Wednesday, May 13, 2020

Salamu – Aprili, 2020

Salamu – Aprili, 2020

Ninawasalimu wapendwa woote katika jina la Bwana Yesu Kristo. Tunamshukuru sana Mungu ambaye ametupa mwezi huu wa nne. Naamini unajua kabisa kuwa kupewa mwezi mwingine ni neema kubwa mno.

Hasa katika kipindi hiki ambacho dunia inapitia janga kubwa la tauni ya Corona. Na hapa nchini imefika na tayari watu wengi wameambukizwa na wengine wamefariki na serikali imetoa utaratibu wa nini kila mtu afanye ikiwemo kunawa, kutokukaa kwenye mikusanyiko na hata vyuo na shule zote kufungwa.

Ni kipindi kigumu mnoo, nchi zingine wamefungiwa watu ndani kwa kupewa amri ya kutokutoka nje. Tunashukuru serikali yetu imeweka utaratibu wa kila mtu afanye kazi na pia imeruhusu ibada. Hili ni jambo la kumshukuru Mungu sana.

Somo hili ambalo tunalipata hapa linaweza kukusaidia sana katika kipindi hiki. Ngoja nikupe taarifa fupi ya mwezi uliopita. Mwezi uliopita tulikuwa na semina Bethlehemu na Mbalizi Bethani KKKT. Semina hii tulianza nayo mwishoni mwa mwezi wa pili na tukaendelea nayo mpaka tarehe tano mwezi wa nne.

Ninapokuletea salamu hizi nipo jijini Mbeya kwa sababu ratiba yetu ya mwezi huu ilikuwa tuwe Dodoma na Manyoni. Kutokana na mambo yaliyo nje ya uwezo wetu semina hizi tumeziahirisha.

Hiyo ndiyo taarifa fupi ya huduma mwezi uliopita. Hebu tusogee mbele kidogo katika salamu za mwezi huu. Kumbuka tuna salamu zenye kichwa.

MAMBO MUHIMU UNAYOTAKIWA UYAFANYE ILI UPATE WOKOVU (ENEO LA KUOKOLEWA KATIKA KIPINDI CHA MAJANGA ULIMWENGUNI)

Tuangalie jambo la tano

JAMBO LA TANO: JIFUNZE KUFANYA TOBA BILA KUANGALIA UKAMILIFU WOWOTE

Sikiliza, Unapomwendea Mungu katika kipindi hiki cha kumwomba kwa ajili ya wokovu wa tauni au nzige, n.k. iliyopelekwa na Mungu, unatakiwa wewe kama kuhani uhakikishe moyoni mwako unaondoa ile hali ya kujiona uko msafi.

Angalia mistari hii uone: “Maana kila kuhani mkuu aliyetwaliwa katika wanadamu amewekwa kwa ajili ya wanadamu katika mambo yamhusuyo Mungu, ili atoe matoleo na dhabihu kwa ajili ya dhambi; awezaye kuwachukulia kwa upole wao wasiojua na wenye kupotea, kwa kuwa yeye mwenyewe yu katika hali ya udhaifu; na kwa sababu hiyo imempasa, kama kwa ajili ya watu, vivyo hivyo kwa ajili ya nafsi yake mwenyewe, kutoa dhabihu kwa ajili ya dhambi.Na hapana mtu ajitwaliaye mwenyewe heshima hii, ila yeye aitwaye na Mungu, kama vile Haruni. Vivyo hivyo Kristo naye hakujitukuza nafsi yake kufanywa kuhani mkuu, lakini yeye aliyemwambia, Ndiwe mwanangu, Mimi leo nimekuzaa. kama asemavyo mahali pengine, Ndiwe kuhani milele Kwa mfano wa Melkizedeki. Yeye, siku hizo za mwili wake, alimtolea yule, awezaye kumwokoa na kumtoa katika mauti, maombi na dua pamoja na kulia sana na machozi, akasikilizwa kwa jinsi alivyokuwa mcha Mungu;” (Waebrania 5:1-7)

Ukiitazama hiyo mistari utaona tunafundishwa hapo kuwa, kuhani yeye mwenyewe anapomwendea Mungu inatakiwa atubie kwanza uovu wake. Kama anatakiwa atubue uovu wake maana yake anao.

Unaposoma maandiko ni kuhani wetu mkuu Bwana Yesu Kristo peke yake ndiye ambaye hakuwa na hatakuwa na dhambi. (Hakufanya ingawa alichukua dhambi za ulimwengu)

Katika kipindi cha kuutafuta uso wa Mungu makuhani lazima tujihadhari na mtazamo wa moyoni wa kujihesabia haki kama hao wengine woote tuwaonao wakikumbwa na hili tatizo kama ni wadhambi mnoooo kuliko sisi. MWENYE MASIKIO NA ASIKIE!!!!!

Ondoa moyoni mwako wazo kuwa Mungu atakusikia kwa sababu wewe ni mwenye matendo mema kuliko wengine, hapana. Mungu atakusikia kwa sababu kuu moja tu: umeona kosa lako wewe na hao wengine woote na umeamua kuliungama na kujutia. Ndiyo maana ya unyenyekevu.

Ngoja nikupe mfano huu uone hiki ninachotaka nikutazamishe Angalia Danieli alivyomwendea Mungu katika kipindi ambacho aliwakasirikia wana wa Israeli. 

“Katika mwaka wa kwanza wa Dario, mwana wa Ahasuero, wa uzao wa Wamedi, aliyetawazwa kuwa mfalme juu ya milki ya Wakaldayo; katika mwaka wa kwanza wa kumiliki kwake, mimi Danieli, kwa kuvisoma vitabu, nalifahamu hesabu ya miaka, ambayo neno la BWANA lilimjia Yeremia nabii, ya kuutimiza ukiwa wa Yerusalemu, yaani, miaka sabini. Nikamwelekezea Bwana Mungu uso wangu, ili kutaka kwa maombi, na dua, pamoja na kufunga, na kuvaa nguo za magunia na majivu. Nikamwomba BWANA, Mungu wangu, nikaungama, nikasema, Ee Bwana, Mungu mkuu, mwenye kutisha, ashikaye maagano na rehema kwao wampendao, na kuzishika amri zake; tumefanya dhambi, tumefanya ukaidi, tumetenda maovu, tumeasi, naam, hata kwa kuyaacha maagizo yako na hukumu zako; wala hatukuwasikiliza watumishi wako, manabii, ambao kwa jina lako walisema na wafalme wetu, na wakuu wetu, na baba zetu, na watu wote wa nchi. Ee Bwana, haki ina wewe, lakini kwetu sisi kuna haya ya uso, kama hivi leo; kwa watu wa Yuda, na kwa wenyeji wa Yerusalemu, na kwa Israeli wote, walio karibu na hao walio mbali, katika nchi zote ulikowafukuza, kwa sababu ya makosa yao waliyokukosa. Ee Bwana, kwetu sisi kuna haya ya uso, kwa wafalme wetu, na wakuu wetu, na baba zetu, kwa sababu tumekutenda dhambi. Rehema na msamaha ni kwa Bwana Mungu wetu, ingawa tumemwasi; wala hatukuitii sauti ya BWANA, Mungu wetu, kwa kwenda katika sheria zake, alizoziweka mbele yetu kwa kinywa cha watumishi wake, manabii. Naam, Israeli wote wameihalifu sheria yako, kwa kugeuka upande, wasiisikilize sauti yako; basi kwa hiyo laana imemwagwa juu yetu, na uapo ule ulioandikwa katika sheria ya Musa, mtumishi wa Mungu; kwa sababu tumemtenda dhambi.” (Danieli 9:1-11)

Ukiisoma hiyo mistari kumi na moja utagundua Danieli alikuwa anautafuta uso wa Mungu ili Mungu awaondolee adhabu ambayo aliwapelekea kwa sababu walimkasirisha. Aliwapeleka utumwani.

