama ndotoni. Binti huyo alikuwa miongoni mwa watu wengi waliokuja mbele. Nilipomwuliza unakulaje, ndipo nilipogundua kuwa binti huyo ni mchawi.
Nilipokaa naye na kumwuliza mambo mengi sana alifunguka sana na moja ya jambo aliloniambia ni hili la kuwapandikizia mabinti walio wazuri roho mbaya au mapepo ya namna mbalimbali ili huko mbeleni hao waliobanwa wajikite wakimtumikia shetani.
Aliniambia mabinti wote waliokuwa wakianguka hapo shuleni yeye ndiye aliyekuwa anawafanyia hivyo. Siku kama tatu hivi kuna binti alianguka hapo shuleni, nikaagiza akaletwe, alipoletwa niligundua ni kweli alikuwa anawachagua mabinti wazuri wazuri.
Nakuambia ukweli kuna watu hasa wanawake ni wazuri sana lakini ni wazinzi mpaka unashangaa. Hawajui kusema hapana, wanawaka tamaa ya uzinzi hata wao ukikaa nao wanakuambia wanashangaa.
Unamwuliza uliwahi kwenda kwa mganga, anakuambia nimelelewa katika familia ya Kikristo hasa. Unakemea pepo la uzinzi unashangaa linalipuka na likitolewa tu, anakua binti mzuri tu.
Kuna habari nyingine niliwahi kusikia, kuna mtu aliyekuwa na mapepo yeye anasema aliyapata akiwa ameenda mtoni. Anadai aliona kitu ndani ya maji kikimjia kilikuwa kizuri akakiokota anasema alipokichukua tu akahisi kama kuna kitu kimemwingia mwilini. Tokea siku hiyo akawa na mapepo.
Unajua huko kwenye mito au ziwani au baharini mapepo yanawavamia watu wengi sana tena kwa kuwaonea tu.
Unaweza kusema kivipi? Biblia inatufundisha hivi. “Pepo mchafu amtokapo mtu, hupitia mahali pasipo maji, akitafuta mahali pa kupumzika; asipoona, husema, Nitairudia nyumba yangu niliyotoka. Hata afikapo, akaiona imefagiwa na kupambwa, ndipo huenda akachukua pepo wengine saba, walio waovu kuliko yeye mwenyewe, wakaingia na kukaa humo; na mtu yule hali yake ya mwisho huwa mbaya kuliko ya kwanza.” (Luka 11:24-26)
Ukiipitia hiyo mistari utaona kuwa hayo mapepo yanapotolewa yanatakiwa yaende huko majini. Sasa kabla hayajaenda huko yanatafuta mahali nchi kavu, na watu wengi wakienda huko kuoga ndipo wengi huonewa na hayo mapepo na kuwavamia.
Kama unataka kujua kwa uzuri wewe fuatilia watu wanaoishi jirani na bahari na mito nk. Ukifanya utafiti utaona watu wengi wa maeneo hayo wanasumbuliwa mno na mapepo au majini kuliko wale wa maeneo ambayo hayana maji kwa wingi wengi huitwa watu wa pwani.
Sina maana maeneo hayo mengine hakuna shida, yana shida lakini kitakwimu utagundua watu wa maeneo ya pwani au kando kando ya mito wengi hujikuta wakionewa sana. Hebu tuangalie sababu nyingine.
SABABU YA SITA; KUWEPO MAHALI PENYE UWEPO MBAYA USIO NA HOFU YA MUNGU
Moja ya sababu inayoweza kuwa chanzo cha mtu kuvamiwa na mapepo ni maeneo hatarishi ambayo kwa kweli yametengenezwa maalumu kwa ajili ya kufanyia maovu.
Nitakupa mfano. Watu wengi hawajui kuwa unaposhinda maeneo kama baa, vilabuni au kwenye majumba yaitwayo casino ni rahisi mno kujikuta huko ukivamiwa na mapepo kwa sababu ni maeneo ambayo hayana hofu ya Mungu.
