Wednesday, January 9, 2019

4⃣ MAMBO MUHIMU UNAYOTAKIWA UYAFANYE ILI UPATE KUISHINDA DHAMBI YA UZINZI

Na: MWL STEVEN & BETH MWAKATWILA

FUATANA NASI FACEBOOK

FUATANA NASI YOUTUBE

FUATANA NASI ONLINE RADIO
👉🏼 radio.mwakatwila.org

19 Dec, 2018

Bwana Yesu Kristo asifiwe, leo hii tena nimeona nikufundishe tena namna unavyoweza kufanya ili uanze kuwa mshindi dhidi ya tabia ya uzinzi.

Nilikuonyesha unavyoweza kuidhibiti tabia ya uzinzi au mwenendo wa kiurithi au ulioupokea kutoka kwa baba au uzao uliokuwa na mwenendo huu wa uzinzi. Nilikuonyesha namna damu ya Bwana Yesu Kristo inavyoweza  kukukomboa.
Unaweza kupata shida kuhusu damu hiyo kuushughulikia tabia fulani mwilini, Kumbuka damu ina uhai, damu ya Yesu Kristo pia ina uhai.

Sikiliza uhai wa mwili wa Bwana Yesu Kristo umo kwenye damu yake, unaposikia neno Bwana Yesu Kristo alitoa uhai wake maana yake alitoa damu yake. Damu ya Bwana Yesu Kristo ina uhai, ukiamini fahamu inaweza kutumika kabisa kukufungua au kukutoa katika hiyo tabia ya uzinzi iliyomo mwilini mwako.

Damu ya Yesu Kristo inaweza kunena “na Yesu mjumbe wa agano jipya, na damu ya kunyunyizwa, inenayo mema kuliko ile ya Habili.(Waebrania 12:24).

Damu ya Bwana Yesu Kristo ndiyo damu ya agano jipya ambayo inaweza kihalali kuondoa kila agano lolote lililofungwa iwe na mtu au watu.

Ili uingie katika agano jipya au ili uuweke mwili wako katika agano jipya baada ya kuwa chini ya agano la urithi ulilolipokea ni  lazima ulipokee agano jipya au ulitafute hilo agano jipya.

Sikiliza mtu atakayetaka kutoka katika agano la kwanza ni lazima alitafute agano jipya, Damu ya Bwana Yesu Kristo ndiyo pekee imebeba nguvu za kuyavunja maagano yote ya kwanza ambayo watu waliingia na shetani.

Ninaposema damu ya Yesu, kumbuka damu ya Yesu ndiyo uhai wa yeye mwenyewe Bwana Yesu. Huwezi ukamtenganisha Bwana Yesu Kristo na uhai wake. Angalia mfano huu tena. “Kisha mtu awaye yote wa nyumba ya Israeli, au miongoni mwa hao wageni wakaao kati yao, atakayekula damu, ya aina yo yote, nitakunja uso wangu juu ya mtu huyo alaye damu, nami nitamkatilia mbali na watu wake. Kwa kuwa uhai wa mwili u katika hiyo damu; nami nimewapa ninyi hiyo damu juu ya madhabahu, ili kufanya upatanisho kwa ajili ya nafsi zenu; kwani ni hiyo damu ifanyayo upatanisho kwa sababu ya nafsi. Kwa hiyo naliwaambia wana wa Israeli, Hapana mtu miongoni mwenu aliye na ruhusa kula damu, wala mgeni aketiye kati yenu asile damu. Mtu ye yote aliye wa wana wa Israeli, au wa hao wageni wakaao kati yenu, ambaye amemshika mnyama, au ndege ambaye huliwa, katika kuwinda kwake; atamwaga damu yake, na kuifunika mchanga. Kwa maana kuliko huo uhai wa mnyama, hiyo damu yake ni moja na uhai wake; kwa hiyo naliwaambia wana wa Israeli, Msile damu ya mnyama wa aina yo yote; kwa kuwa uhai wa wanyama wote ni katika hiyo damu yake; atakayeila awaye yote atakatiliwa mbali.” (Mambo ya Walawi 17:10-14)

Ukiipitia hiyo mistari utagundua hiki ninachokufundisha. Uhai wa mtu na damu ya huyo mtu ni kitu kimoja. Sasa sikia Unapoitumia damu ya Bwana Yesu Kristo kukutoa kwenye mwenendo au tabia mbaya  iliyofungwa mwilini mwako (YAANI ILIYOBEBWA KWENYE DAMU YAKO) fahamu kuna uhai mpya unaanza kutokea katika mwili wako.