Danieli anaposimama ili azungumze na Mungu, kwanza alijua kabisa kuwa kisa cha tatizo wanalopitia ni dhambi, na alijua kabisa kuwa wanapitia adhabu kali sana.

Alipokuwa anaziungama dhambi mbele za Mungu, Danieli hakujihesabia haki kabisaa.

Sikiliza anasema hivi: “Nikamwomba BWANA, Mungu wangu, nikaungama, nikasema, Ee Bwana, Mungu mkuu, mwenye kutisha, ashikaye maagano na rehema kwao wampendao, na kuzishika amri zake; tumefanya dhambi, tumefanya ukaidi, tumetenda maovu, tumeasi, naam, hata kwa kuyaacha maagizo yako na hukumu zako;wala hatukuwasikiliza watumishi wako, manabii,”

Sikiliza kwa makini hayo maombi. Hasemi Wamefanya dhambi, hawajaisikiliza sauti ya watumishi wako, n.k. Anasema TUMEFANYA DHAMBI!!!!

Angalia kitu cha ajabu hapo, Danieli ni mtumishi wa Mungu kabisaa yeye ni nabii, angalia anasema hatukuwasikiliza watumishi wako. Anapotubu na kuungama anajihesabu yeye na hao wana wa Israeli ni wakosaji, ingawa kwa kweli utaona yeye huenda hakuifanya hiyo dhambi.

Sikiliza Bwana Yesu Kristo kama kuhani mkuu, aliichukua dhambi ya ulimwengu, unajua maana ya kuuichukua dhambi ya ulimwengu? Maana yake ni hii yeye alijitwisha hiyo dhambi kama ni yeye amefanya, ndiyo maana ya kuchukua dhambi ya ulimwengu.

Kwa maana nzuri maombi yake alisema vivyo hivyo kama alivyosema Danieli. Tumekutenda dhambi, n.k!!! Hakuwa na mtazamo kama huu wa kusema wamefanya dhambi …..

Ngoja nikuambie kitu; unapoiombea nchi yako ya Tanzania ili Mungu aiokoe katika majanga ya namna hii, unajua ni rahisi sana mpendwa ukiwa humu ndani ya nchi hii ukaona kama hao watu wa nchi za Ulaya, China, Amerika, Uarabuni n.k kama ni watu waovu kweli.

Ni rahisi kuona aisee Wachina bwana hawana Mungu wale ndiyo maana Mungu anawachapa kwa tauni hii ya Corona, ni rahisi kufikiri wazungu bwana wako tofauti na sisi Waafrika, wamemwacha Mungu, ndiyo maana ameamua kuwachapa. n.k.

Sikiliza mpendwa ukitaka leo hii kuwa kuhani wa ulimwengu yaani ukasimama mahali palipoharibika ulimwenguni jifunze kuomba maombi ya mfumo wa kutokuwaona hao ni waovu.

Ukisikia vita sehemu nchi fulani usifikiri Watanzania ni watu watakatifu kuliko hao wa taifa hilo. Au ukisikia nzinge na tauni inazipiga nchi fulani usifikiri sisi huku ni bora kuliko hao. Unapokwenda kuomba ulinzi kwa Mungu tubu mpendwa bila kujiona wewe ni bora.

Mimi naamini sisi Watanzania tutaokolewa tu kwa maombi ya toba na unyenyekevu. Si kwa sababu eti tuna Mungu.

Ngoja nikuulize swali wewe usemaye unajua hao wazungu walimwacha Mungu n.k. hivi kweli sisi Waafrika tuna Mungu? Hivi sisi Waafrika hatuna maovu? Wewe angalia namna tunavyoabudu miungu, angalia uzinzi, angalia uchawi, angalia namna wanaume wasivyowatunza wake zao na watoto.

Mungu anasema  hivi: “Lakini mtu ye yote asiyewatunza walio wake, yaani, wale wa nyumbani mwake hasa, ameikana Imani, tena ni mbaya kuliko mtu asiyeamini.” (1 Timotheo 5:8)

Maana yake Mkristo wa sifa hiyo hana tofauti na mpagani aliyesema hakuna Mungu.

Angalia nchi hii ilivyo na damu za watu wengi tu katika ardhi. Watu wengi hutoa mimba na kuua katika nchi hii nakuambia. Nchi hii ndiyo unasikia watu wanaua wanadamu wenzao wenye ulemavu wa ngozi ili tu wapate mali au ukuu, n.k.

Nchi hii ina watu wengi mnooo wanaoamini ushirikina, n.k. mtu haolewi mpaka akaloge, akiolewa analoga ili mume akae naye.

Nenda kanisani uone dhambi zipo nje nje, si watumishi na waaminio kila siku unaona na kusikia wameanguka na hata kuwa waongo angalia watu wengi mnoo wamejeruhiwa na kuumizwa mno na sisi watumishi katika nchi hii n.k.

Angalia dhambi ya uongo na udanganyifu n.k. Mimi nimejaliwa kutembea nchini humo, aisee nchi hii ina makahaba wengi mnoo na wengine wako makanisani kabisaa.

Angalia humo makanisani namna tupatavyo viongozi, wewe angalia namna nchi hii tunavyopata viongozi n.k. Wengi hutoa rushwa n.k.

Angalia kanisani namna tunavyoiba fedha na sadaka ya Mungu n.k. Umewahi ona mradi wa kanisa unaenda?

Angalia wivu na husuda na kudhulumu wajane na mayatima nchini humu tulivyo.

Angalia dhambi ya uvivu na kutolipa kodi sijakosea nasema kodi jinsi tulivyo.

Angalia namna tunavyoiba hiyo kodi ya serikali jinsi tulivyo. Angalia dhambi ya ulevi jinsi ilivyo nchini mwetu.

Kwa haya tu ninayokuambia unaweza ukaniambia sisi tupo salama kuliko hao wanaokufa huko na Corona? Na nchi zao kuliwa na nzige n.k?

Sikilizeni makuhani hebu tuondoe hayo mawazo ya kitoto kuwa sisi tuna haki kama taifa kuliko mataifa mengine.

Wengine wanasema unajua sisi Waafrika mafua hayatatudhuru. Sikia ni tauni. Kama tusipomwomba Mungu kwa unyenyekevu mafua tunayofikiri tutayamudu; yatatumudu nawaambia.

Katika kipindi kama hicho tusijiangalie tulivyo TUNAHITAJI TUMRUDIE MUNGU KWA KILIO BILA KUJIHESABIA HAKI. TUKUBALI KUWA TUMEMKOSEA MUNGU NA ANA HAKI KABISAA YA KUTURUDI. KINACHOTAKIWA TUKIFANYE TUSIJIONE NI WENYE HAKI.

Hatuna haki tuungane makuhani tumwambie BWANA TUMEKUFANYIA DHAMBI.

Danieli naamini hakufanya hayo maovu lakini alilijua hili ninalokuambia alisema tumekufanyia dhambi sisi na Israeli woote!!

Ukiwa ni mtu wa tabia hii, Mungu ni rahisi kukuokoa wewe na nyumba yako. Mungu alimsikia Danieli na makuhani wengine, fahamu hata wewe na mimi atatusikia tu. Hebu chukua hii na uanze kuliweka kwenye matendo.

Tuonane katika katika salamu za mwezi ujao.

Ukihitaji masomo yetu unaweza kuyapata kwa njia hizi zifuatazo;
1. App yetu ya huduma yenye jina  “HUSONEMU (MWAKATWILA)” utaipata Play Store kwenye link pale juu, ambapo kuna masomo mengi sana hapo.

