9⃣ MAMBO MUHIMU UNAYOTAKIWA UYAFANYE ILI UPATE KUISHINDA DHAMBI YA UZINZI
Na: MWL STEVEN & BETH MWAKATWILA
FUATANA NASI YOUTUBE
KUPATA APP YETU “HUSONEMU (MWAKATWILA) APP”, BONYEZA LINK HAPA:
FUATANA NASI WHATSAPP
FUATANA NASI FACEBOOK
FUATANA NASI INSTAGRAM
&
FUATANA NASI ONLINE RADIO
👉🏼 radio.mwakatwila.org
🗓 10 Januari, 2019
Bwana Yesu Kristo asifiwe sana. Nilikuahidi kuwa nitakuonyesha namna ya kushughulikia akili ili ikae vizuri katika eneo la kuutawala mwili wako hasa katika kona ya kuizishinda dhambi hasa dhambi ya uzinzi.
Nilikuonyesha jambo la kwanza nalo lilikuwa uweke bidii ya wewe mwenyewe ujue namna ulivyoumbwa. Nilikuonyesha ulivyoumba na akili zinakaa wapi na ndani ya akili kuna nini.
Nilikuonyesha namna nafsi ilivyoambatana na mwili. Na namna akili au ufahamu wa mtu ulivyoharibiwa baada ya dhambi kuingia tu.
Baada ya kukuonyesha jambo la kwanza kuna mambo kama matatu hivi yanafuata ili uanze kuzijenga au kuziweka sawa akili zako mpaka ufahamu wako au akili zako ziwe na Mungu.
Ngoja nikuonyeshe hayo mambo matatu
1. Jambo la kwanza ni maombi maalumu yanayohusu akili zako tu.
2. Jifunze kuilisha akili chakula chake.
3. Jifunze kushughulikia milango mitano ya ufahamu.
Hebu tuanze kuliangalia moja baada ya lingine.
WEKA BIDII YA KUJIFUNZA KUILISHA AKILI YAKO CHAKULA
Sijakosea ninapokuambia jifunze kuilisha akili yako chakula chake. Watu wengi sana hawajui kuwa akili zetu zina chakula yaani zinaweza kula na zikawa na afya kabisa na kukua na kuwa kubwa mno.
Sikiliza hapo sizungumzii chakula cha roho, nazungumzia chakula cha akili. Kumbuka ndani ya akili kumefungiwa vitu vingi sana. Ndani ya akili kumefungiwa ufahamu, kuna kuelewa, kukusudia au kuwaza au kunia au kudhamiria, kujua, kukumbuka, kubuni, kufikiri, kutafakari, nk.
Hayo mambo yote ili yakae sawa kuna namna ya kuyatengeneza. Fahamu dhambi ilipoingia, mwili wako wenyewe uliyachagua mambo mabaya ya duniani, ili mwili ufanikiwe katika kuona mambo yake yanatekelezwa uliamua kufanya shambulio kwenye eneo linaloitwa nafsi, na mwili ukafanikiwa kwa asilimia kubwa kuziteka nyara akili au fikra.
Sasa sikia mtu yaani (roho) anapookoka yaani mwili wake hauokoki, kumbuka nafsi iliyobeba akili hisia na utashi viliambatana na mwili. Sasa unapozaliwa mara ya pili fahamu hata hizo akili zako zinazaliwa mara ya pili.
Sasa zinapozaliwa zinahitaji chakula ili ziwe hai. Kumbuka zilikuwa chini ya mamlaka ya mwili sasa ili zibadike Biblia inaita zigeuzwe. Angalia mistari hii. “Basi, ndugu zangu, nawasihi, kwa huruma zake Mungu, itoeni miili yenu iwe dhabihu iliyo hai, takatifu, ya kumpendeza Mungu, ndiyo ibada yenu yenye maana. Wala msiifuatishe namna ya dunia hii; bali mgeuzwe kwa kufanywa upya nia zenu, mpate kujua hakika mapenzi ya Mungu yaliyo mema, ya kumpendeza, na ukamilifu.” (Warumi 12:1-2)
Angalia ili usizifute tamaa za mwili au hapo anasema namna ya Dunia anasema unatakiwa ugeuzwe nia yako. Ili mwili wako wewe uwe dhabihu ya kumpendeza Mungu fahamu kuna mahusiano makubwa na nia yako.
