2⃣ NAMNA YA KUFANYA ILI UPATE KUISHINDA DHAMBI YA UZINZI
Na: MWL STEVEN & BETH MWAKATWILA
FUATANA NASI YOUTUBE
FUATANA NASI ONLINE REDIO
👉🏼 radio.mwakatwila.org
🗓 5 Disemba, 2018
Bwana Yesu asifiwe sana. Nimeupata muda huu nimeona nikuletee mwendelezo wa ujumbe niliokuahidi kukuletea katika eneo la namna ya kuishinda dhambi ya uzinzi. Nakumbuka nilianza kukuonyesha eneo la namna ya ili uanze kuishinda dhambi ya uzinzi ni lazima ufahamu kuhusu njia kuu mbili zinazoweza kuwa chanzo cha dhambi hiyo.
Nilikuonyesha eneo la chanzo cha mwili na chanzo cha roho ya uzinzi yaani pepo. Hebu tuendelee mbele kidogo katika eneo hili hili la mwili wako kama chanzo cha uzinzi.
Ili upate kuushinda mwili katika eneo hili la uzinzi pia unatakiwa uanze kushughulikia tabia ya uzinzi iliyo katika mfumo wa urithi. Neno urithi maana yake ni tendo lile la mtu kumiliki kitu au tabia zisizo zake ila anapewa kihalali na kuwa mali yake.
Mwili wako unaweza ukajikuta umebeba tabia ya uzinzi kisa ni uzao wako tu. Ngoja nikupe mfano huu utanielewa. Unajua Adamu alipokuwa anazaa watoto wake fahamu watoto wake hawakufanana.
Angalia mistari hii “Hiki ndicho kitabu cha vizazi vya Adamu. Siku ile Mungu alipoumba mtu, kwa sura ya Mungu alimfanya;mwanamume na mwanamke aliwaumba, akawabariki akawaita jina lao Adamu, siku ile walipoumbwa. Adamu akaishi miaka mia na thelathini, akazaa mwana kwa sura yake, kwa mfano wake, akamwita jina lake Sethi. Siku za Adamu baada ya kumzaa Sethi zilikuwa miaka mia nane, akazaa wana, waume na wake.” (Mwanzo 5:1-4)
Ukiipitia hiyo mistari utagundua kuwa Adamu alimzaa Sethi baada ya kuwazaa akina Kaini na Habili. Unaposoma maandiko huoni ya kuwa Kaini na Habili wana sifa kama hii aliyopewa Sethi
Angalia kuzaliwa kwao hao Kaini na Habili, “Adamu akamjua Hawa mkewe; naye akapata mimba, akamzaa Kaini, akasema, Nimepata mtoto mwanamume kwa BWANA.Akaongeza akamzaa ndugu yake, Habili. Habili alikuwa mchunga kondoo, na Kaini alikuwa mkulima ardhi.” (Mwanzo 4:1-2).
Kaini na Habili hawakuwa na sifa kama ya Sethi. Sethi alipozaliwa maandiko yanasema hivi “Adamu akaishi miaka mia na thelathini, akazaa mwana kwa sura yake, kwa mfano wake, akamwita jina lake Sethi.” Sethi alikuwa na sifa ya kuwa na sura na mfano wa Adamu.
Ukisoma Biblia kwa kutulia utaona Adamu aliumbwa kwa mfano na kwa sura ya Mungu. “Mungu akaumba mtu kwa mfano wake, kwa mfano wa Mungu alimwumba, mwanamume na mwanamke aliwaumba.” (Mwanzo 1:27)
Adamu na mkewe waliumbwa kwa mfano na kwa sura ya Mungu. Ukisoma maandiko utagundua kuwa Adamu alipoteza hiyo sifa baada ya kula tunda bustanini Edeni.
