Thursday, January 17, 2019

🔟 MAMBO MUHIMU UNAYOTAKIWA UYAFANYE ILI UPATE KUISHINDA DHAMBI YA UZINZI

Na: MWL STEVEN & BETH MWAKATWILA

FUATANA NASI:- APP, FACEBOOK, INSTAGRAM, ONLINE RADIO 📻, WHATSAPP, WEBSITE & YOUTUBE, Kwa links zilizoko kwenye link hapa:

KUPATA APP YETU “HUSONEMU (MWAKATWILA) APP” BONYEZA LINK HAPA:

🗓 18 Januari, 2019

Bwana Yesu Kristo asifiwe sana naamini unaendelea vizuri huko uliko.  Nikupe pole na kila changamoto unayoipitia. Nimeupata huu muda nimeona niutumie kukuletea tena somo hili la Namna ya kufanya ili upate kuishinda dhambi ya uzinzi. Kama nilivyokuahidi kuwa nitajaribu kukuandikia mambo muhimu unayotakiwa uyafanye ili uanze kuidhibiti dhambi hii.

Nisamehe pale ninapokucheleweshea kukupa mfululizo wa somo kama nilivyokuahidi. Kama unakumbuka tulikotokea tunaangalia nguvu au mlango wa dhambi hii ya uzinzi inayotokana na chanzo cha mwili.

Bado sijaanza kukuonyesha chanzo cha pili ambacho ni roho au mapepo.

Niliishia eneo lile la kushughulikia akili. Nilikuambia kuwa kuna mambo kama matatu hivi unayotakiwa uyashughulikie ili akili zako zikae sawa na zisianze kukubaliana na mwili pindi mwili unavyowasha tamaa zake.

Kulikuwa na mambo haya:-
1. Jambo la kwanza ni maombi maalumu yanayohusu akili zako tu.
2. Jifunze kuilisha akili chakula chake
3. Jifunze kushughulikia milango mitano ya ufahamu

Hebu tuanze kuliangalia moja baada ya lingine.

1⃣. JIFUNZE KUILISHA AKILI CHAKULA CHAKE

Nilikuonyesha hilo jambo la jifunze kuilisha akili yako chakula chake na nilikuambia chakula cha akili ni neno au elimu maalumu apewayo mtu.

Nilikuonyesha mistari hii nataka pia tuanze nayo leo. “Basi, wekeni mbali uovu wote na hila yote, na unafiki na husuda na masingizio yote. Kama watoto wachanga waliozaliwa sasa yatamanini maziwa ya akili yasiyoghoshiwa, ili kwa hayo mpate kuukulia wokovu;’  (1 Petro 2:1-2).

Sikiliza mtoto anapozaliwa anakuwa na kitu mimi naita mbengu ya akili. Kumbuka ndani ya neno akili kumebebwa vitu vingi mno, kuna kutambua, kuelewa, kujua, kufahamu, kunia, kukusudia au kudhamiria, kukumbuka na hata kusahau nk.

Sasa mtoto anapokua anaangaliwa kwenye maeneo makuu mawili; Eneo la kwanza ni mwili, mwili unakua ulikuwa mdogo sana tunaita mchanga leo hii unaitwa msichana au binti au kijana au mzee nk.

Si mtoto tena, hapo kwenye kukua mwili kuna mambo mengi sana ambayo yanafanyika mpaka huo mwili ukue chakula kinahusika mno. Si unafahamu habari za mtu kudumaa? Fahamu hakuumbwa adumae alikosa tu chakula bora.

Eneo la pili analoangaliwa ni kwenye akili. Tunaanza kuangalia kiwango cha ufahamu wake wa mambo, uelewa wake, kumbukumbu zake kujua mambo kwake nk.

Sasa pia huko kwenye akili kuna chakula chake. Nacho ni neno au taarifa mbalimbali anazozipokea huyo mtoto ziwe kwa kusikia au kwa kuona.

Ngoja nikupe mfano huu kama wewe ni mtoto wa kike fahamu uliupata ufahamu huo wa kuwa wewe ni mwanamke kwa kusikia. Kama ungesikia neno linalosema wewe ni wa kiume unajua ufahamu wako ungedaka hivyo.

