Monday, January 7, 2019

8⃣ MAMBO MUHIMU UNAYOTAKIWA UYAFANYE ILI UPATE KUISHINDA DHAMBI YA UZINZI

Na: MWL STEVEN & BETH MWAKATWILA

FUATANA NASI WHATSAPP

FUATANA NASI FACEBOOK

FUATANA NASI YOUTUBE

FUATANA NASI INSTAGRAM

FUATANA NASI ONLINE RADIO
👉🏼 radio.mwakatwila.org

🗓 6 Januari, 2019

Bwana Yesu Kristo asifiwe sana. Leo nimepata muda huu nimeona nikuletee tena mwendelezo wa NAMNA UNAVYOTAKIWA UFANYE ILI UPATE KUISHINDA DHAMBI YA UZINZI.
Nilikuahidi kukuonyesha namna unavyotakiwa ushughulikie akili zako au ufahamu wako ili uanze kuushinda mwili wako katika eneo la kuushinda uzinzi.

Ili ushughulikie eneo la akili lazima kwanza ujue jambo hili. Kumbuka kujua ni sehemu ya kazi ya akili. Nilikuambia ndani ya akili kumebebwa kujua, kufahamu, kuelewa, kukumbuka, kuwaza, kutafakari, kufikiri, dhamiri au kukusudia, nia, nk.

Mimi sina nia ya kukufundisha hapa somo la AKILI. Kwani ni somo pana mno, hapo sasa itatakiwa nikufundishe utofauti wa kujua, kuelewa, kufikiri, kuwaza nk. Hapo nitatoka kabisa kwenye jambo ninalotaka kukuonyesha.

Ili ushughulikie akili zako lazima kwanza tujue namna tulivyoumbwa.

WEKA BIDII KUTAFUTA AKILI AU UFAHAMU WA NAMNA ULIVYOUMBWA.

Mungu alikuumba kwenye maeneo maalumu matatu. Angalia uliumbwa kwa mfano wa Mungu, “Mungu akasema, Na tumfanye mtu kwa mfano wetu, kwa sura yetu; wakatawale samaki wa baharini, na ndege wa angani, na wanyama, na nchi yote pia, na kila chenye kutambaa kitambaacho juu ya nchi. Mungu akaumba mtu kwa mfano wake, kwa mfano wa Mungu alimwumba, mwanamume na mwanamke aliwaumba.” (Mwanzo 1:26-27).

Lazima ujue na ufahamu Mungu yukoje. Angalia mistari hii “Nawe, Sulemani mwanangu, mjue Mungu wa baba yako......” (1 Nyakati 28:9)

Ninachotaka ukitazame hapo ni neno hili la mwanangu mjue Mungu wa baba yako. Kumbuka kujua ni kazi mojawapo ya akili, Lazima uweke bidii kumjua na kumfahamu Mungu yaani kiwango chako cha ufahamu wako kwa ajili ya Mungu kiwe kikubwa.
Mungu huyu aliyetuumba maandiko yanatupa taarifa kuwa ni Roho.  “Mungu ni Roho, nao wamwabuduo yeye imewapasa kumwabudu katika roho na kweli.” (Yohana 4:24)

Angalia hapo, kuna utofauti wa neno roho. kuna roho imeandikwa kwa herufi kubwa na nyingine ina herufi ndogo. Hiyo ya herufi kubwa inamzungumzia Mungu, hiyo ya herufi ndogo inatuzungumzia sisi.

Wewe umeumbwa kwa mfano wa Mungu ambaye ni Roho. Kwa hiyo hata wewe ni roho.
Ukapewa kitu cha pili kinaitwa mwili. “BWANA Mungu akamfanya mtu kwa mavumbi ya ardhi, akampulizia puani pumzi ya uhai; mtu akawa nafsi hai.” (Mwanzo 2:7).

Ukapewa kitu cha tatu kinaitwa nafsi au moyo au pumzi hai ya Mungu. “BWANA Mungu akamfanya mtu kwa mavumbi ya ardhi, akampulizia puani pumzi ya uhai; mtu akawa nafsi hai.” (Mwanzo 2:7).