Damu ya Yesu si tu itakufungua katika mwenendo huo, fahamu itaanza kuachilia tabia zake kwenye mwili wako. Kama damu ya baba yako ilipitisha tabia mwilini unafikiri damu ya Bwana Yesu Kristo itashindwa kupitisha tabia yake mwilini mwako?

Siku Mungu ananifundisha kipengele cha namna ya kuishi duniani bila kufanya dhambi kama mistari hii isemavyo. “Kila mtu aliyezaliwa na Mungu hatendi dhambi, kwa sababu uzao wake wakaa ndani yake; wala hawezi kutenda dhambi kwa sababu amezaliwa kutokana na Mungu.” (1 Yohana 3:9).

Ukiisoma hiyo mistari utaona mtu aliyezaliwa na Mungu hatendi dhambi. Na tumepewa sababu za mtu huyo kutokutenda kwake dhambi kunasababishwa na nini. Anasema ni kwa sababu uzao wake wakaa ndani ya huyo mtu.

Uzao wa Mungu unakaaje ndani ya mtu? Kumbuka tulikotoka, damu yoyote ina uhai, na damu inahusika mnoo katika kutengeneza uzao, ndiyo maana tunasema huyu ni damu yangu yaani huyu ni wa kizazi au ndugu yangu.

Angalia mfano damu inavyohusika Kibiblia katika suala la uumbaji wa mtu. “Na katika habari za kuzaliwa kwako, siku ile uliyozaliwa, kitovu chako hakikukatwa, wala hukuoshwa kwa maji usafishwe; hukutiwa chumvi hata kidogo, wala hukutiwa katika nguo kabisa. Hapana jicho lililokuhurumia, ili kukutendea lo lote la mambo hayo kwa kukuhurumia; lakini ulitupwa nje uwandani, kwa kuwa nafsi yako ilichukiwa, katika siku ile uliyozaliwa.Nami nilipopita karibu nawe, nikakuona ukigaagaa katika damu yako, nalikuambia, Ujapokuwa katika damu yako, uwe hai; naam, nalikuambia, Ujapokuwa katika damu yako, uwe hai.” (Ezekieli 16:4-6)

Ukiisoma hiyo mistari unaona namna ya damu na uhai inavyohusishwa katika suala la kuzaliwa kwa mtu, Anasema hivi, “Ujapokuwa katika damu yako, uwe hai; naam, nalikuambia, Ujapokuwa katika damu yako, uwe hai.” Mungu ameweka uhai kwenye hiyo damu,
Damu inahusika Kibiblia katika uumbaji wa mtu, sasa angalia kitu hiki, tabia mbaya tunazipokea kutoka kwa wahusika waliohusika katika kuzaliwa kwetu yaani mababa. “Nanyi mfahamu kwamba mlikombolewa si kwa vitu viharibikavyo, kwa fedha au dhahabu; mpate kutoka katika mwenendo wenu usiofaa mlioupokea kwa baba zenu;” (1 Petro 1:18).

Kumbuka tena jambo hili, mababa wanadamu, damu yao ndiyo itengenezayo uzao wetu ndani yetu. Sasa kwa kuwa uzao huo wa mababa umebeba uzinzi usifikiri wewe unayezaliwa katika uzao huo utapona hiyo tabia ndani yako. Ukinielewa hapo itakuwa rahisi kujua ni kwa nini Mungu anasemea kuwazaa upya watu wanaomwamini.
Anapokuzaa fahamu ataishughulikia damu yako kama alivyoishughulikia hapo juu kwa huyo mtu aliyemwambia “Ujapokuwa katika damu yako, uwe hai; naam, nalikuambia, Ujapokuwa katika damu yako, uwe ha” Kuna uhai mpya ambao atauachilia kwenye mwili wako yaani ATAACHILIA DAMU YAKE AMBAYO NDIYO UHAI.

Bwana Yesu Kristo hakuitoa damu yake kirahisi rahisi kama watu wengi wanavyofikiri na kuitazama. Damu inaumba uhai wa mwili, Mungu alijua sana hili kuwa hao ndugu miili yao ina uhai au damu ambayo imebeba uzinzi, uongo, uasherati nk.