Akili inakula kile inachosikia na inakua kwa mtindo huo. Ili leo hii uanze kuwa na akili nzuri lazima uanze kusikia taarifa zilizo nzuri iwe umesikia kwa kuona au kwa masikio.
Sikiliza wewe huwezi kunifahamu au kunijua mpaka umeniona au umesikia habari zangu iwe kwa kusimuliwa au mimi nimekusimulia nilivyo.

Nimewahi kutana na watu wengi sana huwa wana msemo tunakusikia sana ila hatukujui. Ili leo hii uanze kuigeuza akili yako iliyobeba uzinzi na ukawa ni mtu unayetawaliwa na tamaa hiyo ya mwili lazima uanze kuliweka neno la Mungu au kusikia taarifa mbalimbali zinazozungumzia uzinzi au dhambi yoyote.

Angalia mfano huu. “Moyoni mwangu nimeliweka neno lako, Nisije nikakutenda dhambi.” (Zaburi 119:11). Kumbuka moyoni kuna akili,hisia na utashi.

Anaposema moyoni mwangu nimeliweka neno lako anataka kutuambia kuwa akilini mwake ameliweka neno la Mungu na ndiyo maana hatendi dhambi.

Ukikaa na kuutafakari sana mstari huu, utagundua kuwa nje ya neno la Mungu kwenye akili za mtu atajikuta akitenda dhambi tu. Narudia tena kukusisitiza soma Biblia sikiliza mafundisho USIISHIE HAPO TU KWENYE KUSIKILIZA JIFUNZE KULIWEKA MOYONI AU AKILINI HILO ULILOLISIKIA.

Kumbuka tunaliweka kwa KULITAFAKARI KWA MUDA MREFU WEE. Kwa mfano mimi katika kutafakari kwangu niligundua kuwa Mfalme Daudi alipolisikia neno akaingiza jambo la pili nalo ni kuliweka neno moyoni. Nikajiuliza moyoni kuna nini na hilo neno linakaakaaje moyoni?

Nikaanza kujifunza kuwa ohoo moyoni kuna mawazo unasema ulijuaje. Angalia mistari hii. “BWANA akasikia harufu ya kumridhisha; BWANA akasema moyoni, Sitailaani nchi tena baada ya hayo kwa sababu ya wanadamu, maana mawazo ya moyo wa mwanadamu ni mabaya tangu ujana wake; wala sitapiga tena baada ya hayo kila kilicho hai kama nilivyofanya.” (Mwanzo 8:21)

Umeona hapo Biblia inasema mawazo ya moyo wa mwanadamu? Angalia na mstari huu. “Nawe, Sulemani mwanangu, mjue Mungu wa baba yako, ukamtumikie kwa moyo mkamilifu, na kwa nia ya kumkubali; kwa kuwa BWANA hutafuta-tafuta mioyo yote, na kuyatambua mawazo yote ya fikira; ...” ( 1 Nyakati 28:9).

Ukiipitia hiyo mistari utaona wazi kuwa ndani ya moyo kuna mawazo, fikra nk. Kwa hiyo anaposema moyoni mwako nimeliweka neno lako anatuambia kuwa hilo neno linakwenda kukaa katika mawazo na fikra za huyo mtu.

Sasa unaposikia neno na usiliweke mawazoni kwa kulifikiria weeeee fahamu hilo neno halitakusaidia kuishinda dhambi. Umeelewa hapo? Najaribu kukusisitizia  hapo ili uanze kuwa na akili.

Kipindi fulani kuna baba mmoja alinifuata akaniambia  Mwakatwila unapokuwa unafundisha usirudie kwa urefu kutukumbusha somo la jana, tupe kitu kipya tusogee mbele.

Nikamjibu nashukuru baba. Baadaye nilipokuwa nautafakari ushauri ule niligundua  moja ya kosa kubwa tulilonalo wanadamu ni kutafuta mambo mapya wakati hayo tuliyoyasikia na kujifunza awali hatujayashika hata kuyaweka kwenye matendo bado hata hatujaona mabadiliko katika maisha yetu lakini tunakimbizana weeee kutafuta mambo mapya.

