Saturday, January 26, 2019

1⃣2⃣ MAMBO MUHIMU UNAYOTAKIWA UYAFANYE ILI UPATE KUISHINDA DHAMBI YA UZINZI

Na: MWL STEVEN & BETH MWAKATWILA

FUATANA NASI:- APP, FACEBOOK, INSTAGRAM, ONLINE RADIO 📻, WHATSAPP, WEBSITE & YOUTUBE, Kwa links zilizoko kwenye HII LINK hapa:

KUPATA APP YETU “HUSONEMU (MWAKATWILA) APP” BONYEZA LINK HII HAPA:

🗓 26 Januari, 2019

Bwana Yesu Kristo asifiwe sana. Pole na mambo yote magumu unayokutana nayo. Naamini Mungu atakuvusha salama katika magumu hayo unayopitia.

Nimekuletea somo hili la Namna ya Kufanya ili Upate Kuishinda Dhambi ya Uzinzi.
Katika somo lililopita nilikufundisha lile eneo la jifunze kumwomba Mungu ashughulikie akili eneo la kuelewa kwako.

Hebu tusogee mbele kidogo. Tuangalie eneo lingine la kushughulikia nalo ni hili:-

JIFUNZE KUISHUGHULIKIA MILANGO YA UFAHAMU WAKO KWA KUTUMIA MAOMBI.

Ili leo uwe na akili nzuri ambayo haitaambatana na mavumbi yaani mwili ni lazima ujifunze kuishughulikia milango mitano inayozalisha au inayotumika kutengenezea ufahamu wa mtu.

Kumbuka akili ndani yake imebeba ufahamu ninaposema ufahamu namaanisha mfumo mzima wa akili, yaani kujua, kuelewa, kutambua, kuwaza, kufikiri, kunia, kudhamiria, kubuni au kuvumbua, nk

Kuna milango mitano hivi ambayo iliumbwa pia kwa kazi ya kupitisha ufahamu wa mtu. Iwe ufahamu wa mambo mema au mambo mabaya. Hiyo milango ndiyo itumikayo kupitisha au ndiyo vyanzo vya ufahamu.

Mungu alipokuwa anaiumba nafsi kumbuka aliiwekea akili “Lakini imo roho ndani ya mwanadamu, Na pumzi za Mwenyezi huwapa akili.” (Ayubu 32:8).

Pumzi ya Mungu inaitwa  nafsi sehemu nyingine inaitwa moyo, sasa ndani ya hiyo pumzi ndiyo kumewekwa mfumo huo wa akili. Mungu aliitengenezea hiyo nafsi milango ambayo itatumika kuiletea hiyo nafsi ufahamu.

Kwa mfano ili uwe na ufahamu wa kitu fulani lazima usikie, uone nk ufahamu wa mtu wa kujua kitu fulani unategemea hiyo milango mitano. Ambayo ni macho, masikio, pua, mdomo, kuguswa au mwili wengine wameita kuhisi/mguso (ngozi).

Ngoja nikupe mifano hii naona ndiyo utanielewa. “Na neno la nabii Isaya linatimia kwao, likisema, Kusikia mtasikia, wala hamtaelewa; Kutazama mtatazama, wala hamtaona. Maana mioyo ya watu hawa imekuwa mizito, Na kwa masikio yao hawasikii vema, Na macho yao wameyafumba; Wasije wakaona kwa macho yao, Wakasikia kwa masikio yao, Wakaelewa kwa mioyo yao, Wakaongoka, nikawaponya.” ( Mathayo 13:14-15).

Ukiipitia hiyo mistari utagundua kuwa mfumo mzima wa akili wa mtu unategemea kuona  na kusikia. Angalia anasema kwa kuwa watu hawa mioyo yao ni mizito na masikio yao hawasikii vema na macho yao yamefumbwa wasije wakaona kwa macho yao wakasikia kwa masikio yao WAKAELEWA KWA MIOYO YAO.

Angalia ili mtu awe na akili ambayo ina kuelewa na akili kumbuka inakaa moyoni lazima macho ya huyo mtu yawe yanaona vema na masikio ya huyo mtu yawe yanasikia vizuri.
Kama kutatokea tatizo kwenye macho au masikio ya mwanadamu fahamu huyo mtu moyo wake ambao unabeba akili na hisia na utashi hautakaa sawasawa utakuwa mzito tu.

Watu wengi hawapendi kusikia neno hili HAWANA AKILI!!! Wanalipenda neno hili WANA AKILI NZITO KIDOGO KUELEWA!!! Hata Biblia inasema hivyo hivyo kuwa mioyo ya hawa ndugu ni mizito. Yaani akili hamna.

