Salamu – Oktoba, 2019
Bwana Yesu Kristo asifiwe sana. Nimekuletea salamu za mwezi wa kumi. Katika mwezi wa tisa tumekuwa na semina Makete. Na Chunya. Tulifunga hema yetu katika miji hiyo. Tulikuwa na semina nzuri sana.
Asanteni kwa maombi yenu. Hebu pokea salamu za mwezi huu wa tisa.
Kumbuka tuna salamu zenye kichwa
JIFUNZE KUISHI MAISHA YA UTAKASO
Na tunaangalia namna ya kushughulikia nakala za matendo yetu ambayo yanatunzwa mbinguni.
Katika salamu zilizopita tulijifunza kwa sehemu eneo lile la ni matendo ya aina ipi yanayoweza kutunzwa katika nakala hizo. Nikakuonyesha tendo moja kati ya matendo mbalimbali yayoweza kutunzwa humo nalo lilikuwa ni matendo ya midomo.
Sikiliza kwenye vitabu hivyo kunatunzwa matendo ya aina nyingi mnoo. Angalia tena mistari hii: “Nikawaona wafu, wakubwa kwa wadogo, wamesimama mbele ya hicho kiti cha enzi; na vitabu vikafunguliwa; na kitabu kingine kikafunguliwa, ambacho ni cha uzima; na hao wafu wakahukumiwa katika mambo hayo yaliyoandikwa katika vile vitabu, sawasawa na matendo yao. Bahari ikawatoa wafu waliokuwamo ndani yake; na Mauti na Kuzimu zikawatoa wafu waliokuwamo ndani yake. Wakahukumiwa kila mtu kwa kadiri ya matendo yake. Mauti na Kuzimu zikatupwa katika lile ziwa la moto. Hii ndiyo mauti ya pili, yaani, hilo ziwa la moto. Na iwapo mtu ye yote hakuonekana ameandikwa katika kitabu cha uzima, alitupwa katika lile ziwa la moto.” (Ufunuo 20:12-15)
Ukiipitia hiyo mistari utagundua kuna vitabu. Na kuna kitabu ambacho kinaitwa kitabu cha uzima.
Kitabu hicho kilitunza majina ya watu ambao watakwenda kuurithi uzima wa milele. Unajua kuna vitabu neno limesema vitabu vikafunguliwa ambavyo ndani yake utaona vilibeba kumbukumbu za matendo ya watu. Watu walihukumiwa kutokana na vile vilivyomo ndani ya hivyo vitabu.
Na ninafikiri vitabu hivyo viko vingi mnoo. Ndiyo maana Biblia inasema vitabu, haisemi kitabu. Biblia imetofautisha kitabu kimoja cha uzima na vitabu vingi va matendo ya watu.
Ninapokuambia angalia kitabu chako kimetunza nini ndani yake sikosei. Humo ndani hakuandikwi matendo yako ya midomo tu. Humo ndani kunaandikwa kila aina ya matendo mabaya uyatendayo.
Mfano: unazini, unakunywa pombe, unaua watu, unaiba, unasingizia, unatukana, wewe ni mchawi, mshirikina, una hila, unafitinisha watu, n.k.
Sikia unaweza ukawa umeokoka na ukawa na jina zuri tu lakini ukawa na tabia mbaya unayoifanya tena kwa siri. Hakuna anayejua leo kuwa ulikuwa unayafanya hivyo.
Fahamu kule mbinguni wametunza nakala ya video yako ambayo siku hiyo itafunguliwa na itakuwa dhahiri yaani wazi wazi.
Fikiria yamkini wewe ndiyo uliyemwua fulani, au unazini na mke wa mtu au mume wa mtu na unajificha sana, unazini na watumishi na umejificha kweli kweli. Inawezekana wewe ndiyo ulienda kumchongea mtu fulani akafukuzwa kazi na hakuna anayejua kuwa ni wewe ulifanya hayo yoote.
Fahamu siku ile kila kitu ni wazi. Kama unaona aisee ni aibu siku hiyo kwa nini leo usianze kutubu na kuomba nakala hizo zitakaswe au zifutwe?
