Wednesday, January 9, 2019

1⃣ NAMNA YA KUFANYA ILI UPATE KUISHINDA DHAMBI YA UZINZI

Na: MWL STEVEN & BETH MWAKATWILA

FUATANA NASI YOUTUBE

FUATANA NASI ONLINE REDIO
👉🏼 radio.mwakatwila.org

🗓 2 Disemba, 2018

Bwana Yesu Kristo asifiwe sana. Leo nimeona nikuandikie somo hili, ili upate kuishinda dhambi ya uzinzi kuna mambo unatakiwa uyaangalie.

Jambo la kwanza ni:-
Angalia chanzo cha uzinzi unaokukabili.

Kuna aina  mbili za vyanzo vya uzinzi.

Aina ya kwanza ni mwili wa mtu. “Lakini mkiongozwa na Roho, hampo chini ya sheria. Basi matendo ya mwili ni dhahiri, ndiyo haya, uasherati, uchafu, ufisadi, ibada ya sanamu, uchawi, uadui, ugomvi, wivu, hasira, fitina, faraka, uzushi, husuda, ulevi, ulafi, na mambo yanayofanana na hayo, katika hayo nawaambia mapema, kama nilivyokwisha kuwaambia, ya kwamba watu watendao mambo ya jinsi hiyo hawataurithi ufalme wa Mungu.Tunda la Roho" (Wagalatia 5:18-21)

Ukiangalia hapo unaona wazi kuwa matendo ya mwili au chanzo kimojawapo cha uzinzi  afanyao mtu (YAANI ROHO YAKO) kinaweza kuwa mwili wa mtu tu wala si shetani.

Fahamu mwili na roho ni vitu viwili tofauti. Mtu ni roho alipewa mwili. Mwili una mambo yake na roho pia ina mambo yake.

Mtu au roho ni wewe, dhambi ilipotendwa na Adamu na mkewe ilisababisha mtengano wa tabia kati ya mwili wako na roho yako.  “Kwa maana wale waufuatao mwili huyafikiri mambo ya mwili; bali wale waifuatao roho huyafikiri mambo ya roho. Kwa kuwa nia ya mwili ni mauti; bali nia ya roho ni uzima na amani. Kwa kuwa ile nia ya mwili ni uadui juu ya Mungu, kwa maana haitii sheria ya Mungu, wala haiwezi kuitii.Wale waufuatao mwili hawawezi kumpendeza Mungu." (Warumi 8:5-8)

Ukiipitia hiyo mistari utagundua kuwa mwili wako wewe yaani wewe (roho) una nia yake na roho yako nayo ina nia yake.

Moja ya nia ya mwili ni uzinzi (KUFANYA TENDO LA NDOA NJE YA UTARATIBU ULIOWEKWA).

Fahamu mwili uliumbiwa na Mungu ufanye tendo hilo kihalali kabisaa. Mungu aliweka utaratibu mzuri wa namna mwili ulifanye tendo hilo, aliumba mwanaume na mwanamke.

Aliwapa nafasi ya kulifanya tendo la ndoa wengine wanaita kujamiiana. Angalia mistari hii. “Mungu akaumba mtu kwa mfano wake, kwa mfano wa Mungu alimwumba, mwanamume na mwanamke aliwaumba. Mungu akawabarikia, Mungu akawaambia, Zaeni, mkaongezeke" (Mwanzo 1:6-27-28)

Mungu aliwapa hawa ndugu ruhusa ya kuzaana, fahamu hauwezi ukazaa bila kushiriki tendo la ndoa au kujamiiana. ONDO SUALA LA KISAYANSI AU MIUJIZA.

Najua kwa dunia ya sasa watu wanaweza pata mtoto kwa njia nyingi tu nje ya hii iliyowekwa ya kushiriki tendo la ndoa au Biblia inaliita ‘KUMJUA’. "Adamu akamjua Hawa mkewe; naye akapata mimba, akamzaa Kaini, akasema, Nimepata mtoto mwanamume kwa BWANA." (Mwanzo 4:1)

Pia tunaona namna Bwana Yesu Kristo alizaliwa kimiujiza. Haujawahi sikia au kuona mtu anakuwa na mimba kabisaa na anajifungua misumari au maembe? Ehee adui naye anaweza kutungisha wanawake mimba kwa njia za kichawi bila hao wanawake kujamiiana na wanaume.

