5⃣ MAMBO MUHIMU UNAYOTAKIWA UYAFANYE ILI UPATE KUISHINDA DHAMBI YA UZINZI
Na: MWL STEVEN & BETH MWAKATWILA
FUATANA NASI FACEBOOK
FUATANA NASI YOUTUBE
FUATANA NASI ONLINE RADIO
👉🏼 radio.mwakatwila.org
20 Dec, 2018
Bwana Yesu Kristo asifiwe sana. Ni imani yangu unaendelea vizuri, nimepata muda huu naona nikuletee tena mfululizo wa somo hili kama nilivyokuahidi.
Hebu tuangalie tena jambo lingine la kuangalia ili upate kuudhibiti mwili katika eneo la uzinzi. Kumbuka tunaangalia kipengele cha uzinzi ambao chanzo chake ni mwili.
Baada ya kukuonyesha namna ya tabia ya uzinzi mwilini unaotokana na kurithi hebu tuangalie jambo lingine ambalo linaweza kuwa chanzo cha uzinzi mwilini mwako.
JIFUNZE KUONDOA MIUNGANIKO YA UZINZI KUTOKANA NA WALE ULIOZINI NAO
Unaposoma Biblia na kuona Mungu Agizo la kutukataza tusizini fahamu kuwa moja ya madhara ambayo unaweza kukutana nayo ni kuunganika mwilini mwako na huyo uliyezini naye.
Watu wengi hujikuta wakivutwa kwenye uzinzi na hasa wale waliozini nao zamani hawajui chanzo ni nini hasa. Chanzo kinachoamsha mwili kulifanya tendo hilo ni muunganiko uliotokea baada ya kulifanya tendo hilo.
Biblia inasema hivi “Je! Hamjui ya kuwa miili yenu ni viungo vya Kristo? Basi nivitwae viungo vya Kristo na kuvifanya viungo vya kahaba? Hasha! Au hamjui ya kuwa yeye aliyeungwa na kahaba ni mwili mmoja naye? Maana asema, Wale wawili watakuwa mwili mmoja.” (1 Wakorintho 6:15-16).
Angalia kwa makini, tendo la mtu kuzini linatengeneza jambo la muunganiko kati ya hao watu wawili, maandiko yanasema viungo vyao vinaungana na kuwa mwili mmoja.
Angalia kilichowaunganisha mwilini ni tendo la kujamiana tu. Dhambi hii ni dhambi ya ajabu sana, inaweza kuwaunganisha watu wa jinsia tofauti bila wao kujua kuwa kuna muunganiko umetokea mwilini kwao.
Miunganiko hiyo isiposhughulikiwa ndiyo inaamsha miili ya hao watu wawili kujikuta wakiwa wazinzi, unaweza kuniuliza kwa nini? Angalia chanzo cha muunganiko wao ni uzinzi. Kumbuka uzinzi ni tabia, tabia hiyo inaweza kupitia tendo hilo na KUMWAMBUKIZA MTU MWILINI MWAKE.
Waangalie watu wengi ambao wamekutana na wanawake makahaba, nakuambia ukweli wanajikuta ghafla ile tabia ya uzinzi inawabana kiasi ambacho hata wao wanashangaa, wengi hufikiri ni kutokana na ufundi wa hao makahaba, sikiliza nikuambie siyo hivyo tu, kuna zaidi ya hivyo. Unaweza ukawa na mke fundi kumzindi huyo kahaba lakini ukigusa tu kwa huyo kahaba UNAAMBUKIZWA TABIA YA UZINZI.
Kuanzia hapo utashangaa kwanza uhitaji wako wa kufanya uzinzi unakuwa mkubwa mno. Angalia mistari hii. “Maana kwa malaya mtu hutiwa katika hali ya kuhitaji kipande cha mkate;...” (Mithali 6:26A).
Uhitaji au nguvu ya kufanya tendo la ndoa huwa kali mnoo kwa mtu ambaye amekutana na malaya. Kwa nini isiwe uhitaji huo uwe wa mtu aliyekutana na mke wake? Tafuta mstari usemao maana kwa mke mtu hutiwa katika hali ya kuhitaji yaani tendo la ndoa kama kuhitaji kipande cha mkate. Hakuna mstari huo.
Neno kuhitaji kama kipande cha mkate maana yake ni mtu mwenye njaa kali anahitaji kipate tu cha mkate ili ale aishi. Sasa jiulize kwanini ni pale mtu anapofanya uzinzi?