Ukifuatilia masomo yangu utagundua somo moja tunaweza kujifunza kwa miaka hata mitatu. Ni lile lile linabadilika kidogo tu lakini huko ndani ukitulia utaona wala hupati kitu kipya ila unajengwa kwenye msingi wa kukishika hicho ulichojifunza awali.

Kama unafikiri nakutania rudi nyuma pitia masomo yote ya mwaka jana. Utaona ninachokuambia. Watu wengi hiki hawapendi. Wanataka kusikia habari mpya mafundisho mapya tena magumu magumu hivi wakati yale tu ya awali hayako moyoni mwao.

Na Mungu alivyo hawezi kuwapa kitu kipya kama hiki cha kwanza hakijakubadilisha katika mfumo wa maisha yako. Ndiyo maana unasikia mtu anakuambia mtumishi mara kwa mara nashangaa naota ndoto nimerudia darasa tena la tano wakati nilishamaliza chuo kikuuu!!!

Inawezekana hiyo ikawa ni taarifa kuwa tatizo ulilonalo ni kutokuyashika yale mambo ya awali kabisaa ambayo Mungu alikufundisha hayako moyoni mwako. Umekwenda chuo kikuu yaani unatafuta mambo makubwa wakati yale ya huku mwanzoni Mungu anakuona akili zako mawazo yako hayakuyashika.

Kwa lugha nzuri unaambiwa tafuta maneno ya awali uliyojifunza yashike hayo ndiyo uhangaike na hayo yaliyo juu.

Ngoja nirudie tena, kuna faida gani Mungu akuvushe darasa la kwanza akupeleke kidato cha pili wakati hujui hata kusoma? Ndivyo tulivyo, watoto wa Mungu wengi hapa adui ametutenga hatupendi kuyashika na kujishughulisha na mambo ya kwanza tunatamani tujishughulishe sana na yajayo.

Mungu anapokupa neno na ukalielewa ni rahisi kupata ufahamu. “Farao akamwambia Yusufu, Kwa kuwa Mungu amekufahamisha hayo yote, hapana mwenye akili na hekima kama wewe.” ( Mwanzo  41:39).

Kitendo cha Yusufu KUFAHAMISHWA NA MUNGU TATIZO LA FARAO NA AKALIELEWA NA KUJUA NINI AFANYE KWA WAKATI GANI MAANDIKO YANASEMA ALIONEKANA NDIYE MTU MWENYE AKILI KULIKO WOTE.

Ohoo kumbe basi Mungu anapokufahamisha jambo lolote lile kwa kupitia ndoto, Biblia au mafundisho ya kweli ndipo anapokupatia wewe akili.

Sasa nimekuambia anza kuliweka neno  moyoni mwako kwa kulifikiria na kulitafakari wee wengi wanaita kuliwaza weee au kuliwaza weee hapo ndipo utaanza kupata akili au ufahamu.

NGOJA NIKUONYESHE JAMBO LA PILI KATIKA KUSHUGHULIKIA AKILI

2⃣. ANZA PIA KUOMBA MUNGU AKUPE AKILI.

Sijakosea ninapokuambia kuwa ili uanze kushughulikia hiyo akili yako ambayo imejiungamanisha na mwili kwa kuanza kuomba.

Biblia inasema wazi kuwa Mungu ndiye atupaye akili au ufahamu, kujua, kutambua nk.
Mfano wewe leo hii unaona kabisaa kuwa hauna akili ya kuushinda uzinzi, unachotakiwa ukifanye ni kurudi kwa Mungu ambaye yeye ndiye atupaye AKILI NJEMA AU NZURI.

Biblia inasema hivi. “Farao akamwambia Yusufu, Kwa kuwa Mungu amekufahamisha hayo yote, hapana mwenye akili na hekima kama wewe.” (Mwanzo 41:39)

Unapoisoma hiyo mistari unaona Yusufu alipata akili kutoka kwa Mungu. Hazikuwa akili zake, Mungu ndiye aliyemfahamisha  Yusufu kila kitu na ndani ya hizo akili kulibebwa na maarifa ya namna ya kukitatua hilo tatizo litakaloikabili hiyo nchi.