Mungu alikupa wewe nafsi, kazi kubwa ya nafsi ni kufanya kazi ya kuiunganisha roho ya mtu ikaayo katika ulimwengu wa roho na mwili unaoishi katika ulimwengu huu unaoonekana.

Fahamu ili roho iishi huku duniani ni lazima ipewe mwili. Mungu aliumba mwili wako ili uiwezeshe roho yako kuishi humu duniani.

Mwili na roho ili viweze kuwa na mawasiliano mazuri vikapewa nafsi au kiunganishi maalumu kutoka kwa Mungu. Fahamu mwili wako na roho yako ni vitu viwili tofauti.
Kwa lugha nzuri niseme nafsi ilipewa jukumu la kutafsiri vitu vya rohoni na kuvipeleka mwilini na vitu vya mwili kuvipeleka rohoni.

Huko ndani ya nafsi pia kuliwekwa utashi yaani nguvu inayomwezesha mtu kufanya maamuzi sahihi katika wakati sahihi.

Unaposoma maandiko pia unapata ufahamu kuwa akili zimewekwa kwenye nafsi au moyo. Angalia hii mistari. “Lakini imo roho ndani ya mwanadamu, Na pumzi za Mwenyezi huwapa akili.” (Ayubu 32:8).

Ukiipitia hiyo mistari utaona vitu hivyo vitatu yaani roho, mwili hapa kasema mwanadamu na nafsi au pumzi hai ya Mungu. Mpaka hapa unanielewa lakini? Kama hunielewi hebu fanya maombi haya.

Omba Roho Mtakatifu akufunulie akili ili uelewe “Ndipo akawafunulia akili zao wapate kuelewa na maandiko.” (Luka 24:45).

Kumbuka kuelewa kuko ndani ya akili kama huelewi maandiko fahamu kuna tatizo kwenye akili omba utendewe kama hawa ndugu Bwana Yesu Kristo alivyowatendea.
Fahamu pumzi hiyo ya Mungu au nafsi ndiko Mungu alikoziweka akili. Sasa angalia kilichotokea. Dhambi ilipoingia moyoni mwa mtu ilitengeneza uharibifu wa akili za huyo mtu.

Akajikuta anaanza kufahamu mambo mabaya ambayo yaliingizwa humo ndani na shetani. Mungu alipokuwa anamuumba mtu na kumpa nafsi na mwili hakumpa mtu akili zenye utambuzi au ufahamu au uelewa wa mambo mabaya.

Mtu alipofanya dhambi akajikuta ndani ya moyo wake ameingiza kitu cha pili kinachoitwa mabaya, akawa anajua mema na mabaya.

Fahamu Mungu alipokuwa anampa mtu akili alimpa akili nzuri kabisa ambayo aliibebesha vitu vizuri mno ili vimsaidie mtu katika kuishi kwake kwenye ulimwengu wa roho na huu ulimwengu wa mwili.

Ndani ya akili kuliwekwa ubunifu au uumbaji nk. Mungu alipomuumba mtu alimwekea huko ndani mfumo mzima wa kubuni, kuunda na kutengeneza vitu mbalimbali na mambo mengi mno.

Dhambi ilipoingia moyoni mwa mtu akajikuta ghafla amebeba vitu viwili kwa wakati mmoja. Alijikuta huko ndani yake amebeba akili au ufahamu na kujua mambo mabaya.
Msikilize Mungu asemavyo “BWANA akaona ya kuwa maovu ya mwanadamu ni makubwa duniani na kwamba kila kusudi analowaza moyoni mwake ni baya tu sikuzote.BWANA akaghairi kwa kuwa amemfanya mwanadamu duniani, akahuzunika moyo.” (Mwanzo 6:5-6).

Kusudi la mtu limebebwa kwenye akili, moyoni ndiko kuna mawazo ambayo ndiyo yabebayo makusudio ya mtu.