Biblia inasema hivi. “Maana yale yasiyowezekana kwa sheria, kwa vile ilivyokuwa dhaifu kwa sababu ya mwili, Mungu, kwa kumtuma Mwanawe mwenyewe katika mfano wa mwili ulio wa dhambi, na kwa sababu ya dhambi, aliihukumu dhambi katika mwili; ili maagizo ya torati yatimizwe ndani yetu sisi, tusioenenda kwa kufuata mambo ya mwili, bali mambo ya roho. Kwa maana wale waufuatao mwili huyafikiri mambo ya mwili; bali wale waifuatao roho huyafikiri mambo ya roho. Kwa kuwa nia ya mwili ni mauti; bali nia ya roho ni uzima na amani. Kwa kuwa ile nia ya mwili ni uadui juu ya Mungu, kwa maana haitii sheria ya Mungu, wala haiwezi kuitii. Wale waufuatao mwili hawawezi kumpendeza Mungu. Lakini ikiwa Roho wa Mungu anakaa ndani yenu, ninyi hamwufuati mwili; bali mwaifuata roho. Lakini mtu awaye yote asipokuwa na Roho wa Kristo, huyo si wake.” (Warumi 8:3-9)

Sheria au maagizo aliyopewa mtu yaani roho yako, iligonga mwamba kwa sababu mwili ulikuwa na nguvu kuliko sheria au maagizo aliyopewa mtu asiyafanye.
Maana ya neno hukumu ni kutoa maamuzi katika kesi, au kupokea maagizo ya utaratibu au sheria iliyowekwa, maana nyingine ni kutumia mamlaka.

Sasa angalia Mungu alijua dhambi imebebwa katika mwili akaamua kuihukumu dhambi katika mwili, swali aliihukumuje? Unajua aliuhukumuje? aliamua kutumia mamlaka au nguvu ilikuudhibiti mwili, kumbuka mwili uhai wake umo kwenye damu.
Kwa maana nzuri aliamua kuuthibiti uhai wa mwili yaani damu. Aliiamua kuachilia damu yake yeye yenye nguvu ili ikomeshe nguvu ya mwili ambao uhai wake ni damu. UMENIELEWA HAPO?

Damu ya Bwana Yesu Kristo inahusika sana katika habari za kuzaliwa kwako mara ya pili. “Kwa maana wako watatu washuhudiao [mbinguni, Baba, na Neno, na Roho Mtakatifu, na watatu hawa ni umoja.Kisha wako watatu washuhudiao duniani], Roho, na maji, na damu; na watatu hawa hupatana kwa habari moja. Tukiupokea ushuhuda wa wanadamu, ushuhuda wa Mungu ni mkuu zaidi; kwa maana ushuhuda wa Mungu ndio huu, kwamba amemshuhudia Mwanawe.” (1 Yohana 5:8-9)

Ili kumzaa mara ya pili mtu, Roho, na Maji, na Damu vyote kwa habari hii vinapatana na vinatenda kazi pamoja. Huwezi kuvitenganisha. Na vyote viliachiliwa na Bwana Yesu Kristo.

Si unajua nilikufundisha namna ya kuufisha mwili kwa Roho? Fahamu roho huyo anaitwa Roho wa Kristo. Yaani ndiye Bwana Yesu Kristo Mwenyewe. “Na kwa kuwa ninyi mmekuwa wana, Mungu alimtuma Roho wa Mwanawe mioyoni mwetu, aliaye, Aba, yaani, Baba.” (Wagalatia 4:6)

Fahamu pia Damu ya Yesu Kristo ndiyo uhai wake Yesu mwenyewe yaani ni Yesu mwenyewe. Na maji hayo nitakufundisha hapo mbeleni yalitoka kwenye ubavu wa Yesu mwenyewe. Si unajua maji na uhai wa mtu ulivyo?

Mungu aliamua kutupa vitu hivi vitatu ili kukamilisha mamlaka ya Mungu katika mwili wa mtu. Sasa sikia, tunavipokea kwa imani, na tunavitumia kwa imani.

Imani ni kuwa na hakika wa mambo yatarajiwayo ni bayana ya mambo yasiyooneka. Mfano, damu ya Yesu  au maji ya Yesu au Roho wa Yesu hatuvioni hivi kwa macho haya ya nyama. Lakini vipo. Ukiwa na hakika kuwa vipo na ukaanza kuvitumia jenga tarajio la kuona mabadiliko katika mwili wako.

Ngoja nikupe mfano huu. Mimi nilikuwa na tabia mbaya sana; uongo, hasira yaani nilikuwa mtu wa kisasi, wivu, husuda, kuhukumu hivi vilinijaa. Mimi kuutunga uongo na kuusema kwangu ilikuwa kawaida tu, nilikuwa mtu wa hasira mkali kweli, si kuwa mtu ninaishi kwa ukweli nilikuwa kama msanii hivi, nje mpole mtaratibu lakini kwa kweli ndani yangu nilikuwa mtu mbaya sana.