Anaposema mgeuzwe nia zenu ana maana ubadilike katika mtazamo wako wa AKILI. Kumbuka huko ndani ya akili kuna ufahamu, kujua, kuwaza, kufikiri, nk.
Ili uushinde mwili siyo tu eti umeokoka na ni mtumishi, kuna kazi ya kufanya ambayo wewe mwenyewe unatakiwa hatua ya kuanza kufanya nayo ni kuhakikisha unaanza kubadilika katika ufahamu wako au katika akili zako.
Mungu anataka ubadilike katika kutazama kwako. Fahamu akili ndiyo macho ya mtu ya ndani. Mtume Paulo anaposema macho yao ya ndani yatiwe nuru fahamu anazungumzia mfumo wa akili zetu.
Ndani ya akili huko ndiko tunakotazama au tunakoona mambo mengi mnoo kuliko macho haya ya nyama yanavyoona. Macho ya nyama yataona mpaka ukomo fulani lakini akili au ufahamu wako wa ndani wenyewe utaona kwa undani zaidi.
Nikikuuliza swali hili: hivi ukitazama juu angani macho yako ya nje yanaona nini? Macho yako ya ndani yaani ufahamu nao unaona nini? Sikiliza ukiwa leo hii unataka kujenga nyumba na ukawa umeitengeneza ramani fahamu ukienda hapo uwanjani macho yako ya nyama yaona poli hivi ila macho yako ya ndani yaani akili yatatazama au yataona nyumba mpaka bustani nk.
Ndiyo hivyo hivyo kwenye eneo la kuushinda mwili. Lazima huko ndani yako yaani kwenye akili zako uhakikishe unaanza kutazama tofauti ulivyokuwa unatazama zamani.
Ngoja nikupe mfano. Ukiwachukua watu wawili leo mmoja aliyebadilika ndani ya mtazamo wake na yule ambaye hajabadilika uwaletee mwanamke au mwanaume aliye uchi mwanamume au mwanamke aliyebadilika katika mtazamo wake wa kumtazama mwanamke usishangae hatababaika. Ila yule ambaye bado mtazamo wake umekaa kizinzi zinzi utaona atakavyohangaika.
Ukimwuliza kwa nini unapata shida atakuambia aisee huyu mwanamke yuko uchi bwana, ananiletea shida tu. Ehehee unajua shida yake iko wapi?
Akili zake hazijawa na afya. Kumbuka sisemi roho yake haina afya nasema akili.
Angalia maneno haya. “Basi, wekeni mbali uovu wote na hila yote, na unafiki na husuda na masingizio yote. Kama watoto wachanga waliozaliwa sasa yatamanini maziwa ya akili yasiyoghoshiwa, ili kwa hayo mpate kuukulia wokovu;” (1 Petro 2:1-2).
Angalia tumeagizwa tuyatamani maziwa ya akili ili tukue katika wokovu. Ili wokovu uliopewa UWE MKUBWA LAZIMA UHAKIKISHE UNAIPA AKILI CHAKULA.
Kwa nini watu wanazini? Jibu ni rahisi ni UCHANGA WA AKILI ZAO TU.
Siyo mimi nasema Biblia inasema ili mtu asiwe mnafiki, mwongo, mwovu, mwenye masingizio, mzinzi, mchawi, mwabudu sanamu nk. Inatakiwa atamani maziwa ya akili.
Angalia jambo hili. Watoto wa Mungu wengi tunashughulikia sana chakula cha kiroho na kuzitafutia roho zetu nguvu lakini kwenye eneo la kuzitafutia hizo akili chakula, ndiyo tumeshindwa.
