Saturday, May 9, 2020

Salamu – Septemba, 2019

 Salamu – Septemba, 2019

Bwana Yesu Kristo asifiwe sana. Mimi na familia yangu ni wazima tunamshukuru Mungu.

Tumekuwa na semina Mbeya katika kanisa la KKKT Isyesye. Na tulipomaliza tukaanza kesho yake tu Tukuyu Mjini.

Tukuyu ndiyo kwetu haswa. Mimi ni Mnyakyusa. Kwetu ni Tukuyu katika wilaya ya Rungwe. Ingawa wazazi wangu wanaishi Mbeya mjini lakini ukoo wetu upo Tukuyu. Na mimi nimekulia hapo Tukuyu mjini na nimeokokea hapo mwaka tisini na tano tarehe kumi na tisa mwezi wa kumi na moja (19-11-1995) kwenye viwanja vya mpira vya CCM.

Sasa fikiri jirani na huo uwanja ndipo tulifunga hema yetu kwenye viwanja vya shule ya Bulyaga. Shule hiyo mimi nilisoma hapo tokea darasa la tatu mpaka darasa la saba.

Na mke wangu pia na yeye alisoma hapo hapo. Kwa hiyo tuliipeleka injili ya Bwana Yesu Kristo nyumbani.

Hebu pokea salamu zetu hizi. Kumbuka tuna salamu zenye kichwa.

JIFUNZE KUISHI MAISHA YA UTAKASO

Katika salamu za mwezi uliopita nilikufundisha eneo la kumshirikisha Roho Mtakatifu kwenye eneo la kukusaidia kuzisafisha nakala za mbinguni zilizoandikiwa kumbukumbu za matendo yako mabaya.

Unaweza kuwa na swali je! Ni matendo yote yanaweza kutunzwa kwenye vitabu hivyo?
Sikiliza ni kila tendo ovu au dhambi au makosa. Ngoja nikuonyeshe mfano ili ujifunze kuondoa hizo kumbukumbu mbaya kwenye hivyo vitabu.

Angalia mistari hii' “Basi, nawaambia, Kila neno lisilo maana, watakalolinena wanadamu, watatoa hesabu ya neno hilo siku ya hukumu. Kwa kuwa kwa maneno yako utahesabiwa haki, na kwa maneno yako utahukumiwa.” (Mathayo 12:36-37)

Ukiipitia hiyo mistari utaona wazi kuwa maneno yetu yatokayo vinywani mwetu hutunzwa kwenye hizo nakala za mbinguni.

Fikiria kidogo, kila ulilolisema utalikuta huko mbinguni. Lipo dhahiri kama picha ya video hivi. Maandiko yatufundisha hapo kuwa kila neno lisilo maana au lisilofaa au neno baya unalolinena utalitolea hesabu siku hiyo ya mwisho.

Leo hii hakuna mtu anaweza kuyakumbuka maneno yake yoote tokea alipozaliwa. Au hata alipokuwa tumboni mwa mamaye. Unaweza kusema mtoto anaweza kusema akiwa tumboni mwa mamaye?

Biblia inasema mtoto anaweza kusema. Angalia mistari hii: “Wasio haki wamejitenga tangu kuzaliwa kwao; Tangu tumboni wamepotea, wakisema uongo. Sumu yao, mfano wake ni sumu ya nyoka; Mfano wao ni fira kiziwi azibaye sikio lake. Asiyeisikiliza sauti ya waganga, Ijapo wanafanya uganga kwa ustadi.” (Zaburi 58:4-3)

Angalia na mistari hii: “Na vipofu na viwete wakamwendea mle hekaluni, akawaponya. Lakini wakuu wa makuhani na waandishi walipoyaona maajabu aliyoyafanya, na watoto waliopaza sauti zao hekaluni, wakisema, Hosana, Mwana wa Daudi! Walikasirika, wakamwambia, Wasikia hawa wasemavyo? Yesu akawaambia, Naam; hamkupata kusoma, Kwa vinywa vya watoto wachanga na wanyonyao umekamilisha sifa?” (Mathayo 21:14-16)

Watoto wanasema isipokuwa hatuielewi lugha yao na kila aliyepitia hatua hii ya utoto amesahau ni nini alikisema tokea tumboni mwa mama yake.

Sasa fikiria huko mbele kuna nakala zimetunza maneno yako yoote yasiyo na maana au mabaya uliyoyasema.