2. Tovuti yetu ya www.mwakatwila.org

3. YouTube - Mwakatwila au HUDUMA YA SOMA NENO LA MUNGU (HUSONEMU).

4. Facebook ingia katika hiyo tovuti au website yetu utaona alama ya Facebook (f) "like" na utapata maelezo ya kujiunga au ingia Facebook halafu andika “SOMA NENO LA MUNGU”

5. Instagram ingia Instagram app halafu andika “Steven Mwakatwila

6. DVDs 📀 au CDs 💿

7. VITABU.

NB: Wasiliana na mhudumu ofisini kwa namba +255 763 109 733, ili kupata VITABU, DVD & CD.

8. Kwa njia ya REDIO:- Utapata mafundisho yetu kwa redio zifuatazo:-
➖Rungwe FM 102.5 Kila siku ya Jumapili  saa tatu mpaka saa nne usiku.
➖Baraka FM 107.7 Kila siku ya Jumanne saa kumi na mbili jioni mpaka saa moja usiku.
➖Bomba FM 104.1 Kila siku ya Ijumaa saa tatu usiku mpaka saa nne usiku.

9. Unaweza kutupata kwenye ONLINE RADIO yetu:- radio.mwakatwila.org

Kwa Mawasiliano zaidi Utatupata kwa namba hizi:-
+255 754 849 924 Au
+255 756 715 222

Wako
Mwl Mr & Mrs Steven Mwakatwila.

Salamu – Machi, 2020

Salamu – Machi, 2020

Bwana Yesu Kristo asifiwe sana. Ndugu yangu naamini unaendelea vema. Mwezi uliopita yaani wa pili nchi yetu imetangaza rasmi kuhusu ugonjwa wa Corona.

Kumbuka salamu hizi ndani yake zimebeba maarifa ya nini ufanye ikiwa mtu utakutana na tauni kama hizi. Fanyia kazi yale Mungu atakufundisha katika somo hili.

Mwezi uliopita tumekuwa na semina nyingi sana. Tumekuwa na semina iliyochukua wiki karibu mbili katika kanisa la KKKT Bethel. Tulikuwa na semina ilikuwa inaanza saa kumi na moja mpaka saa moja yaani Morning glory

Pia tulikuwa na kongamano la maombi pale KKKT Mjini ilikuwa ni kongamano la wiki mzima. Lilikuwa kongamano zuri. Pia tulipata nafasi ya kufundisha ibada mbili pale katika kanisa la Moravian Luanda.

Tunamshukuru Mungu kwa ajili ya maombi yenu. Pia nikuhimize ombea sana taifa letu madhara ya Corona yasitupate. Usikae kimya omba. Kumbuka tuna salamu zenye kichwa

MAMBO MUHIMU UNAYOTAKIWA UYAFANYE ILI UPATE WOKOVU (ENEO LA KUOKOLEWA KATIKA KIPINDI CHA MAJANGA ULIMWENGUNI)

Hebu tusogee mbele kidogo.

Katika salamu zilizopita tulijifunza jambo la tatu nalo lilikuwa LAZIMA UOMBE KWA MFUMO WA MAOMBI YA KUUTAFUTA USO WA MUNGU.

Katika salamu za mwezi huu wa tatu nataka tuendelee mbele kidogo kwenye eneo hilo hilo.

MUNGU HUWA ANA TABIA YA KUUFICHA USO WAKE

Angalia tena mistari hii: “BWANA akamtokea Sulemani usiku, akamwambia, Nimesikia uliyoyaomba, na mahali hapa nimejichagulia kuwa nyumba ya dhabihu. Nikizifunga mbingu isiwe mvua, tena nikiamuru nzige kula nchi, au nikiwapelekea watu wangu tauni; ikiwa watu wangu, walioitwa kwa jina langu, watajinyenyekesha, na kuomba, na kunitafuta uso, na kuziacha njia zao mbaya; basi, nitasikia toka mbinguni, na kuwasamehe dhambi yao, na kuiponya nchi yao. Sasa macho yangu yatafumbuka, na masikio yangu yatasikiliza maombi ya watu waombao mahali hapa.” (2 Mambo ya Nyakati 7: 12-15)

Ukiipitia hiyo mistari utaona Mungu anasema “….Watajinyenyekesha, na kuomba na kunitafuta uso …..” Ukisikia neno tafuta maana yake hakipo, kimepotea, au hakionekani au ni kazi kubwa kukiona, n.k.

Kwa nini Mungu katika kipindi hicho ambacho anasema akipeleka tauni inatakiwa watu walioitwa kwa jina lake waombe na wamtafute uso wake?

Uso wake unakuwa umekwenda wapi? Na kwa nini kipindi hicho watu wake walioitwa kwa jina lake waingie gharama ya kuutafuta uso wake? Kwa nini ajifiche? Mungu hawezi kusema mnitafute kama hajajitenga na hao watu.

Sikiliza, sababu inayomfanya Mungu aufiche uso wake katika kipindi hicho inakuwa ni kwasababu ya hasira yake

Sikiliza, Mungu huwa anakasirika sana tu, na pia huwa anafurahi sana tu n.k.

Hasira zake hutokea anapoona dhambi za wanadamu zimezidi kiwango, hapo ndipo hukasirika sana. Na akikasirika ana tabia ya kuachilia adhabu na anapoachilia adhabu huwa ana tabia kuuficha uso wake kwa sababu nyingi tu.

Moja ya sababu ya kuuficha uso wake ni hii, ILI ASISIKIE KILIO CHA HAO WATU!!!! Kwa maana nzuri ndani yake huwa anakuwa na hasira kali.

Mungu anapofurahia watu wake huzungumza nao uso kwa uso na haufichi uso wake. Na apouleta uso wake maana yake watu hao hukaa nuruni ambako ulinzi wao huwa ni mkubwa mno.

Mungu anapo wafurahia watu wake uso wake anauleta au haufichi, Angalia mistari hii uone hiki ninachokuambia: “Naye BWANA akasema na Musa uso kwa uso, kama vile mtu asemavyo na rafiki yake. Kisha akageuka akarejea hata maragoni; bali mtumishi wake Yoshua, mwana wa Nuni, naye ni kijana, hakutoka mle hemani.” (Kutoka 33:11)

Mungu alizungumza hapo na Musa uso kwa uso kabisaa kama rafiki yake. Angalia mistari hii mingine utaona kitu cha kujifunza katika eneo ambalo anasema wakiutafuta uso wake.

“BWANA akanena na Musa, Haya, ondokeni, katokeni hapo, wewe na hao watu uliowaleta wakwee kutoka nchi ya Misri, waende nchi hiyo niliyomwapia Ibrahimu, na Isaka, na Yakobo, niliposema, Nitakipa kizazi chako nchi hii; nami nitamtuma malaika aende mbele yako; nami nitawafukuza Mkanaani, na Mwamori, na Mhiti, na Mperizi, na Mhivi, na Myebusi; waifikilie nchi imiminikayo maziwa na asali; kwa maana mimi sitakwenda kati yenu; kwa sababu ninyi ni watu wenye shingo ngumu; nisiwaangamize ninyi katika njia. Watu waliposikia habari hizo mbaya wakaomboleza wala hapana mtu aliyevaa vyombo vyake vya uzuri. BWANA akamwambia Musa, Waambie wana wa Israeli, Ninyi ni watu wenye shingo ngumu; kama mimi nikiingia kati yenu dakika moja, nitawaangamiza; basi sasa vueni vyombo vyenu vya uzuri ili nipate kujua nitakalowatenda. …….Basi, sasa nakuomba, ikiwa nimepata neema mbele zako, unionyeshe njia zako, nipate kukujua, ili nipate neema mbele zako; ukakumbuke ya kuwa taifa hilo ndilo watu wako. Akasema, Uso wangu utakwenda pamoja nawe, nami nitakupa raha. Naye akamwambia, Uso wako usipokwenda pamoja nami, usituchukue kutoka hapa. Kwa maana itajulikanaje kuwa nimepata neema mbele zako, mimi na watu wako? Siyo kwa sababu unakwenda pamoja nasi, hata mimi na watu wako tutengwe na watu wote walio juu ya uso wa nchi? BWANA akamwambia Musa, Nitafanya na neno hili ulilolinena, kwa maana umepata neema mbele zangu, nami nakujua jina lako.” (Kutoka 33:1-5 na 13-17)

Ukiipitia hiyo mistari utaona Mungu alipowakasirikia wana wa Israeli aliuficha uso wake. Alisema akiingia kati yao au akiuleta uso wake kwa sababu ya dhambi zao atawaangamiza dakika moja.