Sikikiza nikuambie dhambi ilipoingia iliharibu kabisa mfumo wa akili za mwanadamu. Uelewa wa mema wa mwanadamu uliharibiwa, ufahamu wa mambo mema wa mwanadamu uliharibiwa nk.

Sasa kumbuka Mungu ndiye yeye pekee ambaye alikupa wewe mbegu hiyo ya akili ila ilichakachuliwa na adui shetani. Akili zako zikaanza kutafakari uzinzi tuuu.

Mimi nakuambia ukweli kabisa ukipewa leo nafasi na Mungu ya kuingia ndani ya mioyo ya wanadamu uone wanachokitafakari cha kwanza duniani ni uzinzi. WENGI HUITA MAPENZI. Ehehee!,

Utasikia mtu anajitetea UNAJUA MUNGU ALITUUMBIA MAMBO HAYA BWANA.
Kama unataka kujua hili wewe siku moja jiachie tu sikiliza redio zinazopendwa na watu hasa vijana sikiliza nyimbo zinazoimbwa zinazungumzia nini, nenda kwenye TV angalia tamthilia uone zinazo pendwa weeee kama zile zinazoonyesha uchimbaji wa madini na visima vya maji?

Eti mwiambaji anaimba nyimbo anahamasisha tuchimbe madini na mabwawa ya samaki, hiyo nyimbo nani leo ataisikiliza? Duniani pote zunguka utaelewa ninachokuambia akili ya mwanadamu imedaka uzinzi kuliko unavyofikiri.

Tafuta wanaume kumi waulize na wawe wakweli akili yao inapopanga na nguvu zao zinapotumika mnoooo kutafuta fedha wanatafuta ili iweje! Akiwa mkweli kidogo atakuambia anatafuta fedha ili awe na familia maana yake anakuambia ili atafute mwanamke!!!

Sasa hapoo kwenye kutafuta mwanamke akiwa na fedha, mfuatilie utagundua akili yake jinsi ilivyovurugwa na uzinzi. Mpaka atakutajia orodha ndefu tu ya wadada aliowajaribisha ili atengeneze familia kwa fedha hizo anazozitafuta.

Nataka unielewe siwalaumu hao wanaume najaribu kukuonyesha umuhimu wa kuishughulikia akili kwa njia ya maombi ulivyo. Akili zetu nakuambia ukweli ni lazima kila siku zipelekwe msalabani kushughulikiwa na Bwana Yesu Kristo.

Ngoja nikupe mfano huu, fikiria ulishazini na wanaume  au wanawake wengi tu au mmoja.
Biblia inasema ukifanya hivyo unaungana na huyo mtu. Angalia mistari hii. - “Je! Hamjui ya kuwa miili yenu ni viungo vya Kristo? Basi nivitwae viungo vya Kristo na kuvifanya viungo vya kahaba? Hasha! Au hamjui ya kuwa yeye aliyeungwa na kahaba ni mwili mmoja naye? Maana asema, Wale wawili watakuwa mwili mmoja.” (1 Wakorintho 6:15-16).

Ukiipitia hiyo mistari unaona kuwa mtu anapozini anatengeneza muunganiko na huyo aliyefanya nae tendo hilo.

Swali la kujiuliza anaungana naye kivipi? Mbona walipofanya kila mtu alichukua hamsini zake? Anaunganika naye wapi?

Kuna maeneo mengi tu ataunganika naye, nataka nikuonyeshe eneo la nafsini mwake au moyoni mwake. Angalia mistari hii. “Maana kwa malaya mtu hutiwa katika hali ya kuhitaji kipande cha mkate; Na kahaba humwinda mtu anase nafsi yake iliyo ya thamani” (Mithali 6:26).

Unajua kinachotokea baada ya kuzini? Nafsi ya huyo mtu inatekwa. Biblia inasema kahaba anaiteka nafsi ya mtu hasemi mwili, hasemi roho, anasema nafsi au moyo.
Hata kwa wanawake ni hivyo hivyo unapozini na mwanaume fulani kinachotokea kwako ni nafsi yako KUTEKWA NA HUYO ULIYEZINI NAYE. Unafahamu neno kutekwa?

