Saturday, May 9, 2020

Salamu – Novemba, 2019

Salamu – Novemba, 2019

Bwana Yesu Kristo asifiwe sana. Ni imani yangu kuwa Mungu amekuwa pamoja nawe katika mwezi uliopita. Tumekua na semina Dodoma na Manyoni. Tumemwona Mungu sana.

Leo hii tumekuletea salamu za mwezi wa kumi na moja; naomba zipokee. Kumbuka tuna mfululizo mrefu sana wa salamu zenye kichwa

JIFUNZE KUISHI MAISHA YA UTAKASO

Hebu tusogee mbele kidogo tuone eneo lingine muhimu ambalo unatakiwa uliwekee bidii ya kulitakasa nalo ni;

JIFUNZE KUITAKASA HEMA AU HEKALU YA KUKUTANIA (ENEO LILE MNAPOKUTANA ILI KUMFANYIA MUNGU IBADA)

Sikiliza, unaweza kuitazama hema ya kukutania na Mungu kwa maana nyingi kidogo. Maana ya kwanza ni mwili wako wewe uliyemwamini Bwana Yesu Kristo.
Biblia inatuita sisi tumwaminio Bwana Yesu kuwa ni nyumba ya Mungu au hekalu. 

Angalia mistari hii: “Au hamjui ya kuwa mwili wenu ni hekalu la Roho Mtakatifu aliye ndani yenu, mliyepewa na Mungu? Wala ninyi si mali yenu wenyewe;” (1 Wakorintho 6:19)

Mimi na wewe tuliomwamini Bwana Yesu Kristo ni hekalu au hema au nyumba ya Mungu. Tuliisha jifunza huko nyuma.

Hema ya kukutania pia au hekalu inaweza kuwa ni mahali palipotengwa kwa ajili ya kanisa yaani waaminio kukutana na Mungu. Mahali hapo fahamu Mungu anataka pia pawe patakatifu au pawe safi sana.

Mungu wetu ni mtakatifu na anakaa mahali patakatifu. Yaani anakaa ndani yako lazima uwe msafi tumeisha jifunza tayari.

Lakini Mungu pia fahamu anataka eneo lile ambalo watoto wake watamkaribisha aje ili wamwabudu, wamtolee sadaka, na hata kujifunza mambo mbalimbali kutoka kwake au kupokea uponyaji au kumsifu na kumwimbia n.k. ENEO HILO ANATAKA LIWE SAFI.

Unajua ni rahisi kuona hema ya kukutania kama ni mwili tu, sikiliza hata eneo lolote lile ambalo watoto wa Mungu watakutana iwe kwa kuomba, iwe semina au ibadani eneo hilo fahamu litaitwa Hema ya kukutania au hekalu au sinagogi au nyumba ya ibada. Wengi wamezoea kuita kanisani.

Kuna utofauti wa neno kanisani na kanisa. Ukisikia watu wanasema kanisani wanamaanisha kwenye jengo ambalo kanisa linakutanika ili kumfanyia Mungu ibada. 

Ukisia neno kanisa wanamaanisha mtu aliyemwamini Bwana Yesu Kristo. Sasa sikia, eneo lolote la mfumo wa kukutana na Mungu lazima liwe takatifu.

Neno takatifu maana yake lililotengwa kwa shughuli hiyo, au lililosafishwa na kuondolewa uchafu wa aina yoyote.

Angalia mifano hii michache: “Nami nitakutana na wana wa Israeli hapo, na hiyo Hema itafanywa takatifu na utukufu wangu. Nami nitaitakasa hiyo hema ya kukutania, na hiyo madhabahu; pia Haruni na wanawe nitawatakasa, ili wanitumikie katika kazi ya ukuhani. Na mimi nitakaa kati ya wana wa Israeli, nami nitakuwa Mungu wao. Nao watanijua kuwa mimi ndimi BWANA, Mungu wao, niliyewaleta watoke katika nchi ya Misri, nipate kukaa kati yao; ni mimi BWANA Mungu wao.” (Kutoka29:43-46)

Ukiipitia hiyo mistari utaona wazi kuwa hema ilitakiwa itakaswe au iwekwe safi. Mungu anasema yeye ataitakasa kwa utukufu wake.

Kwa hiyo ni lazima tujue kuwa mahali pa kukutana na Mungu pawe pasafi sana.

Angalia na mistari hii: “BWANA alipoona ya kuwa amegeuka ili atazame, Mungu akamwita kutoka katikati ya kile kijiti, akasema, Musa! Musa! Akasema, Mimi hapa. Naye akasema, Usikaribie hapa; vua viatu vyako miguuni mwako; maana mahali hapo unaposimama ni nchi takatifu.” (Kutoka 3:4-5)

Mungu alimwambia Musa eneo au mahali hapo ni patakatifu. Atoe vistu vyake. Alikua anatufundisha kuwa Mungu hata tunapo mandalia mahali ili tumuite aje katikati yetu eneo hilo lazima liwe safi au tulifanyie utakaso.