Sikiliza, Mungu anapokasirika na kuachia adhabu fahamu anakuwa ameuficha uso wake. Kipindi hicho usifikiri utakutana naye kama ulivyokuwa unakutana naye zamani.

Ngoja nikupe mfano. Mungu alipowakasirikia wana wa Israeli baada ya kuabudu sanamu, Musa alikaa mlimani akiutafuta uso wa Mungu kwa muda wa siku arobaini.

Fikiria siku ya arobaini ndipo akauonyesha uso wake na kumwambia Musa amekubali.

Kwa lugha nzuri siku zote hizo thelathini na tisa Mungu aliuficha uso wake.

Ngoja nikupe mfano mwingine. Unakumbuka Bwana wetu Yesu Kristo alipoichukua tu dhambi ya ulimwengu Mungu aliyekuwa pamoja naye siku zote aliuficha uso wake?

Bwana Yesu Kristo alijua ndiyo maana alilia “Baba mbona umeniacha?” Uso wake Mungu ulifichwa, dunia yote ikawa giza, muda wa masaa matatu hivi. Alipourudisha uso wake nchi ikapata nuru tena.

Mungu anapouficha uso wake fahamu giza hutawala, hapo ndipo wanadamu hukutana na magumu kutoka ulimwengu wa giza kwa kiwango cha juu mno.

Sikiliza nikuambie. Uso wa Mungu unapotutazama humu ulimwenguni ulinzi wa ulimwengu na kila kitu huwa mkubwa. Mimi nakuambia Mungu akificha uso wake ambao ni nuru kwa ulimwengu watu waishio humo ulimwenguni hujikuta kwenye misiba ya kila aina.

Uso wake unapokwenda nasi fahamu anatuona na anatuhurumia mnooo na kutuokoa na maradhi nk. Sasa Anapokasirika na kuachilia tauni ulimwenguni au nzige n.k. ana tabia ya kuuficha uso wake ili asiwaone wanadamu wanavyoteseka. Ili akawaokoe. KWA SABABU ANA HURUMA SANA!!!

Mungu ana akili nyingi mnoo anajua akituangalia tu atatuonea huruma kwa hiyo hukimbilia kuuficha uso wake ili asiangalie.

Umewahi kufikiri siku ile ya Sodoma na Gomora kwa nini hakwenda kule? Unaweza kuniuliza kivipi. Sikiliza maneno haya: “BWANA akasema, Kwa kuwa kilio cha Sodoma na Gomora kimezidi, na dhambi zao zimeongezeka sana, basi, nitashuka sasa nione kama wanayotenda ni kiasi cha kilio kilichonijia; na kama sivyo, nitajua. Basi wale watu wakatoka huko wakaelekea Sodoma; lakini Ibrahimu alikuwa akali akisimama mbele za BWANA. Ibrahimu akakaribia, akasema, Je! Utaharibu mwenye haki pamoja na mwovu? …..Akasema, Bwana asiwe na hasira, nami nitasema mara hii tu, Huenda wakaonekana huko kumi? Akasema, Sitaharibu kwa ajili ya hao kumi. Basi BWANA alipokwisha kuzungumza na Ibrahimu, akaenda zake; Ibrahimu naye akarudi mahali pake….” (Mwanzo 18:20-23 na 32)

Angalia na hii mistari uone ninachokuambia: “Basi, wale malaika wawili wakaja Sodoma jioni; na Lutu alikuwa amekaa mlangoni pa Sodoma. Lutu akawaona akaondoka akaenda kuwalaki, akainama kifudifudi.” (Kutoka 19:1)

Ukiipitia hiyo mistari utaona Mungu alipomfuata Ibrahimu hakuwa peke yake, alikuwa na malaika wawili. Mungu alibaki na Ibrahimu akiongea naye kwa ajili ya Sodoma na Gomora, wale malaika wawili wakawaacha wakiongea.

Mungu alipomaliza mazungumzo na Ibrahimu aliondoka. Biblia haisemi alienda Sodoma na Gomora. Walioingia Sodoma na Gomora ni malaika wawili. Jiulize Mungu alienda wapi?

Mimi naamini alirudi mbinguni na alienda kuuficha uso wake. Kwani alichokitarajia kukipata kutoka kwa Ibrahimu alikikosa, nacho kilikuwa ni utetezi. Ibrahimu hakufanya toba iliyoshiba kwa ajili ya watu wa Sodoma na Gomora kama Musa alivyofanya kwa ajili ya wana wa Israeli.

Malaika walichoma Sodoma na Gomora kilio chao hakikusikika kwa sababu Mungu aliuficha uso wake asione.

Mungu hapendi kututesa au kutuua: “Kwa kuwa Bwana hatamtupa mtu Hata milele. Maana ajapomhuzunisha atamrehemu, Kwa kadiri ya wingi wa huruma zake. Maana moyo wake hapendi kuwatesa wanadamu. Wala kuwahuzunisha.” (Maombolezo ya Yeremia 3:31-33)

Mungu ukiona ameamua kuachia tauni fahamu hata uso wake huuficha kwa sababu hapendi kuona wanadamu wakiteseka.

Mungu ni Baba yetu, ndiye aliyetuumba, kama mzazi yeyote yule mwenye uungwana ana tabia ya kuwachapa au kuwapiga watoto wake ili wawe na adabu.

Unajua watu wengi hawajui kuwa Mungu anapiga. Angalia mistari hii: “Basi hivi karibu nitamwaga ghadhabu yangu juu yako, nitazitimiza hasira zangu juu yako, nami nitakuhukumu sawasawa na njia zako; nami nitakupatiliza machukizo yako yote. Jicho langu halitaachilia, wala sitaona huruma; nitakupatiliza njia zako na machukizo yako yote yatakuwa katikati yako; nanyi mtajua ya kuwa mimi, BWANA, napiga.” (Ezekieli 7:8-9)

Umesikia maneno hayo mpendwa? Anasema “nanyi mtajua ya kuwa mimi, BWANA, napiga.” Mungu akikasirika anapiga tena anapiga kweli. Unaweza kusema haiwezekani bwana!!

Umewahi kufikiria hivi. Kama Mungu huyu alimwua mtoto wake wa kwanza ampendaye sana yaani Bwana Yesu Kristo ili amwokoe mwanadamu?

Kama aliweza kuua mtoto wake mpendwa asiye na dhambi kwa ajili ya wenye dhambi unafikiri itakuwa shida kuwaua hao wanadamu halafu wenye dhambi na jeuri na ukorofi?

Mimi nawaambia ukweli Mungu anaweza kabisa kuruhusu tauni na akauficha uso wake kabisaa ili dawa au adhabu iwaingie vizuri wanadamu!!!!