Mungu alipokuwa anamwumba mwanadamu alimtengenezea njia ya kawaida ya namna ya kushiriki tendo la ndoa kabisaa, si kwa sababu ya kupata watoto hapana, pia ni sehemu ya uhitaji wa mwili.

Biblia inasema “Basi kwa habari ya mambo yale mliyoandika, ni heri mwanamume asimguse mwanamke. Lakini kwa sababu ya zinaa kila mwanamume na awe na mke wake mwenyewe, na kila mwanamke na awe na mume wake mwenyewe. Mume na ampe mkewe haki yake, na vivyo hivyo mke na ampe mumewe haki yake. Mke hana amri juu ya mwili wake, bali mumewe; vivyo hivyo mume hana amri juu ya mwili wake, bali mkewe. Msinyimane isipokuwa mmepatana kwa muda, ili mpate faragha kwa kusali; mkajiane tena, Shetani asije akawajaribu kwa kutokuwa na kiasi kwenu." (1 Wakorintho 7:1-5)

Tendo la ndoa hilo Mungu hakuliweka ili litumike kuzaana tu, liliwekwa pia ili kuwafanya hao watu wasiingie katika uzinzi.

Kumbuka mwili unapofikia kipindi fulani unafunguka katika hali ya kulihitaji hilo tendo la ndoa. Sasa Mungu alijua hilo kuwa mwili utahitaji hiko tendo akaamua kutengeneza mfumo huu tunaouita leo ndoa.

Ili mwili wa mwanamume ukilihitaji hilo tendo  mke wake ndiye atakaye litimiza na kwa mwanamke ni hivyo hivyo mtimizaji ni mume wake.

Mungu alifanya hivyo ili kuondoa dhambi ya uzinzi yaani mtu kulifanya tendo la ndoa nje ya mumewe au mkewe kwa wasiooa au kuolewa pia wasifanye hilo tendo wengine wanaita uasherati.

Narudia tena, Kila mtu aliyepewa mwili akifikia umri fulani niseme majira fulani  mwili wake utaanza kulihitaji tendo hilo kabisa.

Sasa ili kuudhibiti huo mwili utulie kuna mambo unatakiwa uyafanye.

Jambo la kwanza anza kuviondoa vyanzo au vichochezi vinavyouamsha mwili ili uhitaji hilo tendo la ndoa kabla ya majira au wakati. Biblia inasema hivi. “Nawasihi, enyi binti za Yerusalemu, Kwa paa na kwa ayala wa porini, Msiyachochee mapenzi, wala kuyaamsha, Hata yatakapoona vema yenyewe" (Wimbo ulio bora 3:5)


Angalia na hii pia. “Wapenzi, nawasihi kama wapitaji na wasafiri, ziepukeni tamaa za mwili zipiganazo na roho" (1Petro 2:11).

Ukiipitia hiyo mistari utagundua kuwa mapenzi yanayoweza kuzaa tendo la ndoa linaweza kuchochewa. Mwili unapotengenezewa vichochezi vya mapenzi huanza kuamka na kuanza kulihitaji hilo tendo.

Maandiko yanatufundisha kuwa moja ya tamaa za mwili ni hiyo hali ya mwili kutamani tendo la ndoa.  Lakini tunaambiwa tuziepuke hizo tamaa zinazouamsha mwili katika kuhitaji mambo yake. Moja ya mambo ya mwili ni zinaa. Yaani mwili wenyewe unatamani kila mwanamke au kila mwanaume.

Unajua ukiuendekeza unaweza ukamtamani hata mwanamke mwenzio au mwanamume mwenzio?