Maandiko yanasema hivi, “BWANA Mungu akasema, Basi, huyu mtu amekuwa kama mmoja wetu, kwa kujua mema na mabaya; na sasa asije akanyosha mkono wake akatwaa matunda ya mti wa uzima, akala, akaishi milele; kwa hiyo BWANA Mungu akamtoa katika bustani ya Edeni, ailime ardhi ambayo katika hiyo alitwaliwa.Basi akamfukuza huyo mtu, akaweka Makerubi, upande wa mashariki wa bustani ya Edeni, na upanga wa moto uliogeuka huko na huko, kuilinda njia ya mti wa uzima.” (Mwanzo 3:22-24)
Umewahi kujiuliza kwa nini Mungu alimfukuza Adamu na mkewe bustanini Edeni? Hebu isome hiyo mistari utagundua kuwa kilichomfanya Adamu afukuzwe ni mfumo wa ALIVYOKUWA.
Alipoteza sifa ya kufanana na Mungu kwa sura na kwa mfano wa Mungu. Mungu alisema wazi kuwa kwa kuwa huyu mtu AMEKUWA KAMA MMOJA WAO KWA KUJUA MEMA NA MABAYA. Huyo ajuaye mema na mabaya ni shetani. Sasa naona umeanza kuelewa kuwa Adamu hakuwa vile alivyoumbwa.
Ukilijua hili ndiyo utaona umuhimu wa kuzaliwa mara ya pili. Nje ya Bwana Yesu Kristo fahamu HAUNA MFANO NA SURA YA MUNGU!!!
Sasa sikia unaweza ukazaliwa ukawa na sura na mfano wa baba yako au mama yako kabisaa. Kwa lugha nzuri hapo maana yake mwili wako utafanana na baba au mama, kutembea, sura, kusema, kuwaza, na TABIA MTAFANANA KABISA. Sikia hakuna anayeomba afanane na baba yake. Ila tunapokea tu.
Umewahi fikiria unakuta msichana sura ni baba kabisaaa, ehehee. Msichana anayefanana na baba yake sura maana yake hapo aisee nisiseme mengi. Haujawahi ona msichana ana miguu na kutembea kama mwanaume?
Wewe nenda kamwangalie baba yake utagundua ndiyo kamlandisha au kamfananisha. Mwingine ndiyo umbo sasa kifua ni baba yake mtupu wakati ni msichana. Wengi huita kifua cha simba. Ukimkuta mvulana kafanana na mama yake aisee wengi humwita mzuri wa sura.
Ila usiombe umbo afanane na mama yake, Ehehee!! Fikiria mama amebinuka hivi na makalio makubwa na kamlandisha mtoto wa kiume!!! Mara nyingi watu wa namna hii utakuta hata tabia zitafanana. Kama mama mshari basi usishangae huyo kijana ni mshari kama mama yake.
Sasa sikia kama baba huyo au mama huyo alikuwa ni mzinzi hata huyo mtoto aliyefananana naye atamwachia hiyo tabia. Usifikiri miili ya hao watoto itafanana katika kusumbuliwa na uzinzi au tabia fulani.
Huyo aliyefanana kwa sura na mfano wake fahamu YEYE ATAKUWA NA MWILI ULIO NA NGUVU MNO YA KUZINI NAKUAMBIA. Haujawahi sikia watu wanasema hivi. Yaani huyu amechukua tabia zoote za baba yake au babu yake au mama yake? Jiulize kwa nini wengine hawajachukua hiyo tabia?
Fahamu huyo kairithi hiyo tabia. Mimi nakuambia kuna uzao wa zinaa kabisaa. Yaani unawakuta ni wazinzi tokea watoto mpaka wanazeeka NI UZAO.
Bwana Yesu Kristo alilijua sana jambo hili. Alisema hivi “Akajibu, akawaambia, Kizazi kibaya na cha zinaa chatafuta ishara, wala hakitapewa ishara, ila ishara ya nabii Yona.” (Mathayo 12:39)
Aliyarudia tena maneno haya . Angalia mistari hii. “Kizazi kibaya na cha zinaa chataka ishara; wala hakitapewa ishara, isipokuwa ishara ya Yona. Akawaacha, akaenda zake.” (Mathayo 16:4)
Unaweza ukatokea pia kwenye kizazi cha namna kama hiyo pia. Fikiria unakuta baba au babu alioa wake wengi, tena alikuwa anawaoa dada anamuoa na mdogo na mdogo kabisaa. Ukiona hivyo fahamu kuwa kizazi chako cha tabia hii.