Watu wengi sana wana nguvu za rohoni lakini kila siku ni waongo wee, wambea wee, wazinzi wee. Wewe mwulize Roho Mtakatifu tatizo liko wapi atakuambia akili zao zina shida.
Akili zina chakula chake. Chakula hicho kina mifumo yake. Kuna chakula cha kitoto, na cha watu wazima, na pia kuna chakula cha akili za mambo mazuri yatakayokusaidia namna ya kuishi humu duniani.
Na kuna akili za mambo ya rohoni. Ukikosa akili njema mpendwa za namna ya kuishi humu duniani fahamu utakwama tu na Bwana Yesu Kristo unaye. Akili ni ufahamu, uelewa, kujua, kubuni, kuumba, kukumbuka, nk. Ili ulime shamba na uvune unahitaji akili yenye imani.
Ukiwa huna akili huku unaniambia una imani, fahamu hauwezi kusogea kabisa. Ngoja nikupe mfano huu. Unataka fedha? Jibu ni ndiyo, sasa unafikiri utazipata wapi? Jibu nitamwomba Mungu? Mungu anakupa fedha au akili ya wewe kupata fedha?
Ninachotaka nikuonyeshe hapo ni mfumo wa akili jinsi tunavyouangalia hasa sisi tuliookoka. Usifikirie kabisa kuwa Bwana Yesu Kristo anafurahia anapoona watoto wake tunakosa akili au ufahamu hata wa namna ya kufanya tu ili tupate fedha.
Tunaanza kutegemea miujiza, unasema kivipi, wewe tu angalie watoto wa Mungu tulivyo. Nakuambia ukweli matatizo yetu mengi mno tunayapa kisa hatujatumia akili tu. Ufahamu wetu wa mambo ni mdogo mno kwenye mambo mengi mnoo.
Kuna wakati huwa nikiwaangalia wapendwa nalia machozi, ngoja nikupe mfano, umewahi kukutana na wapendwa waliookoka na ni mafundi wa ujenzi wa nyumba?
Wengi hulalamika kuwa hawapati wateja nk. Wewe waulize ni nyumba zipi wamejenga. Kaziangalie. Unashangaa kuona fundi mpendwa kajenga nyumba ambayo hata mtu asiyeokoka anaweza kuijenga.
Unajua kwa nini nasema hivyo? Angalia mistari hii. “Basi Bezaleli na Oholiabu watatenda kazi, na kila mtu mwenye moyo wa hekima, ambaye BWANA amemtia akili na hekima ili ajue kufanya kazi hiyo yote kwa huo utumishi wa mahali patakatifu, kama hayo yote BWANA aliyoyaagiza. Basi Musa akawaita Bezaleli na Oholiabu, na kila mtu aliyekuwa na moyo wa akili, ambaye BWANA alimtia moyoni mwake hekima, kila mtu ambaye moyo wake ulimhimiza ili aende kuifanya kazi hiyo;” (Kutoka 36:1-2).
Umewaona wajenzi hawa? Walijenga KWA AKILI, WALIBUNI VITU VIZURI KATIKA UJENZI WAO. HIYO NDIYO INAITWA AKILI.
Sasa fundi hata kujiongeza tu hajiongezi kapewa ramani anajenga chini ya kiwango cha hiyo ramani, Unafikiri atapata fedha huyo? Ila ameokoka, ukimwuliza Mungu atakuambia huyu ndugu kaokoka ni mwaminifu kweli ila akili hamna.
Fundi wa kushona ndiyo hivyo hivyo. Niliwahi mwambia mke wangu kuwa mafundi waliookoka kwa kweli kuna shida. Ukimpa kitambaa akushonee nguo wewe tarajia tu kilio.
Wewe umemweleza hivi yeye atafanya yaliyo chini ya kiwango kile ulichomwagiza.