Uzinzi unaotokana na chanzo cha mwili fahamu utayatumia macho na masikio na kuguswa ili kulikamilisha tendo zima la uzinzi. Macho yako ndiyo yanayowatazama wanaume na masikio yako ndiyo yanatumika kuyasikia maneno yakukushawishi ili uzini nao.
Akili itadaka kile macho inapeleka au masikio yanavyopeleka huko moyoni. Unapoguswa na mwanaume mwili wako kwa mguso fulani ndipo unapohisi moto wa kimapenzi moyoni mwako ambao ndiyo inakuwa chanzo cha anguko lako.
Hata unapokuwa peke yako na ukawaka tamaa unapojiruhusu tu kugusa maeneo fulani yanayosisimka haraka kimapenzi yaani maziwa, sehemu za siri, nk fahamu mguso huo uwe wako wewe au wa mwanaume au mwanamke utapelekea taarifa kwenye akili na akili itadaka hicho kitu.

Ndipo utashi au msukumo wa kutenda mambo utajiruhusu asilimia kubwa kukifanya kile akili imekidaka yaani ndipo watu wengi huingia jumla jumla kufanya tendo la uzinzi.

Najaribu kukuonyesha uone hiyo milango ya ufahamu au akili  ilivyo. Angalia pia mistari hii. “Na tazama, siku ile ile watu wawili miongoni mwao walikuwa wakienda kijiji kimoja, jina lake Emau, kilichokuwa mbali na Yerusalemu kama mwendo wa saa mbili. Nao walikuwa wakizungumza wao kwa wao habari za mambo hayo yote yaliyotukia. Ikawa katika kuzungumza na kuulizana kwao, Yesu mwenyewe alikaribia, akaandamana nao. Macho yao yakafumbwa wasimtambue............. Ikawa alipokuwa ameketi nao chakulani, alitwaa mkate, akaubariki, akaumega, akawapa. Yakafumbuliwa macho yao, wakamtambua; kisha akatoweka mbele yao. Wakaambiana, Je! Mioyo yetu haikuwaka ndani yetu hapo alipokuwa akisema nasi njiani, na kutufunulia maandiko?” (Luka 24:13-16 na 30-32)

Ukiipitia hiyo mistari unaona kuwa macho ya hao ndugu yalifumbwa, yalipofumbwa tu na ufahamu wao ulifumbwa, Maandiko yanatumia neno WASIMTAMBUE.

Fahamu kutambua kuko ndani ya akili, kwa mujibu wa mistari hiyo unajifunza kuwa mlango wa kutambua upo katika macho. Macho yakifumba tu ufahamu wa huyo mtu unakuwa gizani.

Unaweza ukamwona mtu lakini usimtambue mpaka uisikie sauti yake. Ukiisikia hiyo sauti unaweza kukumbuka hiyo sauti ni ya nani na ndipo utambuzi wako unatokea akilini kuwa ohoo huyu ni fulani nimemtambua kwa kupitia sauti yake.

Milango hii ya akili au ufahamu inahitaji kushughulikiwa sana, kwa sababu mwili ili upitishe mambo yake na kuipelekea akili fahamu itatumia milango hiyo hiyo ya ufahamu.
Hata Roho Mtakatifu ili apeleke mambo yake kwenye akili ya mtu fahamu atatumia milango hiyo hiyo ya ufahamu. Humsikii Bwana anavyosema kuhusu tatizo la watu la kuona kwao kusikia kwao?

Kama macho au masikio ya mtu hayajashughulikiwa fahamu hawezi kusikia habari za neno la Mungu na kulielewa na kulishika.

Hata kuona kwa watu kukiwa na matatizo fahamu hawawezi kuyaona mambo ya Mungu kabisaa. Mimi nakuambia ukweli, Kuna mambo Bwana Yesu Kristo aliyafanya watu wakayaona sasa waliokuwa na macho yaliyokuwa mazuri waliona utukufu wa Mungu.

Hapo hapo walikuwepo watu ambao macho yao hayakuwa mazuri macho yao  yaliona lakini waliona huyu ni Beelzebuli yaani mkuu wa mapepo.

Umewahi kyfikiri kwa nini leo hii watu wanaojiita watoto wa Mungu unawakuta wanabishana kuwa aisee ile siyo nguvu ya Mungu mwingine anasema aisee hiyo ni nguvu ya Mungu kabisaa. Mwingine anakuambia mimi ninanavyoona huyo siyo Roho Mtakatifu mwingine anakuambia mimi ninavyoona huyo ni Roho Mtakatifu.

Jiulize swali kwa nini hawa watu kila mmoja anaona tofauti na mwingine aonavyo? Kumbuka anachoona mtu ndicho asilimia kubwa ndicho kinachooenda kuzalisha ufahau au kujua au kutambua nk kwa mtu.

Shetani alipokuwa anatafuta kumvuruga mtu alilenga kwenye vyanzo vya ufahamu wa mtu yaani hiyo milango mitano. Alipoiharibu tu hiyo milango mtu akajikuta asilimia kubwa nafsi yake inapokea kutoka kwenye milango mambo mabaya tu.

