Salamu – Julai, 2019
Bwana Yesu Kristo asifiwe sana. Ninamshukuru Mungu kwa kutupa uzima wa kuuona mwezi wa saba. Mwezi uliopita yaani mwezi wa sita tumekuwa na semina Mbili kubwa.
Tumekuwa na semina ya vijana jijini Mbeya na semina ya watu wote jijini Mbeya. Na tulizifanya kwenye hema katika viwanja vya CCM mama John au Luanda Nzovwe.
Ilikuwa ni semina nzuri sana. Tunamshukuru sana Mungu kwa semina hizo, na tunawashukuru watu woote ambao walituombea na kutoa sadaka zao kwa ajili ya semina hizo.
Nimekuletea tena Salamu za mwezi huu wa saba. Kumbuka tunasalamu zenye kichwa
JIFUNZE KUISHI MAISHA YA UTAKASO
Na tunaendelea kujifunza kipengele hiki Cha JIFUNZE KUTAKASA KILA TENDO LILILOANDIKWA KATIKA VITABU VYA MATENDO MBINGUNI NA DUNIANI
ITUMIE DAMU YA BWANA YESU KRISTO
Ili uanze kuzifuta hizo kumbukumbu za matendo yako mabaya zilizohifadhiwa katika nakala za mbinguni au za duniani lazima ujue kuwa ni damu ya Bwana Yesu Kristo tu iliyochaguliwa au kupewa dhamana ya kufanya hivyo.
Sikiliza hakuna damu yoyote au sadaka yoyote ambayo inaweza kuzifuta hizo nakala nje ya damu ya Yesu Kristo.
Angalia kwa makini mistari hii: “Na katika Torati karibu vitu vyote husafishwa kwa damu, na pasipo kumwaga damu hakuna ondoleo. Basi ilikuwa sharti nakala za mambo yaliyo mbinguni zisafishwe kwa hizo, lakini mambo ya mbinguni yenyewe yasafishwe kwa dhabihu zilizo bora kuliko hizo. Kwa sababu Kristo hakuingia katika patakatifu palipofanyika kwa mikono, ndio mfano wa patakatifu halisi; bali aliingia mbinguni hasa, aonekane sasa usoni pa Mungu kwa ajili yetu; wala si kwamba ajitoe mara nyingi, kama vile kuhani mkuu aingiavyo katika patakatifu kila mwaka kwa damu isiyo yake; kama ni hivyo, ingalimpasa kuteswa mara nyingi tangu kuwekwa msingi wa ulimwengu; lakini sasa, mara moja tu, katika utimilifu wa nyakati, amefunuliwa, azitangue dhambi kwa dhabihu ya nafsi yake. Na kama vile watu wanavyowekewa kufa mara moja, na baada ya kufa hukumu; kadhalika Kristo naye, akiisha kutolewa sadaka mara moja azichukue dhambi za watu wengi; atatokea mara ya pili, pasipo dhambi, kwa hao wamtazamiao kwa wokovu.” (Waebrania 9:22 28)
Ukiipitia hiyo mistari utaona nakala hizo zilizo mbinguni na zile zilizopo duniani zinatakiwa zisafishwe kwa damu ya Bwana Yesu Kristo. Angalia hiyo mistari inazungumzia habari za utakaso katika kila kitu yaani duniani.
Na pia utaona hapo maneno hayo yanazungumzia utakaso wa nakala zilizoko mbinguni. Kumbuka unaweza safisha, moyo, unaweza safisha roho, unaweza safisha mwili. Angalia hii mistari: “Basi, wapenzi wangu, kwa kuwa tuna ahadi hizo, na tujitakase nafsi zetu na uchafu wote wa mwili na roho, huku tukitimiza utakatifu katika kumcha Mungu.” (2 Wakorintho 7:1)
Pia fahamu kuna jambo la kuzisafisha hizo nakala za mambo yaliyoko mbinguni. Ambayo yako kwenye vitabu vya ajabu vitunzavyo matendo yoote ambayo mwanadamu anatenda.