Maana yake nzuri huyo kahaba au huyo mwanamume ndiye atakayeimiliki KWA NGUVU HIYO NAFSI YAANI UMETEKWA HUNA LA KUFANYA MPAKA ATOKEE MTU MWENYE NGUVU KULIKO MTEKAJI ILI AJE AKUTOE HAPO.

Sikiliza kitu hiki, ndani ya hiyo nafsi huko kuna mfumo mzima wa akili. Kumbuka nilikufundisha kuwa hata utashi mara nyingi unaamua kufanya mambo ambayo akili INAYAJUA INAYAELEWA INAYATAMBUA INAYAFAMU NA IMEYAKUSUDIA AU KUYAVUMBUA NK.

Sasa unaposikia nafsi imetekwa maana yake mawazo, fikra, ufahamu, uelewa nk utashi na hisia za huyo mtu zinakuwa haziko huru tena. Shetani akitaka kucheza na akili zako ili aziteke anakirusi kinaitwa zinaa. Mtu akifanya tu tayari anajitengenezea yeye mwenyewe uteka wa fikra zake. Ndiyo maana unaweza ukawa unaota ndoto mara kwa mara umefungwa pingu au umeshikiliwa mahali fulani hujui hata umefikaje na unatokaje.

Angalia inawezekana Mungu anakuambia nafsi yako imetekwa. Nimewasikia watu wengi wanasema nafsi ya huyu imetekwa mwulize imetekwaje? Wengi hawajui ila wameambiwa na Mungu nafsi imetekwa inatumiwa na mtu. Ehehee.

Uzinzi mbaya sana mwanangu ukimbie. Kuna vitu vingi hutokea ngoja nikuambie hiki. Ndani ya akili zilizomo moyoni mwako kuna kitu kinaitwa kumbukumbu. Nikuambie unapolala na mwanaume yeyote hilo tendo hukaa moyoni mwako. Yaani akilini, fikra zako, mawazo yako yanabebeshwa hilo tendo.

Fahamu mapenzi yanaanzia kwenye kitu kinaitwa hisia ziko huko huko moyoni. Sasa angalia mwili unapowaka tamaa mbaya ya uzinzi lazima upeleke taarifa kwenye hisia hisia zitatoa taarifa kwenye akili HAPO SASA NDIPO AKILI YENYEWE IMETUNZA KUMBUKUMBU ZA TUKIO KAMA HILO AMBALO HUYO MTU ALILIFANYA NA FURANI.
Ndipo watu wengi hujikuta wakiwatafuta haoo watu. Mwingine utamsikia anakemea toka pepo, ehehee usishangae pepo hayupo ni mfumo wa akili umeharibiwa yaani fikra zimetekwa.

Ili utoke hapo lazima ujifunze kumwomba Mungu ashughulikie mfumo mzima wa akili zako, tubu, kama ulishatubu basi anza kuomba mara kwa mara Mungu aziponye hizo hisia zako za kizinzi na fikra zako za kizinzi.

Mungu yupo tayari hata kukupatia akili mpya. Kama alimpa akili Sulemani kwa nini sisi asitupe?

Mfalme Daudi alimwambia mwanawe maneno haya. “Sasa mwanangu, BWANA na awe pamoja nawe; ukafanikiwe, na kuijenga nyumba ya BWANA, Mungu wako, kama alivyonena kwa habari zako. BWANA na akupe busara na akili, akakuagizie juu ya Israeli; ili uishike torati ya BWANA, Mungu wako.” (1 Nyakati 22:11-12).

Mungu ana akili za aina nyingi sana. Sulemani alipewa akili za kutawala watu, kufanya maamuzi, na kujenga nyumba ya Mungu.

Wewe nenda kwa Mungu mwombe ashughulikie akili zako kwenye eneo la kuushinda mwili kwenye eneo la uzinzi.

Anazo akili atakupa. Ukizipata tu utajua namna ya wewe ufanye nini kama wewe ili uushinde uzinzi unaokusumbua kutokea mwilini mwako. Unapopewa akili yaani ufahamu lazima utajua nini chanzo cha hiyo nguvu ya zinaa.

Utajua una roho ya uzinzi, ninavyosema utajua fahamu kujua kuko ndani ya akili. Mungu ana njia nyingi sana za kukujulisha.