Na kwa kuwa milango hiyo ilitekwa ilipitisha kwa haraka sana mno mambo ya mwili kuliko mambo ya roho yaani mambo ya Mungu.  

Ngoja nijaribu tena kukuonyesha mfano huu angalia mistari hii. “Mwanangu, nipe moyo wako; Macho yako yapendezwe na njia zangu Kwa maana kahaba ni shimo refu; Na malaya ni rima jembamba.” (Mithali 23:26-27).

Angalia kitu hiki. Ili mtu asiingie kwenye uzinzi hapo anazungumzia malaya na kahaba, Mungu anatupa akili au ufahamu au maarifa kuwa ni lazima Mtu huyo ampe Mungu moyo wake.

Kwa lugha nzuri ni lazima huyo mtu ampe Mungu kila kitu kilicho moyoni mwake. Sasa huko ndani ya moyo kuna akili, hisia na utashi. Akili imebeba ufahamu, kuelewa, kujua, kutambua nk.

Na ukiipitia hiyo mistari unaona Mungu anapodai apewe moyo anazungumzia na macho ya huyo mtu yanatakiwa yaweje. Macho ya mtu ndiyo mlango wa kila kitu kinachoingia moyoni yaani akilini.

Sasa ili moyo wa mtu uwe salama macho yake yanatakiwa yaanze kupendezwa kuona mambo ya aina fulani yaitwayo mambo mema. Kama yataanza kupenda kuangalia hayo mema fahamu akili za mtu huyo huko moyoni mwake zitakuwa njema tu.

Sasa tatizo lipo hapa. Macho ya wanadamu baada ya shetani kuyafanyia utekaji yanapenda kuona mambo mabaya. Hata masiko ni vivyo hivyo yanapenda sana kusikia umbea, kusikia neno nakupenda, yaani vitu vibaya vibaya ndiyo masikio yanapenda kusikiliza.

Fikiria wewe mwenyewe unatamani leo kusikia habari gani? Si kusikia kuwa yule ndugu aliyekutukana juzi kafukuzwa kazi, hapoo ndipo moyo unapata amani. Si ndiyo? Ehehee naona sasa unanielewa kwa nini nasema jifunze kushughulikia hiyo milango ya ufahamu.

Ukisikia mtu anasema nasumbuliwa mno na zinaa wewe fahamu jambo la kwanza kabisa kuwa kuna shida kwenye mfumo wa kutazama kwake wanaume au wasichana.

Anawatazama vibaya yaani hawatazami vema kuna shida katika kutazama au kuona kwake anaona VIBAYA. Umewahi jiuliza swali kwa nini Bwana Yesu Kristo anasema ‘amtazamaye mwanamke kwa kumtamani amezini moyoni mwake?(Mathayo 5:28)

Bwana Yesu Kristo anajua kuwa macho yanayotazama vibaya yatasababisha uharibifu tu kwenye akili za huyo mtazamaji, atazini tu. Ohoo kumbe macho yana sehemu kubwa ya mtu kuingia kwenye uzinzi ukahaba na umalaya. Macho tu SI PEPO NASEMA MACHO!!

Bwana Yesu Kristo anasema “LITOE”. Ehehee. Muulize swali mbona wewe macho yako uliondoka nayo yote mawili maana yake hukuwa ukiwatazama hao wanawake na kuwatamani uliwezaje?

Nakuambia ukweli atakufundisha kama ninavyokufundisha kuwa shughulikia katika maombi yako mara kwa mara hayo macho yako. Yapofushe yasitazame yasiyofaa.

Ngoja nikupe mfano anza kuomba maombi ya mfumo huu. “Ee BWANA, uweke mlinzi kinywani pangu, Mngojezi mlangoni pa midomo yangu. Usiuelekeze moyo wangu kunako jambo baya, Nisiyazoelee matendo yasiyofaa, Pamoja na watu watendao maovu; Wala nisile vyakula vyao vya anasa.” (Zaburi 141:3-4).

Anza kuomba mara kwa mara maombi ya mfumo huo, mwambie Mungu weka ulinzi kinywani pangu. Sikiliza kinywa ni mlango wa ufahamu, kwa kupitia kinywa chako ndiyo unapeleka maneno kwa watu na wanaanza kufahamu kwa kupitia hicho usemacho.

Sasa angalia kama wewe ni fundi wa kutongoza wanaume au wanawake ukianza kuomba maombi ya namna hii fahamu kuna nguvu kutoka katika ufalme wa Mungu itaanza kugombana na nguvu iliyokiteka kinywa chako inayosababisha mabaya.

Kinywa chako kinapenda kusema kwa kila mwanaume “NIMEKUBALI TUANZE MAHUSIANO” mimi najua kuna wadada hawezi hata siku moja kusema hapana. Yeyey ni neno moja tu. NDIYO NAKUBALI !!