Sikiliza muunganiko huo mbaya huchochewa mnoo na nguvu ya mwili ili kumpeleka mtu jehanamu. Watu wengi hufikiri kuwa malaya hao hutumia dawa au wanaume hao wanaozini nao wana dawa, sikiliza hakuna dawa yoyote ni NGUVU YA UOVU ILIYOBEBWA MIILINI MWAO INAWASHA TAMAA KWA UKALI MNO.
Mimi ni mtumishi nimekutana na watu wengi. Mtu anakuambia mtumishi, nahitaji maombi kuna mke wa mtu au mume wa mtu tuliwahi kuzini, lakini mtumishi nashangaa kila wakati navutwa mnoo kwake yaani naona kanipa dawa hivi. Na mimi simtaki ili niilinde ndoa yangu na nimemrudia Mungu. Yaani mtumishi namfikiria yeye tuuu, wala si mke wangu au mume wangu, niombee.
Sikiliza kinachochochea ni muunganiko mliounganika mwilini tu. Haujawahi sikia msemo usemao “watu waliowahi kuzini wakikutana ni lazima wakumbushie. Hata kama wameoa au kuolewa?”
Mwili ukibeba unganiko la namna hiyo fahamu utakusukuma mnoo ufanye uzinzi ili tu upishane na Mungu. Maandiko yanasema “Kwa kuwa nia ya mwili ni mauti; bali nia ya roho ni uzima na amani. Kwa kuwa ile nia ya mwili ni uadui juu ya Mungu, kwa maana haitii sheria ya Mungu, wala haiwezi kuitii. Wale waufuatao mwili hawawezi kumpendeza Mungu.” (Warumi 8:6-8).
Mwili unatamani wewe kila muda usimpendeze Mungu, kwa hiyo unapoufungulia mlango wa kuzini na kutengeneza muunganiko na huyo uliyezini naye, fahamu mwili utakusukuma mnoo uende huko nje kuliko kwa mkeo au mumeo ili TU UKUTIE MAUTINI NA USIMPENDEZE MUNGU.
Watu wengi wakikutana na hali hii hufikiri ni pepo au ni dawa wamewekewa, hana na usishangae hakuna pepo wala dawa ni mwili unashindana na maangizo ya Mungu na wewe ulijichomeka kwa kujiunganisha na mtu kwa kutumia uzinzi mlioufanya.
Ngoja nikupe mfano, huu. Mwili wako unashindana kila nukta na roho yako. Mwili unamchagua shetani na roho imemchagu Mungu. Sasa unapoufungulia mwili mlango wa wewe kuzini fahamu hapo ndipo unapoupa mwili nguvu ya kukusumbua wewe ili utoke kwenye uzima uufuate mwili upate mauti.
Watu wengi waliowahi kuzini na watu fulani wanajidanganya sana kuwa wakikutana mahali hawawezi kuzini, wengi mno mwisho wa siku huishia kujutia kukutana kwao. Wasipogombana basi watakuwa wamezini, unajua kwanini hugombana?
Lazima mmoja atakuwa ANAUTAWALA MWILI WAKE KWA UKALI, Atajitahidi kwa akili zake kuongea maneno magumu ili kuiondoa ile hali ya kuwakiana tamaa. Kama wote watachekeana chekeana hata kama wameoa au kuolewa usishangae wasipozini kwa kitendo basi mioyoni mwao wamezini kwa mawazo tu.
Ndiyo hapo unakutana na mmoja wao anaomba maombi kuwa anahisi huyo mtu wake wa zamani kama anamlogezea ili wazini. Sikia hakuna mlozi hapo ni mwili tu, nimewahi kukutana na watu wengi wenye shida hii.
Anakuambia mtumishi kuna mwanaume zamani niliwahi kuwa naye tuliachana muda mrefu tu, yeye kaoa lakini ananifuata fuata sana, na anadai alikosea kuoa. Eheheeee!!! Mwili ni mbaya sana.
Mwingine anakuambia ananijia ndotoni mtumishi nahisi kaniendea kwa mganga. Sikia inawezekana ni mwili wako tu unabeba miunganiko usishangae huyo mwanaume hana mpango na wewe kabisaa, ila kuna alama au muunganiko uliokupata mwilini mwako siku zile mlipokuwa mkizini.
Ngoja nikupe mfano huu. Kuna kabila moja nchini Zambia, akifa mke au mume, wazee au watu maalumu, watamchukua huyo aliyebaki na kumuuliza swali hili. Je! Umewahi kutumia mdomo wako kuupitisha ulimi wako kwenye sehemu za siri za mkeo au mumeo aliyekufa?