Akili zetu wengi bado ni ndogo mno yaani za kichanga, ndiyo maana utaona hata magomvi makanisani nk.
Angalia mistari hii. “Lakini, ndugu zangu, mimi sikuweza kusema nanyi kama na watu wenye tabia ya rohoni, bali kama na watu wenye tabia ya mwilini, kama na watoto wachanga katika Kristo. Naliwanywesha maziwa sikuwalisha chakula; kwa kuwa mlikuwa hamjakiweza. Naam, hata sasa hamkiwezi,kwa maana hata sasa ninyi ni watu wa tabia ya mwilini. Maana, ikiwa kwenu kuna husuda na fitina, je! Si watu wa tabia ya mwilini ninyi; tena mnaenenda kwa jinsi ya kibinadamu” (1 Wakorintho 3:1-3).
Ukiona ugomvi au fitina na husuda au wivu kwa watoto wa Mungu wewe fahamu tatizo ni hili ninalokuambia akili zao zimekosa chakula.
Sasa hakuna kitu kibaya kama uliletwa maziwa ya akili halafu ukashindwa kuyanywa. Yaani huyo mtu kuyafanya mambo ya mwili yaani mabaya kwake itakuwa rahisi tu.
Mtume Paulo alijitahidi kuwapatia hao maziwa ya akili, lakini bahati mbaya
hawakuyaweza.
Unafikiri watu wa namna hiyo unawafanya nini? Fikiria maziwa ya akili hawawezi kuyanywa, maziwa tu ya akili hawawezi kuyanywa unafikiri watabadilika kitabia?
Hawawezi kubadilika kitabia kwa kuwa wao wenyewe hawajayakubali maziwa ya akili, ndiyo maana nakuambia weka bidii katika kuilisha akili yako chakula.
Usifikiri ni kitu rahisi tu, inahitaji wewe mwenyewe uweke bidii na kuyapenda hayo maziwa. Ukisikia neno hamkuweza maana yake kuna maudhi fulani, unaweza kuyapata katika kuyanywa mazima ya akili.
CHAKULA CHA AKILI NI NENO LILILOJEMA (MAALUMU)
Ili uwe na ufahamu au akili au ujue au uelewe ni lazima ujifunze kusikia neno lenye kukuletea wewe ufahamu katika akili zako. Neno litakalobadilisha mtazamo wako wa kwanza kabisa na kukujengea wewe kuvumbua au kubuni au kutengeneza uwe mfumo wa maisha nk.
Na neno hilo likujengee akilini mwako ujuzi uliokamili katika maisha yako yote. Unaweza kuniambia mbona neno nasikiliza? Ngoja nikuulize ukisikiliza je! Limebadilisha mfumo wa maisha yako?
Ukiona watu wanasikiliza neno na hawabadiliki kuna mawili. Walisikiliza ila hawakuelewana nalo au halikukaa katika akili au ufahamu wao. Jifunze kusikiliza neno KWA FAIDA. Ngoja nikupe mfano unaweza kulisikiliza neno na ukalisema lakini kama hukuliruhusu likabadili mtazamo wako au likageuze hiyo nia yako ya zamani fahamu hilo neno halitakufaa kitu.
Ndani ya neno la Mungu huko ndiko kuna akili, sasa tunatofautiana namna ya kukisikia, kulitafakari, na kuwa sehemu ya maisha yetu. Watu wengi huja kusikiliza neno lakini wengi bahati mbaya hutengeneza ngome mawazoni mwao kabla hata hawajalisikiliza. Hili ndilo tatizo kubwa.
Ngoja nikupe mfano: fikiria wewe ni mzinzi kabisaa unapoambiwa tu habari za uzinzi je! Unaliweza neno hilo kuliingiza akilini mwako? Akili zako zinaweza kulibeba hilo neno au ndiyo tayari unamchukia aliyetoa hilo neno?
