Wednesday, January 9, 2019

3⃣ NAMNA YA KUFANYA ILI UPATE KUISHINDA DHAMBI YA UZINZI

Na: MWL STEVEN & BETH MWAKATWILA

FUATANA NASI FACEBOOK

FUATANA NASI ONLINE RADIO
👉🏼 radio.mwakatwila.org

14 Dec, 2018

Bwana Yesu Kristo apewe sifa sana. Naamini unaendelea vizuri, hii ni sehemu ya tatu ya somo nililokuahidi kuwa nitakufundisha ili uanze kuishinda dhambi au tabia ya uzinzi.

Kama ulivyonieleza wazi kuwa hiyo tabia haupendi naamini umeanza kuyafanyia kazi yale niliyotangulia kukueleza. Baada ya kukuonyesha eneo lile la angalia waliokutangulia huenda ukawa na tabia ya kurithi ambayo imeubana mwili wako.

Hebu tuendelee mbele kidogo hapo hapo kwenye mwili. Ninavyosema mwili unaweza rithi tabia fulani mbaya sikosei. Maandiko yanasema hivi. “Nanyi mfahamu kwamba mlikombolewa si kwa vitu viharibikavyo, kwa fedha au dhahabu; mpate kutoka katika mwenendo wenu usiofaa mlioupokea kwa baba zenu;” (1Petro 1:18).

Kuna kitu hapo ambacho nataka nikutazamishe hapo ni hiki “mpate kutoka katika mwenendo wenu usiofaa mlioupokea kwa baba zenu;” Kuna neno mpate kutoka, Maana yake unaweza kuokoka kabisa lakini ukawa umebanwa na mwenendo mbaya ulioupokea kutoka kwa wazazi hapo imesemwa mababa.

Nguvu ya uzinzi katika mwili inaweza ikawa na chanzo chake miongoni mwa chanzo ni ni namna ulivyopokea kutoka kwa wazazi tabia fulani.

Mfano usishangae sana ukaona katika tabia zako fulani fulani tabia hizo hata wazazi wako wanazo, unaweza kukuta wazazi walikuwa waongo weee au hasira weee yaani wakali kweli kweli, na wewe ukajikuta una tabia hizo hizo tena umewazidi hata hao wazazi wako.

Hata kwenye tabia ya uzinzi inaweza kuwa hivyo hivyo. Ngoja nikupe mfano kuna familia utaona ni wazinzi mnoo!! Unajua asilimia kubwa utaona ni mwenendo au tabia waliyoipata kutoka kwa wazazi, niliwahi msikia binti mmoja ambaye alikuwa mzinzi kweli, yeye kutembea uchi hana shida.

Alisema huku akilia machozi kuwa aliipata hiyo tabia kutoka kwa mama yake. Alisimulia kuwa alipozaliwa alizaliwa kwa mama ambaye alikuwa kahaba. Kwa hiyo tokea anakua alikuwa anawapisha hao wanaume wakilala na mama yake kitandani yeye analala kwenye kochi.
Alikuwa anaona mpaka anakua anamwona mama yake yuko hivyo, anadai alikuwa anachukia sana, lakini ghafla akashangaa hata yeye akaanza kuwa na mwenendo ule ule aliokuwa nao mama yake.

Akajikuta akiwa mdogo tu anazini na watu wakubwa tu. Tabia hii inapomkalia mtu maandiko yanasema anaweza kutoka kwenye huo mwenendo.

Sikiliza, unaweza okoka kabisaa lakini usiwe umetoka kwenye tabia au mwenendo fulani. Ili utoke unahitaji mafundisho. Maandiko yanasema hivi. “Maana neema ya Mungu iwaokoayo wanadamu wote imefunuliwa; nayo yatufundisha kukataa ubaya na tamaa za kidunia; tupate kuishi kwa kiasi, na haki, na utauwa, katika ulimwengu huu wa sasa;” (Tito 2:11-12).

Angalia hiyo mistari utaona ndani ya neema ya Mungu ambayo ndani yake imebeba wokovu pia kumebebwa mafundisho maalumu yanayotufundisha namna ya kuukataa ubaya.

Sikiliza ukiokoka na bahati mbaya ukayakosa hayo mafundisho utajikuta huna uwezo wa kuukataa ubaya na tamaa za mwili.

Ili uikatae hiyo tabia au mwenendo ulioupokea mimi naita “kurithi” Biblia inasema kinachoweza kukomboa ni damu. Angalia anasema mlikombolewa kwa damu ili mpate kutoka katika mwenendo usiofaa mlioupokea kutoka kwa baba zenu.