Ukisema ndiyo, watakutengenezea dawa wao wanasema ya kuondoa muunganiko mkali mlioungana. Wanaamini mtu aliyefanya hivyo hatakawia na yeye kufa kwa sababu ya muunganiko wa namna hiyo.
Sasa hao ni watu wa dunia tu wanajua hivyo, umewahi fikiri kwa mtu ambaye hajaolewa na hajaoa anashiriki tendo la ndoa na wanaume au wanawake kwa mtindo wa namna hiyo unafikiri muunganiko huo mwilini unakaakaaje kwa mujibu wa ile mistari isemayo?
“Je! Hamjui ya kuwa miili yenu ni viungo vya Kristo? Basi nivitwae viungo vya Kristo na kuvifanya viungo vya kahaba? Hasha! Au hamjui ya kuwa yeye aliyeungwa na kahaba ni mwili mmoja naye? Maana asema, Wale wawili watakuwa mwili mmoja.” (1 Wakorintho 6:15-16).
Angalia ulimi si ni kiungo? Unafikiri kitatokea nini baada ya kufanya jambo hilo? Sitaki kuamini kile hao Wazambia wanaamini, nataka tuamini neno la Mungu kuwa chanzo kimojawapo kinachoweza kuusumbua mwili wa mtu aliyewahi kuzini ni muunganiko alioungana na huyo aliyezini naye.
Uzinzi haupitishi tabia tu ya uzinzi, nikifikia sehemu ya kukuonyesha madhara ya uzinzi utaona uzinzi una madhara mengi mno hata kukupatia roho za mapepo mbalimbali. Watu huona magonjwa ya zinaa hawajui kuna zaidi ya magonjwa ya zinaa yanayoupata mwili baada ya kuzini tu.
Anza kuishughulikia hiyo miunganiko inaweza ikawa ndiyo chanzo cha mwili wako kukusumbua kwenye dhambi ya zinaa.
Tubu,Tumia damu ya Bwana Yesu Kristo kukuondolea kila muunganiko wa namna hii ambao umeubeba mwilini mwako. Vunja ushirika ulio mwilini mwako wa mtu yeyote uliyezini naye, kama ni kumi wapange mmoja mmoja waondoe mwilini mwako fahamu wapo humo mwilini.
Angalia mistari hii. “Piga kelele, usiache, Paza sauti yako kama tarumbeta; Uwahubiri watu wangu kosa lao, Na nyumba ya Yakobo dhambi zao. Walakini wanitafuta kila siku; hupenda kujua njia zangu; kama vile taifa waliotenda haki, wasioacha sheria ya Mungu wao, hutaka kwangu amri za haki; hufurahi kumkaribia Mungu. Husema, Mbona tumefunga, lakini huoni? Mbona tumejitaabisha nafsi zetu, lakini huangalii? Fahamuni, siku ya kufunga kwenu mnatafuta anasa zenu wenyewe, na kuwalemea wote watendao kazi kwenu. Tazama, ninyi mwafunga mpate kushindana na kugombana, na kupiga kwa ngumi ya uovu. Hamfungi siku hii ya leo hata kuisikizisha sauti yenu juu. Je! Kufunga namna hii ni saumu niliyoichagua mimi? Je! Ni siku ya mtu kujitaabisha nafsi yake? Ni kuinama kichwa kama unyasi, na kutanda nguo za magunia na majivu chini yake? Je! Utasema ni siku ya kufunga, na ya kukubaliwa na BWANA? Je! Saumu niliyoichagua, siyo ya namna hii? Kufungua vifungo vya uovu, kuzilegeza kamba za nira, kuwaacha huru walioonewa, na kwamba mvunje kila nira?” (Isaya 58:1-6)
Tumia Damu ya Bwana Yesu Kristo, pia unaweza kufunga na kuomba ufunguliwe kama au miunganiko hiyo uliyoungana na hao uliowahi kuzini nao huwezi kuvunja muunganiko aliouunganisha Mungu yaani ndoa halali hapo mpaka kifo tu.
Lakini hii ya malaya, wahuni, makahaba inavunjwa tu wala usiogope. Jitie nguvu tu ya kuomba AU KUSEMA katika maombi yako sema hivi, kwa jina la Yesu Kristo, navunja kila muunganiko niliyoungana mwilini mwangu naaaa ..... (mtaje jina,) tumia jina la Bwana Yesu Kristo, tumia Damu ya Bwana Yesu Kristo kuvunja muunganiko huo.