Angalia mistari hii, tena ipo katika agano jipya: “tena mmeyasahau yale maonyo, yasemayo nanyi kama kusema na wana, Mwanangu, usiyadharau marudia ya Bwana, Wala usizimie moyo ukikemewa naye; Maana yeye ambaye Bwana ampenda, humrudi, Naye humpiga kila mwana amkubaliye. Ni kwa ajili ya kurudiwa mwastahimili; Mungu awatendea kama wana; maana ni mwana yupi asiyerudiwa na babaye? Basi kama mkiwa hamna kurudiwa, ambako ni fungu la wote, ndipo mmekuwa wana wa haramu ninyi, wala si wana wa halali. Na pamoja na hayo tulikuwa na baba zetu wa mwili walioturudi, nasi tukawastahi; basi si afadhali sana kujitia chini ya Baba wa roho zetu na kuishi? Maana ni hakika, hao kwa siku chache waliturudi kama walivyoona vema wenyewe; bali yeye kwa faida yetu, ili tuushiriki utakatifu wake. Kila adhabu wakati wake haionekani kuwa kitu cha furaha, bali cha huzuni; lakini baadaye huwaletea wao waliozoezwa nayo matunda ya haki yenye amani.” (Waebrania 12:5-11)

Mungu anaweza kabisa kuturudi sisi watoto wake. Fikiria wasio watoto wake itakuwaje? Kumbuka watoto wake tu huturudi ili tuwe na adabu fikiria watu wake waliomo ulimwenguni je!

Kama anaweza kupiga kuanzia madhabahuni huko nje itakuwaje? Hebu tuliangalie pia jambo la Nne

JAMBO LA NNE: JIFUNZE KUUTAFUTA USO WAKE KWA TOBA NENDA KWA KUTUMIA NAFASI YA UKUHANI TU.

Sikiliza Mungu anapokuwa katika hali ya namna hii lazima wamwombao wabadili mfumo wa maombi yao, inatakiwa waanze kuomba maombi ya toba tu.

Pia fahamu ili Mungu asikie huko aliko katika kipindi kama hicho atawasikia makuhani tu.

Kwa sababu kuhani ni mpatanishi, au kwa lugha nzuri ni mwombezi. Kuhani si mchungaji, au nabii, au mwalimu, au mtume. Mungu akikasirika na kuuficha uso wake ni kuhani peke yake anaweza kumsikiliza.

Kipindi hicho hasikilizagi nabii, mwalimu, mchungaji, mwinjilisti au mtume. Ngoja nikupe mfano uone: “Musa akamwambia Haruni, Haya, shika chetezo chako, ukatie moto ndani yake, moto wa madhabahuni, kisha utie na uvumba juu ya moto, ukakichukue haraka, wende nacho katika huo mkutano, ukawafanyie upatanisho; kwa kuwa ghadhabu zimetoka kwa BWANA; hiyo tauni imeanza. Basi Haruni akakishika chetezo kama Musa alivyonena, akapiga mbio akaenda katikati ya mkutano; na tazama, tauni ilikuwa imeanza kati ya watu; akatia uvumba juu ya moto na kufanya upatanisho kwa ajili ya hao watu. Akasimama kati ya hao waliokufa na hao waliokuwa wakali hai; tauni ikazuiwa. Basi waliokufa kwa tauni walikuwa kumi na nne elfu na mia saba, zaidi ya hao waliokufa katika jambo la Kora. Haruni akamrudia Musa pale mlangoni pa hema ya kukutania; hiyo tauni ikazuiwa.” (Hesabu 16:46-50)

Ukiipitia hiyo mistari utaona hiki ninachokuambia. Musa ni nabii hakugusa chetezo wala hakuingia katika huduma ya kufanya upatanisho.

Huduma hiyo ya upatanisho aliifanya kuhani tu. Mungu anapoleta tauni na tauni ikaanza kuua watu fahamu uso wake anakuwa ameuficha. Wanaoweza kumbembeleza na uso wake ukaonekana ni makuhani peke yao.

Hapo hakuna wafalme, wakuu, manabii au walimu, au waimbaji, au wainjilisti au mitumie. Atawasikiliza makuhani peke yao.

Sikiliza makuhani leo hii ni kanisa, unaweza kuwa mchungaji au askofu au mwalimu au padri au mwinjilisti au mtume au nabii lakini usiwe kuhani.

Katika agano jipya kuhani ni mtu yeyote aliyenunuliwa kwa damu ya Bwana Yesu Kristo

“Tena zitokazo kwa Yesu Kristo, shahidi aliye mwaminifu, mzaliwa wa kwanza wa waliokufa, na mkuu wa wafalme wa dunia. Yeye atupendaye na kutuosha dhambi zetu katika damu yake, na kutufanya kuwa ufalme, na makuhani kwa Mungu, naye ni Baba yake; utukufu na ukuu una Yeye hata milele na milele. Amina.” (Ufunuo 1:5-6)

Angalia na mistari: “Nao waimba wimbo mpya wakisema, Wastahili wewe kukitwaa hicho kitabu na kuzifungua muhuri zake; kwa kuwa ulichinjwa, ukamnunulia Mungu kwa damu yako watu wa kila kabila na lugha na jamaa na taifa, ukawafanya kuwa ufalme na makuhani kwa Mungu wetu; nao wanamiliki juu ya nchi.” (Ufunuo 5:9-10)

Kila aliyenunuliwa kwa hiyo damu ni kuhani. Sikiliza makuhani, wewe ndiwe pekee umewekewa kazi hii ya kufanya maombezi yaliyobeba toba iletayo upatanisho ili Mungu aturehemu na tauni izuiliwe.

 Kanisa tusipojitambua katika kipindi na sisi tukakaa kama watu wengine nawaambia ukweli uso wa Mungu utakuwa mbali; ataendelea kuuficha tu na tauni haitazuiliwa ulimwenguni.

Angalia mistari hii uone hiki ninachokuambia: “Pigeni tarumbeta katika Sayuni, Takaseni saumu, kusanyeni kusanyiko kuu; Kusanyeni watu, litakaseni kusanyiko, Kusanyeni wazee, kusanyeni watoto, Na hao wanyonyao maziwa; Bwana arusi na atoke chumbani mwake, Na bibi arusi katika hema yake. Hao makuhani, wahudumu wa BWANA, na walie Kati ya patakatifu na madhabahu, Na waseme, Uwaachilie watu wako, Ee BWANA, Wala usiutoe urithi wako upate aibu, Hata mataifa watawale juu yao; Kwani waseme kati ya watu, Yuko wapi Mungu wao? Hapo ndipo BWANA alipoona wivu kwa ajili ya nchi yake, akawahurumia watu wake. BWANA akajibu, akawaambia watu wake; Tazameni, nitawaletea nafaka, na divai, na mafuta, nanyi mtashiba kwa vitu hivyo; wala sitawafanya tena kuwa aibu kati ya mataifa; lakini jeshi lililotoka kaskazini nitaliondolea mbali nanyi, nami nitalifukuza mpaka nchi ya ukame na ukiwa; sehemu yake iliyo mbele itaingia katika bahari ya mashariki, na sehemu yake iliyo nyuma itaingia katika bahari ya magharibi; na uvundo wake utapanda juu, na harufu yake mbaya itapanda juu, kwa sababu ametenda mambo makubwa.” (Yoeli 2:17-20)

Ukiipitia hiyo mistari utaona Mungu aliuficha uso wake ili awaadhibu wanadamu. Alichokifanya ili aone yaani uso wake urudi kuwatazama hao watu, aliagiza makuhani walie au wakamtafute.

Hakusema manabii, n.k. Alisema makuhani. Sikilizeni kanisa, MUNGU ANAWASUBIRI NINYI MLIE. Bahati mbaya kipindi kama hiki akili ya kanisa inakuwa kwa viongozi wa nchi, au kwa maaskofu au kwa manabii, n.k.