Angalia kuna utakaso Mungu anasema yeye ataufanya, pia ukisoma maandiko utaona kuna utakaso ambao watu walitakiwa waufanye.
Hebu tuangalie namna ya kutakasa.

1: JIFUNZE KULIWEKA SAFI HILO ENEO.
Sikiliza tunatakiwa tuhakikishe eneo hilo ikiwa ni nyumba ikae vizuri na kuwa safi, na ikiwa ni hema fahamu lazima kuanzia turubai zake zoote vyuma n.k viko safi yaani havijachakaa na kuchanika chanika. Na kushonwa ovyo ovyo n.k.

Ukitaka kujifunza hili angalia maagizo Mungu aliyompa Musa ayafanye alipokuwa akitengeneza hema. Alimfundisha hiyo hema kuwa safi mnoo kila wakati yaani hiyo hema ilitiwa mpaka manukato.

Angalia mistari hii uone: “Kisha BWANA akasema na Musa, na kumwambia, Jitwalie manukato yaliyo bora, manemane mbichi shekeli mia tano, na mdalasini wenye harufu nzuri nusu ya kiasi hicho, yaani, shekeli mia mbili na hamsini, na kane shekeli mia mbili na hamsini, na kida shekeli mia tano, kwa kuiandama shekeli ya mahali patakatifu, na mafuta ya zeituni kiasi cha vibaba vitano; nawe utayafanya mafuta ya kutiwa matakatifu, marhamu iliyochanganywa kwa kazi ya ustadi ya mtengezaji manukato; yatakuwa ni mafuta matakatifu ya kutiwa. Nawe utaipaka hema ya kukutania kwa mafuta hayo, na hilo sanduku la ushuhuda, na hiyo meza, na vyombo vyake vyote, na kinara cha taa, na vyombo vyake, na madhabahu ya kufukizia uvumba, na madhabahu ya kuteketezea sadaka, pamoja na vyombo vyake vyote, na birika, na tako lake. Nawe utavitakasa vitu hivyo, ili viwe vitakatifu sana; tena kila kivigusacho vyombo vile kitakuwa kitakatifu. Nawe utawatia mafuta Haruni na wanawe, na kuwatakasa, ili wanitumikie katika kazi ya ukuhani. Nawe utanena na wana wa Israeli na kuwaambia, Haya yatakuwa ni mafuta matakatifu ya kutiwa kwa ajili yangu mimi katika vizazi vyenu vyote. Hayatamiminwa katika kiwiliwili cha binadamu, wala msifanye mengine mfano wa haya kama yalivyoungwa kwa viungo vyake; ni matakatifu, na kwenu ninyi yatakuwa matakatifu. Mtu awaye yote atakayechanganya mafuta mfano wa haya, au mtu awaye yote atakayetia mafuta haya juu ya mgeni, mtu huyo atakatiliwa mbali na watu wake. BWANA akamwambia Musa, Jitwalie manukato mazuri, yaani, natafi, na shekelethi, na kelbena; viungo vya manukato vizuri pamoja na ubani safi; vitu hivyo vyote na viwe vya kipimo kimoja; nawe utafanya uvumba wa vitu hivyo, manukato ya kazi ya ustadi wa mtengenazaji manukato, yatakuwa yamekolea, safi, matakatifu; nawe baadhi yake utayaponda sana, na kuyaweka mbele ya ushuhuda ndani ya hema ya kukutania, hapo nitakapokutana nawe; nayo yatakuwa kwenu matakatifu sana. Na uvumba utakaofanya, hamtajifanyia uvumba wenye viungo sawasawa na uvumba huo; utakuwa kwenu mtakatifu kwa ajili ya BWANA. Mtu ye yote atakayefanya mfano wa huo, ili kuunusa, mtu huyo atakatiliwa mbali na watu wake.” (Kutoka 30:22-37)

Ukiipitia hiyo mistari utaona wazi Mungu alivyotaka hema hiyo iwe safi mno. Hiki ni kipande tu. Soma Biblia utashangaa hiyo hema ilivyokuwa safi na bora na yenye uthamani na ilikuwa ghali mnoo.

Yaani ilikuwa ya gharama kubwa mnooo. Hata hekalu lilipokuja kujengwa wewe soma utaona hekalu hilo lilikuwa la thamani na ubora na lilikuwa la gharama kubwa mnooo.

Ninachotaka nikuonyeshe ni hiki lazima tujifunze kutakaswa mahali tunapokutania na Mungu.