Unamwuliza baadaye wewe yaani unamkubalia yule mwanaume kwa nini unafanya hivyo ? Anakuambia HATA MIMI NASHANGAAA!!! Yaani hata yeye anashangaa alikubalije tena kwa mdomo wake kabisaa.

Wengine ndiyo wamepanwa hivi. “Mtu asiyefaa kitu, mtu wa uovu; Huenda njiani mwenye kinywa cha upotofu.  Hukonyeza kwa macho, hunena kwa miguu, Huwaashiria watu kwa vidole vyake.” (Mithali 6:12-13)

Umewahi kumwona mwanaume mzinzi au mwanamke mzinzi? Wewe mwangalia macho yake, anavyoyabinya. Unamwuliza wewe umeokoka anasema ndiyo, kwa nini macho yako hayajatulia? Yaani huyu umemminyia jicho, miguu ulipokaa haijatulia unayagonga gonga mabaja wee ili iwe?

Anasema haka mwaya!! Mimi nimezoea hivyo!! Mwingine ndiyo utaona vidole vyake havijatulia kabisaa, mara kaweka mdomo, mara kavivunja mara anajichora chora mara kaviinua juu huku akajinyoosha nyoosha nk.

Sikiliza nikuambie. Hizo ni ishara na tabia za mwilini zinazochochea moja utongozwe au uonekane machoni pa watu kuwa wewe ni mzinzi. Utasikia vijana wanasema, yaaani huyo binti ni maharage ya Mbeya maji mara moja?

Wewe unaongea na mvulana unajilegeza weee unamrembulia macho haukazi sauti umeilegeza weee!!! Utatongozwa tu, na ndipo wengi hujifikiria wana mapepo yanayowavuta wavulana kumbe ni ujinga wao tuuu wa kutokuidhibiti milango ya ufahamu inayowachochea hao wanaume wawavute.

Na ukitongozwa tu ndiyo kinywa chako wewe ni wa ndiyooo !! Unasikia anasema moyoni nilimkataa ila nikasema tu ndiyoo ili yaishe!!! Mjinga wewe huna akili kabisaa.

Unapomwambia mwanaume ‘Ndiyo’. Utapata tabu sana. Atakushawishi tu, utajikuta umeanza mahusiano ambayo hata wewe mwenyewe ulikuwa haujayatarajia kabisaa.
Weka ulinzi kwenye mwili wako, kinywa chako, macho yako masikio yako, nk.

Mwambie Mungu usiuelekeze moyo wangu kwenye njia zisizofaa.  Ndipo utakuwa unampa Mungu nafasi na uhalali wa kuangalia kila kitu kinachohusiana na moyo wako yaani akili, hisia, utashi, macho, midomo, masikio, kuguswa, nk.

Ni maombi ya mara kwa mara si ya siku moja. Mwili unashindana na roho, na roho inashindana na mwili, unajua roho inatafuta kumiliki hiyo milango mitano ya akili  na mwili nao unatafuta kumiliki hiyo milango mitano ya akili.

Mwenye nguvu kati ya mwili na roho  ndiye anayeiendesha nafasi au moyo wa mtu.
Swali langu ni nani kati ya wewe yaani roho na mwili wako anaemiliki hiyo milango mitano ya ufahamu? Kama wewe roho utafanikiwa kuimiliki hiyo milango mitano ya akili nakuhakikishia utaumudu mwili wako tu kila siku.

Si unajua mwili unataka dhambi tuuu? Basi kila mara angalia sukumo wa macho yako unataka utazame nini ni vitu vinavyoupendeza mwili au roho? Je! Midomo yako inanena nini kila siku au inaonja nini?

Angalia masikio yako yanapenda kusikia habari gani? Mimi najua unaweza kujikagua tu, angalia unapopita barabarani  unawatazamaje wanaume, au wanawake.
HAKUNA SHIDA YA KUMTAZAMA MTU AWE WA KIKE AU WA KIUME LAKINI WEWE MWENYEWE DHAMIRI NDANI YAKO INASEMAJE JUU YA NAMNA UNAVYOWATAZAMA ?
Ngoja nikufundishe neno la kiutu uzima kidogo, Wakati naokoka nilikuwa nakutana na mafundisho  magumu sana, kila mdada aliyekuwa anavaa mpasuo aliambiwa aondoke, kila mdada akija kavaa kanguo kakumchora mwili aliambiwa ondoka, kila mdada aliyevaa nguo ambayo inaleta mvuto hivi aliambiwa achague aje hapo au aondoke.

Unajua nilishangaa sana mle ndani kanisani pale kuwakuta mabinti walikuwa wachache sana, vijana ndiyo kabisaa, unawakuta wamama na wabibi nk.