Sasa dhambi ilipoingia iliharibu mfumo mzima wa akili za mtu. Mwili wake ambao ulichagua mabaya ukawa na nguvu mno kuliko roho ya mtu ambayo inataka kutenda mema.

Ngoja nikuambie ukweli nje ya Bwana Yesu Kristo mwili wa mwanadamu utaitawala roho yako tu. Unajua ni kwa nini?

Fahamu akili za mtu zilitekwa kabisaa zikawa zinashughulikia mno upande wa mwili tu. Ukinielewa hapo utajua ni kwa nini mtume Paulo anasema kuwa tunatakiwa tuziteke nyara fikra yaani akili.

Kama unafikiri nakutania wewe angalia watu walivyo na uwepesi wa kuelewa au kufahamu au kujua au kutenda mambo mabaya.

Watu wengi si wepesi kuelewa mambo ya Mungu yaliyo mema, unajua ni kwa nini? Ni mfumo kwasababu ya mfumo wa akili zao ulivyobebeshwa mambo ya mwili na namna mwili ulivyo na nguvu mno dhidi ya roho ya mtu.

Nilikuwa najiuliza kila mara kwa nini watu wengi mno unapowaambia habari za mambo mema au mambo ya Mungu huwachukua muda mrefu mno kukuelewa?  
Mungu akanifundisha kuwa tatizo lipo kwenye akili zao.

Wewe jaribu leo kuwaeleza watu habari zingine tu tena mbaya mbaya hivi utaona, uelewa wao huwa mkubwa haraka sana.

Ukitaka kujua hiki ninachokuambia wewe fuatilia mtu atoaye kozi ya kawaida tu ya watu kupata fedha kihalali na zile kozi za watu kupata fedha kwa njia ambazo ndani yake watu hao wataingia kuibiwa au kutapeliwa nk.

Utagundua watu wanaovutwa mno kwenye habari hizo mbaya huwa ni wengi mnoo.Wewe angalia watu wengi hupenda kuusikiliza mno uovu kuliko wema.

Kisa milango ya ufahamu au akili ipo mwilini, mwili hauwezi kukubali kirahisi rahisi wewe upokee vema habari njema ambazo zitazifanya akili kupata ufahamu mwema.
Si unajua milango ya ufahamu au akili iko mwilini? Kuna macho, masikio, midomo, pua na kuguswa (mwili).

Mwili uliopewa hiyo milako ya ufahamu au akili usifikirie utaruhusu kirahisi rahisi milango hiyo ya ufahamu uachilie taarifa njema ndani ya nafsi.

Kutatokea upinzani mnoo. Ngoja nikupe mfano umewahi fikiria kwa nini watu wengi wanapenda mno kusikiliza mambo yasiyowasaidia kabisaa?

Ona muda unaouchukua kuangalia picha za watu ambao hawana msaada kabisa na wewe huko Instagram. Fikiria yaani nasema wewe mwenyewe fikiria hili. Nikuulize je! Ukiulinganisha muda wako wa kusoma Biblia au kusoma habari za kufuga kuku au kulima mbogamboga muda huo unafanana?

Au angalia mlango wako wa ufahamu uitwao macho jinsi unavyokusukuma uangalie, utashangaa husukumwi kwa wepesi kuangalia vema ila vile vibaya vyenye madhara kwa roho yako ndiyo unavutwa kuviangalia au kuvisoma.

Umewahi fikiria muda unaoupoteza Facebook? Nikikuuliza unapata faida gani. Wewe mwenyewe utaona hakuna cha maana kwa kweli, lakini kila unapofikiria kuupunguza huo muda unashangaa ndiyo unavutwa mnoo huko.

Siyo dhambi kuingia Facebook au Instagram nk, ninachotaka nikutazamishe hapo ni namna ya mfumo wa nafsi ulivyoharibiwa baada ya dhambi kuingia moyoni mwa mtu.
Unapookoka Biblia inakutaka wewe uanze kushughulikia mfumo mzima wa akili zako. Maandiko yanatuagiza yanasema hivi.