Cha msingi wewe anza kuishughulikia akili yako kwenye maombi. Unaweza ukakuta huna pepo la uzinzi ila ni mfumo wa vyakula tu unavyokula.

Unapomwomba Mungu akupe AKILI YA KUUSHINDA UZINZI  AU KUUSHINDA MWILI UNAOKUSUMBUA KWA TAMAA YA UZINZI anaweza kabisa akakupa ufahamu kwa kukuambia iwe kwa maono au ndoto au kwa kupitia masomo kama haya akakuambia usile sana  aina fulani ya chakula.

Kumbuka tulikotoka mwili uliumbiwa tendo la ndoa kabisa ila ulipewa utaratibu na Mungu wa namna ya kulifanya. Sasa ili mwili ukifanye hilo tendo vizuri (KWA WAFUATA UTARATIBU ULIOWEKWA) ili uwe imara katika jambo hilo kuna mfumo wa vyakula ambao mtu anatakiwa aulishe mwili wake na ndipo mwili utakuwa na nguvu au utawaka au utalihitaji mno tendo hilo la ndoa.

Sasa fikiria wewe huna hiyo akili hufahamu kuwa unapokula KWA WINGI AINA FULANI YA CHAKULA KITU GANI KINAKWENDA KUTOKEA MWILINI MWAKO. Utajikuta unapata shida sana kumbe ungeomba Mungu akupe akili angekufundisha au kukufahamisha punguza kula chakula cha aina fulani. SIKIA CHAKULA TU!!!!

Ngoja nikuchekeshe. Mabinti wengi siku hizi wanakula sana ubuyu!! Sijakosea ubuyu!! Mara ubuyu wa Zanzibar, mara sijui wa Singinda huu mwaya!!!! Ehehee hawajui ndani ya hicho chakula kuna nini.

Tafuta wataalamu watakuambia. Mwaka fulani nilisikia kama siyo waziri wa afya yule basi ni mtu mkuubwa Serikalini alizungumza bungeni wazi wazi kuhusu kazi ya ubuyu. Mwili unaamsha na kutengeneza nguvu za kulifanya tendo la ndoa.

Ngoja nikupe akili tena. Siku moja kipindi sijaoa nilikuwa nimekutana na wapendwa wenzangu, na ilikuwa jioni ya kulekea saa moja moja hivi. Niliwakuta wanakula karanga nyingi tu. Wote wameokoka na wote walikuwa wameoa.

Kutokana na neema ya utumishi huu kwa kweli walikuwa wananiheshimu sana ingawa sijaoa. Nilipofika pale walipo walinikaribisha karibu mtumishi. Wakaniambia tupo hapa tunapotezapoteza muda ili turudi manyumbani baada ya kazi nyingi za mchana.
Wakanikaribisha hizo karanga zilikuwa nyingi tu, wakati nataka kuchukua nile, mtu mmoja kati yao ambaye alikuwa na umri mkubwa kwetu wote. Akasema “hivi ninyi mnampa huyu bwana mdogo karanga hizi hamjui kuwa huyo bado mtoto?”

Nikashangaa wooote wakacheka!!! sana tu. Unajua huyo baba alinikataza kabisa nisile zile karanga. Nikatii sikula, akasema tena wewe haufai ukae na sisi hapa utatuambia nini wakati wewe ni mtoto?

Wakanicheka sana, Alizungumza kama utani akinihimiza nioe kwa umri wangu, kwa kweli uliniruhusu kipindi hicho nioe.

Nikaondoka hapo, lakini moyoni mwangu nilipata wazo la kutafuta kujua kwa nini huyo baba kanikataza nisile karanga akidai mimi ni mtoto zisije zikaniletea usumbufu.

Nikafikiri hivi usumbufu gani? Ikanipa kipindi nitafute kujifunza au nipate ufahamu. Nikaanza kuuliza, kusoma, niligundua si karanga tu vipo vyakula vingi ambavyo vinaweza kuchangia tena kwa sehemu kubwa mwili wako ukavutwa na wanaume au wasichana.