Siku moja Roho Mtakatifu alinikalisha chini. Akaniambia chukua kalamu na karatasi nataka nikufundishe somo. Unajua alinipa kichwa cha somo kiliitwa USAFI WA BINTI SAYUNI.

Siku ile Roho alipoanza kunifundisha somo lile niliogopa sana na niligundua Mungu anavyotamani kushugulikia ushindi dhidi ya dhambi ni tofauti mno na sisi tunavyojaribu kushughulikia.

Ndani ya hilo somo Mungu alinifundisha tatizo langu ni hili. Angalia mistari hii. “Basi ikiwa mlikufa pamoja na Kristo mkayaacha yale mafundisho ya awali ya ulimwengu, kwa nini kujitia chini ya amri, kama wenye kuishi duniani, Msishike, msionje, msiguse; (mambo hayo yote huharibika wakati wa kutumiwa); hali mkifuata maagizo na mafundisho ya wanadamu? Mambo hayo yanaonekana kana kwamba yana hekima, katika namna ya ibada mliyojitungia wenyewe, na katika kunyenyekea, na katika kuutawala mwili kwa ukali; lakini hayafai kitu kwa kuzizuia tamaa za mwili.” (Wakolosai 2:20-23).

Ndani ya hiyo mistari Roho Mtakatifu alinifundisha namna ya kosa langu ninavyotaka kuutawala mwili. Akanifundisha kuwa hauwezi kuutawala mwili kwa ibada hiyo mliyojitungia.

Akanifundisha mwili hautawaliwi kwa amri. Angalia hapo anasema “lakini hayafai kitu kwa kuzizuia tamaa za mwili.” Niliulizwa swali unafikiri hivyo mnavyofanya mnawafukuza hao wadada unafikiri ndiyo utautawala mwili?

Akanileta kipindi kile yupo duniani akaniuliza swali kwa nini Mafarisayo na Makuhani walisema anakula na kunywa na makahaba na wenye dhambi? Unafahamu kahaba anavaaje? Wale makuhani na washika dini walikuwa wanafikiri kuwa watautawala mwili kwa ibada walizojitungia wakajikuta ni wazinzi tu, wauaji tu, wana wivu tu, nk.

Roho Mtakatifu alianza kunifundisha namna unavyoweza kuutawala mwili kwa mfumo huo ninaokufundisha. Sina maana naruhusu watu wavae hivyo unielewe mpendwa nakufundisha ufanye nini ukikuta wamevaa.

Kama milango yako mitano ya ufahamu haijashughulikiwa utapata shida sana nakuambia utawaka tamaa kila siku nakuambia. Hebu anza kuyafanyia kazi mambo haya yoote niliyokufundisha utaona.

Badili mfumo wako wa maombi, jifunze siku nyingine kuomba kwa kufunga ukimtumia Roho Mtakatifu kuufisha mwili wako na KUIPELEKA MARA KWA MARA MILANGO HIYO MITANO YA AKILI.

Ndipo macho yataanza KUONA VEMA KUONA YALIYOMEMA NA MASIKIO YAKO YAANZE KUSIKIA NA KUYASIKIA YALIYOMEMA.

Kumbuka uzinzi umehusishwa sana na mfumo wa akili za mtu kama akili zipo sawa huwezi kuzini, ukiwa na akili fahamu utajua mwili unaudhibiti au unautawala kwa mfumo gani.

Naamini umenielewa.

Mungu akubariki

Ukihitaji masomo yetu unaweza kuyapata kwa njia hizi zifuatazo:-

1. Tovuti yetu ya www.mwakatwila.org

2. YouTube - Mwakatwila au HUDUMA YA SOMA NENO LA MUNGU (HUSONEMU).

3. Facebook ingia katika hiyo tovuti au website yetu utaona alama ya facebook(f) like na utapata maelezo ya kujiunga au ingia Facebook halafu andika  “SOMA NENO LA MUNGU”

4. Instagram ingia Instagram app halafu andika “Steven Mwakatwila”

5. DVDs 📀 au CDs 💿

6. VITABU.
NB: Wasiliana na Brigitha kwa namba +255 (0) 763 109 733, kupata VITABU, DVD & CD.

7. Kwa njia ya REDIO:- Utapata mafundisho yetu kwa redio zifuatazo:-
➖Rungwe FM 102.5 Kila siku ya Jumapili  saa tatu mpaka saa nne usiku.
➖Baraka FM 107.7 Kila siku ya Jumanne saa kumi na mbili jioni mpaka saa moja usiku.
➖Bomba FM 104.1 Kila siku ya Ijumaa saa tatu usiku mpaka saa nne usiku.