Biblia inasema hivi “Kwa ajili ya hayo Mungu aliwaacha katika tamaa za mioyo yao, waufuate uchafu, hata wakavunjiana heshima miili yao. Kwa maana waliibadili kweli ya Mungu kuwa uongo, wakakisujudia kiumbe na kukiabudu badala ya Muumba anayehimidiwa milele. Amina. Hivyo Mungu aliwaacha wafuate tamaa zao za aibu, hata wanawake wakabadili matumizi ya asili kwa matumizi yasiyo ya asili; wanaume nao vivyo hivyo waliyaacha matumizi ya mke, ya asili, wakawakiana tamaa, wanaume wakiyatenda yasiyopasa, wakapata nafsini mwao malipo ya upotevu wao yaliyo haki yao. Na kama walivyokataa kuwa na Mungu katika fahamu zao, Mungu aliwaacha wafuate akili zao zisizofaa, wayafanye yasiyowapasa. Wamejawa na udhalimu wa kila namna, uovu na tamaa na ubaya; wamejawa na husuda, na uuaji, na fitina, na hadaa; watu wa nia mbaya, wenye kusengenya, wenye kusingizia, wenye kumchukia Mungu, wenye jeuri, wenye kutakabari, wenye majivuno, wenye kutunga mabaya, wasiowatii wazazi wao, wasio na ufahamu, wenye kuvunja maagano, wasiopenda jamaa zao, wasio na rehema; ambao wakijua sana hukumu ya haki ya Mungu, ya kwamba wayatendao hayo wamestahili mauti, wanatenda hayo, wala si hivyo tu, bali wanakubaliana nao wayatendao." (Warumi 1:24-32)

Ukiipitia hiyo mistari utaona chanzo cha mabaya hayo yoote ni vichocheo fulani ambavyo mtu anaviendekeza mpaka vinawasha tamaa ya mwili na roho ya huyo mtu inajikuta inalemewa na kuuruhusu mwili kufanya kile ikitakacho.

Si unajua kinachohesabika kimefanya dhambi ni roho? Biblia inasema

"Roho itendayo dhambi, ndiyo itakayokufa; mwana hatauchukua uovu wa baba yake, wala baba hatauchukua uovu wa mwanawe, haki yake mwenye haki itakuwa juu yake, na uovu wake mwenye uovu utakuwa juu yake." (Ezekieli 18:20)

Roho yako ndiyo ina maamuzi ya mwisho ya kukifanya hicho cha mwili (Biblia inasema kufuata tamaa za mwili) au kuukatalia huo mwili yaani kujiepusha au kutokuufuata mwili.

Jifunze kujilinda kila siku na vyanzo vyote vinavyotafuta kuamsha mwili katika kufanya zinaa.
Angalia mambo yafuatayo. Achana na mazungumzo yanayozungumzia tendo la ndoa.

“Msidanganyike; Mazungumzo mabaya huharibu tabia njema.” (1 Wakorintho 15:33)

Tabia za mwili zinautumia sana mlango huu wa mazungumzo ili kuzishinda tabia njema. Angalia wewe ni binti au mwanaume haujaolewa au kuoa au umeoa au kuolewa na mkeo yupo mbali au mumeo yupo mbali, unajiruhusuje kuzungumza au kujadili mambo ya tendo la ndoa wakati unajua kabisaa mwili utahitaji tendo hilo? Fikiria kidogo utakimbilia wapi mwili ukikutinga?

Ni rahisi  kujikuta unanguka na kuwa miongoni mwa vijana au wasichana wapumbavu. Biblia inasema wazi mtu afanyalo tendo hilo anaingia kwenye kundi la wapumbavu. Msome Tamari alivyomwambia Amnoni.

Jilinde na mazungumzo mabaya hasa unapokuwa na mtu wa jinsia tofauti, ni rahisi sana mkaanza mazungumzo kama utani ghafla ukajikuta unapata shida sana. Si unajua mlango mmoja wapo wa ufahamu ni masikio?

Angalia sana masikio yako yanasikia nini? Hayo unayoyasikia je! Hayakuharibu tabia wewe?

Jambo lingine jihadhari na yale macho yako yanayotamani mnoo kuyaona hasa mabaya yahusuyo uzinzi.

Bibilia inasema tujiepushe na tamaa za macho. “Msiipende dunia, wala mambo yaliyomo katika dunia. Mtu akiipenda dunia, kumpenda Baba hakumo ndani yake. Maana kila kilichomo duniani, yaani, tamaa ya mwili, na tamaa ya macho, na kiburi cha uzima, havitokani na Baba, bali vyatokana na dunia.” (1 Yohana 2:15-16).