Watu wengi tumeokoka ila hatujui kazi za damu ya Yesu Kristo. Moja ya kazi ya damu ni kumtoa mtu katika tabia au mwenendo usiofaa. Unajua Biblia inapoizungumzia damu inaizungumzia kiajabu sana.

Angalia mfano huu. “BWANA akamwambia Kaini, Yuko wapi Habili ndugu yako? Akasema, Sijui, mimi ni mlinzi wa ndugu yangu? Akasema, Umefanya nini? Sauti ya damu ya ndugu yako inanililia kutoka katika ardhi.” (Mwanzo 4:9-10).

Angalia na mistari hii. “Bali nyama pamoja na uhai, yaani, damu yake, msile.Hakika damu yenu ya uhai wenu nitaitaka; na kwa mkono wa kila mnyama nitaitaka; na kwa mkono wa mwanadamu, kwa mkono wa ndugu ya mtu nitataka uhai wa mwanadamu. Atakayemwaga damu ya mwanadamu, damu yake huyo itamwagwa na mwanadamu, maana kwa mfano wake Mungu alimfanya mwanadamu.” (Mwanzo 9:4-6).

Angalia na mistari hii pia. “Kisha mtu awaye yote wa nyumba ya Israeli, au miongoni mwa hao wageni wakaao kati yao, atakayekula damu, ya aina yo yote, nitakunja uso wangu juu ya mtu huyo alaye damu, nami nitamkatilia mbali na watu wake. Kwa kuwa uhai wa mwili u katika hiyo damu; nami nimewapa ninyi hiyo damu juu ya madhabahu, ili kufanya upatanisho kwa ajili ya nafsi zenu; kwani ni hiyo damu ifanyayo upatanisho kwa sababu ya nafsi. Kwa hiyo naliwaambia wana wa Israeli, Hapana mtu miongoni mwenu aliye na ruhusa kula damu, wala mgeni aketiye kati yenu asile damu. Mtu ye yote aliye wa wana wa Israeli, au wa hao wageni wakaao kati yenu, ambaye amemshika mnyama, au ndege ambaye huliwa, katika kuwinda kwake; atamwaga damu yake, na kuifunika mchanga. Kwa maana kuliko huo uhai wa mnyama, hiyo damu yake ni moja na uhai wake; kwa hiyo naliwaambia wana wa Israeli, Msile damu ya mnyama wa aina yo yote; kwa kuwa uhai wa wanyama wote ni katika hiyo damu yake; atakayeila awaye yote atakatiliwa mbali.” (Mambo ya Walawi 17:10-14)

Hebu isome some hiyo mistari kwa kutulia utakiona hiki ninachotaka nikutazamishe. Sikiliza, na damu yako na uhai wako ni kitu kimoja angalia anasema hivi. “Kwa maana kuliko huo uhai wa mnyama, hiyo damu yake ni moja na uhai wake; kwa hiyo naliwaambia wana wa Israeli, Msile damu ya mnyama wa aina yo yote; kwa kuwa uhai wa wanyama wote ni katika hiyo damu yake; atakayeila awaye yote atakatiliwa mbali”

Sasa sikia, unaposikia neno huyu ni damu moja nami maana yake kuna ufanano katika hizo damu, kwa lugha nzuri tabia mbaya inabebwa kwenye damu. Ndiyo maana hata agano la kale damu ya mnyama iliyotakiwa itumike kwa kazi maalumu utaona asilimia kuwa ilitafutwa damu ya mnyama aliye safi.

Safi kivipi? mfano asiyepandwa au kupanda kama ni dume nk. Umewahi jiuliza kwa nini damu ya Yesu Kristo ina nguvu? Haikubeba kitu chochote cha mababa. Mababa ndiyo wanaotengeneza nasaba au tabia za kizazi. Sasa kama ni wazinzi fahamu uhai wao uliomo mwilini yaani damu inabeba hiyo tabia, na damu hiyo hiyo ndiyo itaisukuma hiyo tabia mpaka kwa watoto nk.

Unaweza kujiuliza mbona damu ni kama kimiminika tu? Sikiiza damu ni zaidi ya kimiminika nakuambia. Mwili wako unaendeshwa na uhai ambao ni damu. Damu inasema, kama inasema fahamu ina tabia. Na tabia ya damu ndiyo tabia iitwayo matendo ya mwili.
Ngoja nikupe mfano. Hakuna mtu anayemfundisha mtu kufanya tendo la ndoa. NI DAMU INAPOSHUKA KWA KIWANGO FULANI KATIKA SEHEMU ZA SIRI NA INAZIINUA HIZO SEHEMU NA KUFANYA HICHO KINACHOFANYWA.