Mwili wangu ulikuwa unawaka sana tamaa ya uzinzi, lakini sikuwahi zini, ila nilikuwa mzinzi mzuri tu moyoni, nilikuwa natamani weee nk. Nilipookoka tu. Mungu alianza kunifundisha haya ninayo kufundisha, Nikigundua mimi sijawahi zini lakini ninasumbuliwa mno na tamaa ya uzinzi.

Nilianza kujifunza habari za urithi wa tabia au mwenendo. Niligundua babu yangu mzaa baba alikuwa na wake watatu, baba alipona ana mke mmoja tu yaani mama yetu. Baba aliwahi nisimulia kuzaliwa kwangu kulivyokuwa, baba yangu alimwekea Mungu nadhiri katika kunipata mimi.

Anasema alikuwa ananiombea sana hata nilipozaliwa. Niligundua nguvu iliyonisaidia nisizini kwa kweli alikuwa ni Mungu tu. Kwa sababu si kuwa nilikuwa sina wasichana, walikuwepo, lakini kulala nao hivi hapo nilishindwa kabisa.

Si kuwa nilikuwa siwapati. Aisee nikikusimulia unaweza usiamini. Niliwahi chukua na msichana mmoja(kwa sasa ni marehemu ndiyo maana nasema) nikatoa nguo zote, sikiliza nilipotaka kupanda kitandani nilale naye, nilisikia sauti, ikisema Steven jambo hili unalotaka kulifanya Mungu halipendi na baba yako halipendi na mama yako akijua atakuchapa sana!!!

Wakati huo nilikuwa naishi na wazazi wangu ila nina shughuli zangu za kibiashara. Unajua sauti ile ilinitetemesha mwili wote, nguvu zikaniishia fyuuuuu!!! Nikakimbilia chooni.
Yule binti hakusikia, nikakaa chooni mpaka mwili wangu ulipokaa sawa. Niliporudi nikamwambia huyo binti vaa nguo twende, akakataa, nikamwambia sawa mimi naenda hii gheto siyo langu shauri yako.

Nikamwambia ukifunga mlango funguo weka mahali fulani, nikakimbia. Nilikaa nikajiuliza ile sauti ni ya nani? Kwa nini imetokea hivyo? Unajua nilipokuja kuokoka nikajua Roho Mtakatifu kipindi hicho yupo nje yangu aliwajibika kunipasha habari ya hiyo dhambi.

Mungu alinifundisha kuwa, mwili wangu unabeba sana tamaa ya uzinzi kisa niangalie mwenendo wa mababa yaani ukoo. Nikagundua upande wa mama Aisee babu alikuwa ana wake kama thelathini na tano hivi.
Eheheee!!! Babu mzaa baba wako watatu, nikaangalia baba zangu wengine wakubwa kwa wadogo, nikaangalia kaka zangu wa baba zangu wakubwa na wadogo yaani huko nikaona ndiyo hatari kabisaa, wajomba aisee huko ndiyo hatari.

Nikaona nimepokea nini mwilini mwangu ingawa Mungu kwa nguvu zake ananipigania tu. Sasa kila mtu ana neema yake. Mungu alinifundisha nikiwa nyumbani kwangu. Nianze maombi ya kuufisha mwili.

Au kuihukumu dhambi au kutumia mamlaka dhidi ya dhambi katika mwili. Sikia mwili hauwezi kutii neno la Mungu au kumtii Mungu wenyewe umechagua dhambi tu. Moja ya dhambi ni uzinzi.

Sasa ili utii inatakiwa uamrishwe. Na nguvu ya kimamlaka ya kuudhibiti mwili imekaa kwenye hivi vitu yaani damu, maji, Roho, na Neno. Nitajaribu kukuonyesha kazi ya neno na maji huko mbeleni.

Nilitaka nikutazamishe leo kuhusu damu kwa upana kidogo ili uone umuhimu wa kuanza kuitumia damu hii ya Bwana Yesu Kristo ili kuihukumu dhambi katika mwili na ukajikuta unaingiza uzao wa Mungu ndani yako.

Unaweza sema Roho Mtakatifu yuko ndani yangu. Ni kweli, lakini upanga wake unajua ni Neno la Mungu? Na ndani ya Neno huko ndiyo unakuta mafundisho yanayokufundisha habari za damu nk.