Fikiria kidogo wewe ni mwanaume au mwanamke, macho yako yanakusukuma haswaa kuangalia nini?  Macho yako mwilini, mwili unaweza kuyatumia hayo macho yako kuziwasha tamaa za uzinzi kabisa usipokuwa makini na hayo macho yako.

Narudia tena kukufundisha kuwa, macho yanaweza kutamani kuangalia kitu fulani, Biblia inasema tamaa ya macho, sasa wewe uliyepewa hayo macho lazima ujue kuwa hayo macho hicho inachotaka kukitazama je! Kinafaa kutazamwa au kitakupelekekea kuziamsha tamaa za mwili za uzinzi?

Bwana Yesu anaposema ni heri kwenda mbinguni ukiwa na jicho moja anatufundisha hiki ninachokuambia. Jicho linaweza kukukosesha usipolifanya KUTOKUONA.

Sina maana ufumbe, ninamaanisha usikiangalie kitu kinachotafutwa kuangaliwa na macho kinachokuvuta kwenye uzinzi.

Usiangalie video za ngono achana nazo kabisaa, kwanza huko hakuna jambo jipya utakalolipata zaidi tu ni kuichafua nafsi yako na picha chafu hizo zitakazo kujengea kumbukumbu mbaya maishani mwako.

Ikiwa wewe ni mwanamke jihadhari sana na tabia ya kuyaruhusu macho yako yamtazame mvulana weee mpaka unauamsha mwili kuwaka tamaa, hata kwa wanaume ni vivyo hivyo.

Wewe fikiria unamtazama msichana mwenye makalio makubwa nk unajiruhusu kumtazama weee!!! Hapana ukiona na utajua tu kuona kwako kunakupeleka wapi jipofue mpendwa!!!!! Acha kuangalia yaruhusu macho yako yatazame MTI ULEE EHEHEE!!!

Biblia inasema wazi kuwa macho yanaweza kutumika kutazama vibaya au vizuri, sasa unakaa unatazama picha chafu hapo ni rahisi kujikuta unavutwa kuzini, ndiyo wengi husema mwili unanisumbua sana. Kumbe wewe mwenyewe ndiyo umekuwa chanzo cha kujitengenezea usumbufu.

Unajua watu wana simu lakini wanatofautiana namna ya kuzitumia hizo simu. Ndiyo vivyo hivyo hata kwenye macho, sote tuna macho, lakini namna ya kuyatumia macho ndiyo tunatofautiana.

Mke wangu nitamtazama KWA KUMTOLEA MIMACHO YOOOTE kwa sababu ni mke wangu, nimeruhusiwa yeye lakini mwanamke mwingine yeyote yule sina ruhusa ya kumtazama kama nimtazamavyo mke wangu.

Angalia mistari hii. “Maana maagizo hayo ni taa, na sheria hiyo ni nuru,Na maonyo ya kumwadilisha mtu ni njia ya uzima. Yakulinde na mwanamke mwovu, asikupate,Na kukuponya na ubembelezi wa mgeni. Usiutamani uzuri wake moyoni mwako; Wala usikubali akunase kwa kope za macho yake. Maana kwa malaya mtu hutiwa katika hali ya kuhitaji kipande cha mkate; Na kahaba humwinda mtu anase nafsi yake iliyo ya thamani" (Mithali 6:23-26)

Macho yanaweza kutengeneza mtengo wa kiuzinzi kabisaa, sasa lazima uwe makini kwenye kuangalia kwako na kuangaliwa kwako. Wewe unaona ghafla nguvu ya macho yako inalegea kwa mvulana fulani, kwanini uyaendekeze? Si ndiyo unamfungulia mlango wa kukutongoza?

Macho yanatoa taarifa mpendwa, mtu akikuangalia macho tu anapata taarifa kuwa huyu anasema nini. Hebu jifunze kujilinda na kile unachokiangalia.

Jifunze pia kuyatawala mawazo yako. Sikiliza uzinzi au tendo la ndoa huchochewa pia na fikra za ndani ambazo zinainuka kukiwaza na kukitafakari hicho kitendo.