Sikiliza wewe kuhani yaani wewe uliyenunuliwa kwa damu ya Bwana Yesu Kristo unaweza ukawa askofu, kiongozi fulani au mchungaji, mwinjilisti na inawezekana kabisa usiwe kiongozi au nabii au mwinjilisti, n.k. ANZA KUUTAFUTA USO WA MUNGU KWA TOBA UONAPO TAUNI AU NZIGE NK VIMEPELEKWA ULIMWENGUNI NA MUNGU.

Utafute uso wa Mungu, ingia gharama, kwa ajili ya watu wako, nchi yako, taifa lako, na ulimwengu woote.

Tubia maovu au dhambi au makosa ya aina yoyote ambayo ndiyo chanzo cha hasira kutoka kwa Mungu.

Jifunze KULIA, SI KUKEMEA TUUUU MPENDWA; KUHANI LIA MBELE ZAKE MUNGU NDIPO USO WAKE UTAONEKANA NA TAUNI AU NZINGE AU MAJANGA YOYOTE KAMA CORONA N.K ZITAZUIWA KWA MAARIFA ATAKAYOYAACHILIA.

Au kama tauni imepelekwa, Mungu akiuleta uso wake fahamu atawaokoa wale waliao kwa ajili ya uovu utendwao katika mji wao au taifa lao au nyumba yao.

Nataka kukutia moyo usijidharau wewe kuhani ndiwe pekee mwenye kuurejesha uso wa Mungu ili uende na watu walioko duniani.

Unaweza kumshirikisha mpendwa mwingine ujumbe huu.

Tuonane mwezi ujao katika kona hii ya salamu za mwezi. BARIKIWA

Ukihitaji masomo yetu unaweza kuyapata kwa njia hizi zifuatazo;
1. App yetu ya huduma yenye jina  “HUSONEMU (MWAKATWILA)” utaipata Play Store kwenye link pale juu, ambapo kuna masomo mengi sana hapo.

2. Tovuti yetu ya www.mwakatwila.org

3. YouTube - Mwakatwila au HUDUMA YA SOMA NENO LA MUNGU (HUSONEMU).

4. Facebook ingia katika hiyo tovuti au website yetu utaona alama ya Facebook (f) "like" na utapata maelezo ya kujiunga au ingia Facebook halafu andika “SOMA NENO LA MUNGU”

5. Instagram ingia Instagram app halafu andika “Steven Mwakatwila

6. DVDs 📀 au CDs 💿

7. VITABU.

NB: Wasiliana na mhudumu ofisini kwa namba +255 763 109 733, ili kupata VITABU, DVD & CD.

8. Kwa njia ya REDIO:- Utapata mafundisho yetu kwa redio zifuatazo:-
➖Rungwe FM 102.5 Kila siku ya Jumapili  saa tatu mpaka saa nne usiku.
➖Baraka FM 107.7 Kila siku ya Jumanne saa kumi na mbili jioni mpaka saa moja usiku.
➖Bomba FM 104.1 Kila siku ya Ijumaa saa tatu usiku mpaka saa nne usiku.

9. Unaweza kutupata kwenye ONLINE RADIO yetu:- radio.mwakatwila.org

Kwa Mawasiliano zaidi Utatupata kwa namba hizi:-
+255 754 849 924 Au
+255 756 715 222

Wako
Mwl Mr & Mrs Steven Mwakatwila.


Monday, May 11, 2020

Salamu – Februari, 2020

Salamu – Februari, 2020

Ndugu yangu ninakusalimu katika jina la Bwana Yesu Kristo. Nimekuletea salamu za mwezi huu wa pili. Mwezi wa kwanza umeanza kwetu tukiwa na semina Katika kanisa la Bethel KKKT, tukawa na semina Chuo cha wachungaji cha Moravian Utengule na pia tulikuwa na semina maalumu ya shukrani jijini Mbeya.

Semina hizi zilikuwa za baraka sana. Hebu tuanze kupokea salamu za mwezi huu. Kumbuka tuna salamu zenye kichwa;
MAMBO MUHIMU UNAYOTAKIWA UYAFANYE ILI UPATE WOKOVU (ENEO LA KUOKOLEWA KATIKA KIPINDI CHA MAJANGA ULIMWENGUNI)

Katika salamu zilizopita nilikuonyesha  mambo mawili ambayo unatakiwa uyafanye ili upate kuokolewa na tauni iliyoachiliwa ulimwenguni kutoka kwa Mungu. Ambayo yalikuwa;

Jambo la kwanza: Ni lazima uitwe kwa jina la Bwana. Tukaona lazima umwamini na umpokee Bwana Yesu Kristo kama Bwana na mwokozi wako

Jambo la pili: Ni lazima uwe mnyenyekevu. Naamini ulijifunza kitu. Hebu tusogee mbele kidogo tuliangalie jambo la tatu.

JAMBO LA TATU: LAZIMA UOMBE KWA MFUMO WA MAOMBI YA KUUTAFUTA USO WA MUNGU

Angalia hii mistari tena: “BWANA akamtokea Sulemani usiku, akamwambia, Nimesikia uliyoyaomba, na mahali hapa nimejichagulia kuwa nyumba ya dhabihu. Nikizifunga mbingu isiwe mvua, tena nikiamuru nzige kula nchi, au nikiwapelekea watu wangu tauni; ikiwa watu wangu, walioitwa kwa jina langu, watajinyenyekesha, na kuomba, na kunitafuta uso, na kuziacha njia zao mbaya; basi, nitasikia toka mbinguni, na kuwasamehe dhambi yao, na kuiponya nchi yao. Sasa macho yangu yatafumbuka, na masikio yangu yatasikiliza maombi ya watu waombao mahali hapa.” (2 Mambo ya Nyakati 7: 12-15)

Ninachotaka tukione katika hili jambo la tatu ni hiki Mungu asemacho hapo kuwa. “Tena nikiamuru nzige kula nchi, au nikiwapelekea watu wangu tauni; ikiwa watu wangu, walioitwa kwa jina langu, watajinyenyekesha, na kuomba, na kunitafuta uso…”

Mungu anaporuhusu tauni kama Corona n.k au nzige au vita n.k, ili iwapige watu na kuua miili yao, ili awaokoe hao watu na hiyo tauni au awalinde hao watu na hiyo tauni anasema ni lazima hao watu waingie katika maombi ya kuutafuta uso wake.

kumbuka hao watu wanaoambiwa wafanye hivyo ni wale walioitwa kwa jina lake na walio wanyenyekevu. Ili leo hii mpendwa Mungu akulinde na kukuokoa na tauni inatakiwa ujifunze kuomba ili Mungu akuokoe wewe, nduguzo, taifa lako, n.k.

Unajua unaweza ukasema si nimeokoka mimi na nina matendo mema mimi tauni haitanipata kwa sababu nimeahidiwa na Mungu kulindwa. Sikia ndugu, Mungu huyo aliyetuahidi kutulinda ndiye anatupa maarifa hapo ya nini tufanye ili tauni isitupige.

Anasema watu walioitwa kwa jina lake walio wanyenyekevu lazima waombe tena maombi ya kuutafuta uso wake.

Unapokutana na kipindi cha namna hiyo fahamu ni kipindi ambacho kwa kweli wewe uliyeokoka unatakiwa uombe kuliko kipindi chochote. Usijidanganye kuwa utapona kisa umeokoka. Msikilize Mungu anasema wakijinyenyekesha na kuomba na kuutafuta uso wangu….!!!!
Watoto wa Mungu wengi sana hawajui pona yao itategemea kiwango cha wao kuomba.