Pingu au mafungo au miunganiko kwa kutumia damu ya agano jipya ya Bwana Yesu Kristo inavunja au kufungua. “Na kwa habari zako wewe, kwa sababu ya damu ya agano lako, nimewatoa wafungwa wako katika shimo lile lisilo na maji. Irudieni ngome, enyi wafungwa wa tumaini; hata hivi leo nasema ya kwamba nitakurudishia maradufu.” (Zekaria 9:11-12)
Damu iliwatoa wafungwa, unajua kufungwa kunamweka mtu kwenye eneo ambalo hauwezi toka, na wafungwa ni watu walio chini ya mamlaka fulani inayowasimamia na kuwaogoza pia, mwili hutumia kifungo au muunganiko huo wa uzinzi ili kuifanya roho yako kuwa chini ya mamlaka ya mwili katika eneo la kuhitaji tendo la ndoa kama mtu anaehitaji kipande cha mkate.
Damu ya Yesu Kristo inaweza kukukomboa hapo ulipopokea huo muunganiko. Gharama ya kutoka hapo ni ndogo tu, ni wewe kuanza maombi ya namna hiyo.
Unaweza ukaomba leo, leo leo ukajikuta upo huru, lakini si wote hujikuta wapo huru katika jambo hili siku moja, Omba mpaka uone dalili za mwili wako kuwa tofauti na zamani.
Tumia pia maombi ya Kumruhusu Roho Mtakatifu kuvunja hiyo miunganiko. “Tena itakuwa katika siku hiyo mzigo wake utaondoka begani mwako, na nira yake shingoni mwako, nayo nira itaharibiwa, kwa sababu ya kutiwa mafuta.” (Isaya 10:27)
Nira ni kifungo, mimi naita muunganiko, Sasa ili hizo nira zivunjwe au zifunguliwe yanahitajika pia mafuta. Mafuta ni Roho Mtakatifu. Biblia inasema hivi. “Nimewaandikia haya katika habari za watu wale wanaotaka kuwapoteza. Nanyi, mafuta yale mliyoyapata kwake yanakaa ndani yenu, wala hamna haja ya mtu kuwafundisha; lakini kama mafuta yake yanavyowafundisha habari za mambo yote, tena ni kweli wala si uongo, na kama yalivyowafundisha, kaeni ndani yake.” (1 Yohana 2:26-27)
Roho mtakatifu ndiye atufundishaye habari za mambo yote. “Lakini huyo Msaidizi, huyo Roho Mtakatifu, ambaye Baba atampeleka kwa jina langu, atawafundisha yote, na kuwakumbusha yote niliyowaambia.” (Yohana 14:26)
Kwa mujibu wa mistari hiyo mafuta yenye kutufundisha habari za mambo yote ni Roho Mtakatifu. Sasa anza kumwomba huyo Roho Mtakatifu auchunguze mwili wako umefungamana na nani? Unamuunganiko na nani? Na mpe ruhusa kwa njia ya maombi auvunje huo muunganiko. Achilia hayo mafuta Au Roho Mtakatifu mwilini mwako.
Mafuta ni upako, sasa jifunze pia kutafuta upako wa namna hii, utaanza kuona mabadiliko makubwa kwenye tabia yako, utashangaa ile nguvu ya mwanzo wa uzinzi mwilini unapungua na kuondoka kabisa.
Mungu akusaidie kuelewa na kuyaweka haya kwenye matendo.
Ubarikiwe sana na Mungu.
Ukihitaji masomo yetu unaweza kuyapata kwa njia hizi zifuatazo:-
1.Website yetu ya www.mwakatwila.org
2.YouTube - Mwakatwila au HUDUMA YA SOMA NENO LA MUNGU (HUSONEMU).
3.Facebook ingia katika hiyo tovuti au website yetu utaona alama ya facebook(f) like na utapata maelezo ya kujiunga au andika “SOMA NENO LA MUNGU”
4.DVDs📀 au CDs💿
5.VITABU
6.Kwa njia ya Redio:-
➖Rungwe FM 102.5 Kila siku ya Jumapili saa tatu mpaka saa nne usiku.
➖Baraka FM 107.7 Kila siku ya Jumanne saa kumi na mbili jioni mpaka saa moja usiku.
➖Bomba FM 104.1 Kila siku ya Ijumaa saa tatu usiku mpaka saa nne usiku.
7.Unaweza kutupata kwenye radio yetu online ya. radio.mwakatwila.org
Kwa mawasiliano zaidi Utatupata kwa namba hizi:- +255754849924 - +255756715222
Wako
Mwl Steven & Beth Mwakatwila.
20/12/2018
No comments:
Post a Comment