Watu wengi huanza kuwafikiria watu wengine kabisa. Utaona akili yake inasema yaani huyu ananisema hivi kuna mtu kamwambia, atakuwa fulani, akili yake badala ya kuyanywa hayo maziwa inaanza kunyweshwa hasira, hukumu na kujitetea.
Watu wa namna hii hawawezi kubadilika kabisa kiakili kimwili na kitabia. Umewahi kujiuliza swali kwa nini Mungu alimpenda mfalme Daudi? Unapomsoma mfalme Daudi alikuwa ni mtu mwenye tabia za mwili tu.
Lakini, mabadiliko ya tabia zake yalichangiwa sana na tabia ya namna alivyopokea neno la kumbadilisha mtazamo wake. Daudi hakuwa mbishi anapoletewa neno “wewe mzinzi”.
Anakubali ndiyo unamsikia akimwambia Mungu “Aisee, Aisee mimi nahitaji msaada nafsi yangu imeambatana na mavumbi” angalia hii mistari uone. “Nafsi yangu imeambatana na mavumbi, Unihuishe sawasawa na neno lako.” (Zaburi 119:25).
Umeona maneno hayo? Kinachohuisha nafsi ni neno, kumbuka ndani ya nafsi kuna akili ambayo imebeba mambo mengi sana. Unapotaka leo hii kuona unaanza kuwa na ufahamu mzuri au akili nzuri jifunze kuitafutia akili neno la Ufahamu au neno la akili litakalokupa kujua.
Watu wengi husoma Biblia husikikiza mafundisho lakini wanajikuta wako vile vile. Unajua sababu nyingine ni nini?
Angalia usomaji wao na usikilizaji wao. Wengi hutafuta neno na husikiliza neno lakini hawajui kutafuta neno linalohitajika kwa ajili ya akili zao.
Ngoja nikuambie, wewe una shida ya uzinzi yaani ufahamu wako, kujua kwako na kuelewa kwako kumefungiwa uzinzi. Ili uzipate hizo akili ni lazima uzitafutie maneno mema yanayohusu uzinzi.
Tafuta kila neno ndani ya Biblia linalozungumzia uzinzi. Ilishe akili yako hayo maneno yatafakari weee hayo maneno yawaze wee hayo maneno yaseme weee hayo maneno utaona ghafla akili yako inaanza kupata afya katika suala la tabia ya uzinzi, mwili ukianza kuwaka tamaa fahamu utakutana na pingamizi kutoka kwenye akili.
Moja ya tatizo lingine ambalo watu wengi waliookoka wanalo ni hili la kusikia neno ila ni wavivu wa kulifikiria hilo walilolisikia. Angalia mistari hii utaona agizo tulilopewa ni hili la lazima ulifikirie au ulitafakari kwa muda mrefu lile neno jema ulilolisikia.
“Nasema kama na watu wenye akili; lifikirini ninyi ninenalo.” (1 Wakorintho 10:15)
Kama huna muda wa kulifikiria neno lile ulilolisikia fahamu hautakuwa mwenye akili. Kwa nini watu wengi hawabadiliki akilini? Angalia muda wao wa kukifikiria lile walilolisikia.
Ni kitu rahisi tu, nikuulize swali somo hili ninalokufundisha kama ni jema umechukua muda gani kufikiri yoote au kiasi cha yale nikufundishayo? Angalia muda wa wewe kufikiria au kukila akilini hicho ulichojifunza?
Akili ili idake neno jema itamuhitaji mtu huyo atakaye akili zake zikae sawa, awe na muda mrefu wa kukifikiria hicho alichojifunza. Nje na hapo huwezi kuwa na akili. Mimi nawaona watu wengi ni mafundi wa kuandika weee.
Wewe waangalie wanavyochukua muda wa kukitafakari yaani zaidi kuwaza kile walichojifunza. Utaona ni watu wachache sana huchukua muda wa kutulia na kuanza kukifikiria weee na kukizungusha akilini kile walichosikia.