Nimekutana na vijana wengi wakisema wana tatizo wakilala hujikuta wakiwa wamejichafua. Na wengi hukimbilia kusema pepo la mahaba. Watakemea weeee. Kesho kutwa anajikuta vivyo hivyo.

Hata wasichana pia hutoa hivyo. Si kila mtu huwa ni pepo la mahaba wengine ni mfumo wa miili na akili zao zimebeba nini. Mara nyingi mtu huota kile alichojishughulisha nacho mchana.

Sasa akili hubeba pia kumbukumbu ya kile kilichoshughulishwa, kama uliwaza tendo la ndoa wee au mwili umebeba mfumo fulani wa chakula kwa wingi bila kiasi kilichotakiwa mwilini nakuambia utaziota sana ndoto za namna hii.

Sasa ili zitokee utaota unafanya tendo hilo. Wengine ni pepo au wachawi ndiyo chanzo nitakufundisha huko mbele. Hapa nataka upate akili ya namna mwili unavyoweza kuziwasha tamaa zake.

Sasa unapomwendea Mungu kumwomba akupe akili au ufahamu anaweza kukufahamisha wewe kama wewe nini ufanye ili kuudhibiti mwili.

Omba Mungu nipe akili usishangae atakupa ufahamu wa uanze kuomba maombi ya mfumo huu. “Nami nitawanyunyizia maji safi, nanyi mtakuwa safi; nitawatakaseni na uchafu wenu wote, na vinyago vyenu vyote. Nami nitawapa ninyi moyo mpya, nami nitatia roho mpya ndani yenu, nami nitatoa moyo wa jiwe uliomo ndani ya mwili wenu, nami nitawapa moyo wa nyama. Nami nitatia roho yangu ndani yenu, na kuwaendesha katika sheria zangu, nanyi mtazishika hukumu zangu, na kuzitenda.” (Ezekieli 36:25-27).

Anza kuomba maombi ya mfumo huo ili kushughulikia akili zako. Angalia hapo vinyago sehemu nyingine vinatajwa kama ni mawazo mabaya yaliyomo moyoni.

Kumbuka mawazo hukaa moyoni na ndiyo chanzo cha akili. Sasa Mungu anasema anao uwezo wa kumwondolea mtu moyo wa zamani yaani mfumo wa akili zake za kizamani zilizoambatana na mwili. Hapo kauita moyo wa jiwe.

Angalia jiwe kama lina akili. Moyo wa namna hii sehemu nyingine unaitwa mgumu, hauna ufahamu, umeharibiwa na mfumo wa mwili yaani dhambi. Sasa Mungu anasema anaweza kushughulikia mioyo ya watu kabisaa na kuifanya upya.

Anza kumwomba akutakase kwa hayo maji yake safi na kukuondolea moyo mgumu na kukuondolea vinyago au kumbukumbu mbaya.

Ubarikiwe sana na Mungu

Ukihitaji masomo yetu unaweza kuyapata kwa njia hizi zifuatazo:-

  1. Kwa Website yetu ya www.mwakatwila.org

2. YouTube - Mwakatwila au HUDUMA YA SOMA NENO LA MUNGU (HUSONEMU).

3. Facebook ingia katika hiyo tovuti au website yetu utaona alama ya facebook(f) like na utapata maelezo ya kujiunga au andika “SOMA NENO LA MUNGU”

4. Instagram ingia kwa link pale juu au ingia Instagram na andika Steven Mwakatwila

5. DVDs📀 au CDs 💿

6. VITABU

7. Kwa njia ya REDIO:-
➖Rungwe FM 102.5 Kila siku ya Jumapili  saa tatu mpaka saa nne usiku.
➖Baraka FM 107.7 Kila siku ya Jumanne saa kumi na mbili jioni mpaka saa moja usiku.
➖Bomba FM 104.1 Kila siku ya Ijumaa saa tatu usiku mpaka saa nne usiku.

8. Unaweza kutupata kwenye ONLINE RADIO yetu:-  radio.mwakatwila.org

Kwa mawasiliano zaidi Utatupata kwa namba hizi:- +255754849924 - +255756715222

Wako
Mwl Steven & Beth Mwakatwila.
18/01/2019

No comments:

Post a Comment