Ngoja nikupe mfano huu. Msikilize Bwana Yesu Kristo asemavyo: “Alipofika mahali pale aliwaambia, Ombeni kwamba msiingie majaribuni. Mwenyewe akajitenga nao kama kiasi cha kutupa jiwe, akapiga magoti akaomba, akisema, Ee Baba, ikiwa ni mapenzi yako, uniondolee kikombe hiki; walakini si mapenzi yangu, bali yako yatendeke. [Malaika kutoka mbinguni akamtokea akamtia nguvu.Naye kwa vile alivyokuwa katika dhiki, akazidi sana kuomba; hari yake ikawa kama matone ya damu yakidondoka nchini.] Alipoondoka katika kuomba kwake, akawajia wanafunzi wake, akawakuta wamelala usingizi kwa huzuni. Akawaambia, Mbona mmelala usingizi? Ondokeni, mkaombe, msije mkaingia majaribuni.” (Luka 22:40-46)

Ukiipitia hiyo mistari utaona hiki ninachokuambia. Bwana Yesu Kristo aliwapa hao ndugu maarifa ya nini wafanye ili wasiingie kwenye magumu. Kumbuka magumu hayo Mungu ndiye aliyeyaruhusu.

Unaweza kuniuliza ulijuaje? Sikiliza, Bwana Yesu Kristo aliwaambia hao ndugu shetani anawataka ili awapepete kama ngano. Umewahi kujiuliza aliwataka kwa nani? Angalia alitafuta kibali kwa Mungu. 

Bwana Yesu alilijua hili, akawahi haraka kuwapa taarifa hao walioitwa kwa jina lake kuwa na wao waende kwa Mungu wakaombe Mungu awapitishe mbali na ombi hilo.

Wao walizembea walilala. Unaweza kujiuliza kwa nini Mungu asiwaokoe tu na hilo jaribu au teso au gumu? Sikiliza, Mungu ameweka utaratibu huo tokea zamani sana. Usipoomba yeye haangalii tu kuwa wewe ni nani kwake.

Ngoja nikupe mfano huu labda utaelewa. Siku moja wana wa Israeli waliambiwa na Mungu kuwa, Mungu amepania kuleta tauni Misri. Tauni iliyowalenga watu wa sifa ya wazaliwa wa kwanza, wawe wanyama, n.k.
Ili tauni hiyo isiwapige wazaliwa wa kwanza wa Waisraeli ambao ni watu wa Mungu walioitwa kwa jina lake, Mungu aliwaambia kila mmoja akaweke alama katika milango ya nyumba zao.

Ili tauni ikianza isiwapige hao wazaliwa wa kwanza waliomo ndani ya nyumba zao. Fikiria kwa nini asiwaokoe tu? Kwani alikuwa hawajui hao wazaliwa wa kwanza wa wana Waisraeli? 
Mungu aliwafahamu wazaliwa wa kwanza wooote wawe wa Wamisri au wa wana wa Israeli. Lakini alitafuta kuona unyenyekevu na uhitaji wa kuokolewa wa hao wana wa Israeli.

Fahamuni wapendwa kuwa Mungu anatafuta kuona mtu akiomba kuokolewa, asipoomba usifikiri atamwokoa.

Ngoja nikupe mfano huu mwingine. Angalia mistari hii: “Hata baada ya siku zile nyingi mfalme wa Misri akafa; wana wa Israeli wakaugua kwa sababu ya ule utumwa, wakalia; kilio chao kikafika juu kwa Mungu kwa sababu ya ule utumwa. Mungu akasikia kuugua kwao, Mungu akakumbuka agano lake alilolifanya na Ibrahimu na Isaka na Yakobo. Mungu akawaona wana wa Israeli, na Mungu akawaangalia.” (Kutoka 2:23-25)
Ukiipitia hiyo mistari utaona kitu hiki ninachokufundisha. Hao ndugu, Mungu aliwaona na kuwaangalia na kulikumbuka agano hilo kipindi hao watu walipotafuta msaada kutoka kwake, tena walipolia na kuugua kwa sababu ya ule utumwa.

Fahamu, walipokuwa hawalii, hawaugui, kwa sababu ya utumwa wao Mungu hakuwaangalia wala hakuwaona.

Kumbuka sana hao ndugu ni watu wa Mungu walioitwa kwa jina lake kabisaa. Ili Mungu awaokoe alisubiri waombe kwa maombi ya mfumo huo ndipo akawaokoa.

JIFUNZE KUJIWEKEA ALAMA ILI TAUNI ISIKUPATE Unapoingia kuomba kwa ajili ya tauni ili isikupate ndipo unapojiwekea alama maalumu ili tauni inapoijilia nchi yako au mji wako ikiona alama hiyo inakupita.

Usipojiwekea hiyo alama fahamu itakupiga tu haitajalisha wewe ni askofu, daktari, mchungaji, n.k.

Ngoja nikupe mfano huu ili uone tauni inaletwaje katika ulimwengu wa roho na watu watakaopona wanakuwa na sifa zipi hasa.

Pata picha hii ndiyo utanielewa sana ninapokuambia omba, Angalia mistari hii:
“Kisha akalia kwa sauti kuu masikioni mwangu, akisema, Waamuru wale wanaousimamia mji wakaribie, kila mmoja na awe na kitu chake cha kuangamiza mkononi mwake. Na tazama, watu sita wakaja, wakitokea kwa njia ya lango la juu, lielekealo upande wa kaskazini, kila mmoja ana kitu chake cha kufisha mkononi mwake; na mtu mmoja kati yao amevaa bafta, naye ana kidau cha wino cha mwandishi kiunoni. Wakaingia, wakasimama karibu na madhabahu ya shaba. Na huo utukufu wa Bwana wa Israeli ulikuwa umepanda juu kutoka kwa kerubi, ambaye ulikuwa juu yake, mpaka kizingiti cha nyumba; akamwita mtu yule aliyekuwa amevaa bafta, mwenye kidau cha wino cha mwandishi kiunoni. BWANA akamwambia, Pita kati ya mji, kati ya Yerusalemu, ukatie alama katika vipaji vya nyuso vya watu wanaougua na kulia kwa sababu ya machukizo yote yanayofanyika kati yake. Na hao wengine aliwaambia, nami nalisikia, Piteni kati ya mji nyuma yake, mkapige; jicho lenu lisiachilie, wala msione huruma; Waueni kabisa, mzee, na kijana, na msichana, na watoto wachanga, na wanawake; lakini msimkaribie mtu ye yote mwenye hiyo alama; tena anzeni katika patakatifu pangu. Basi, wakaanza kwa wazee waliokuwa mbele ya nyumba. Akawaambia, itieni nyumba unajisi, mkazijaze nyua mizoga ya hao waliouawa; haya, enendeni. Wakaenenda, wakapiga-piga katika mji. Tena ikawa, walipokuwa wakipiga, nami nikiachwa, nalianguka kifudifudi, nikalia, nikasema, Ee Bwana MUNGU! Utaangamiza mabaki yote ya Israeli, wakati wa kumwaga ghadhabu yako juu ya Yerusalemu? Ndipo akaniambia, Uovu wa nyumba ya Israeli na Yuda ni mwingi sana, nayo nchi imejaa damu, nao mji umejaa kupotosha hukumu; maana husema, BWANA ameiacha nchi hii, naye BWANA haoni. Nami, jicho langu halitaachilia, wala sitaona huruma; lakini nitaleta njia yao juu ya vichwa vyao. Na tazama, mtu yule aliyevaa bafta, mwenye kidau cha wino kiunoni, akaleta habari, akisema, Nimefanya kama ulivyoniamuru.” (Ezekieli  9:1-11)

Hebu irudie hata mara tatu kuisoma hiyo mistari. Utaona kinachofanyika katika ulimwengu wa roho kinakuwaje.
Ni rahisi ninyi huku duniani kuona virusi. Lakini kwenye ulimwengu wa roho huwa ni viumbe kamili wanaoifanya hiyo kazi. Sikiliza jambo hilo Ezekieli aliliona likifanywa katika ulimwengu wa roho. Na likatokea kabisaa katika ulimwengu huu wa mwili.