Mimi nikianza maombi ya namna hiyo, unajua nilishangaa ghafla naanza kuwa mtu asemaye kweli. Wakati nilikuwa mwongo kweli kweli, na niligundua chanzo cha uongo ni wapi. Pande zote mbili, upande wa baba na upande wa mama huko kote uongo ni kawaida tu.

Hasira ndiyo hivyo hivyo, yaani usiseme mtu yaani mtu kumfukuza mtoto wake na kumzira na ndugu tu kugombana  ni kitu cha kawaida tu. Niliona wababa wachache ndiyo wamepona na kilichowasaidia ni wale waliookoka, na walikuwa si wengi. Nikagundua kuwa hii ni tabia nimeipokea hata kama baba ni mpole, lakini kwa ujumla niliona hakuna upole ila ni wakimya.

Kwenye eneo la kisasi niliangalia nikagundua aisee hapo tumebanwa, yaani niliona namna pande zote yaani upande wa baba na mama hiyo tabia ilikuwepo tena kali tu. Watu wanalipiziana visasi tu, nikajua hii nimepokea, unajua roho ya kisasi inaletwa na tabia ya kutosamehe.

Niliona mimi si mtu wa kusamehe. Kwenye wivu na husuda ndiyo hivyo hivyo. Yaani niligundua nimebanwa hapo kabisaa. Nikaangalia pande zote nikaona aisee hii tabia nimeipokea kabisaa.

Nilikuwa namwuliza baba, ananisimulia baba zake walivyokuwa, kaka zake mama zake nk, niliona hayo. Sasa nikaanza maombi, nikiitumia damu ya Yesu kunitenganisha na tabia hizo nilizopokea tena kihalali kutoka kwa mababa.

Nilikuwa naomba angalau kwa mwezi mara tatu. Nafunga naomba. Natumia damu ya Bwana Yesu Kristo kunikomboa na tabia hizo. Huwezi amini siku moja nilipokuwa naomba nikiachilia damu ya Yesu kwenye mwili wangu wenye damu iliyochakachukiwa, nilikuwa naona kabisaa mwili unatetemeshwa  na kama umeme unatembea naogopa naacha. Ehehee.

Siku moja Mungu akaniambia usiogope endelea kuomba. Niliendelea mpaka leo huwa nayaomba maombi ya namna hii. Matokeo yake kwa kweli niliona roho yangu inavyoweza kuushinda mwili. Na nimekuwa na mwenendo tofauti na zamani.

Mpaka mtu mmoja aliwahi niuliza mtumishi unawezaje kukaa na wanawake walio uchi ukawafundisha? Aliniuliza hivi baada ya mimi na timu yangu kwenda eneo lenye watu ambao wanaitwa bushman. Na nikawaambia habari za Yesu kwa muda wa wiki mbili hivi. Watu hao hawavai nguo wapendwa  wako uchi. Shukuru ukikutana na aliyevaa kisepe.

Nilimjibu “Mungu alinifundisha namna ya kuufisha mwili.” Sikiliza hata wewe ukiamini na ukaamua kuyafanya haya kwa imani ambayo inakuja kwa kusikia neno la Kristo, na ukaanza kuyafanyia kazi huku ukitarajia badiliko nakuhakikishia utaona mabadiliko mwilini mwako.

Mungu akubariki sana. Nikipata muda nitakufundisha mambo mengine ya kufanya ili kuudhibiti mwili kwenye eneo la uzinzi.

Ukihitaji masomo yetu unaweza kuyapata kwa njia hizi zifuatazo:-

1.Website yetu ya www.mwakatwila.org

2.YouTube - Mwakatwila au HUDUMA YA SOMA NENO LA MUNGU (HUSONEMU).

3.Facebook ingia katika hiyo tovuti au website yetu utaona alama ya facebook(f) like na utapata maelezo ya kujiunga au andika “SOMA NENO LA MUNGU”

4.DVDs📀 au CDs💿

5.VITABU

6.Kwa njia ya Redio:-
➖Rungwe FM 102.5 Kila siku ya Jumapili  saa tatu mpaka saa nne usiku.
➖Baraka FM 107.7 Kila siku ya Jumanne saa kumi na mbili jioni mpaka saa moja usiku.
➖Bomba FM 104.1 Kila siku ya Ijumaa saa tatu usiku mpaka saa nne usiku.

7.Unaweza kutupata kwenye radio yetu online ya. radio.mwakatwila.org

Kwa mawasiliano zaidi Utatupata kwa namba hizi. +255754849924 - +255756715222

Wako
Mwl Steven & Beth Mwakatwila.
19/12/2018

No comments:

Post a Comment