Kitendo hicho cha kuwa na muda mrefu kukifikiria kitu hicho ulichojifunza ndiyo tunaita KUILISHA AKILI CHAKULA. Sijui wewe ukoje? Unailisha kweli akili yako chakula kwa kujipa muda mrefu kufikiri neno la Mungu ulilolisikia?
Najua ukisikia kitu, ukachukua muda kukitafakari huwezi kukisahau. Angalia watu waotao ndoto wanasikia huko ndotoni, wakiamka wanakumbuka tatizo lao. Kabla hawajaanza shughuli ilitakiwa wafikirie weee hicho walichokiota ndipo waondoke kitandani.
Kwa kuwa hawana muda wa kutulia na kufikiri ndoto hizo huyeyuka. Sikiliza jifunze kuilisha akili yako chakula kwa kufikiria kile ulichokisikia hapo ndiyo tunaita umeliweka neno jema ndani yako.
Ni rahisi mno akili zako kupokea neno jema na ukajikuta unaanza kuushinda mwili na tamaa zake.
Ngoja nikupe mfano huu. Angalia mistari hii. “Maana sijui nifanyalo, kwa sababu lile nilipendalo, silitendi; bali lile nilichukialo ndilo ninalolitenda. Lakini kama nikilitenda lile nisilolipenda, naikiri ile sheria ya kuwa ni njema.Basi sasa si mimi nafsi yangu ninayetenda hilo, bali ni ile dhambi ikaayo ndani yanguKwa maana najua ya kuwa ndani yangu, yaani, ndani ya mwili wangu, halikai neno jema; kwa kuwa kutaka nataka, bali kutenda lililo jema sipati. Kwa maana lile jema nilipendalo, silitendi; bali lile baya nisilolipenda ndilo nilitendalo.Basi kama lile nisilolipenda ndilo nilitendalo, si mimi nafsi yangu nilitendaye, bali ni ile dhambi ikaayo ndani yangu.Basi nimeona sheria hii, ya kuwa kwangu mimi nitakaye kutenda lililo jema, lipo lililo baya. Kwa maana naifurahia sheria ya Mungu kwa utu wa ndani,lakini katika viungo vyangu naona sheria iliyo mbali, inapiga vita na ile sheria ya akili zangu, na kunifanya mateka ya ile sheria ya dhambi iliyo katika viungo vyangu. Ole wangu, maskini mimi! Ni nani atakayeniokoa na mwili huu wa mauti? Namshukuru Mungu, kwa Yesu Kristo Bwana wetu. Basi, kama ni hivyo, mimi mwenyewe kwa akili zangu naitumikia sheria ya Mungu, bali kwa mwili wangu sheria ya dhambi” (Warumi 7:15-25).
Ukiisoma hiyo mistari utanielewa ninapokuambia ili uanze kuushinda mwili kwa dhambi yoyote lazima yatokee mapinduzi kwenye akili yako. Na ili mapinduzi hayo yafanyike lazima akili yako ianze kupokea neno jema.
Mtume Paulo anasema wazi kuwa kitendo cha yeye kujikuta akiyafanya mambo ya mwili ni kwa sababu ya neno jema kutokukaa ndani yake. Yaani ndani ya akili.
Alipookolewa tu angalia kilichotokea anasema “Namshukuru Mungu, kwa Yesu Kristo Bwana wetu. Basi, kama ni hivyo, mimi mwenyewe kwa akili zangu naitumikia sheria ya Mungu, bali kwa mwili wangu sheria ya dhambi”
Mwili ulipofarakana na akili za mtume Paulo ghafla mtume Paulo akajikuta akili zake zikimtumikia Mungu ila mwili ulikataa kumtumikia Mungu.
Kumbuka mwili ulioambatana na nafsi yaani akili utakuwa na nguvu ya kuyatekeleza mambo ya mwili.