2: JIFUNZE KULITAKASA HILO ENEO KWA DAMU.

Angalia hii mistari: “Kwa maana agano la urithi lina nguvu palipotukia kufa kwa mtu; kwa kuwa halina nguvu kabisa, akiwa yu hai yeye aliyelifanya. Kwa hiyo hata lile la kwanza halikuanzwa pasipo damu. Maana kila amri ilipokwisha kunenwa na Musa kwa hao watu wote, kama ilivyoamuru sheria, aliitwaa damu ya ndama na ya mbuzi, pamoja na maji na sufu nyekundu na hisopo, akakinyunyizia kitabu chenyewe, na watu wote, akisema, Hii ni damu ya agano mliloamriwa na Mungu. Na ile hema nayo na vyombo vyote vya ibada alivinyunyizia damu vivyo hivyo. Na katika Torati karibu vitu vyote husafishwa kwa damu, na pasipo kumwaga damu hakuna ondoleo. Basi ilikuwa sharti nakala za mambo yaliyo mbinguni zisafishwe kwa hizo, lakini mambo ya mbinguni yenyewe yasafishwe kwa dhabihu zilizo bora kuliko hizo.” (Waebrania 9:17-23)

Ukiipitia hiyo mistari utagundua kuwa hema ilitakaswa pia kwa damu. Musa alikuwa anaifanyia hiyo hema utakaso kwa kutumia damu ya kunyunyizia.

Kama damu hiyo ilitumika kufanyia utakaso lazima na sisi tujifunze kuitaka hema au jengo au ardhi ambayo tutatumia kama mahali maalumu pa kukutana na Mungu.

Sisi tumepewa leo hii Damu ya Bwana Yesu Kristo. Lazima tujifunze kuitumia hiyo damu kufanyia mara kwa mara utakaso wa mahali hapo pakukutanikia na Mungu.

Kwa hiyo kuna mambo mawili ya kufanya. Jambo la kwanza ni kujenga au kuweka mpangilio mzuri katika eneo hilo hata kufagia au kupaka rangi, n.k. Kama ni hema turubai ziwe bora na vitu vilivyomo humo ndani yake iwe vitambaa vya mapambo, mazulia, viti, maua na kila kitu kuwa safi na bora.

Jambo la pili ni hili la kulitaka hilo eneo kwa damu ya Bwana Yesu Kristo kwa kutumia maombi.

Omba kila mara jengo, hema n.k. liwe safi kwa damu ya Bwana Yesu Kristo. Takasa eneo hilo mlilopo loote yaani ardhi na kila kilichomo au kilichopo hapo.

Mkimaliza ibada kesho fanyeni hayo maombi tena yaani iwe kila siku. Ni rahisi kuanza kumwona Mungu kila mara kwenye hilo kusanyiko mlilonalo.

Naamini umeelewa kwa sehemu. Hebu tumalizie salamu hizi hapa. Tuonane tena katika kona hii mwezi ujao.

Ukihitaji masomo yetu unaweza kuyapata kwa njia hizi zifuatazo;
1. App yetu ya huduma yenye jina  “HUSONEMU (MWAKATWILA)” utaipata Play Store kwenye link pale juu, ambapo kuna masomo mengi sana hapo.

2. Tovuti yetu ya www.mwakatwila.org

3. YouTube - Mwakatwila au HUDUMA YA SOMA NENO LA MUNGU (HUSONEMU).

4. Facebook ingia katika hiyo tovuti au website yetu utaona alama ya Facebook (f) "like" na utapata maelezo ya kujiunga au ingia Facebook halafu andika “SOMA NENO LA MUNGU”

5. Instagram ingia Instagram app halafu andika “Steven Mwakatwila

6. DVDs 📀 au CDs 💿

7. VITABU.

NB: Wasiliana na mhudumu ofisini kwa namba +255 763 109 733, ili kupata VITABU, DVD & CD.

8. Kwa njia ya REDIO:- Utapata mafundisho yetu kwa redio zifuatazo:-
➖Rungwe FM 102.5 Kila siku ya Jumapili  saa tatu mpaka saa nne usiku.
➖Baraka FM 107.7 Kila siku ya Jumanne saa kumi na mbili jioni mpaka saa moja usiku.
➖Bomba FM 104.1 Kila siku ya Ijumaa saa tatu usiku mpaka saa nne usiku.

9. Unaweza kutupata kwenye ONLINE RADIO yetu:- radio.mwakatwila.org

Kwa Mawasiliano zaidi Utatupata kwa namba hizi:-
+255 754 849 924 Au
+255 756 715 222

Wako
Mwl Mr & Mrs Steven Mwakatwila.

No comments:

Post a Comment