Hofu ya Mungu inaweza kuwepo mahali na kuna mahali inaweza isiwepo kabisaa. Angalia mfano huu. Soma mistari hii. “Abimeleki akamwambia Ibrahimu, Umeona nini hata ukatenda jambo hili? Ibrahimu akasema, Kwa sababu naliona, Yakini hapana hofu ya Mungu mahali hapa, nao wataniua kwa ajili ya mke wangu.” (Mwanzo 20:10-11).
Ukiisoma hiyo mistari utagundua kuwa kuna maeneo hofu ya Mungu inaweza kuwepo na kuna maeneo hofu ya Mungu inaweza isiwepo kabisaa. Kama mahali hofu ya Mungu haipo sifa yake ni roho mbaya au mapepo kutawala eneo au mahali hapo.
Fikiria mtu anakwenda mahali watu wanacheza uchi kabisaa au sehemu watu wanacheza mziki lakini uchezaji wao kwa kweli unachochea watu kufanya ngono tu unafikiri eneo hilo ni roho gani inatawala?
Watu wengi hujikuta wakivamiwa na pepo wa uzinzi huko kwenye maeneo hayo. Fikiria mtu anakaa eneo akiangalia video za ngono. Wewe wafuatilie watu wanaozitazama video hizo utagundua wengi hujikuta mfumo mzima wa akili zao hata miili yao kuharibiwa na roho hizi mbaya.
Ninakuambia ukweli vijana wengi wamevamiwa na mapepo ya uzinzi kwa kutumia simu zao tu za mkononi au laptop zao au ipad zao. Nimewahi usikia ushuhuda wa watu wengi wakisema roho hizo za uzinzi walikutana nazo kwa kutumia mitandao ya ngono.
Kuna dada mmoja yeye alipokuwa anazifuatilia hizo video za ngono kwenye mitandao online akajikuta anaongea na mtu mmoja ambaye kumbe si mtu, unajua huyo mtu alimwambia atamjia usiku na kweli alimjia kiukweli kweli toka nchi moja.
Anadai tokea siku hiyo mambo yoote yaliharibika akawa mzinzi wa ajabu sana. Umewahi fikiria kwa nini adui anazitengeneza video za ngono? Nakuambia ukweli ni mlango mkubwa adui anautumia kuwapandikizia watu roho ya uzinzi.
Ndiyo unakuta watu wa jinsia moja wanaanza hapo kujamiiana nk. Hebu angalia tabia yako wewe ikoje?
Futa hizo video za ngono kama unazo, acha kabisaa kuzitafuta, tubu, ukiona huwezi kuziacha tafuta watumishi wakemee ni roho hiyo imekubana.
Naamini umenielewa. Barikiwa
Ukihitaji masomo yetu unaweza kuyapata kwa njia hizi zifuatazo:-
1. Tovuti yetu ya www.mwakatwila.org
2. YouTube - Mwakatwila au HUDUMA YA SOMA NENO LA MUNGU (HUSONEMU).
3. Facebook ingia katika hiyo tovuti au website yetu utaona alama ya facebook(f) like na utapata maelezo ya kujiunga au ingia Facebook halafu andika “SOMA NENO LA MUNGU”
4. Instagram ingia Instagram app halafu andika “Steven Mwakatwila”
5. DVDs 📀 au CDs 💿
6. VITABU.
NB: Wasiliana na mhudumu ofisini kwa namba +255 763 109 733, kupata VITABU, DVD & CD.
7. Kwa njia ya REDIO:- Utapata mafundisho yetu kwa redio zifuatazo:-
➖Rungwe FM 102.5 Kila siku ya Jumapili saa tatu mpaka saa nne usiku.
➖Baraka FM 107.7 Kila siku ya Jumanne saa kumi na mbili jioni mpaka saa moja usiku.
➖Bomba FM 104.1 Kila siku ya Ijumaa saa tatu usiku mpaka saa nne usiku.
Kwa Mawasiliano zaidi Utatupata kwa namba hizi:-
+255 754 849 924 Au +255 756 715 222
Wako
Mwl Steven & Beth Mwakatwila.
06/03/2019
No comments:
Post a Comment