Mfano angalia mistari hii. “Maana maagizo hayo ni taa, na sheria hiyo ni nuru,Na maonyo ya kumwadilisha mtu ni njia ya uzima. Yakulinde na mwanamke mwovu, asikupate, Na kukuponya na ubembelezi wa mgeni. Usiutamani uzuri wake moyoni mwako; Wala usikubali akunase kwa kope za macho yake. Maana kwa malaya mtu hutiwa katika hali ya kuhitaji kipande cha mkate; Na kahaba humwinda mtu anase nafsi yake iliyo ya thamani" (Mithali 6:24-26)

Ukiipitia hiyo mistari utaona tunaonywa juu ya kutamani au kutafakari kwetu humo moyoni. Mapenzi huanzia katika hisia za ndani, sasa lazima uzitawale hisia zako za kimapenzi zisivuke mpaka na kukubaliana na mwili.

Usijiruhusu kukubaliana na hali ya kuutafakari uzuri wa huyo mwanaume au mwanamke. Kwenye kutafakari ndipo hapo wengi hushindwa kuutawala mwili wao.

Usijiruhusu kuchukua muda mrefu weee kutakari ngono, kiasili wazo hilo litakuja tu, lakini uwe makini kuliangalia huko ndani yako.

Niseme hivi tamaa ikija usiiruhusu mpaka ikachukua mimba mpaka ikazaa.

Mungu anajua kuna watu wana mwili ambao una nguvu mnoo kwenye kuhitaji tendo la ndoa. Fahamu hatufanani katika hili jambo. Na hili linatokana na mambo mengi.

Kumbuka tunazungumzia CHANZO CHA MWILI KUMSUKUMA MTU KUZINI. SASA Ili kuupunguzia huo mwili ukali wa kutaka kuzini Mungu akaamua kumtumia mtu msaada.

Msaada huo ni Roho Mtakatifu aliyetupatia. Sikiliza nikuambie unaweza kuwa na neno na ukashika mno utaratibu huo wa kutokuzini.

Lakini bado mwili wako ukawa na nguvu kuliko roho yako. Hapo ndipo Mungu alipoamua kutusaidia.

Biblia inasema. “kwa maana kama tukiishi kwa kufuata mambo ya mwili, mwataka kufa; bali kama mkiyafisha matendo ya mwili kwa Roho, mtaishi.” (Warumi 8:13)

Angalia matendo ya mwili fahamu moja ya tendo la mwili ni uzinzi. Matendo hayo ya mwili  hufishwa na ROHO MTAKATIFU.

Jifunze kuwa na maombi mruhusu Roho Mtakatifu afishe tabia ya uzinzi uliobebwa mwilini mwako.

Omba nguvu za Roho Mtakatifu ziutawale Mwili wako. Roho Mtakatifu ameletwa pia atusaidie udhaifu wetu wa kutawaliwa na mwili.

Angalia mistari hii "Basi nasema, Enendeni kwa Roho, wala hamtazitimiza kamwe tamaa za mwili. Kwa sababu mwili hutamani ukishindana na Roho, na Roho kushindana na mwili; kwa maana hizi zimepingana, hata hamwezi kufanya mnayotaka. Lakini mkiongozwa na Roho, hampo chini ya sheria." (Wagalatia 5:16-17)

Mwili unatakiwa USHINDANE NA ROHO MTAKATIFU, Si roho yako. Angalia hiyo Roho imeandikwa kwa herufi kubwa. Fahamu huyo ni Roho Mtakatifu.

Mwombe Roho Mtakatifu autawale mwili wako, roho yako kwa kweli haiwezi kuushinda mwili. Ukijifunza hilo utashangaa hauishi kwa sheria
Kwani najua umejitengenezea sheria nyingi lakini bado unashangaa unazini tu.

Hebu jifunze kumwamini Roho Mtakatifu na ujiachie kwake ili ashindane yeye na mwili wako. Mwombe, atakusaidia, jifunze kuomba ujazo na nguvu za Roho Mtakatifu pia.

Naamini umenielewa. Nikipata muda nitakuonyesha kiini cha roho (pepo kinachoweza kuwa chanzo cha tabia ya uzinzi pia).

Barikiwa sana

Wako
Mwl Steven & Beth Mwakatwila

No comments:

Post a Comment