“Basi, wekeni mbali uovu wote na hila yote, na unafiki na husuda na masingizio yote.Kama watoto wachanga waliozaliwa sasa yatamanini maziwa ya akili yasiyoghoshiwa, ili kwa hayo mpate kuukulia wokovu; ikiwa mmeonja ya kwamba Bwana ni mwenye fadhili.” (1Petro 2:1-3).

Unapookoka mpendwa Biblia inasema hapo unatakiwa uhakikishe unaanza kuishughulikia akili kwa kuipatia maziwa yaani kwa lugha nzuri akili yako inatakiwa ipate chakula ili iwe hai na afya.

Hayo maziwa Biblia inasema maziwa ya akili..Anaposema habari za kuukulia wokovu ameuweka ukuaji huo kwenye eneo la akili pia. Kwa nini watu wameokoka lakini ni wazinzi waongo, wanafiki, wenye hila au husuda, hila nk?

Angalia hapo kwa kutulia utaona tatizo lipo kwenye eneo la ukuaji kwenye akili. Sikia. Dhambi ilipoingia akili za mtu ziliharibiwa kabisaa ndiyo zikawa na uelewa wa mambo hayo mabaya ya uongo, hila, unafiki, nk.

Ukimuona mtu ana wivu mwongo mwenye masingizio mzizi nk Usimkasirikie huyo mtu wewe fahamu kuwa AKILI ZA HUYO MTU ZINA MATATIZO. Usiweke bidii kumlaumu wewe ingia kushughulikia akili zake.

Unamkuta mtu anazusha mambo mnamwuliza anaanza kulia kuwa kwa kweli yeye hajasema!! Kila kitu kiko wazi unashangaa anasema jamani wananisingizia. Ukitulia utagundua huyo mtu ana matatizo kwenye ufahamu wake. Haelewi tu kuwa watu wamefahamu na kujua kuwa yeye ndiye kasema hayo. Ufahamu wake unamjukisha kuwa HAWAJUI KUWA NI YEYE KASEMA UONGO HUO.

Baadaye akipata ufahamu kuwa aisee nimezusha mambo na wamenitambua kuwa ni mimi ndipo taratibu anaanza kukubaliana na kosa lake kuwa naomba mnisamehe ni shetani tu.

Ni sawa na mtu anayesema uongo kuwa ananyumba yake nzuri mno huku akiwa aishi kwenye nyumba ya shemeji yake,siku dada yake akifarakana na mume wake tu, basi ndiyo hata hapo alipohifadhiwa ndiyo hatapaona tena.

Mtu wa namna hiyo fahamu tatizo lipo kwenye akili tu. Tena asiposaidiwa ili akili zake zipewe maziwa yake na kukua kidogo huko moyoni mwake nakuambia usishangae akaamini hiyo nyumba ni yake. Siku mwenye nyumba akihitaji hiyo nyumba ugomvi atakaouanzisha usishangae utapita kizazi mpaka kizazi.

Unapokoka lazima uanze kushughulikia akili zako ili hata dhambi usifanye. Biblia inasema mtu ambaye hana akili au akili zikiwa na matatizo hawezi hata kupambanua mambo mema na mabaya. Yaani hajui hiii ni dhambi au siyo dhambi.

“Kwa maana, iwapasapo kuwa waalimu, (maana wakati mwingi umepita), mnahitaji kufundishwa na mtu mafundisho ya kwanza ya maneno ya Mungu; nanyi mmekuwa mnahitaji maziwa wala si chakula kigumu. Kwa maana kila mtu atumiaye maziwa hajui sana neno la haki, kwa kuwa ni mtoto mchanga.Lakini chakula kigumu ni cha watu wazima, ambao akili zao, kwa kutumiwa, zimezoezwa kupambanua mema na mabaya.” (Waebrania 5:12-14).

Ukiipitia hiyo mistari utagundua mtu ambaye ni mtoto kwenye akili zake hawezi kupambanua mema na mabaya.