8. Unaweza kutupata kwenye ONLINE RADIO yetu:-  radio.mwakatwila.org

Kwa Mawasiliano zaidi Utatupata kwa namba hizi:-
+255 (0) 754 849 924 Au +255 (0) 756 715 222

Wako
Mwl Steven & Beth Mwakatwila.
26/01/2019

Monday, January 21, 2019

1⃣1⃣ MAMBO MUHIMU UNAYOTAKIWA UYAFANYE ILI UPATE KUISHINDA DHAMBI YA UZINZI

Na: MWL STEVEN & BETH MWAKATWILA

FUATANA NASI:- APP, FACEBOOK, INSTAGRAM, ONLINE RADIO 📻, WHATSAPP, WEBSITE & YOUTUBE, Kwa links zilizoko kwenye link hapa:

KUPATA APP YETU “HUSONEMU (MWAKATWILA) APP” BONYEZA LINK HAPA:

🗓 22 Januari, 2019

Bwana Yesu Kristo asifiwe sana. Naamini unaendelea vizuri. Nakuletea mfululizo wa somo hili ambalo ndani yake. Kuna maarifa mbalimbali ya namna unavyoweza kuwa mshindi dhidi ya tamaa za mwili na tunaiangalia dhambi ya uzinzi.

Ngoja nikuambie kitu. Nimekuwa na mawazo ya kukaa angalau siku mbili na vijana wawe waliooa au walioolewa na wale wasiooa au kuolewa lakini ni vijana.

Tujifunze na kuwaombea sana kwa ajili ya namna ya kuzishinda tamaa za mwili. Ninaona kibali moyoni mwangu. Tutakuwa na semina ya vijana tarehe 14-15/06/2019.

Siku inayofuata tutaanza semina kwa watu wote kwa muda wa siku nane jijini Mbeya, naamini tutakuwa pale kwenye viwanja vya CCM Mama John. Ombea tarehe hizo usipange kijana kukosa.

Hebu tuendelee kujifunza. Nilikuonyesha kuhusu eneo lile la maombi maalumu ya kuombea akili zako. Unajua ili uwe na akili unatakiwa ufundishwe namna ya kupata akili. “Unifundishe akili na maarifa, Maana nimeyaamini maagizo yako.” (Zaburi 119:66).
Maandiko matakatifu hapo yanatupa ufahamu kuwa ili tuwe na akili tunatakiwa tufundishwe AKILI. Ninapokufundisha haya yote fahamu nakufundisha akili.

Watu wengi tuliookoka tunafikiri tukiokoka tu tunapewa akili. Sikiliza tukiokoka faida tunayoipata ni kufundishwa akili. Fahamu si kila fundisho ndani yake linafundisha akili.
Yapo mafundisho yanayofundisha akili. Unajua ni rahisi ukatafuta mistari ukaihubiri wee lakini watu wasipate akili kabisaa.

Hapo kuna sababu nyingi zinazosababisha hilo. Moja ya sababu ni hii ya watoto wa Mungu kutokuwa na muda mrefu wa kuziombea akili zao. Ngoja nikuonyeshe kitu kingine cha namna ya  kuombea akili

OMBEA AKILI ZAKO ZIPATE UELEWA

Moja ya maombi ambayo unatakiwa uyaombe kila mara unaposhughulikia akili zako ni hili la kuziombea hizo akili zako zipate uwezo wa kuelewa.

Fahamu kuelewa au uelewa umo ndani ya akili. Huwezi kuwa na akili ikiwa una tatizo kwenye eneo la uelewa. Huwezi kuwa na ufahamu au kujua hata kukumbuka ikiwa huna uwezo wa kuelewa kile unachofundishwa ili uwe na akili.

Na hapo ndipo watoto wa Mungu wengi mno wamebanwa. Uelewa wetu haujakaa vizuri. Unajua unaweza ukamjua mtu lakini usimwelewe kabisaa?

Unajua unaweza kumsikiliza mwalimu yeyote yule lakini usimwelewe kabisaa ila umesikia? Unajua unaweza kuona kitu lakini ukapata shida katika kukielewa kile ulichokiona?

Mimi naweza kukufundisha weeeee lakini wala usinielewe kabisa. Tatizo hilo liliwabana wanafunzi tena woote wa Bwana Yesu Kristo. Hawakuwa na uelewa ule waliotakiwa wawe nao. Kwa maana nzuri kama walikuwa hawana uelewa katika akili zao maana yake walikosa akili.

Angalia hii mistari “Kisha akawaambia, Hayo ndiyo maneno yangu niliyowaambia nilipokuwa nikali pamoja nanyi, ya kwamba ni lazima yatimizwe yote niliyoandikiwa katika Torati ya Musa, na katika Manabii na Zaburi. Ndipo akawafunulia akili zao wapate kuelewa na maandiko. Akawaambia, Ndivyo ilivyoandikwa, kwamba Kristo atateswa na kufufuka siku ya tatu; na kwamba mataifa yote watahubiriwa kwa jina lake habari ya toba na ondoleo la dhambi, kuanza tangu Yerusalemu. Nanyi ndinyi mashahidi wa mambo haya.” (Luka 24:44-48)

Angalia hiyo mistari kwa makini nataka hasa uangalie maneno haya “Ndipo akawafunulia akili zao wapate kuelewa na maandiko.” Hao ndugu zetu walikaa chini ya darasa lililofundishwa na mwalimu wetu mkuu Bwana Yesu Kristo miaka mitatu.