Jambo lingine acha dhambi mpendwa ili kusiwemo katika hizo nakala kitu kibaya. Bwana Yesu Kristo anatuonya akisema: “Nayajua matendo yako, na taabu yako, na subira yako, na ya kuwa huwezi kuchukuliana na watu wabaya, tena umewajaribu wale wajiitao mitume, nao sio, ukawaona kuwa waongo; tena ulikuwa na subira na kuvumilia kwa ajili ya jina langu, wala hukuchoka. Lakini nina neno juu yako, ya kwamba umeuacha upendo wako wa kwanza. Basi, kumbuka ni wapi ulikoanguka; ukatubu, ukayafanye matendo ya kwanza. Lakini, usipofanya hivyo, naja kwako, nami nitakiondoa kinara chako katika mahali pake, usipotubu. Lakini unalo neno hili, kwamba wayachukia matendo ya Wanikolai, ambayo na mimi nayachukia.” (Ufunuo 2:2-6)
Bwana Yesu Kristo anasema anayajua matendo yako. Na anasema si mazuri. Anataka utubu yaani uyaache hayo matendo mabaya na uanze kuyatenda matendo mema.
Kwa hiyo lazima uone umuhimu wa kubadilika kitabia wewe uliye kanisa ili kumbukumbu za matendo yako mabaya huko mbinguni zikose kuchukua picha ya matendo mabaya zichukue matendo mema.
Fikiria wewe ni mtumishi siku hiyo picha inaletwa iliyodhahiri uko kwa mganga wa kienyeji unakunywa dawa au unachanjwa?
Fikiria wewe ni mume wa mtu picha inaonyeshwa uko na binti fulani wa kwaya na kumbe ulimpa mimba hakuna anayefahamu.
Aisee fikiria unaonekana ni mwanaume wa shoka kumbe siku hiyo picha inaonyesha tena dhahiri kuwa wewe ni shoga.
Fikiria unaonekana siku hiyo ukiiba fedha kwenye sanduku la sadaka kanisani. Unajifanya unatoa kumbe unachukua fedha bila watu kujua.
Mungu anayajua matendo yako yoote, na anayatunza ili kuwaonyesha watu siku ile ya hukumu.
Tubu leo mpendwa. Anza kuomba utakaswe, mwili, roho, na nafsi yako na pia kuondoa kila tendo ovu ulilolifanya kwa njia ya toba na maombi ili nakala za vitu vya mbinguni zilizotunga kumbukumbu mbaya zitakaswe kwa dhabihu ya damu ya Bwana Yesu Kristo.
Mungu akubariki tuonane katika sehemu hii mwezi ujao.
Ukihitaji masomo yetu unaweza kuyapata kwa njia hizi zifuatazo;
1. App yetu ya huduma yenye jina “HUSONEMU (MWAKATWILA)” utaipata Play Store kwenye link pale juu, ambapo kuna masomo mengi sana hapo.
2. Tovuti yetu ya www.mwakatwila.org
3. YouTube - Mwakatwila au HUDUMA YA SOMA NENO LA MUNGU (HUSONEMU).
4. Facebook ingia katika hiyo tovuti au website yetu utaona alama ya Facebook (f) "like" na utapata maelezo ya kujiunga au ingia Facebook halafu andika “SOMA NENO LA MUNGU”
5. Instagram ingia Instagram app halafu andika “Steven Mwakatwila”
6. DVDs 📀 au CDs 💿
7. VITABU.
NB: Wasiliana na mhudumu ofisini kwa namba +255 763 109 733, ili kupata VITABU, DVD & CD.
8. Kwa njia ya REDIO:- Utapata mafundisho yetu kwa redio zifuatazo:-
➖Rungwe FM 102.5 Kila siku ya Jumapili saa tatu mpaka saa nne usiku.
➖Baraka FM 107.7 Kila siku ya Jumanne saa kumi na mbili jioni mpaka saa moja usiku.
➖Bomba FM 104.1 Kila siku ya Ijumaa saa tatu usiku mpaka saa nne usiku.
Kwa Mawasiliano zaidi Utatupata kwa namba hizi:-
+255 754 849 924 Au
+255 756 715 222
Wako
Mwl Mr & Mrs Steven Mwakatwila.
No comments:
Post a Comment