Fahamu katika kila mji au taifa kuna malaika wamewekwa ili kuwa wasimamizi wa miji au taifa. Kazi yao ni kutoa taarifa kwa Mungu kwa ajili ya hiyo miji au hilo taifa.
Sikiliza Mungu anapotaka kuachilia tauni ikaipige miji au mataifa hao unaowasikia hapo wapo hata hii leo ndiyo wanaohusika kuyafanya hayo. Wapo ambao kazi yao ni kutia alama watu ambao tauni inatakiwa isiwapate. Hata ikiwapata hawatakufa
Kwa taarifa yako hakuna kinga zaidi ya hiyo alama. Kama unafikiri nakutania Angalia mfano, tauni ya Corona ilipokuja ulimwenguni wanadamu waliambiwa wanawe mikono, n.k.
Umewahi kufikiri Ulaya na Marekani walivyo wasafi? Huku sisi ndiyo tunafundishwa kunawa, wenzetu hunawa na hizo sabuni za kuua wadudu kila siku.

Lakini virusi hivyo havikuja wewe ni nani vimewavaa hata mawaziri wakuu, wafalme, n.k. Kuna waziri mkuu wa nchi kubwa ya Uingereza alikutwa na tauni hiyo, Kama waziri mkuu anatauni hiyo fahamu baraza looote la mawaziri hawakuwa salama.
Cha ajabu watu wengine usishangae hawapati hiyo tauni. Ni sawa na UKIMWI nakuambia ungejua kinachotendeka kwenye ulimwengu wa roho mpaka mtu akapata UKIMWI nakuambia ukweli watu wengi wangeacha kuzini kwa sababu HAKUNA KINGA.

Ngoja nikuonyeshe labda utaniekewa. Angalia mistari hii: “Na kwa malaika wa kanisa lililoko Thiatira andika; Haya ndiyo anenayo Mwana wa Mungu, yeye aliye na macho yake kama mwali wa moto, na miguu yake mfano wa shaba iliyosuguliwa sana. Nayajua matendo yako na upendo na imani na huduma na subira yako; tena kwamba matendo yako ya mwisho yamezidi yale ya kwanza. Lakini nina neno juu yako, ya kwamba wamridhia yule mwanamke Yezebeli, yeye ajiitaye nabii na kuwafundisha watumishi wangu na kuwapoteza, ili wazini na kula vitu vilivyotolewa sadaka kwa sanamu. Nami nimempa muda ili atubu, wala hataki kuutubia uzinzi wake. Tazama, nitamtupa juu ya kitanda, na hao wazinio pamoja naye, wapate dhiki kubwa wasipotubia matendo yake; nami nitawaua watoto wake kwa mauti. Na makanisa yote watajua ya kuwa mimi ndiye achunguzaye viuno na mioyo. Nami nitampa kila mmoja wenu kwa kadiri ya matendo yake. Lakini nawaambia ninyi wengine mlioko Thiatira, wo wote wasio na mafundisho hayo, wasiozijua fumbo za Shetani, kama vile wasemavyo, Sitaweka juu yenu mzigo mwingine.” (Ufunuo 2:18-24)

Ukiipitia hiyo mistari utanielewa haraka ninapokupa picha hii ili uone ni nini huwa kinafanyika kwenye ulimwengu wa roho. Haya mambo yanavyofanyika kwenye ulimwengu wa roho ni ngumu huku kwenye ulimwengu wa mwili kukinga.
Lazima utafute msaada kutoka kwenye ulimwengu wa roho ili Mungu aamue yeye kukuwekea alama. Tauni inapoachiliwa usifikiri kuna kinga, ni malaika hutumwa kufanya hivyo. Angalia Ezekieli aliona picha nzima ilivyokwenda. Aliyewekewa alama alipona; hakufa.

Ukiitazama ile mistari waliowekewa alama ni wale tu waliokuwa wanaomba au kulia kwa ajili ya maovu yaliyokuwa yakifanywa katika mji ule. Nitakuonyesha vizuri katika huko mbele
Fikiria kidogo, adhabu ile au tauni ile ilianzia madhabauni pa Mungu. Wale viumbe walimwacha Ezekieli kwa sababu tu alikuwa na alama, kumbuka huyo alikuwa mtu wa madhabahuni. Wenzie walikufa, kisa hawakuwa na alama.

Kwa lugha nzuri walikuwa hawaombi hao. Nikuulize swali umenielewa? Unaposikia tauni usifikiri itakaa mahali fulani tu, fahamu inaweza kuja kwenye taifa lako au mji wako,
Mfano tauni ya Corona ilipoanza huko China, Wamerekani na Ulaya na Afrika n.k hawakufikiri kuwa tauni hiyo itawapiga. Angalia mfano, Waitalia wengi walifikiri itawapiga Wachina tu, sikiliza ukisikia tauni au nzige nk wapo katika taifa fulani au mji fulani. Lazima uombe ili isije au ikija isilete madhara.
Lazima Watanzania tuombe tena tuombe sana tunaposikia mambo kama haya yakitokea katika mataifa fulani.
Sikilizeni viongozi wa serikali hii MUNGU ANALIPENDA SANA TAIFA HILI. Si kuwa sisi ni wema kuliko hayo mataifa mengine. Ni NEEMA.
Inapotokea tauni au majanga ya nzige, viongozi wa nchi kuwahimiza watu kuomba sana. Itakuwa vema sana kila kiongozi eneo aliopo ahimize watu wa eneo hilo waombe juu ya tauni au nzige, n.k.
Ni vema wapangeni hata siku maalumu ya maombi ya mfumo mzuri wa watu wakae mkao wa kuomba kama Taifa, Mkoa, Wilaya, Kitongoji, n.k.

NAWAAMBIENI UKWELI KWA KUFANYA HIVI NDIYO TUTAVUKA.
Naamini kwa sehemu umenielewa FANYIA KAZI HAYO.

Mungu akubariki tuonane katika sehemu hii mwezi ujao.

Ukihitaji masomo yetu unaweza kuyapata kwa njia hizi zifuatazo;
1. App yetu ya huduma yenye jina  “HUSONEMU (MWAKATWILA)” utaipata Play Store kwenye link pale juu, ambapo kuna masomo mengi sana hapo.

2. Tovuti yetu ya www.mwakatwila.org

3. YouTube - Mwakatwila au HUDUMA YA SOMA NENO LA MUNGU (HUSONEMU).

4. Facebook ingia katika hiyo tovuti au website yetu utaona alama ya Facebook (f) "like" na utapata maelezo ya kujiunga au ingia Facebook halafu andika “SOMA NENO LA MUNGU”

5. Instagram ingia Instagram app halafu andika “Steven Mwakatwila

6. DVDs 📀 au CDs 💿

7. VITABU.

NB: Wasiliana na mhudumu ofisini kwa namba +255 763 109 733, ili kupata VITABU, DVD & CD.

8. Kwa njia ya REDIO:- Utapata mafundisho yetu kwa redio zifuatazo:-
➖Rungwe FM 102.5 Kila siku ya Jumapili  saa tatu mpaka saa nne usiku.
➖Baraka FM 107.7 Kila siku ya Jumanne saa kumi na mbili jioni mpaka saa moja usiku.
➖Bomba FM 104.1 Kila siku ya Ijumaa saa tatu usiku mpaka saa nne usiku.

9. Unaweza kutupata kwenye ONLINE RADIO yetu:- radio.mwakatwila.org

Kwa Mawasiliano zaidi Utatupata kwa namba hizi:-
+255 754 849 924 Au
+255 756 715 222

Wako
Mwl Mr & Mrs Steven Mwakatwila.