Mimi nakuambia ukweli kama baba au mama alizaa nje ya ndoa (uzinzi au uasherati) mimi nakuambia ni kitu rahisi watoto kama siyo wote basi mmoja usishangae na yeye atazaa nje ya ndoa.
Na mtoto ni matokeo ya tabia ya kujamiana au tendo la ndoa. Sasa wengine wanaweza wasizae lakini wanajikuta wamebanwa na tabia hiyo ya uzinzi.
Ngoja nikupe mfano huu. Umewahi jiuliza swali kwa nini familia ya Ibrahimu walijikuta wana tabia ya kuzaa na wafanyakazi? Ibrahimu alizaa na mfanyakazi, Mjukuu wake ambaye ni Yakobo yeye ndiyo akatembea nao wengi kweli.
Unaona hata Mtoto wa Yakobo Reubeni naye akazini na mfanyakazi wa baba yake ambaye alimzalia baba huyo yaani Yakobo. Isaka alipona ila mtoto wa Isaka yaani Yakobo aliipokea hiyo tabia. Mimi naamini ikaenda mpaka kwa mfalme Daudi.
Eheheee!! Mfalme Daudi kuchukua wake za watu na akaua kisa mwanamke kwake ilikuwa kitu rahisi tu. Fikiri mfalme Daudi hata alipokuwa mzee kweli kweli yaani hata mwili wake hauwezi kuwa na nguvu yaani haupati joto alitafutiwa kabinti fulani hivi ili kamlalie tu na jamaa alikuwa anapata joto.
Biblia inasema hivi. “Mfalme Daudi alikuwa mzee, mkongwe katika siku zake, nao wakamfunika nguo, lakini asipate moto.Kwa hiyo watumishi wake wakamwambia, Bwana wangu mfalme na atafutiwe kijana mwanamwali; naye asimame mbele ya mfalme, amtunze; alale kifuani mwako, ili bwana wangu mfalme apate moto. Basi wakatafuta kijana mzuri mipakani mwote mwa Israeli, wakamwona Abishagi, Mshunami, wakamleta kwa mfalme.Naye kijana huyo alikuwa mzuri sana; akamtunza mfalme, akamtumikia; walakini mfalme hakumjua.” (1 Wafalme1:1-4)
Jiulize swali kwanini wasimlalie kifuani hao wanawake zake wazee mpaka kabinti? Yaani jamaa mpaka uzeeni anatafuta kabinti. fikiria hiyo ni tabia ya uzinzi tu, inausumbua mwili hata ukizeeka.
Nirudi kwako sasa, Ukiona waliokutangulia mababa au mama walikuwa hivyo fahamu ni rahisi wewe kuwa na tabia ya uzinzi tu. Sasa unapotafuta kuishughulikia tabia hiyo iliyo mwilini mwako lazima ukatae urithi huo.
Kataa kwa toba, tubia tabia hiyo kwa ulioipokea kutoka kwa waliokutangulia.
Ukihitaji masomo yetu unaweza kuyapata kwa njia hizi zifuatazo
1.Website yetu ya www.mwakatwila.org
2.YouTube - Mwakatwila au HUDUMA YA SOMA NENO LA MUNGU (HUSONEMU).
3.Facebook ingia katika hiyo tovuti au website yetu utaona alama ya facebook(f) like na utapata maelezo ya kujiunga
4.DVDs📀 au CDs💿
5.VITABU
6.Kwa njia ya Redio:-
➖Rungwe FM 102.5 Kila siku ya Jumapili saa tatu mpaka saa nne usiku.
➖Baraka FM 107.7 Kila siku ya Jumanne saa kumi na mbili jioni mpaka saa moja usiku.
➖Bomba FM 104.1 Kila siku ya Ijumaa saa tatu usiku mpaka saa nne usiku.
7.Unaweza kutupata kwenye radio yetu online ya. radio.mwakatwila.org
Kwa mawasiliano zaidi Utatupata kwa namba hizi. +255754849924 - +255756715222
Mungu akubariki sana
Wako
Mwl Steven & Beth Mwakatwila.
05 /12/ 2018
No comments:
Post a Comment