Mwili ukifarakana na akili fahamu ni vigumu mwili kuyafanya mambo yake. Sikiliza, unaposoma Biblia unaona kuwa nguvu ya kutenda jambo tunaita utashi au msukumo wa kutenda jambo umeambatana mno na akili za mtu. Msikilize Musa asemavyo
“Musa akasema, Kwa jambo hili mtajua ya kwamba BWANA amenituma, ili nifanye kazi hizi zote; kwa kuwa mimi sikuzifanya kwa akili zangu mwenyewe” (Hesabu 16:28).
Neno “sikuzifanya kwa akili zangu” linatupa picha kuwa msukumo wa kufanya jambo unafungamana pia na akili. Akili zikiwa njema ni rahisi msukumo wako wa kufanya jambo ukalifanya jambo jema. Hivi vitu vinafanya kazi pamoja ingawa ni vitu viwili tofauti. Utashi na akili ni vitu viwili. Utashi hauwezi kufanya jambo kama akili haijapeleka huko taarifa ya nini akili inataka kifanyike.
Akili ikiwa na ufahamu au uelewa wa kitu kinachoitwa kukataa “usizini” nakuambia utashi utaamua hicho. Roho yako pia inategemea hizo akili ili maamuzi sahihi ya roho yako ya kukataa dhambi yawe na mashiko.
Akili ikiwa imebeba mabaya fahamu utashangaa roho yako haitaki kuzini lakini akili na utashi na mwili vimepatana kuzini utashangaa unazini tu.
Unapookoka lazima uanze kuliweka neno jema akilini au ndani yako. Hilo neno likikaa akili mwako, taratibu litaanza kupishana na mambo ya mwili.
Watu wengi hukimbilia kuombewa tu, kumbe maombi hayo hayamsaidii huyo mtu kuwa na nguvu ya kuushinda mwili kila siku. Sikia mwili wenyewe umechagua dhambi tuuu.
Ili usiupe nguvu lazima uhakikishe unabomoa ushirika kati ya mwili na nafsi yaani mfumo wa akili. Akili zikijazwa neno jema ninakuhakikishia maamuzi yako yataegemea kwenye kile akili imebeba.
Watu wengi hufanya maombi ya kujazwa nguvu rohoni hilo ni zuri sana, tatizo lao wanasahau au hawajui kuwa kama akili zao hazijahuishwa kwa neno ni ngumu kwao kuushinda mwili.
Nakuambia ukweli akili ina nafasi kubwa mno katika eneo la wewe kuishinda dhambi. Angalia mistari hii. “Tumieni akili kama ipasavyo, wala msitende dhambi;....” (1 Wakorintho 15:34)
Ili usitende dhambi fahamu akili zako zinahusika mno. Anza kuilisha akili yako chakula chake cha Akili.
Mungu akubariki sana
Ukihitaji masomo yetu unaweza kuyapata kwa njia hizi zifuatazo:-
- Website yetu ya www.mwakatwila.org
2. YouTube - Mwakatwila au HUDUMA YA SOMA NENO LA MUNGU (HUSONEMU).
3. Facebook ingia katika hiyo tovuti au website yetu utaona alama ya facebook(f) like na utapata maelezo ya kujiunga au andika “SOMA NENO LA MUNGU”
4. Instagram ingia kwa link pale juu au ingia Instagram na andika Steven Mwakatwila
5. DVDs📀 au CDs 💿
6. VITABU
7. Kwa njia ya REDIO:-
➖Rungwe FM 102.5 Kila siku ya Jumapili saa tatu mpaka saa nne usiku.
➖Baraka FM 107.7 Kila siku ya Jumanne saa kumi na mbili jioni mpaka saa moja usiku.
➖Bomba FM 104.1 Kila siku ya Ijumaa saa tatu usiku mpaka saa nne usiku.
8. Unaweza kutupata kwenye ONLINE RADIO yetu:- radio.mwakatwila.org
Kwa mawasiliano zaidi Utatupata kwa namba hizi:- +255754849924 - +255756715222
Wako
Mwl Steven & Beth Mwakatwila.
10/01/2019
No comments:
Post a Comment