Hebu ipitie hii mistari uone hiki ninachokuambia “Kisha nikaona kiti cha enzi, kikubwa, cheupe, na yeye aketiye juu yake; ambaye nchi na mbingu zikakimbia uso wake, na mahali pao hapakuonekana. Nikawaona wafu, wakubwa kwa wadogo, wamesimama mbele ya hicho kiti cha na vitabu vikafunguliwa; na kitabu kingine kikafunguliwa, ambacho ni cha uzima; na hao wafu wakahukumiwa katika mambo hayo yaliyoandikwa katika vile vitabu, sawasawa na matendo yao.” ( Ufunuo 20:11-12)
Umeona hiyo mistari mpendwa? Vipo vitabu au nakala zinazotunza kumbukumbu za matendo yako. Natamani unielewe. Unapoomba kuanzia leo jifunze pia kuomba damu ya Bwana Yesu Kristo ifute kila baya kilichoandikwa kwenye vitabu hivyo.
Biblia hapo inasema “mambo hayo yaliyoandikwa katika VILE VITABU SAWASAWA NA MATENDO YAO”
Biblia haisemi kitabu, inasema vitabu. Kwa haraka haraka utaona kumbe kuna vitabu ambavyo vimejazwa matendo ya kila mtu aliyoyatenda akiwa hapa duniani. Fikiria kidogo je! Wewe ni nini kimeandikwa humo? Na je! Umeanza kufanya jitihada za kuhakikisha tendo lolote baya ulilolitenda lililomo humo linafutwa ili ushahidi usionekane siku hiyo ya kujiliwa kwako?
Biblia inasema hivi angalia hii mistari: “Mwe na mwenendo mzuri kati ya Mataifa, ili, iwapo huwasingizia kuwa watenda mabaya, wayatazamapo matendo yenu mazuri, wamtukuze Mungu siku ya kujiliwa.” (1 Petro 2:12)
Angalia na mistari hii: “Nikasikia sauti kutoka mbinguni ikisema, Andika, Heri wafu wafao katika Bwana tangu sasa. Naam, asema Roho, wapate kupumzika baada ya taabu zao; kwa kuwa matendo yao yafuatana nao.” (Ufunuo 14:13)
Ukiipitia hiyo mistari utakiona hiki ninachokuambia kuwa kuna siku yakujiliwa ambayo Mungu anataka matendo yako mema tu ndiyo yaonekane. Na matendo hayo yataoneka mbele za watu wote.
Sasa sikia fikiria matendo yako yanafuatana na wewe angalia ni matendo ya aina gani? Kama ni matendo mafu nakushauri anza leo kutakasa au kufuta au kuondoa au kutenganisha matendo mafu na hizo nakala au hivyo vitabu ili usifuatane au kuyakuta huko matendo mabaya.
Damu ya Bwana Yesu Kristo pekee ndiyo inaweza kushughulikia hizo nakala.
Naamini umeelewa kwa sehemu. Hebu tumalizie salamu hizi hapa. Tuonane tena katika kona hii mwezi ujao.
Ukihitaji masomo yetu unaweza kuyapata kwa njia hizi zifuatazo;
1. App yetu ya huduma yenye jina “HUSONEMU (MWAKATWILA)” utaipata Play Store kwenye link pale juu, ambapo kuna masomo mengi sana hapo.
2. Tovuti yetu ya www.mwakatwila.org
3. YouTube - Mwakatwila au HUDUMA YA SOMA NENO LA MUNGU (HUSONEMU).
4. Facebook ingia katika hiyo tovuti au website yetu utaona alama ya Facebook (f) "like" na utapata maelezo ya kujiunga au ingia Facebook halafu andika “SOMA NENO LA MUNGU”
5. Instagram ingia Instagram app halafu andika “Steven Mwakatwila”
6. DVDs 📀 au CDs 💿
7. VITABU.
NB: Wasiliana na mhudumu ofisini kwa namba +255 763 109 733, ili kupata VITABU, DVD & CD.
8. Kwa njia ya REDIO:- Utapata mafundisho yetu kwa redio zifuatazo:-
➖Rungwe FM 102.5 Kila siku ya Jumapili saa tatu mpaka saa nne usiku.
➖Baraka FM 107.7 Kila siku ya Jumanne saa kumi na mbili jioni mpaka saa moja usiku.
➖Bomba FM 104.1 Kila siku ya Ijumaa saa tatu usiku mpaka saa nne usiku.
9. Unaweza kutupata kwenye ONLINE RADIO yetu:- radio.mwakatwila.org
Kwa Mawasiliano zaidi Utatupata kwa namba hizi:-
+255 754 849 924 Au
+255 756 715 222
Wako
Mwl Mr & Mrs Steven Mwakatwila.
No comments:
Post a Comment