Aliwafundisha akili  weee lakini hawakujua au kufahamu lolote unajua ni kwa nini? Bwana Yesu alilijua hilo. Aliona uelewa wao ulifunikwa. Kwa lugha nzuri kulikuwa na kifuniko kilichozibana akili zao kwenye eneo la kuelewa kwao tu.

Si kuwa hawakusikia fundisho la akili, walifundishwa tatizo lilikuwa hawakielewi kile wakisikiacho wakakosa akili. Wangeelewa hao ndugu kwanza wala wasingepata shida ya kulia wee kisa eti Bwana Yesu ameshikwa na amekufa.

Si wangetulia tulii wakiisubiri siku ya kufufuka kwake? Umewahi kujiuliza swali kwa nini Bwana Yesu alimwambia Petro maneno haya siku ile anamzuia asiende msalabani? “Petro akamchukua, akaanza kumkemea, akisema, Hasha, Bwana, hayo hayatakupata. Akageuka, akamwambia Petro, Nenda nyuma yangu, Shetani; u kikwazo kwangu; maana huyawazi yaliyo ya Mungu, bali ya wanadamu.” (Mathayo 16:22-23)

Petro kama angelikuwa na uelewa wa nini kinaenda kufanyika huko Yerusalemu kama maandiko yalivyofundisha tokea zamani wala asingemzuilia Bwana Yesu kwenda kufa msalabani.

Unajua ni rahisi sana ukawa na bidii ya kusikia maneno ya akili yaliyo mema kabisa lakini usiwe na uelewa nayo kabisaa. Angalia mistari hii.

“Kwa sababu hii nasema nao kwa mifano; kwa kuwa wakitazama hawaoni, na wakisikia hawasikii, wala kuelewa.Na neno la nabii Isaya linatimia kwao, likisema, Kusikia mtasikia, wala hamtaelewa; Kutazama mtatazama, wala hamtaona. Maana mioyo ya watu hawa imekuwa mizito, Na kwa masikio yao hawasikii vema, Na macho yao wameyafumba; Wasije wakaona kwa macho yao, Wakasikia kwa masikio yao, Wakaelewa kwa mioyo yao, Wakaongoka, nikawaponya. Lakini, heri macho yenu, kwa kuwa yanaona; na masikio yenu, kwa kuwa yanasikia.” (Mathayo 13:13-16).

Fikiria kidogo hao watu si kuwa walikuwa hawasikii na hawaoni, walisikia na waliona kabisaa ila hawakuwa na uelewa katika yale wanayoyasikia na kuyaona.

Kuna kitu nakiona hapo kinanistaajabisha na kunipa mwanga wa kuombea sana akili zangu eneo hili la uelewa. Bwana Yesu hapo anawaambia wanafunzi wake hivi “heri macho yenu, kwa kuwa yanaona; na masikio yenu, kwa kuwa yanasikia.”

Angalia kitu hiki, hao wanafunzi walioambiwa wana heri kwa kuwa wanasikia na kuona kuliko hao walionje ilibidi hata wao Bwana Yesu Kristo ashughulikie uelewa wao kwa kuwafunulia akili zao ili waelewe.

Kuna kitu hapa nataka nikusisitizie. Watu wengi tuliookoka na tukaanza kumtumikia Mungu tunajifanya tunaelewa weeeee kumbe hatuelewi chochote.

Kama tungekuwa na uelewa mzuri  ungeona maisha yetu tu jinsi yangekuwa. Wewe unamkuta mpendwa amezini halafu anaficha eti siri, siri hiyo inakuja kufichuka wakati binti ana mimba unamwuliza hivi kweli siku zooote hizo tokea umezini ulikuwa wapi kusema ukweli?

Anakuambia nilifikiri yataisha vivyo hivyo!! Unamwuliza hivi hujui kuwa Mungu alikuona tokea siku ile unamtongoza huyo binti? Anasema aisee najua. Unamwuliza kama ulijua kwanini hukutengeneza haraka?

Watoto wa Mungu wengi nakuambia ukweli hawaelewi. Msikilize Mungu asemavyo. “Nao husema, BWANA haoni; Mungu wa Yakobo hafikiri. Enyi wajinga miongoni mwa watu, fikirini; Enyi wapumbavu, lini mtakapopata akili? Aliyelitia sikio mahali pake asisikie? Aliyelifanya jicho asione? Awaadibuye mataifa asikemee? Amfundishaye mwanadamu asijue?” (Zaburi 94:7-10).