Dhambi ilipoingia tu ilitengeneza mfumo kitoto kwenye akili za watu. Tunachotofautiana na watoto wachanga ni kiwango cha ufahamu na umbo. Kwa nini mtoto anajiendea haja ndogo na kubwa  ovyo ovyo?

Unafikiri ni kwa sababu ya uchanga wake? Kuna zaidi ya hapo. Tatizo lipo kwenye akili zake ni za kitoto, zinahitaji kukuzwa, akikua atafahamu kuwa aisee kuna choo nk.
Tendo ni lile lile la kwenda haja ndogo na kubwa lakini hili la mtu mzima linatendwa vema. Mtu mzima akiwa mtoto kwenye akili fahamu atalitenda tendo hilo kama mtoto kabisaa ingawa mwili ni wa mtu mzima.

Ili kumpa akili mtu huyo mara nyingi hushikwa na kupigwa faini na mabwana afya. Kesho harudii tena, akirudia tunaanza kuwaza kuwa huenda huyu ndugu kapungukiwa na akili. Yaani ufahamu, hajitambui hajui madhara ya hicho afanyacho nk.

Mtoto hawezi kupanua mema wala mabaya. Tatizo lake liko ndani ya akili zake zikikua tu anaanza kufahamu baya ni lipi na lipi alifanye.

Namaisha ya wokovu ni vivyo hivyo. Mungu anapokuokoa roho yako fahamu anataka nafsi au moyo wako uanze kushughulikiwa. Biblia inaita kuuhuisha.

Angalia mistari hii. “Nafsi yangu imeambatana na mavumbi, Unihuishe sawasawa na neno lako.” (Zaburi 119:25).

Angalia mistari hiyo. Mfalme Daudi alijua moyo wake au nafsi ambao humo ndani kuna akili, ufahamu, kuelewa, kujua kufahamu utashi na hisia umeambatana na mwili yaani mavumbi.

Sasa akili au nafsi ya mtu aliyeokoka zikiambatana na mavumbi unafikiri roho ya mtu iliyookolewa itaukataa uzinzi? Hili ndilo tatizo la watu wengi, wameokoka ila hawana bidii ya kuzikuza au kuzihuisha  AKILI ZAO AMBAZO ZILIHARIBIKA.

Mfalme Daudi alijua tatizo lake ni mfumo wa nafsi yake ulivyobanwa na mwili. Akaomba msaada wa kuhuishwa nafsi yake. Unapookoka na akili zako au ufahamu wako ukiwa ndani yake hauna Mungu ni rahisi tu kuzini.

Naamini umenielewa nilitaka uanze kupata ufahamu na kuelewa kuwa akili zako zinahitaji kushughulikiwa mno ili uanze kuishinda dhambi ya uzinzi

Mungu akubariki sana.

Ukihitaji masomo yetu unaweza kuyapata kwa njia hizi zifuatazo:-

  1. Website yetu ya www.mwakatwila.org

2. YouTube - Mwakatwila au HUDUMA YA SOMA NENO LA MUNGU (HUSONEMU).

3.Facebook ingia katika hiyo tovuti au website yetu utaona alama ya facebook(f) like na utapata maelezo ya kujiunga au andika “SOMA NENO LA MUNGU”

4. Instagram ingia kwa link pale juu au ingia Instagram na andika Steven Mwakatwila

5. DVDs📀 au CDs💿

6. VITABU

7. Kwa njia ya REDIO:-
➖Rungwe FM 102.5 Kila siku ya Jumapili  saa tatu mpaka saa nne usiku.
➖Baraka FM 107.7 Kila siku ya Jumanne saa kumi na mbili jioni mpaka saa moja usiku.
➖Bomba FM 104.1 Kila siku ya Ijumaa saa tatu usiku mpaka saa nne usiku.

8. Unaweza kutupata kwenye ONLINE RADIO yetu:-  radio.mwakatwila.org

Kwa mawasiliano zaidi Utatupata kwa namba hizi:- +255754849924 - +255756715222

Wako
Mwl Steven & Beth Mwakatwila.
06/01/2019

No comments:

Post a Comment