Ngoja nikupe mfano mwingine uone angalia mistari hii uone: “Maneno yenu yamekuwa magumu juu yangu, asema BWANA. Lakini ninyi mwasema, Tumesema maneno juu yako kwa namna gani? Mmesema, Kumtumikia Mungu hakuna faida; na, Tumepata faida gani kwa kuyashika maagizo yake, na kwa kwenda kwa huzuni mbele za BWANA wa majeshi? Na sasa twasema ya kwamba wenye kiburi ndio walio heri; naam, watendao uovu ndio wajengwao; naam, wamjaribuo Mungu ndio waponywao. Ndipo wale waliomcha BWANA waliposemezana wao kwa wao. Naye BWANA akasikiliza, akasikia; na kitabu cha ukumbusho kikaandikwa mbele zake, kwa ajili ya hao waliomcha BWANA, na kulitafakari jina lake.” (Malaki 3:13-16)

Ukiipitia hiyo mistari utaona kuna kitabu cha ukumbusho huko juu mbinguni. Kitabu hicho hapo inaonekana kiliyatunza maneno mabaya yaliyosemwa na hao watu.

Hao watu walisema kumtumikia Mungu hakuna faida nk. Mungu akasikia, na malaika wakayatunze hayo maneno yaliyosemwa na hao watu. Hii ni hatari kweli kweli.

Fikiria kidogo ni maneno mangapi mabaya uliyoyasema na yametunzwa huko mbinguni kwenye kitabu cha kumbukumbu? Angalia matusi, laumu, hukumu, uongo, masengenyo, kuteta, umbea, uzushi n.k.

Mimi naamini kwa hili tunahitaji usiku na mchana kuomba Mungu afute hizo nakala kwani  asilimia kubwa vinywa vyetu vimesema mabaya mnoo.

Angalia mfano huu: “Ndipo Paulo akamwambia, Mungu atakupiga wewe, ukuta uliopakwa chokaa. Wewe umeketi kunihukumu sawasawa na sheria, nawe unaamuru nipigwe kinyume cha sheria? Wale waliosimama karibu wakasema, Je! Unamtukana Kuhani Mkuu wa Mungu? Paulo akasema, Sikujua, ndugu zangu, ya kuwa yeye ni Kuhani Mkuu; maana imeandikwa, Usimnenee mabaya mkuu wa watu wako.” (Mdo 23:3-5)

Ukiipitia hiyo mistari utaona asilimia kubwa tumewanenea vibaya wakuu wetu wawe wa serikali au wa kanisa n.k.

Fikiria kidogo Mungu ametukataza tusiwanene wakuu wetu vibaya. Lakini angalia maneno yetu yalivyo. Tumepona hapo kweli?

Ninapoyatafakari hayo yoote, ndipo ninapoona umuhimu wa Bwana Yesu Kristo. Nje ya Bwana Yesu Kristo mimi nakuambia hakuna atakayepona. Nasema Hakuna! 

Kila mtu ana maneno mbalimbali maovu anayoyasema kila mara na maneno hayo hutunzwa katika vitabu vya kumbukumbu huko mbinguni. Hebu leo anza mpendwa kushughulikia hizo nakala za mambo yaliyotunzwa mbinguni.

Acha pia kusema yasiyo na maana yaani maovu. Katika maombi yako hebu kumbuka pia kuomba Roho Mtakatifu afanye kazi ya kufuta maneno yako yote maovu yaliyo katika nakala maneno mabaya huko mbinguni au katika copy iliyobaki duniani.

Mungu akubariki sana. Tuonane katika kona hii mwezi ujao.

Ukihitaji masomo yetu unaweza kuyapata kwa njia hizi zifuatazo;
1. App yetu ya huduma yenye jina  “HUSONEMU (MWAKATWILA)” utaipata Play Store kwenye link pale juu, ambapo kuna masomo mengi sana hapo.

2. Tovuti yetu ya www.mwakatwila.org

3. YouTube - Mwakatwila au HUDUMA YA SOMA NENO LA MUNGU (HUSONEMU).

4. Facebook ingia katika hiyo tovuti au website yetu utaona alama ya Facebook (f) "like" na utapata maelezo ya kujiunga au ingia Facebook halafu andika “SOMA NENO LA MUNGU”

5. Instagram ingia Instagram app halafu andika “Steven Mwakatwila

6. DVDs 📀 au CDs 💿

7. VITABU.

NB: Wasiliana na mhudumu ofisini kwa namba +255 763 109 733, ili kupata VITABU, DVD & CD.

8. Kwa njia ya REDIO:- Utapata mafundisho yetu kwa redio zifuatazo:-
➖Rungwe FM 102.5 Kila siku ya Jumapili  saa tatu mpaka saa nne usiku.
➖Baraka FM 107.7 Kila siku ya Jumanne saa kumi na mbili jioni mpaka saa moja usiku.
➖Bomba FM 104.1 Kila siku ya Ijumaa saa tatu usiku mpaka saa nne usiku.

9. Unaweza kutupata kwenye ONLINE RADIO yetu:- radio.mwakatwila.org

Kwa Mawasiliano zaidi Utatupata kwa namba hizi:-
+255 754 849 924 Au
+255 756 715 222

Wako
Mwl Mr & Mrs Steven Mwakatwila.

No comments:

Post a Comment