Watu wengi wanasikia sana kuwa Mungu anakuona lakini ukitaka kujua kuwa hawajaelewa wewe angalia wanavyojitahidi kumficha huyo Mungu mambo yao.
Mimi nakuambia ukweli kama tungekuwa tunaelewa mambo tungekuwa na akili nyingi na mfumo wetu wa maisha usingekuwa hivi tulivyo. Mimi nakuambia ukweli, tuna shida kubwa kwenye kuelewa bahati mbaya tunajifanya tunaelewa weee.

Watoto wa Mungu bwana tunachekesha unakuta mtu anasimama na kumshangilia mtumishi, utasikia ameeeeeeni aaameeeni!!! Ohoo zamani nilikuwa najisikia furaha kweli nilifikiri kuwa aisee hawa ndugu wameelewa kweli namna wanavyokea?

Rudi mwakani unawakuta wako vile vile. Unajiuliza maswali hivi kuna nini hapa? Mwulize Mungu atakuambia hao wanashangilia kitu ambacho hawajakielewa. Mwulize mtu hivi umerukaruka pale umemuelewa mtumishi? utasikia Ndiyo!. Kaa naye sasa akueleze alichokielewa. UTACHOKA KABISAA.

Unamkuta mtu ana vitabu huyo vya kila mwalimu anasoma kweli lakini mchunguze maisha yake utaona anaishi tofauti na hayo anayoyasoma. Ukiona hivyo wewe jua uelewa wake ni shida.

Bora ukutane na anayekuambia aisee mimi sielewi kwa kweli ingawa nasoma sanaa, kuliko yule ajifanyaye anaelewa kabla haujamaliza unachotaka kumwambia yeye tayari kakupa mstari!!!!!

Yaani maandiko yamejaa kahudhuria semina za walimu wakubwa wakubwa aisee ana masomo ya kila mtumishi lakini usishangae wala hana uelewa wowote ule. “Basi ninyi sikilizeni mfano wa mpanzi. Kila mtu alisikiapo neno la ufalme asielewe nalo, huja yule mwovu, akalinyakua lililopandwa moyoni mwake. Huyo ndiye aliyepandwa karibu na njia.” (Mathayo 13:18).

Umeliona hilo ninalokuambia? Huyo mtu si kuwa hakusikia, kasikia sana, Si kuwa kalisahau neno hilo tatizo lake hakulielewa tu. Ukilielewa neno la akili unakuwa na ujuzi nalo yaani utaliweka kwenye matendo na litatenda au kuleta mabadiliko tu maishani mwako.
Unapopokea elimu ambayo umeielewa lazima tu kutatokea badiliko katika maisha yako, Utaishi sawasawa na lile ulilolisikia na ukalielewa, ukalifahamu, ukalijua, utalikumbuka, nk

Anza kumwomba huyu Bwana Yesu Kristo ashughulikie akili zako kwenye eneo la kuelewa kwako, si kuelewa maandiko tu kuwaelewa watu nk. Watu wengi leo hawaelewi hata wafanye nini ili wapate fedha nk.

Mtu haelewi kabisaa ni nini anacho nk. Fikiria wanafunzi walishinda na Bwana Yesu Kristo miaka mitatu lakini hawakuwa wanaelelewa chochote. Mpaka aliposhughulikia uelewa wao.

Hata wewe sasa anza kumwomba Mungu maombi ya namna hiyo. Naamini umenielewa eti; ehee au hata hapa haujanielewa? Ukielewa utajua, utafahamu, utakifikiria hicho ulichokielewa nk

Mungu akubariki

Ukihitaji masomo yetu unaweza kuyapata kwa njia hizi zifuatazo:-

  1. Kwa Website yetu ya www.mwakatwila.org

2. YouTube - Mwakatwila au HUDUMA YA SOMA NENO LA MUNGU (HUSONEMU).

3. Facebook ingia katika hiyo tovuti au website yetu utaona alama ya facebook(f) like na utapata maelezo ya kujiunga au andika “SOMA NENO LA MUNGU”

4. Instagram ingia kwa link pale juu au ingia Instagram na andika Steven Mwakatwila

5. DVDs📀 au CDs 💿

6. VITABU

7. Kwa njia ya REDIO:-
➖Rungwe FM 102.5 Kila siku ya Jumapili  saa tatu mpaka saa nne usiku.
➖Baraka FM 107.7 Kila siku ya Jumanne saa kumi na mbili jioni mpaka saa moja usiku.
➖Bomba FM 104.1 Kila siku ya Ijumaa saa tatu usiku mpaka saa nne usiku.

8. Unaweza kutupata kwenye ONLINE RADIO yetu:-  radio.mwakatwila.org

Kwa mawasiliano zaidi Utatupata kwa namba hizi:- +255754849924 - +255756715222

Wako
Mwl Steven & Beth Mwakatwila.
22/01/2019