Damu isiposhuka huko kwa wingi viuongo hivyo vinatulia tuliii!!! Damu inabeba tabia za mwili kwa sababu uhai wa huo mwili ni hiyo damu. Mungu alichagua damu ili izisafishe hizo tabia. Katika agano la kale alichagua damu za wanyama na ndege. Biblia inasema bado damu hizo hazikukidhi kile Mungu alitaka.

Akaamua kutupatia damu ya mwanawe wa pekee yaani Bwana Yesu Kristo. Damu hiyo ndiyo inaweza kuzishughulikia tabia mbaya zilizobebwa katika damu ya wanadamu.
Ngoja nikupe mfano huu. Ukianza kuitumia damu ya Yesu Kristo kwenye eneo la kuutakasa mwili wako ambao una damu hiyo damu ya Yesu itaanza kuzifisha hizo tabia mbaya za mwili wako zilizobebwa kwenye mwili wako ambao una damu.
Ningekuwa daktari ningesema tumia damu ya Yesu Kristo ili kuviua virusi vya uzinzi vilivyobebwa kwenye damu yako!!!

Kitakachokutoa hapo katika mwenendo huo ni hiyo damu ya Yesu. Unaweza kuitumia kujitasa yaani uliisha ifanya hiyo dhambi, pia unaweza kuitumia hiyo damu kukutoa kwenye mwenendo au tabia ya uzinzi.

Fanya maombi ya mfumo huu. Unaweza kufunga angalau hata kwa wiki mara moja, ukaanza kuomba Mungu kwa kutumia damu ya Bwana Yesu Kristo akutoe kwenye mwenendo wa uzinzi ulionao.

“Piga kelele, usiache, Paza sauti yako kama tarumbeta; Uwahubiri watu wangu kosa lao, Na nyumba ya Yakobo dhambi zao. Walakini wanitafuta kila siku; hupenda kujua njia zangu; kama vile taifa waliotenda haki, wasioacha sheria ya Mungu wao, hutaka kwangu amri za haki; hufurahi kumkaribia Mungu. Husema, Mbona tumefunga, lakini huoni? Mbona tumejitaabisha nafsi zetu, lakini huangalii? Fahamuni, siku ya kufunga kwenu mnatafuta anasa zenu wenyewe, na kuwalemea wote watendao kazi kwenu. Tazama, ninyi mwafunga mpate kushindana na kugombana, na kupiga kwa ngumi ya uovu. Hamfungi siku hii ya leo hata kuisikizisha sauti yenu juu. Je! Kufunga namna hii ni saumu niliyoichagua mimi? Je! Ni siku ya mtu kujitaabisha nafsi yake? Ni kuinama kichwa kama unyasi, na kutanda nguo za magunia na majivu chini yake? Je! Utasema ni siku ya kufunga, na ya kukubaliwa na BWANA? Je! Saumu niliyoichagua, siyo ya namna hii? Kufungua vifungo vya uovu, kuzilegeza kamba za nira, kuwaacha huru walioonewa, na kwamba mvunje kila nira?” (Isaya 58:1-6)

Fungua hiyo kamba ya uovu au tabia ya uzinzi kwa kutumia damu ya Yesu Kristo. Sasa hapo itategemea ugumu wa kamba iliyokufunga, anza taratibu wala usikimbie, omba leo, omba wiki inayofuata, taratibuu itaanza kupotea siku moja usishangae umetolewa kwenye mwenendo huo.

Mungu akubariki sana.

Ukihitaji masomo yetu unaweza kuyapata kwa njia hizi zifuatazo:-

1.Website yetu ya www.mwakatwila.org

2.YouTube - Mwakatwila au HUDUMA YA SOMA NENO LA MUNGU (HUSONEMU).

3.Facebook ingia katika hiyo tovuti au website yetu utaona alama ya facebook(f) like na utapata maelezo ya kujiunga au andika “SOMA NENO LA MUNGU”

4.DVDs📀 au CDs💿

5.VITABU

6.Kwa njia ya Redio:-
➖Rungwe FM 102.5 Kila siku ya Jumapili  saa tatu mpaka saa nne usiku.
➖Baraka FM 107.7 Kila siku ya Jumanne saa kumi na mbili jioni mpaka saa moja usiku.
➖Bomba FM 104.1 Kila siku ya Ijumaa saa tatu usiku mpaka saa nne usiku.

7.Unaweza kutupata kwenye radio yetu online ya. radio.mwakatwila.org

Kwa mawasiliano zaidi Utatupata kwa namba hizi. +255754849924 - +255756715222

Wako
Mwl Steven & Beth Mwakatwila.
14/12/2018

No comments:

Post a Comment